May 5, 2016

LOGO





Mar 28, 2016

ASKOFU: KANISA LINAPASWA KUJICHUNGUZA NA KUJIREKEBISHA KUTOKANA NA UOZO.


Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino Mokiwa.

Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino Mokiwa amewaonya wakristu dhidi ya mambo ambayo yanaelekea kulibomoa kanisa. Ameyasema hayo leo kwenye Ibada ya Pasaka ya kitaifa iliyofanyika Kanisa la Mtakatifu Albano Upanga jijini Dar es Salaam ambako pia Mkuu wa Mkoa Paul Makonda amehudhuria.

Askofu Mokiwa ameyaita mambo hayo yanayolibomoa kanisa kama mawe na kuyataja kuwa ni pamoja na mashindano miongoni mwa madhehebu ya kikristo. 


Amesema kanisa linapaswa kujichunguza na kujirekebisha kutokana na uozo unaofanyika. Alisema madhehebu yanashindana katika kumiliki vitu kama vile shule au hospitali baada ya kumuhubiri Kristo.

Ameyataja mambo mengine ambayo yanatishia uhai wa kanisa ni kitendo cha maaskofu, wachungaji mapadre na waumini kupgina vita. Amesema baadhi ya watumishi hao wa Mungu wamekosa utii na hawafuati taratibu za kanisa badala yake wamejenga tabia ya kusemana vibaya, kutukanana na kupanga mapinduzi ya kupindua wengine.

“Kusemana, kusingiziana na kusema uongo yamekuwa mambo ya kawaida, na ukiwaita wahusika ili myazungumze wanakimbia na hawako tayari kufanya hivyo, nguvu ya makundi ndani ya kanisa inatisha kiasi kwamba chuki ni kubwa na watu hawapendani,” alisema Askofu Mokiwa.

Aidha ameonya nguvu ya fedha kutumika kulivuruga kanisa. Amehoji kama watu wana fedha kwa nini hawaendi kusaidia watoto yatima au kuchangia uenezaji wa Injili badala ya kutumia fedha hizo kulivuruga kanisa? Amesema watu wanafanyabiashara kanisani badala ya kuhubiri Injili.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaonya waumini wenye tabia ya kumpigia simu na kuomba apeleke polisi kanisani kwa sababu ya vurugu. 


Makonda amesema mtu atakayefanya hivyo kuanzia sasa atashughulika naye kwa sababu kanisa lina taratibu zake za kushughulikia migogoro na siyo kupeleka polisi, kwani ni mambo ya aibu

Israel imeua watoto 50 Wapalestina tokea Oktoba


Israel imeua watoto 50 Wapalestina tokea Oktoba
Wanajeshi wa Utawala haramu wa Israel wameua watoto 50 Wapalestina tokea Oktoba mwaka jana, wakati ilipoanza Intifadha au mwamko mpya wa Palestina. 
 
Kwa mujibu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kutetea Watoto- Tawi la Palestina, ukosefu wa uchunguzi huru na wa wazi kuhusu ukatili huo wa Israel ni jambo ambalo limepelekea kuendelea kuuawa watoto Wapalestina kiholela. 

Ayed Abu Qtais, wa jumuiya hiyo amelalamika kuwa Umoja wa Mataifa umefeli kutekeleza majukumu yake kuhusu kutetea haki za watoto Wapalestina. 

Tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2015 hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za utawala wa Kizayuni na njama za utawala huo za kupotosha utambulisho wa Baitul Muqaddas pamoja na mpango wake wa kuugawa kiwakati na kimahali msikiti mtukufu wa Al-Aqsa. Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha ya Quds. 

Wapalestina zaidi 200 wameshauawa shahidi tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba mwaka jana hadi hivi sasa.

'Kampeni za urais zinaiaibisha Marekani'


'Kampeni za urais zinaiaibisha Marekani'
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amekiri kuwepo utovu wa nidhamu katika kampeni za uchaguzi wa rais nchini humo na kusema jambo hilo limepelekea Marekani kuaibika kimataifa.

Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CBS, Kerry amesema, "kila mahala ninapoenda, kila kiongozi ninayekutana naye, wananiuliza ni nini kinachoanedelea Marekani. Hawawezi kuamini yanayojiri na naweza kusema wameshangazwa."

