Makala

 

Kwa kufahamu kadhia ya maradhi mbalimbali yanayotusibu tumeona tuwawekee tiba mbadala ya baadhi maradhi kwa kutumia HABBA SODA.

 Tunaamini ni dawa isiyo na kemikali yenye madhara,Tafadhali Faidika na somo hili.

 

Matumizi Ya Kunufaisha Ya Habbat Sawdaa-1 (haba Soda – Chembe Nyeusi
Imefasiriwa na Iliyasa bint Maulaanah
Al-Bukhaariy anasimulia kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume Muhammad (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema.
((Habbat-Sawdaa inatibu kila kitu isipokuwa mauti)).
Yafuatayo hapa chini ni baadhi ya matatizo na magonjwa ambayo yanaweza kutibika kwa kirahisi kwa kutumia Habbat-Sawdaa.
Kwa faida ya Afya kwa ujumla:
Kunywa kijiko kimoja cha mafuta ya Habbat-Sawdaa asubuhi na usiku, au kunywa japo asubuhi kabla ya kifungua kinywa, unaweza kunywa kijiko kimoja cha mafuta peke yake au ukachanganya na kijiko kimoja cha asali safi. 
Vipele (chunusi) Na Ngozi:
Changanya na pasha moto kwa dakika mbili kikombe kimoja cha Habbat-Sawdaa iliyosagwa, ½ (nusu) kikombe cha maganda ya komamanga yaliyosagwa, na ½ (nusu) kikombe cha siki ambayo inatokana na juisi ya tofaha (apple). 

Paka katika sehemu inayotakiwa kabla ya kwenda kulala kila usiku mpaka vipele (chunusi) vitakapoondoka. Mchanganyiko unaweza kukaa mpaka wiki tatu na ni lazima uwekwe katika hali ya ubaridi. 

Upara (Alopeshia):
Sugua mafuta ya Habbat-Sawdaa katika mabaka yanayokusumuba. 

Pumu:
Tia ½ (nusu) kijiko cha Habbat-Sawdaa iliyochemshwa katika maji ya yaliyochemshwa kisha unywe moto.
Kuumwa kwa Mgongo (Sehemu ya Chini):
Changanya asali pamoja na ¼ (robo) kijiko cha Habbat-Sawdaa na iwe kitu cha kwanza kunywa wakati wa asubuhi kabla ya kufungua kinywa. 

Mwiba Wa Nyuki Na Nyigu:
Tia ½ (nusu) kijiko cha Habbat-Sawdaa iliyochemshwa katika maji ya yaliyochemshwa kisha unywe moto.

Kibofu cha Mkojo/Figo:
Kunywa maji ya moto yaliyochanganywa na½ (nusu) kijiko cha Habbat-Sawdaa pamoja na asali kila asubuhi kabla ya kufungua kinywa. Changanya vikombe viwili vya Habbat-Sawdaa iliyosagwa na ½ (nusu) kikombe cha asali safi. 

Kunywa kijiko kimoja cha mchanganyiko pamoja na kikombe kimoja cha maji ya moto kila asubuhi kabla ya kufungua kinywa. 

Mchanganyiko unaweza kukaa kwa siku 15 na ni lazima uwekwe katika hali ya ubaridi. 

Jiwe La Figo:
Kikombe kimoja cha Habbat-Sawdaa iliyochanganwa pamoja na gilasi (bilauri) moja ya asali, vitunguu saumu vitatu vilivyosagwa na karafuu. 

Changanya vitunguu saumu pamoja na asali na Habbat-Sawdaa. Kunywa kijiko kimoja kabla ya kula chakula na kwa pendekezo kula limau (bila ya kumenywa). 

Rudia haya kwa wiki moja Insha-Allah jiwe litaondoka.
Maathiriko Ya Figo:
Changanya baadhi ya Habbat-Sawdaa pamoja na mafuta ya alizeti. Chukua mchanganyiko na weka katika sehemu ambapo figo limeathirika. Kunywa kijiko cha Habbat-Sawdaa asubuhi. Rudia haya kwa muda wa wiki moja Insha-Allah maathiriko yatatibika. 

Mafua:
Chukua mbegu za Habbat-Sawdaa 21, ziweke katika kitambaa na roweka usiku. Tumia kama matone kwenye pua siku ya pili nusa poda ya Habbat-Sawdaa iliyomo katika kitambaa.

Kikohozi:
Tumia matone matatu au manne ya mafuta ya Habbat-Sawdaa kwenye kahawa au chai. 

Bawasiri:
Kula unga wa Habbat-Sawdaa pamoja na maji. 

Shinikizo la damu (high blood pressure):
Changanya kijiko kimoja cha Habbat-Sawdaa iliyosagwa, kijiko kimoja cha asali safi na kitunguu kiasi kidogo. 

Chukua mchanganyo kabla ya kufungua kinywa kwa siku ishirini.

Uwasho Na Maumivu Ya Jino Na Ufizi:
Chemsha Habbat-Sawdaa katika siki na itumie kwa kusukutulia meno na ufizi. 

Na jikinge kutumia dawa za msuwaki za kibiashara na tumia dawa za msuwaki ambazo zinatengenezwa kutoka kwenye nyuzi za mboga za mti wa siwak ambao kwa karne ulikuwa unatumiwa na Wahindi, Waafrika na Waarabu, ni msuwaki wa kiasili. 

Kumbukumbu (memory):
Kunywa kijiko kimoja cha unga wa Habbat-Sawdaa na changanya na asali mara mbili kwa siku. 

Utaratibu Wa Ulinzi Wa Mwili:
Kula kijiko kimoja cha Habbat-Sawdaa na asali mchana na usiku Kutoweza kuzuia haja ndogo (mkojo): Kunywa kijiko kimoja cha Habbat-Sawdaa pamoja na asali, kisha kunywa maji ya vugu vugu. 

Jaundice:
Tumia Habbat-Sawdaa pamoja na maziwa.
Maumivu Sugu ya kichwa (Maumivu ya kichwa ya upande mmoja, maumivu ya kichwa):
Kaanga Habbat-Sawdaa na iweke katika kitambaa cha pamba, funga au weka tu kitambaa katika kikomo (kipaji cha uso). 

Roweka Habbat-Sawdaa ndani ya siki wakati wa usiku, siku ya pili ivuruge kufanya unga. Ingiza katika pua halafu vuta pumzi. 

Ngozi kavu:
Changanya asali pamoja na robo kijiko cha Habbat-Sawdaa na iwe kitu cha kwanza kunywa wakati wa asubuhi kabla ya kufungua kinywa. 

Upepo:
Changanya asali pamoja na robo kijiko cha Habbat-Sawdaa na iwe kitu cha kwanza kunywa wakati wa asubuhi kabla ya kufungua kinywa. 

Minyoo:
Kunywa Habbat-Sawdaa pamoja na siki kuondoa minyoo.
————————————————————————————————————————–
Matumizi Ya Kunufaisha Ya Habbat-sawdaa-2 (habba Soda – Chembe Nyeusi )

Imefasiriwa na Iliyasa binti Maulana
(Itumieni habba hii, hakika ndani yake muna shifaa (ponyo) ya kila aina ya ugonjwa isipokuwa mauti)). 

(Al-Bukhaariy)Kunyonyoka Nywele
Ataukanda unga wa Habbat-Sawdaa katika juisi ya chirichiri pamoja na kijiko cha siki nyepesi na kikombe cha mafuta ya zeituni, halafu asugue kichwani kwa mafuta hayo kila siku jioni pamoja na kukiosha kichwa kwa maji na sabuni kabla ya kupaka.

