Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mawakala wa Forodha na Bandari
kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam Machi 21, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali
aende Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili akague taarifa za mapato
ambazo zilikuwa zikilipwa na mawakala wa forodha na bandari kupitia
benki ya CRDB lakini hazionekani kwenye mifumo ya benki.
Ametoa
agizo hilo jana jioni (Jumatatu, Machi 21, 2016) wakati akizungumza na
mamia ya mawakala wa forodha na bandari waliohudhuria mkutano
aliouitisha ili kusikiliza kero zinazowapata katika utendaji kazi wao.
Akizungumza
na mawakala hao kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Waziri
Mkuu alisema kuna dalili za kutupiana lawama baina TPA na CRDB kuhusu
malipo yaliyokuwa yakifanyika benki halafu fedha hazionekana na wakala
anaidaiwa kuwa hajalipia mzigo wakati alishaulipia.
“Kimsingi
bado liko tatizo baina ya Mamlaka ya Bandari pamoja na Benki ya CRDB.
Naona kila mmoja hapa anamkana mwenzake. Nitamtuma CAG ili akafanye
ukaguzi wa kina ili tujue ni nani kati yao amehusika na upotevu wa
fedha,” alisema huku akishangiliwa na mawakala hao.
Alimwagiza
pia Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Eng. Aloyce Matei aandae dispatch zote
walizotumia kupokelea malipo za kuanzia mwaka 2015 na ikibidi aandae za
kuanzia mwaka 2014 ili CAG anapozopitia aweze kupata picha halisi.
Vilevile,
Waziri Mkuu alimwagiza Eng. Matei kuhakikisha wananunua mashine ya
photocopy ili iwekwe kwenye chumba cha kupokelea stakabadhi za malipo ya
benki (bank pay in slip) ili mteja anapoleta nakala ya benki aweze
kutolewa photocopy na kubakia na nakala ya malipo aliyofanya.
Waziri
Mkuu alisema Serikali inatambua bandari ni eneo nyeti katika kuinua
uchumi na mapato ya nchi lakini pia ni eneo muhimu katika kutengeneza
ajira. “Ninapenda niwahakikishie kuwa bado tutaendelea kukagua bandari
hadi pawe safi. Hii bandari ni yenu na mtafanya kazi kama kawaida,”
alisema.
Mapema,
akizumgumza kwa niaba ya mawakala hao, Rais wa Chama cha Mawakala wa
Forodha nchini (TAFFA), Bw. Stephen Ngatunga alieleza matatizo
mbalimbali ambayo wao kama mawakala wa forodha wamekuwa wakikumbana nayo
kuanzia ulipaji, utoaji wa mizigo na kuitaka Serikali iongeze nguvu
katika kuikabilia sekta hiyo.
Alizikosoa
baadhi ya sheria ambazo zinaruhusu wamiliki wa bandari kavu kumiliki
pia makampuni ya uwakala wa forodha, sheria kadhaa zinazochangia
kukwamisha utoaji wa mizigo bandarini, ukaguzi hafifu wa kwenye scanner
na uwepo wa vituo vinane vya mizani kuanzia Dar es Salaam hadi Tunduma
ambavyo vimegeuka kuwa kero kwa wasafirishaji wa mizigo kwenda nchi
jirani.
Wakati
huohuo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin
Ngonyani amesema Serikali imeamua kuyafungulia makampuni zaidi ya 150
ambayo yalikuwa yamefungiwa kufanya kazi za uwakala wa forodha kutokana
na madai ya kuhusishwa na ukwepaji wa kodi.
“Hapa
tumegundua kuwa wote siyo wasafi iwe ni mawakala, benki ama bandari.
Mkurugenzi wa Bandari, kuanzia leo watu hawa waruhusiwe waanze kufanya
biashara lakini nyaraka za nyuma zisiguswe hadi CAG atakapokamilisha
uchunguzi wake,” alisema kuibua kelele za shangwe kwenye ukumbi huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMATATU, MACHI 21, 2016. (P.T)
0 comments:
Post a Comment