Kauli hiyo ya Kerry inaonekana kuelekezewa wagombea wawili wanaowania uteuzi wa chama cha Republican kugombea urais, Donald Trump na Ted Cruz ambao wamekuwa wakitoa matamshi makali dhidi ya Uislamu na jamii ya watu weusi nchini Marekani. 

Trump na Cruz wametaka kuchukuliwe hatua kali za kuwadhibiti Waislamu na kuzuia wahamiaji wasiokuwa wazungu kuingia nchini humo. Halikadhalika wagombea hao wawili wenye misimamo ya kufurutu wada wamekuwa wakitusiana hadharani kuhusu masuala mbali mbali wakiwemo wake zao.

Hivi karibuni pia Trump, alitishia kuwa, iwapo hatateuliwa na chama hicho, basi watu wasubiri ghasia na machafuko kote Marekani.

Kerry ameongeza kuwa matamshi ya wagombea hao wawili yamepelekea itibari ya Marekani kutoweka duniani.

Mar 25, 2016

Ushindi wa UPDP Ziwani Pemba waota mbawa

Afisa mdhamini wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC), Ali Mohamed Dadi amesema mshindi wa uwakilishi katika jimbo la Ziwani ni Suleiman Ali wa CCM na si Asaa Hamad wa UPDP ambae alitangazwa awali.

Dadi kutoka ofisi ndogo ya Pemba alisema jana kuwa msimamizi wa uchaguzi katika wilaya ya Chakechake, Othman Khamis alikosea wakati wa kujaza karatasi ya matokeo ya mshindi wa jimbo hilo.

“Nimezungumza naye na amesema kwamba alitoa ufafanuzi kuwa walifanya makosa katika kuandika matokeo, hivyo aliyeshinda ni mgombea wa CCM,” alisema.

Katika karatasi hiyo ya matokeo iliyokuwa imebandikwa ukutani, Asaa Ali Hamad alionekana kuwa amepata kura 221 dhidi ya 121 za mgombea wa CCM, lakini kwa ufafanuzi huo waZEC hakuna chama cha upinzani kilichoshinda nafasi ya uwakilishi au udiwani.

Kwa matokeo hayo, CCM imeshinda majimbo yote ya uwakilishi Unguja na Pemba na hivyo kuzidisha utata kwa rais mteule, Dk.Ali Mohamed Shein anayeapishwa leo, kuunda serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) kwa mujibu wa ibara ya 9 (3) ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 2010.

Awali, kulikuwa na uwezekano wa UPDP kutoa mteule wa nafasi ya makamu wa kwanza wa rais kwa kuwa kilitangazwa kimakosa kupata kiti cha uwakilishi baada ya CCM lakini baada ya ufafanuzi huo wa ZEC matumaini hayo yameyeyuka.

Kuyeyuka kwa ndoto hiyo ya UPDP kunamaanisha kwamba hakuna chama kilichoshika nafasi ya pili kwakupata kura asilimia 10 au zaidi, ambacho kwa mujibu wa katiba hiyo kingekuwa na nafasi ya moja kwa moja kutoa makamu wa kwanza wa rais na baadae mawaziri wa upinzani kuunda SUK.

Tangu Dk.Shein atangazwe kushinda urais katika uchaguzi wa marudio baada ya matokeo ya ule wa awali kufutwa, mjadala mkubwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii umekuwa ni jinsi gani atateua serikali yake kukidhi matakwa ya katiba ya kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa ili kuendeleza maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa baina ya CCM na CUF kabla ya uchaguzi wa 2010.

Wakati naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai akisema rais Shein atatumia busara zake kumpata makamu wa kwanza wa rais, baadhi ya wanasheria wamesema hawaoni ufumbuzi wa moja kwa moja kutokana na upungufu huo wa kikatiba.

Kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, rais atateua makamu wa kwanza wa rais kutoka chama kilichoshika nafasi ya pili na mgombea wake wa urais kupata asilimia 10 ya kura za urais, au nafasi ya makamu wa kwanza itaenda kwa chama chochote cha upinzani kilichoshika nafasi ya pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika baraza la wawakilishi.