Maumivu ya Kichwa
Atachukua unga wa Habbat-Sawdaa , karafuu iliosagwa nusu ya kiwango cha Habbat-Sawdaa  na anisuni (anise), halafu achanganye pamoja. 

Achukue kiasi cha kijiko kimoja (cha chai), wakati wa kuumwa na kichwa, na ale na maziwa lala (mala), pamoja na kupasugua mahala paumapo kwa mafuta ya Habbat-Sawdaa .

Ukosefu Wa Usingizi
Atachukua kijiko cha Habbat-Sawdaa , achanganye na gilasi ya maziwa moto  yaliochanganywa na asali, baada ya kupoa kiasi atakunywa.

Chawa Na Mayai Yake
Atachukua unga wa Habbat-Sawdaa uliosagwa vizuri aukande kwenye siki mpaka uwe kama marhamu, halafu ajipake kichwani – baada ya kunyoa nywele au kuisugua marhamu kwenye mashina ya nywele, halafu aketi katika mwanga wa jua kitambo cha robo-saa. Na hataosha kichwa ela baada ya masaa matano. 
Atafanya hivyo kila siku kwa muda wa wiki moja.


Kisunzi Na Maumivu Ya Sikio
Tone moja la mafuta ya Habbat-Sawdaa ndani ya sikio husafisha sikio, pamoja na kuyanywa na kusugua sehemu za panda na nyuma ya kichwa, humaliza kisunzi.

Upaa Na Mabaka
Utachukua kijiko cha unga wa Habbat-Sawdaa, siki kiasi cha kikombe kimoja na juisi ya kitunguu saumu kiasi cha kijiko kidogo, vyote hivyo utavichanganya na vitakua namna ya   marhamu, utajipaka baada ya kunyoa sehemu  ya nywele na kuchanja kidogo – kisha utafunga bendeji, utaiacha mpaka asubuhi, baadae utajipaka mafuta ya Habbat-Sawdaa,utaendelea hivyo kwa muda wa wiki moja.

Malengelenge ya Neva katika Ngozi
Atajipaka – sehemu ya malengelenge – mafuta ya Habbat-Sawdaa mara tatu kila siku mpaka iondoke kwa Uwezo wa Allah.

Maradhi Ya Wanawake Na Uzazi
Dawa kubwa inayosahilisha kuzaa ni Habbat-Sawdaa iliochemshwa ikachanganywa na asali na kiziduo cha babunaji (chamomile). 

Habat sawdaa  ni kama burashi katika uke wa mwanamke yenye faida kubwa kwao pamoja na kutumia mafuta ya Habbat-Sawdaa katika kila kinywaji cha moto kwa maradhi yote ya wanawake.

Meno Na Maumivu Ya Mafido na Koo
Kiziduo cha Habbat-Sawdaa na kutumia kwa kusukutua kwa kugogomoa, husaidia mno maradhi yote ya mdomo na koo, vivyo hivyo pamoja na kubugia kijiko cha Habbat-Sawdaa na kumeza kwa maji yenye vuguvugu kila siku na kujipaka mafuta yake sehemu ya koo kwa nje na kuusugua ufizi kwa ndani.

Maradhi Ya Tezi
Atachukua unga wa Habbat-Sawdaa na aukande kwa asali na mkate wa nyuki kila siku, kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Chunusi (Acne)

Atachukua unga wa Habbat-Sawdaa aukande katika mafuta ya ufuta (simsimu) pamoja na kijiko cha unga wa ngano. 
Vyote hivyo atajipaka usoni kuanzia jioni hadi asubuhi, halafu ataosha kwa maji yenye vuguvugu kwa sabuni. Ataendelea kufanya hivyo kwa muda wa wiki moja. 

Na awe akinywa mafuta ya Habbat-Sawdaa katika kinywaji chochote cha moto.

Maradhi Yote ya Ngozi
Atachukua mafuta ya Habbat-Sawdaa, mafuta ya waridi (marashi jabali) na unga wa ngano asili, vyote hivyo  kwa viwango sawa, ule unga wa ngano uwe zaidi kuliko mafuta, halafu aukande vizuri. Kabla ya kujipaka, apanguse sehemu yenye ungonjwa kwa kitambaa kilichoroweshwa siki nyepesi, halafu aketi kwenye jua, baadae ajipake dawa hio kila siku. Lakini ajizuie na kila chenye kuchochea hisia kama vile, samaki, mayai, maembe na mfano wake.

Sugu (Chunjua) (Wart)
Atachukua unga wa Habbat-Sawdaa aukande katika siki nzito na asugue kwa kitambaa cha sufi au katani mahala pa sugu asubuhi na jioni kwa muda wa wiki moja.

Kuung`arisha Uso Na Kuurembesha
Ataukanda unga wa Habbat-Sawdaa katika mafuta ya zeituni, na atajipaka usoni halafu apigwe na mwanga wa jua kidogo. Tiba hiyo ataifanya wakati wowote katika mchana na siku yoyote.

Kuunganisha Mvunjiko Haraka
Supu ya adesi (dengu), kitunguu maji pamoja na yai la kuchemsha na kijiko kikubwa cha unga wa Habbat-Sawdaa , utachanganya na supu hiyo japo siku baada ya siku; halafu anywe. 

Na atasugua sehemu zilizo karibu na mvunjiko kwa mafuta ya Habbat-Sawdaa, na baada ya kufungua bendeji atajisugua kwa mafuta ya Habbat-Sawdaa yenye vuguvugu; kila siku.

Mvilio Wa Damu (Contusion)
Atachemsha vizuri konde moja la Habbat-Sawdaa katika chombo cha maji, kisha atakiingiza kiungo kilichovilia damu ndani ya maji hayo- yenye vuguvugu- kwa muda wa robo-saa au zaidi pamoja na kukitaharakisha kiungo hicho. 

Baada ya hapo atajipaka mafuta ya Habbat-Sawdaa bila ya kufunga kitu. Lakini hatakiwi kukipa uzito kiungo hicho au kukitaabisha. Tiba hiyo ataifanya kila siku kabla ya kulala.
Baridi Yabisi (Rheumatism)

Atachemsha mafuta ya Habbat-Sawdaa na atasugua kwayo ile sehemu yenye ugonjwa, atasugua kwa nguvu kama kwamba yuwasugua mfupa wala sio ngozi! Na atayanywa baada ya kuyachemsha vyema na kuyachanganya na asali kidogo. Ataendelea na tiba hiyo huku akiwa ni mwenye imani na yakini kuwa Allah Atamponya.

(Ki) Sukari (Diabetes)
Utachukua unga wa Habbat-Sawdaa kiasi cha kikombe kimoja, manemane (myrrh) iliosagwa kiasi cha kijiko kikubwa, habbarrashad nusu kikombe, komamanga iliosagwa kiasi cha kikombe kimoja, mzizi wa kabichi uliosagwa baada ya kukaushwa kiasi cha kikombe kimoja na kijiko kidogo cha mvuje. 

Vyote hivyo atavichanganya na atakula kabla ya kula chakula kiasi cha kijiko kimoja, atakula na maziwa lala ili iwe rahisi kumeza.