CCM WANAKUOGOPA MAALIM SEIF; JAKAYA KIKWETE


 Image result for MAALIM SEIF

Maalim Seif Shariff Hamad, Mgombea wa Urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana kupitia Chama cha Wananchi (CUF), amesema CUF haitashiriki uchaguzi wowote chini ya Tume ya Jecha Salim Jecha, anaandika Josephat Isango.

Akizungumza na MwanaHALISI Online Hoteli ya Serena ambapo yupo kwa mapumziko baada ya kulazwa, Maalim Seif amesema kuwa kama yatatokea maridhiano yatakaoongozwa na kusimamiwa na taasisi huru za kidemokrasia, bila vitisho vya majeshi na polisi, kuwa na vyombo huru vya habari na tume huru sio hii iliyopo Zanzibar chini ya Jecha, hapo CUF kitaweza kufikiri kushiriki uchaguzi.

Ameongeza kuwa harakati za kudai haki, zitaendelea kwa njia ya amani ili marekebisho ya tume yafanyike kwani kwa utaratibu uliopo hata mwaka 2020 upinzani ukishinda Tanzania bara, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitang’gang’ania madaraka.

“CUF tunaamini katika amani, tusichafue amani, tusichafue nchi yetu, tuendeleze mapambano kwa kutoitambua serikali iliyojiweka madarakani katika uchaguzi haramu wa Machi 20 mwaka huu, wala hatutaipatia ushirikiano wowote katika mambo yote” alisema.

Uchaguzi wa 20 Machi, sio halali. Jecha hakuwa na uwezo wa kisheria wala kikatiba kufuta uchaguzi, mgogoro uliopo sasa umesababishwa na Jecha, ukapewa baraka za CCM, sababu CCM hawataki kushindwa, na hawataki wapinzani kuongoza. Kila CCM ikishindwa hutoa visingizio.

“Kabla Kikwete (Rais Mstaafu Jakaya Kikwete) hajaondoka madarakani, aliniambia kuwa Maalim CCM wanakuogopa, wanajua ukishinda utaweza kuvunja Muungano, lakini nilimwambia, CCM ndio wenye jeshi, wenyewe ndio wenye dola mimi nitavunjaje Muungano? Hiyo ni hofu na visingizio tu ili waendelee kukwapua madaraka.”Alisema.

Ameweka bayana kuwa kwa sasa CCM imewarejesha wananchi miaka 20 iliyopita, kwani uhasama wa watu kutengana kwenye shughuli za kijamii kwa sababu za tofauti za kisiasa zimeanza kurejea baada ya CCM kulazimisha kukwapua madaraka ya wananchi kwa kufuta uchaguzi wa 25 Oktoba mwaka jana.

Akizungumzia suala la Muungano kama ambavyo amekuwa akihusishwa Maalim seif amesema kuwa sasa Muungano utavunjwa na CCM, sio CUF wala yeye kama wanavyosingizia.

Ameongeza kuwa kwa sababu CCM ya bara ndio inalazimisha kuweka viongozi waliokataliwa na wananchi wa Zanzibar na chama chao kwa kutumia majeshi na polisi wao ndio husababisha wananchi wachukie Muungano.

Aidha kuhusu uchaguzi wa marudio wa Machi 20, Seif amesema kuwa CUF imeshinda, kwani wananchi wa Zanzibar waliitikia wito wa CUF, wakasusa, hawakujitokeza kupiga kura. Hizo zilizotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wanajua walipozipata wao na CCM.

“Mimi nilishasema tangu awali, kuwa matokeo yameshajulikana kabla ya uchaguzi, sababu ni ya kupika, namhurumia Dk Shein kwa kujisifu kupata kura ambazo hazipo, mawakala waliweka wao na wasimamizi na kuna taarifa kuwa wapiga kura walikuwa wanapewa rundo la kura, wapige na kutumbukiza ili kukidhi matakwa ya CCM.” Amesema Maalim Seif.

Maalim Seif amewatakia utulivu Wazanzibar wote, na kuwaarifu kuwa afya yake ni imara, na atarejea Zanzibar wakati wowote kuungana nao.

Wazazi mbaroni kwa kuozesha wanafunzi

polisi mkoani Mwanza inawashikilia wazazi wawili kwa tuhuma za kuwaozesha kwa wanaume watoto wao wa kike waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.