Shinikizo la Damu (High Blood)
Kila unywapo kinywaji cha moto, tia matone machache ya mafuta ya Habbat-Sawdaa. Pia ujipake mafuta hayo mwili wote, japo wiki mara moja.

Uvimbe Wa Figo(Nephritis)
Atatengeneza kibandiko (cha kitambaa) kutokana na unga wa Habbat-Sawdaa uliokandwa katika mafuta ya zeituni, atabandika sehemu yenye maumivu ya figo pamoja na kubugia funda la kijiko cha Habbat-Sawdaa kila siku kabla ya kula chakula kwa muda wa wiki moja tu; uvimbe utakwisha insha Allah.

Kuvunjavunja Vijiwe Vya Tumboni
Atachukua unga wa Habbat-Sawdaa kiasi cha kikombe kimoja kisha aukande katika kikombe cha asali, na atasaga kitungu u saumu punje tatu; atakua akichukua nusu yake akila kabla ya kula chakula kila siku. Pia itakua bora lau atakula limau kila baada ya kula dawa; kwani husafisha kabisa.

Kukojoa Kwa Maumivu (Dysuria)
Atapaka mafuta ya Habbat-Sawdaa juu ya kinena kabla ya kulala pamoja na kunywa kikombe cha mafuta hayo yaliochemshwa na kutiwa asali; kila siku kabla ya kulala.
Kukojoa Bila Kukusudia

Atachukua Habbat-Sawdaa na maganda ya mayai yaliosafishwa na yakaokwa na kusagwa halafu yakachanganywa na Habbat-Sawdaa kisha yakaokwa na kusagwa halafu yakachanganywa na Habbat-Sawdaa kisha aingize kwenye maziwa; hatimae anywe kiasi cha kikombe kimoja kila siku na wakati wowote.

Jongo (Edema)
Ataweka kibandiko (cha kitambaa) cha unga wa Habbat-Sawdaa uliokandwa katika siki juu ya kitovu, kwanza ataweka kitambaa. Pia atakula Habbat-Sawdaa kijiko kimoja asubuhi na jioni kwa muda wa wiki moja.

Kifuko Cha Nyongo Na Vijiwe Vyake
Atachukua Habbat-Sawdaa kiasi cha kijiko kimoja, manemane iliosagwa robo kijiko na asali kiasi cha kikombe kimoja; vyote hivyo atavichanganya viwe mraba (kama jamu); halafu awe akila kila asubuhi na jioni.

Wengu
Ataweka kibandiko (kilichopashwa moto) cha Habbat-Sawdaa iliokandwa katika mafuta ya zeti katika ubavu wa kushoto; jioni. 

Na wakati huo huo ata kunywa kikombe cha kiziduo cha uwatu kilichochanganywa asali na mafuta ya Habbat-Sawdaa kidogo, ataendalea na dawa hiyo kwa muda wa wiki mbili mfululizo.

Maradhi Yote ya Kifua na Baridi
Atachukua mafuta ya Habbat-Sawdaa kiasi cha kijiko kikubwa atie kwenye maji halafu ayaweke juu ya moto mpaka ianze kufuka moshi, hapo aanze kuuvuta ule moshi puani huku akiwa amejifunika kichwa ili ule moshi usiende upande mwingine. 

Atafanya hivyo kila siku kabla ya kulala, pamoja na kunywa kiziduo cha zaatari kilichochanganywa na unga wa Habbat-Sawdaa; asubuhi na jioni.

Moyo na Mzungukoa wa Damu
Kuwa na imani katika maneno ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) Kwa sababu jambo hili ni katika muktadha wa imani. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) alipotuambia kuwa Habbat-Sawdaa ni dawa ya kila ugonjwa, basi hakuna shaka hata chembe kuwa ni dawa ya maradhi yote yanayomfika mwanaaadamu. Mgonjwa wa moyo asikate tamaa kutokana na rehma ya Allah; ni juu yake akithirishe kutumia Habbat-Sawdaa kwa namna yoyote iwayo; iwe ni kwa kula nzima au kwa kunywa wakati wowote uwao.
 
Mchango (Msokoto Wa Tumbo) (Colic)
Atachemsha vyema anisuni, kamun na nana kwa vipimo sawa na atatia asali kidogo, halafu atie matone saba ya Habbat-Sawdaa ; atakunywa kinywaji hicho kikiwa na vuguvugu pamoja na kupaka mafuta ya Habbat-Sawdaa mahala panaposokota. Baada ya muda mchache maumivu yataondoka.

Kuhara
Atachukua juisi ya chirichiri iliochanganywa na unga wa Habbat-Sawdaa kijiko kikumbwa, atakunywa kiasi cha kikombe kimoja mara tatu kwa siku.

Uziwi
Atachemsha Habbat-Sawdaa pamoja na karafuu, na atakunywa bila ya kuongeza kitu; mara tatu kwa siku.

Gesi Na Maumivu
Atabugia unga laini wa Habbat-Sawdaa kiasi cha kijiko kimoja kabla ya kula chakula akifwatisha gilasi ya maji yenye vuguvugu iliotiwa asali ya muwa kiasi cha vijiko vitatu; atakariri kila siku kwa muda wa wiki moja
————————————————————————
Matumizi Ya Kunufaisha Ya Habbat-sawdaa-3 (habba Soda – Chembe Nyeusi )
 

Imefasiriwa Iliyasa binti Maulana
Asidi (Acidness)
Motone kadhaa ya mafuta ya Habbat-Sawdaa yaliotiwa kwenye maziwa ya moto na asali; humaliza asidi.

Uvimbe Wa Tumbo
Atachukuwa unga wa Habbat-Sawdaa kiasi cha kijiko kimoja na kijiko cha urkusus (licorice) hivyo atavichanganya na juisi ya pea iliotengenezwa pamoja na kokwa zake; halafu anywe; ataona nafuu kubwa.

Maradhi Ya Macho
Atapaka mafuta ya Habbat-Sawdaa sehemu za panda kandokando ya macho na kope, atafanya hivyo kabla ya kulala pamoja na kunywa matone kadhaa ya mafuta ya Habbat-Sawdaa katika kinywaji chochote cha moto au katika juisi ya karoti.

Amiba (Vijidudu) (Amebiasis)
Atachukua unga wa Habbat-Sawdaa kiasi cha kijiko kimoja pamoja na kijiko cha kitunguusaumu kilichosagwa, atachangana katika kikombe cha juisi ya nyanya iliotiwa chumvi kidogo; atakunywa kila siku kabla ya kula chakula kwa muda wa wiki mbili mfululizo.

Kichocho (Bilharziasis)
Atakula Habbat-Sawdaa kiasi cha kijiko kimoja asubuhi na jioni, yawezekana kuila Habbat-Sawdaa katika chakula kama vile mkate pamoja na kujipaka mafuta yake katika ubavu wa kulia. Ataendelea na dawa hio kwa muda wa miezi mitatu mfululizo. Baadae atapata nguvu na nishati.

Kutoa Wadudu Tumboni
Atakula sandwichi moto ya vitu hivi: kijiko kimoja cha unga wa Habbat-Sawdaa, punje tatu za vitunguu, kijiko kimoja cha mafuta ya zeti, pilipilimanga kidogo na punje kumi za boga (calabash), asubuhi atakunywa kinywaji cha shimari au mafuta ya mbono mara moja pekee.

Utasa
Atachukua unga wa Habbat-Sawdaa, unga wa uwatu na mbegu ya figili kwa vipimo sawa, atakula kijiko kimoja asubuhi na jioni ilihali imekorogwa katika nusu kikombe cha asali, baadae atafuatisha kunywa kikombe kikubwa cha maziwa ya ngamia; basi inshaAllaah itakuwa kheri.

Tezikibofu (Prostate gland)
Atajipaka mafuta ya Habbat-Sawdaa chini ya mgongo na atajipaka chini ya korodani (mapumbu) na kusugua kwa mzunguko pamoja na kula unga wa Habbat-Sawdaa kijiko kimoja, na robo kijiko kidogo cha manemane katika nusu gilasi ya asali iliotiwa katika maji yenye vuguvugu; kila siku na wakati wowote apendao.

Pumu (Asthma)
Atanusa moshi wa mafuta a Habbat-Sawdaa asubuhi na jioni. Pia atakula unga wake asubuhi na jioni kabla ya kula chakula kila siku na pia kujipaka mafuta yake kifuani na kooni kabla ya kulala kila siku.

Kidonda
Atayachanganya matone kumi ya mafuta ya Habbat-Sawdaa, katika kikombe cha asali na kijiko kimoja cha maganda ya komamanga yaliyokaushwa na kusagwa. Atakula kila siku kabla ya kula chakula; baadae atakunywa gilasi ya maziwa yasiyotiwa chochote.

Saratani (Cancer)
Atapaka mafuta ya Habbat-Sawdaa mara tatu kila siku na kula kijiko cha unga wake kila amalizapo kula katika kikombe cha juisi ya karoti. Ataendelea hivyo kwa muda wa miezi mitatu.

Nguvu Za Kiume
Atachukua  unga wa Habbat-Sawdaa kiasi cha kijiko kimoja achanganye (apige) ndani ya mayai saba ya kienyeji; atafanya hivyo siku baada siku kwa muda wa mwezi mmoja. Basi hata kama ana miaka 120 atapata nguvu za barobaro!

Udhaifu kwa Ujumla
Atachukua unga wa habat sosa kiasi cha kikombe kimoja, uwatu mfano wake na ambari ilioyeyushwa kiasi cha kijiko kidogo, vyote atavichanganya katika chombo chenye asali iwe kama jamu; halafu awe akila kama jamu kila siku na wakati wowote apendao lakini kwa mkate wa ngano asili.

Kuleta Hamu Ya Kula
Kabla ya kuanza kula, jipatie Habbat-Sawdaa kiasi cha kijiko kidogo na uitafune kwa meno yako, na unywe maji ya kawaida yaliochanganywa na siki kidogo.

Kutibu Ulegevu Na Uvivu
Atakunywa- kabla ya kula – juisi ya machungwa iliochanganywa matone kumi ya mafuta ya Habbat-Sawdaa. Ataendelea hivyo kwa muda wa siku kumi.  Baada ya hapo ataona nishati na uchangamfu.

Nishati akilini Na Wepesi Wa Kuhifadhi
Atachemsha nanaa (mint leaf), aichanganye na asali na aingize matone saba ya mafuta ya Habbat-Sawdaa; anywe kinywaji hiki kikiwa na vuguvugu wakati wowote apendao. 
Basi ataionea namna fahamu itakavofanya kazi

 

HIJJA NA UMRAA 

 
HILI NI KAABA LIPO NDANI YA MASJID HARAAM


Imekusanywa Na Kufasiriwa Na Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy


Shukrani zote ni zake Allaah, tunashuhudia kuwa hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni Mtume wake.

Ameufikisha ujumbe na kuifikisha amana, kwa hivyo tunakuomba Mola wetu umsalie na kumsalimu Mtume wako huyu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Aali yake na Masahaba wake watukufu - Aamin.

Amma baad,

Allaah Anasema:

{{Na Allaah amewawajibishia watu wafanye Hijjah katika Nyumba hiyo; yule awezaye kufunga safari kwenda huko. Na atakayekanusha (asende na hali anaweza) basi Allaah si mhitaji kuwahitajia walimwengu.}} [Aali ‘Imraan–97]

Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Hijjah ni moja katika nguzo tano za Kiislamu, na ni fardhi ijulikanayo kuwa ni ya lazima. Atakayekanusha kuwajibika kwake huwa ni kafiri aliyertadi na kutoka katika dini ya Kiislamu.

Wanavyuoni wengi wanasema kuwa: Hijjah imefaradhishwa katika mwaka wa sita baada ya Hijra, (baada Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuhamia Madiynah).

Mwanachuoni maarufu Ibnil Qayyim, katika kitabu chake kiitwacho Zaadul Ma-ad, yeye amesema kuwa Hijjah imefaridhishwa mwaka wa tisa, pale ilipoteremshwa aya isemayo:

{{Na timizeni Hijjah na Umra kwa ajili ya Allaah.}} [Al Baqarah – 196]

Ni Katika Amali Bora

Amesimulia Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliulizwa:

"Amali ipi iliyo bora?"
Akajibu:
"Imani juu ya Allaah na Mtume wake"
Akaulizwa: “Kisha ipi?”
Akasema:
"Kisha Jihadi katika njia ya Allaah".
"Kisha ipi?"
Akasema:
"Kisha Hijjah iliyokubaliwa".

Anasema As-Sayid Saabiq, mwandishi wa kitabu ‘Fiq-hus Sunnah’:

"Hijjah iliyokubaliwa ni ile isiyochanganyika na maovu.”

Al-Hassan Al-Basry yeye amesema:

"Hijjah iliyokubaliwa ni ile iliyomfanya aliyehiji anaporudi akawa anaipenda akhera yake kuliko dunia.”

Wajumbe Wa Allaah

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

((Mahujaji na wenye kufanya ‘Umrah ni wageni wa Allaah.Wanachomuomba anawapa, na wakiomba maghfira anawaghufiria.))
[Imepokewa na An-Nasai, Ibni Majah, Ibni Khuzaymah na Ibni Hibban]

Kwa hivyo kila aliyebahatika atambue kuwa tokea siku ile alipoamua kwenda kuhiji, keshakuwa mgeni wa Mola wake Subhanahu wa Taala, na kwa ajili hiyo anatakiwa awe mtu anayekistahiki cheo hicho. Na anapokuwa katika Ibada hiyo tukufu asigombane wala kuzozana na Mahujaji wenzake.

Zimepokelewa Hadiyth nyingi zinazotufahamisha kuwa atakayehiji bila kufanya maovu wala kugombana wala kuzozana, hapana zawadi nyingine anayoistahiki isipokuwa Pepo.


Maimamu wakubwa kama vile Abu Hanifa na Maalik na Ahmad bin Hanbal na baadhi ya wanafunzi wa Imam Ash-Shaafi’iy wanasema:

"Hijjah inamwajibikia kila mtu toke pale anapokuwa na uwezo. Kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

((Anayetaka kuhiji basi aharakishe, kwa sababu huenda akaumwa, mnyama wake akazeeka au akapatwa na shida (akazitumia pesa zake).))