Hatua ya kukamatwa kwa wazazi hao, Josefine Benjamin na Athuman Haruna wakazi wa Kata ya Igogo jijini hapa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga kwa watendaji wa kata zote kufanya tathmini ili kubaini wanafunzi ambao hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa.

Mtendaji wa Kata ya Igogo, Joseph Rulamye alisema uchunguzi uliofanywa kwenye kata hiyo ulioshirikisha walimu wakuu, ofisi ya kata na mratibu elimu ulibaini kuwa kuwapo kwa wanafunzi ambao wameozeshwa kwa wanaume baada ya wazazi wao kupokea mahari.

“Tuliwasaka na kuwatia mbaroni wazazi hawa ili watusaidie kuwapata watoto hao na wanaume waliowaoa,” alisema Rulamye.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi, kuwatafuta watoto hao na kuwasaka ‘waume’ zao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Akizungumzia tuhuma za kumuoza binti yake, mmoja wa wazazi, Athuman Haluna alidai hakushiriki njama hizo, badala yake akamtupia lawama bibi wa mtoto huyo akidai ndiye aliyesuka mipango ya mjukuu wake kuolewa badala ya kuendelea na masomo.

“Mtoto huyu anaishi na bibi yake, mimi nilikuwa najua tayari ameripoti shuleni. Bibi yake ndiye mhusika mkuu wa tuhuma hizi,” alidai Haruna.

Mratibu wa Elimu Kata ya Igogo, Charles Kialiga alisema ofisi yake kwa kushirikiana na mamlaka nyingine inaendelea kufuatilia taarifa za watoto wengine ambao hawajaripoti kwenye shule za umma walizopangiwa ili kubaini iwapo wamejiunga na shule binafsi au la.

Katika kikao chake na wakuu wa shule, waratibu elimu kata na watendaji wa kata zote za wilaya hiyo, Konisaga aliagiza uongozi wa kata kufuatilia taarifa za watoto wote waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari, lakini hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa.

Pia, aliwataka viongozi hao wa kata kwa kushirikiana na walimu wakuu wa shule za msingi na wenzao wa sekondari kubaini iwapo wanafunzi hao wako majumbani au wameozwa.

Serikali imeanza kutekeleza sera ya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari kwa kufuta ada na michango yote ili kutoa fursa kwa watoto wote kusoma bila kujali uwezo kiuchumi wa wazazi au walezi.

MKUU WA KANISA KATOLIKI AWAOSHA MIGUU WANAODAIWA KUA NI WAISLAMU KUELEKEA SIKUKUU YA PASAKA.

Mkuu wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ameosha miguu ya wahamiaji waislamu mjini Rome katika tukio la unyenyekevu linaloambatana na itikadi ya kuanza kwa msimu wa Pasaka.

Papa Francis alitembela makao ya wahamiaji, mjini Roma na kuendesha misa ya kuanza kwa msimu wa pasaka.

Ziara yake katika kituo hicho cha kutathmini uhalali wa wahamiaji cha (Castelnuovo di Porto), inawadia huku uhasama na taharuki ikienea kote barani ulaya kuhusiana na kuwepo kwa wahamiaji waislamu hususan kufuatia mauaji ya Paris mwezi Novemba na ya hivi punde huko Brussels Ubelgiji.

Papa Francis alikashifu mauaji yaliyotokea Ufaransa na Ubelgiji akisema kuwa hizo ni njama za watu wenye kiu cha kumwaga damu ya binadamu.

Kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani alilaumu mtazamo wa watuhumiwa hao kuhusu maafa waliyosababisha.

Aidha papa mtakatifu aliwashauri watu wa dini tofauti duniani kuishi kwa amani.

''Haijalishi iwapo tunaimani tofauti la muhimu kwetu sote ni tuishi kwa amani sisi ni ndugu alisema papa mtakatifu.

Mar 22, 2016

WAZIRI MKUU AMUAGIZA CAG KUKAGUA BANDARI, CRDB


1
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mawakala wa Forodha na Bandari kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam Machi 21, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali aende Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili akague taarifa za mapato ambazo zilikuwa zikilipwa na mawakala wa forodha na bandari kupitia benki ya CRDB lakini hazionekani kwenye mifumo ya benki.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatatu, Machi 21, 2016) wakati akizungumza na mamia ya mawakala wa forodha na bandari waliohudhuria mkutano aliouitisha ili kusikiliza kero zinazowapata katika utendaji kazi wao.