Na katika hadithi nyengine amesema:

((Fanyeni haraka mkahiji, maana hajui mmoja wenu atapatwa na nini.)) [Imepokewa na Ahmad, Al-Bayhaqiy, At-Twahaawiy na Ibn Maajah]

Kuhiji Kwa mali Ya Kukopa

Kutoka kwa Abdullah bin Abu Auf (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:
((Nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya mtu asiyewahi kuhiji iwapo anaruhusiwa kukopa kwa ajili ya kuhiji?” Akaniambia; “La, (asifanye hivyo)”.)) [Imepokewa na Al-Bayhaqiy]

Hijjah Ya Mwenye Deni

Kamati ya kudumu ya Utafiti wa Kielimu na Utoaji Fatwa imetoa fatwa kuhusiana na suala la Hijjah ya mwenye deni kwa kueleza yafuatayo:
Moja ya masharti ya Hijjah ni uwezo, na mtu kuwa na uwezo wa mali wa kuifanya Hijjah. Ikiwa mtu ana deni ambalo anadaiwa na mkopeshaji na mkopeshaji akawa hakubali yule mtu aende Hijjah bila kumlipa pesa zake, basi hatoruhusika kwenda Hijjah hadi alipe deni analodaiwa, kwani mtu huyo atahesabika si mwenye uwezo wa kwenda Hijjah. Lakini endapo mkopeshaji hatomshikilia alipe pesa zake na ima kamruhusu aende Hijjah hali ya kuwa ana deni lake, basi anaweza kwenda na Hijjah yake kwa hali hiyo itakubalika.
[Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah 11/46]

Na katika Fatwa nyingine, Kamati ya Kudumu ya Fatwa walipoulizwa swali kuhusu Hijjah ya mwenye deni la nyumba ambalo muulizaji alisema anapaswa kulilipa kwa awamu, ilieleza ifuatavyo:
Uwezo wa kutekeleza Hijjah ni moja ya masharti ya kuwa kwake ni waajib. Ikiwa una uwezo wa kulilipa deni hilo kwa awamu ambayo imekutana na wakati wa Hijjah, basi unaweza kwenda baada ya kulilipa deni katika awamu hiyo. Lakini ikiwa huwezi kulipa deni hilo kwa awamu hiyo, basi ahirisha Hijjah hadi utakapopata uwezo kwani Allaah Anasema:
“Na kwa ajili ya Allaah imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia (mwenye uwezo) ya kwendea.” [Aal ‘Imraan 3: 97]
Na at-Tawfiyq ni kutoka kwa Allaah
[Al-Lajnah ad-Daaimah lil Buhuuth al-‘Ilmiyyah wal Iftaa 11/45]

Naye Mwanachuoni Shaykh Muhammad bin Swaalih al-‘Uthaymiyn anasema:
Deni linalodaiwa linapaswa kutangulizwa kulipa kuliko Hijjah, kwani wajibu wa kulilipa unawekwa mbele kuliko mtu kwenda kutekeleza Hijjah. Hivyo, anapaswa mtu kulipa kwanza deni kisha ndio kwenda Hijjah. Na ikiwa hatobakiwa na chochote au kitakachobaki hakimtoshelezi gharama za kwenda Hijjah, basi atasubiri hadi Allaah Amjaalie uwezo wa kwend akuitekeleza nguzo hiyo. Lakini likiwa ni deni lenye kuwa na muda mrefu aliopewa mkopeshwa la kulilipa siku za mbele, hivyo, kwa hali hii hata kama mkopeshaji akimruhusu au asimruhusu kwenda Hijjah, hatoruhusika kwenda Hijjah ikiwa hana uhakika au dhamana ya kulilipa kwa ule muda aliopewa/waliokubaliana na mkopeshaji.
Kwa hali hiyo tunasema: Ikiwa mtu anadaiwa deni, na anafahamu kuwa ana uwezo wa kulilipa kwa muda aliopewa (hata ikiwa ni mbeleni baada ya Hijjah), basi Hijjah kwa hali hiyo inakuwa ni wajibu kwake japokuwa ana deni.
[Fataawa Ibn ‘Uthaymiyn, 21/96]


Imepokewa kutoka kwa At-Tabarani kuwa Abu Hurayra (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

((Anapotoka mwenye kuhiji kwa pesa njema akauweka mguu wake juu ya kipandio cha mnyama wake, akasema: "Labbayka Allahumma labbayk", (Nakuitikia ewe Mola wangu nakuitikia) hujibiwa na msemaji kutoka mbinguni, "Labbayka wa Sa’adayka (Mwitikio wako umekubaliwa na utafurahi kwa amali yako njema hii), kwa sababu zawadi yako (chakula na vifaa vyako) ni vya halali, na mnyama wako ni wa halali, na Hijjah yako inakubaliwa na haina madhambi".
Lakini anapotoka anayeihiji kwa pesa za haramu akauweka mguu wake juu ya kipandio cha mnyama wake akasema, "Labbayka Allahumma labbayk" (Nakuitikia ewe Mola wangu nakuitikia), hujibiwa kutoka mbinguni, "Laa labbayaka walaa sa’adayka. (Hakukubaliwi kuitikia kwako wala hutolipwa mema), kwa sababu vifaa vyako ni vya haramu na pesa zako ni za haramu na Hijjah yako ni ya dhambi na wala haikubaliwi".

Kwanza – ‘Umrah

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ameweka Miyqaat ‘mipaka’ maalum ambayo yeyote anayekwenda Makka kwa nia ya kuhiji au kufanya ‘Umrah haruhusiwi kuivuka kabla ya kutia nia ya Ihraam mwahala hapo. Amewawekea watu wa Madiynah mji wa Dhul Hulayfah kuwa ni Mpaka wao. Mji huu unajulikana pia kwa jina la Abaar ‘Ali, nao upo Madiynah, kiasi cha Kilomita 450 mbali na Makkah.

Akawawekea watu wa Sham mji wa Al-Juhfa kuwa ni Miyqaat yao. Na Miyqaat ya watu wa Najd ni Qarn al Manazil. Amma watu wa Yemen Miyqaat yao ni mji wa Yalamlam. Na watu wa Iraaq Miyqaat yao ni Dhaata ‘Irq.

Hii ni mipaka aliyoiweka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kisha akasema:

((Hiyo ni mipaka yao na ya kila apitae njia hizo, kwa wasio wakazi wa miji hiyo, kwa kila atakaye kuhiji au kufanya ‘Umrah.))

Mtu anapowasili katika mipaka hiyo anatakiwa aoge, ajisafishe, akate makucha na kujitia manukato akitaka. (Si vizuri kujitia manukato katika vazi la Ihraam, ingawaje si haram kufanya hivyo, isipokuwa sharti iwe kabla ya kutia nia ya kuhiji).

Unaweza kukoga na kuvaa Ihraam (vazi la kuhijia) pamoja na kufanya yote hayo ukiwa nyumbani kwako, hotelini au popote ulipofikia kabla ya kuifikia mipaka hiyo, isipokuwa nia lazima uitie ufikapo penye mipaka hiyo.

Vizuri Kuswali Kabla Ya Kutia Niyyah

Utakapofika katika mojawapo ya mipaka iliyotajwa ukiwa bado hujaswali Swalah ya fardhi ya wakati huo, basi ni bora kuswali kwanza kisha utie niyyah. Amma ukiwa umekwishaswali, basi ni vizuri (si lazima) kusali raka’ah mbili Sunnah ikiwa wakati huo si katika nyakati zinazokatazwa kuswali, kisha unatia niyyah kwa kusema: “Labbayka ‘Umrah

Kisha unaanza kufanya Talbiyyah kwa kusema:

“Labbayka Allaahumma Labbayk. Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk, Inna Lhamda Wanni-‘mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka Lak.”