Akizungumza na mawakala hao kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu alisema kuna dalili za kutupiana lawama baina TPA na CRDB kuhusu malipo yaliyokuwa yakifanyika benki halafu fedha hazionekana na wakala anaidaiwa kuwa hajalipia mzigo wakati alishaulipia.
 
“Kimsingi bado liko tatizo baina ya Mamlaka ya Bandari pamoja na Benki ya CRDB. Naona kila mmoja hapa anamkana mwenzake. Nitamtuma CAG ili akafanye ukaguzi wa kina ili tujue ni nani kati yao amehusika na upotevu wa fedha,” alisema huku akishangiliwa na mawakala hao.

Alimwagiza pia Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Eng. Aloyce Matei aandae dispatch zote walizotumia kupokelea malipo za kuanzia mwaka 2015 na ikibidi aandae za kuanzia mwaka 2014 ili CAG anapozopitia aweze kupata picha halisi.

Vilevile, Waziri Mkuu alimwagiza Eng. Matei kuhakikisha wananunua mashine ya photocopy ili iwekwe kwenye chumba cha kupokelea stakabadhi za malipo ya benki (bank pay in slip) ili mteja anapoleta nakala ya benki aweze kutolewa photocopy na kubakia na nakala ya malipo aliyofanya.

Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua bandari ni eneo nyeti katika kuinua uchumi na mapato ya nchi lakini pia ni eneo muhimu katika kutengeneza ajira. “Ninapenda niwahakikishie kuwa bado tutaendelea kukagua bandari hadi pawe safi. Hii bandari ni yenu na mtafanya kazi kama kawaida,” alisema.

Mapema, akizumgumza kwa niaba ya mawakala hao, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha nchini (TAFFA), Bw. Stephen Ngatunga alieleza matatizo mbalimbali ambayo wao kama mawakala wa forodha wamekuwa wakikumbana nayo kuanzia ulipaji, utoaji wa mizigo na kuitaka Serikali iongeze nguvu katika kuikabilia sekta hiyo.

Alizikosoa baadhi ya sheria ambazo zinaruhusu wamiliki wa bandari kavu kumiliki pia makampuni ya uwakala wa forodha, sheria kadhaa zinazochangia kukwamisha utoaji wa mizigo bandarini, ukaguzi hafifu wa kwenye scanner na uwepo wa vituo vinane vya mizani kuanzia Dar es Salaam hadi Tunduma ambavyo vimegeuka kuwa kero kwa wasafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani.

Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani amesema Serikali imeamua kuyafungulia makampuni zaidi ya 150 ambayo yalikuwa yamefungiwa kufanya kazi za uwakala wa forodha kutokana na madai ya kuhusishwa na ukwepaji wa kodi.

“Hapa tumegundua kuwa wote siyo wasafi iwe ni mawakala, benki ama bandari. Mkurugenzi wa Bandari, kuanzia leo watu hawa waruhusiwe waanze kufanya biashara lakini nyaraka za nyuma zisiguswe hadi CAG atakapokamilisha uchunguzi wake,” alisema kuibua kelele za shangwe kwenye ukumbi huo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMATATU, MACHI 21, 2016. (P.T)

Salma said: Hivi ndivyo nilivyotekwa

Pg 3NA WAANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MWANDISHI wa habari wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani  (DW) na Mwakilishi wa Mwananchi Communications, Salma Said Humud, jana aliibuka na kusimulia jinsi alivyotekwa na watu wasiojulikana alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam akitokea Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Baraza la Habari Tanzania (MCT) jana, Salima alisimulia mkasa mzima ulioghubika kutekwa kwake.

Akionekana mwenye huzuni muda wote, alisema waliomteka walimpiga na kumsababishia maumivu makali kwenye mwili wake.

“Nilitekwa saa chache baada ya kuteremka kwenye ndege nikitokea Zanzibar saa 8:00 mchana.  

Nilimtafuta dereva wangu kwa simu   aweze kunipeleka hospitali kwa ajili ya kupima afya yangu.