Unaendelea hivyo njia yote, wanaume wanasema kwa sauti kubwa na wanawake kwa sauti ndogo huku ukimuomba Allaah maghfira na kumdhukuru kwa wingi.

Unatakiwa pia uwe ukimswalia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam kwa wingi pamoja na kuamrisha mema na kukataza maovu unapokuwa safarini mpaka utakapowasili Makkah.

Hukmu Ya Talbiyyah

Talbiyyah ni kutamka "Labbayka Allaahumma Labbayk. Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk, Inna Lhamda Wanni-‘mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka Lak.”

Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Talbiyyah ni kitendo kilichotolewa amri juu yake.

Kutoka kwa Ummus-Salama (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema:

((Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema: ‘Enyi watu wa nyumba ya Muhammad, anayehiji kati yenu anyanyuwe sauti yake anapofanya Talbiyyah.)) [Imepokewa na Imam Ahmad na Ibni Hibban]

Maulamaa wamekhitilafiana katika hukmu yake, katika wakati wake, na katika kuichelewesha.

Imam Ash-Shaafi’iy na Imam Ahmad wanasema kuwa kitendo hicho ni Sunnah na kwamba mtu anatakiwa aanze kufanya Talbiyyah mara baada ya kutia nia ya Ihraam. Na iwapo ametia nia ya Hijjah kisha asifanye Talbiyyah, basi Hijjah yake inasihi na wala haina tatizo lolote.

Imam Maalik, yeye anaona kuwa kitendo hicho ni Wajib na mtu asipofanya Talbiyyah baada ya kutia nia ya Ihraam, akaendelea hivyo muda mrefu bila kufanya Talbiyyah, basi inampasa kuchinja mnyama.

Fadhila Zake

Imesimuliwa na Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

((Muislam yeyote atakayefanya Talbiyyah tokea asubuhi mpaka jua linapozama, dhambi zake zitafutwa na atarudi (akiwa hana dhambi) kama alivyokuwa siku aliozaliwa na mama yake.)) [Imepokewa na Ibni Majah]

Imesimuliwa pia na Abu Hurayrah kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

((Kila mwenye kuinyanyua sauti yake kwa kufanya Talbiyyah, anapewa bishara (njema), na kila mwenye kufanya Takbir (kutamka 'Allaahu Akbar') anapewa bishara (njema)” Akaulizwa: “Ewe Mtume wa Allaah, bishara ya Pepo?” Akasema: “Ndiyo”)) [Imepokewa na At-Tabaraniy na Sa’iyd bin Mansuur]

Kunyanyua Sauti Katika Talbiyyah

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

((Alinijia Jibriyl akaniambia: “Waamrishe sahibu zako wanyanyuwe sauti zao katika Talbiyyah, kwani hiyo ni katika alama za Hijjah.”)) [Imepokewa na Ibni Majah. Imam Ahmad, Ibni Khuzaymah na Al Hakim]

Na kutoka kwa Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

((Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliulizwa: “Amali gani iliyo bora katika Hijjah?” Akajibu: “Al ajji wa thajji” (Kunyanyua sauti katika kufanya Talbiyyah na kuchinja).)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy na Ibni Majah]

Twawaafu ya ‘Umrah

Unapowasili Makkah unaanza kufanya ‘Umrah kwa taratibu ifuatayo:

Unatufu’, kwa kuizunguka Al-Ka’abah mizunguko saba ukianzia penye jiwe jeusi (Al Hajar al aswad), ukiwa mbali na jiwe hilo anzia sawa na jiwe jeusi.

Kabla ya kuanza kutufu lielekee Jiwe jeusi kisha linyoshee mkono (ukiweza kulifikia na kulibusu au kuligusa bila ya kuumiza watu ni vizuri), la kama utasababisha madhara kwa watu au kwa nafsi yako, inatosha kuliashiria tu kwa mkono wa kulia kwa mbali huku ukisema: “Bismillahi Allaahu Akbar” Kisha unaizunguka Al-Ka’abah ikiwa kushotoni kwako mizunguko saba.

Kwa wanaume ni vizuri katika mizunguko mitatu ya mwanzo kukimbia kidogo kidogo mfano wa mtu anayekimbia juu ya mchanga, na mizunguko minne iliyobaki unakwenda mwendo wa kawaida. Wanawake wanakwenda mwendo wa kawaida katika mizunguko yote saba.

Wakati wote huo unatakiwa uwe ukisoma du’aa zozote ulizohifadhi. Hapana kisomo maalum au du’aa maalum, bali unaweza kuomba du’aa yoyote na kwa lugha yoyote, na unaweza pia kusoma sura ulizohifadhi katika Qur-aan.

Al-Ka’abah ina nguzo nne, na maarufu katika hizo ni nguzo ya jiwe jeusi na nguzo iliyo kabla yake ambayo ni nguzo ya Yaman (Ar-Rukn al-Yamani). Unapoifikia nguzo ya Yaman (Ar-Rukn al-Yamani) ni vizuri kuigusa. Hutakiwi kuibusu wala kuiashiria kama unavyolifanyia jiwe jeusi. Na unapokwenda baina ya nguzo hiyo ya Yamani na Jiwe Jeusi ni vizuri kuomba na kuikariri du’aa ifuatayo.
“Rabbana Aatina Fidduniya Hasanatan Wa Fil Aakhirati Hasanatan Wa Qinaa ‘Adhaaba Nnaar”.

Na maana yake ni:

(Mola wetu tupe katika dunia yaliyo mema, na katika akhera (tupe) yaliyo mema, na utuepushe na adhabu ya Moto).

Unaendelea hivyo mpaka utakapolifikia Jiwe jeusi. Hapo utakuwa umekwishamaliza mzunguko wa mwanzo, na utaanza mzunguko wa pili kwa kunyanyua mkono wa kulia huku ukiliashiria tena jiwe jeusi na kusema: “Allaahu akbar”, kisha utatenda yale yale uliyotenda katika mzunguko wa mwanzo, mpaka umalize mizunguko saba.

Kila unapolifikia jiwe jeusi au unapokuwa sawa nalo, unanyanyua mkono wa kulia na kulielekea jiwe huku ukisema: “Allaahu Akbar”

Maqaam Ibraahiym

Ukishamaliza kutufu mara saba, unakwenda kuswali raka’a mbili nyuma ya Maqaam Ibraahiym. Katika raka’a ya mwanzo unasoma Alhamdu na Qul ya ayyuha l kaafiruun na katika raka’a ya pili unasoma Alhamdu na QulhuwAllaahu ahad.

Usipoweza kuswali penye Maqaam Ibraahiym kwa sababu ya msongamano mkubwa wa watu, unaweza kuswali popote karibu na hapo au popote mbali na hapo sharti iwe ndani ya msikiti.

Kunywa Maji Ya Zamzam

Baada ya kumaliza kutufu na kuswali raka’a mbili penye Maqam Ibrahim, ni vizuri kunywa maji ya Zamzam. Unaweza kunywa kutoka katika majagi ya maji yaliyoenezwa msikitini hapo, na unaweza pia kwenda penye mifereji (mabomba) ya maji ya Zamzam yaliyokuwepo penye uwanja wa Swafaaa na Marwah.

Imepokewa kutoka kwa Al-Bukhaariy na Muslim kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikunywa maji ya Zamzam kisha akasema: ((Maji haya yamebarikiwa, yanamshibisha mwenye njaa na yanamponesha mgonjwa.))