“Dereva hakupatikana kwa simu, lakini wakati natafuta gari jingine ndiyo ilitokea teksi na kunitaka niingie katika gari hiyo.

“Nilikataa ndipo walipoamua kunivuta ndani kwa nguvu na kumkuta kijana mmoja mfupi ambaye alinipiga kibao akinitaka kufunika macho yangu kwa baibui nililokuwa nimelivaa,”alisema Salma.

Katika simulizi hiyo, mwandishi huyo alisema baada ya kufunika uso wake hakujua alikopelekwa hadi alipojikuta yupo ndani ya jumba ambako alipigwa mateke na mabuti na kumsababishia maamivu makubwa   katika mwili wake.

Alisema wakati wakiendelea kumpiga, watekaji  wawili walimtaka kuacha kazi ya kuripoti matukio ya Uchaguzi wa Zanzibar.

Watekaji hao walikuwa wakimtajia matukio mengine yaliyowawahi kuwatokea watu wengine akiwamo  Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari 2006 Ltd, Absalom Kibanda   na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (Malt), Steven Ulimboka.

“Baada ya kunipiga sana walitoka nje ndipo nami nilichukua  simu yangu ya mkononi na kumtumia meseji mume wangu kumuarifu kuwa nimekamatwa na baada ya hapo nilipiga simu ofisini (DW) kuwaambia nipo mahali pabaya,” alisema.

Alisema watu hao waliporudi na kukuta akiwa na  simu mkononi walimpiga sana hadi akaishiwa nguvu.

“Waliniambia hawataki kuniua isipokuwa shida yao ni kutaka kunidhibiti nisiendelee kuripoti habari za uchaguzi wa marudio Zanzibar.

“Walinirudisha maeneo ya waliponichukua majira ya saa 11 alfajiri na kunitaka nijifunike uso hadi waondoke ndipo nijifunue.

“Nilijikuta nipo maeneo ya Uwanja wa Ndege, nilijikokota  hadi kituo cha daladala ambako nilikutana na mama mmoja aliyenihoji hali yangu na alinitaka nipumzike.  

Baadaye alinisaidia kusimamisha daladala kwenda hospitali ya Aghakan,” alisema.

Alisema baada ya kufika katika Hospitali ya Aghkan hakumkuta daktari wake wa moyo ambaye humtibu hivyo aliamua kwenda Hospitali ya Regency.

Baada ya kufanyiwa vipimo   baadaye aliwatafuta watu mbalimbali akiwamo Mratibu wa Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu,Onesmo ole Ngurumwa.

Akizungumzia hali ya Zanzibar,alisema kuna matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wananchi kukamatwa, kupigwa na kutupwa nje ya miji, vituko ambavyo  vimekuwa vikifanywa na vyombo vya usalama kwa kushirikiana na kundi liitwalo mazombi.

Alisema awali alikuwa akipokea simu za vitisho pamoja na ujumbe mara kwa mara lakini licha ya kuripoti vituo vya polisi hakuna jitihada zilizokuwa zikichukuliwa.

Naye Mratibu wa Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu,Onesmo ole Ngurumwa alisema baada ya kupata taarifa za kupotea kwa mwandishi huyo alimuarifu Msaidizi wa IGP   na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni lakini hakuna walichokifanya.

Regency wamkana
Hospitali ya Regency ambayo Salma alisema alitibiwa, jana  ilikana kumpokea mgonjwa mwenye jina la Salma.

Akizungumza na gazeti hili huku akiombwa asitajwe jina lake kwa kuwa si msemaji wa hospitali hiyo, muuguzi wa zamu aliwaambia waandishi wa MTANZANIA kuwa  hakukuwa na mgonjwa mwenye jina la Salma Said ambaye alidai kutekwa na watu wasiojulikana.

Alisema  idadi ya wagonjwa waliofika kwenye hospitali hiyo wameandikwa kwenye kitabu cha mapokezi pamoja na taarifa zao, hivyo aliwataka waandishi hao kukagua daftari hilo na kujiridhisha  kama mgonjwa huyo yupo.
 
 Mwandishi wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Salma Said akiwa ameshikiliwa na mwandishi mwenzake, Kelvin Matandiko alipokuwa akiondoka katika Kituo cha Polisi cha Kati baada ya kuhojiwa, juzi usiku