Sa’ay Baina Ya Swafaaa Na Marwahh

Swafaaa na Marwah ni vilima viwili vilivyoelekezana, vilivyomo ndani ya msikiti upande wa kisima cha Zamzam.

Ukimaliza kutufu na kunywa maji ya Zamzam, unakwenda penye jabali Swafaaa kwa ajili ya kuanza kufanya ibada ya Sa'ayi, baina ya majabali Swafaaa na Marwah.

Unaanza kwa kupanda Swafaaa huku ukisema:
“Inna Swafaa walMarwahta min shaairi llah". kisha unasema "Abdau maa badaa llahu bihi”, na maana yake ni:

(“Hakika Swafaaa na Marwah ni katika alama za kuadhimisha dini ya Allaah. Ninaanza pale alipoanzia Allaah. (Ambaye ndani ya Qur-aan tukufu ameanza kulitaja jabali Swafaaa kisha Marwah).

Si lazima kutamka maneno hayo, lakini hi ni kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema na kufanya hivyo.

Unapowasili juu ya Swafaaa unaelekea Qiblah kisha unasema:

الحمد لله - الله اكبر - لا إِلهَ إلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ المُلْكُ وَلَهُ الحَمْدُ وهُوَ عَلى كُلِّ شَيءٍ قَديرٌ، لا إِلَهَ إلا اللهُ وَحْدَهُ أَنْجَزَ وَعْدَهُ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ وَهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ.

“Alhamdu Lillahi Allaahu Akbar La Ilaha Illa Llahu Wahdahu Laashariyka Lahu Wahuwa Alaa Kulli Shay-In Qadiir. La Ilaha Illa Llahu Wahdau, Anjaza Waadahu Wanawsara ‘Abdahu Wahazamal Ahzaaba Wahdahu” Unasema hivyo mara tatu.

Hivi ndivyo alivyofanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Kama hukuweza (kutokana na zahma au kama hujaweza kuhifadhi vizuri) basi unasoma hata mara moja tu, au unaomba du’aa yoyote na kusoma chochote unachoweza kusoma. Kisha teremka na ufanye "Sa’ay ya Umra”.

Na Sa’ay ni kwenda baina ya Swafaaa na Marwah mara saba (Kwenda, inahisabiwa mara moja, na kurudi mara moja). Ni vizuri kukimbia kidogo kidogo kila unapozifikia alama za kijani zilizo ukutani baina ya Swafaa na Marwah, lakini wanawake, wao wanakwenda mwendo wa kawaida. Ukifika Marwah, unapanda juu na kusema pamoja na kufanya yale uliyoyafanya ulipokuwa juu ya Swafaaa.
Hakuna katika Twawaafu wala katika Sa’ay, du’aa au kisomo maalum. Soma chochote na omba du’aa yoyote.

Kujihalalisha

Ukishamaliza kufanya Sa’ay, unapunguza nywele zako au unazinyoa zote. Kwa wanaume ni vizuri kunyoa, kama alivyofanya na kupendekeza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Lakini wanawake, wao wanapunguza kidogo tu.

Hapo utakuwa umekwisha maliza ibada ya ‘Umrah na unaweza kuvua nguo za Ihraam na kuvaa nguo zako za kawaida. Na kinakuhalalikia kila kitu  ulichoharamishiwa ulipokuwa katika Umrah, hata mkeo. (Kama ni ‘Umrah ya Hijjah unaisubiri tarehe 8 Dhul-Hijjah ili uanze ibada ya Hijjah.)

Fadhila Za Kunyoa Nywele Zote

Kutoka kwa Abdillahi bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

((“Allaah Awarehemu walionyoa (nywele zote)” Masahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakasema: “Na waliopunguza je ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: “Allaah awarehemu walionyoa (nywele zote).” Wakasema: “Na waliopunguza je ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: “Allaah awarehemu walionyoa (nywele zote).” Wakasema: “Na waliopunguza je ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: “Na waliopunguza.”))

Katika Hadiyth hii Mtume Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amewaombea rehema mara tatu walionyoa nywele zote na akawaombea mara moja tu waliopunguza.

Tunamuomba Allaah atuingize katika Rahmah Yake – Aamin

Hijjah

Tarehe nane Dhul Hijjah inaitwa "Siku ya Attarwiyah”, nayo ni siku inayoanza Ibada za Hijjah. Likishatoka jua la siku hiyo, oga na uvae nguo zako za Ihraam ukiwa nyumbani, hotelini au popote ulipofikia mjini Makkah au nje yake kisha sema: “Labbayka Hijjah”. Masharti ya Ihraam ni yale yale tuliyoyataja hapo mwanzo katika ibada ya ‘Umrah.

Asubuhi ya siku hiyo Mahujaji wanaondoka Makkah kuelekea Minaa na wanaswali mahali hapo Swalah ya Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, Isha ya siku hiyo, pamoja na Swalah ya Alfajiri ya siku ifuatayo. Kila Swalah inaswaliwa katika wakati wake Qasran (kwa kufupisha). Unazifupisha Swalah za raka’a nne unaziswali raka’a mbili, ama Swalah ya Magharibi unaiswali kwa ukamilifu – raka’a tatu.

‘Arafah

Kusimama y ni nguzo kubwa kupita zote katika nguzo za Hijjah, na hii inatokana na Hadiyth ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema:

((Al Haju ‘Arafah – (Kusimama) Arafa ndiyo Hijjah yenyewe - atakayewahi usiku wa kujikusanya kabla ya kuingia alfajiri (ya siku ya ‘Arafah) basi amewahi”.)) [Imepokewa na Imam Ahmad pamoja na ma Imam wengine wa Hadyith]

Kusimama ‘Arafah

Likishatoka jua la tarehe tisa Dhul Hijjah, Mahujaji wanaondoka Minaa na kuelekea ‘Arafah kwa utulivu na tahadhari, huku wakisema: “Allaahu akbar” – au “Laa ilaaha illa Allaah” au huku wakilabiy kwa kusema:
“Labbayka Allahumma Labbayk Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk - Inna Lhamda Wanni’mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka Laka.”
Wanakwenda kwa utulivu bila kuwaudhi wenzao, na wanaziswali Swalah za Adhuhuri na Alasiri wakati mmoja hapo ‘Arafah, Qasran, zote wakati wa Adhuhuri, kwa adhana moja na iqama mbili.

Ni vizuri kubaki katika sehemu ya Namirah, mahali ulipo msikiti mkubwa wa Namirah na wasiingie ‘Arafah mpaka baada ya wakati wa zawaal (Kiasi cha saa sita za mchana).

Hii siyo lazima, hasa kutokana na zahma za hapo ‘Arafah siku hiyo, isipokuwa ni bora kama ikiwezekana. Hakikisha kuwa umo ndani ya mipaka ya ‘Arafah, na unapokuwa mahali hapo patakatifu, zidisha kuomba du’aa na kumtaja Mola wako huku ukiwa umeelekea Qiblah, kwa sababu siku hiyo na mahali hapo ndipo watu wanapoghufiriwa madhambi yao yote na kurudi makwao kama siku waliyozaliwa.

Nyakati za jioni tafuta sehemu za juu juu. Panda, kisha elekea Qiblah na unyanyue mikono yako juu huku ukiomba, kama alivyofanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Imesimuliwa na Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

((“Hakuna siku bora kwa Allaah kuliko siku kumi za (mwanzo) za Dhul Hijjah”. Mtu mmoja akamuuliza: “Siku hizo ni bora, au mtu anapokuwa katika Jihadi kwa muda huo?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamuambia: “Siku hizo ni bora kuliko idadi ya siku hizo katika Jihadi fiy sabiili Llah. Na hapana siku iliyo bora kwa Allaah kuliko siku ya ‘Arafah. Allaah Subhanahu wa Taala huwaambia Malaika wake kwa fahari: “Tazameni waja wangu, wamekuja nywele zao zikiwa zimetimka, wamejaa mavumbi, wametoka kila sehemu za mbali wakitaraji rehema Zangu na wala hawakuwahi kuiona adhabu Yangu”. Hakuna siku ambayo Allaah anawaepusha watu wengi na moto kuliko siku hiyo”.)) [Imepokewa na Abu Ya’ala – Al-Bazzaar – Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan]

Imepokewa pia kuwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

((“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisimama ‘Arafah wakati jua linakaribia kuzama, akasema: “Ewe Bilaal! Ninyamazishie watu.” Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu), akainuka na kuwataka watu wanyamaze. Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
“Enyi watu! Alinijia Jibril hivi punde na kunipa salam zitokazo kwa Mola wangu. (Kisha) Akasema: ‘Allaah Subhanahu wa Taala amewaghufiria watu wa ‘Arafah na watu wa Masha'ari l haraam (Muzdalifah).” Akainuka ‘Umar bin Khattab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akauliza: “Hizi (salam na haya maghfira) ni kwa ajili yetu peke yetu?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: “Hizi ni zenu na za wote watakaokuja (hapa) baada yenu mpaka siku ya Qiiyaamah.” ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema: “Kheri za Allaah ni nyingi na nzuri.”))

Imesimuliwa na Ibnul Mubarak kutoka kwa Sufyaan Ath-Thawriy kuwa:

'Mtu anapokuwa hapo anatakiwa ajishughulishe na kuomba du’aa pamoja na kumtaja Allaah sana ili arudi akiwa amefaidika na ameghufiriwa, na asiwe katika waliokula hasara siku hiyo kwa kuyakosa maghfira ya Allaah.'

Jua likishazama Mahujaji wanaondoka ‘Arafah na kuelekea Muzdalifah. (Usiswali Magharibi hapo ‘Arafah).
 HAPA NI NDANI YA MASJID NNABAWIYY ULIOPO MADINI,NA HII SEHEMU YA RAWDHWAL JANNAH
Muzdalifah

Unapokuwa Muzdalifah utaswali Swalah ya Magharibi na ‘Ishaa wakati wa ‘Ishaa, raka’a tatu za Magharibi kisha mbili za ‘Ishaa kwa adhana moja na Iqama mbili. Kisha utabaki hapo mpaka baada ya Swalah ya Alfajiri.

Ukiwa hapo utaomba du’aaa kwa wingi huku ukinyanyua mikono yako juu na kuelekea Qiblah kama alivyofanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Ukiwa Muzdalifah utaokota mawe ya kupigia Jamaraat. (Jamaraat ni milingoti mikubwa mitatu ya mawe yanayopigwa hapo Minaa ambayo watu wengine huyaita Mashetani). Unaokota mawe saba tu, (si lazima kuokota mawe yote hapo Muzdalifah), na mawe mengine utaweza kuokota ukiwa Minaa. Unaweza pia kuokota mawe yote ukiwa hapo kama ukitaka.

Minaaa

Utaondoka Muzdalifa kwa utulivu na kuelekea Minaa baada ya Swalah ya Alfajiri na kabla ya kutoka jua.

Utakapowasili Minaaa unafanya yafuatayo:

1.     Unalipiga Jamaratul ‘Aqabah ambalo watu wanaliita Shetani Mkubwa, lililo karibu na Makkah kwa mawe saba, moja baada ya jingine. Kila unaporusha jiwe unasema:

“Allaahu Akbar".

(Haijuzu kuvurumisha mawe yote saba kwa pamoja).

Jamaraat’ si mashetani kama wanavyoitakidi baadhi ya watu wenye kuvurumisha mawe kwa ghadhabu na kutukana na wengine huvurumisha mawe makubwa wakidhani kuwa wanampiga na kumkomesha shetani. Hayo yote hayajuzu, kwa sababu ‘Jamaraat’ yamewekwa kwa ajili ya kujikumbusha tu namna gani Nabii Ibraahiym mahali hapo alivyompiga mawe shetani aliyejaribu kumshawishi asimchinje mwanawe kama alivyoamrishwa na Mola wake.

Kwa hivyo mtu anatakiwa arushe mawe madogo sana na kuyapiga Jamaraat kwa nia ya kutii amri ya Allaah tu, bila ya kuingiza fikra nyingine.

Kwa wale wasiojiweza wanaweza kumwakilisha mtu awapigie, na mtu mmoja anaweza kuwakilishwa na wengi.
(Kumbuka siku ya mwanzo unalipiga mawe Jamarat moja tu, tofauti na siku zilizobaki unapoyapiga mawe Jamaraat zote tatu).

2.     Chinja mnyama wako, na ni vizuri kama utakula katika nyama hiyo na nyengine utawapa masikini.

3.     Punguza au nyoa nywele zako. (kunyoa nywele zote ni bora zaidi), na mwanamke anakata nywele zake kidogo tu.

Utaratibu huu ni bora zaidi ingawaje unaweza kutanguliza hiki kabla ya kile. Ukimaliza kupiga mawe, kuchinja na kunyoa, unakuwa umekwisha jihalalisha uhalalisho mdogo na unaweza kuvaa nguo zako za kawaida na kufanya yote uliyokatazwa ulipokuwa na Ihraam, isipokuwa tu huwezi kumwingilia mkeo mpaka umalize Twawaaful Ifaadhwah (Twawaafu ya Hijjah).

Twawaaful Ifaadhwah

Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Twawaaful Ifaadhwah (Twawaafu ya Hijjah) ni katika nguzo za Hijjah, na kwamba asiyetufu Twawaafu hiyo Hijjah yake inabatilika.

Na hii inatokana na kauli Yake Subhanahu wa Taala Aliposema:

{{Kisha wajisafishe taka zao, na watimize nadhiri zao, na waizungike Nyumba ya Kale (Nyumba kongwe – Al-Ka’abah).}} [Al Hajj – 29]

Ukishamaliza shughuli za hapo Minaa, unakwenda Makkah na unafanya Twawaaful Ifaadhwah, nako ni kuizunguka Al-Ka’abah mara saba na kufanya kama ulivyofanya katika Twawaafu ya ‘Umrah. Kisha unafanya Sa’ay, kutembea baina ya Swafaaa na Marwah na kufanya kama ulivyofanya mara ya mwanzo ulipofanya ‘Umrah.

Ukishamaliza, unakuwa umekwisha jihalalishia halalisho kubwa na kwa hivyo, hata mkeo anakuhalalikia. Unaweza kuiahirisha Twawaafu ya Ifaadhwah mpaka baada ya kumaliza shughuli zote za Minaa.

Ukishamaliza Twawaafu ya Ifaadhwah unarudi Minaa na unabaki hapo usiku wa tarehe 11, 12 na 13 kwa wasiokuwa na haraka. Hizo zinaitwa siku za Tashriyq. Inatosha kama utabaki hapo usiku wa tarehe 11 na wa 12 tu.  Katika siku 2 au 3 hizo unapiga mawe Jamaraat zote tatu kila siku kwa mpangilio ufuatao:

Anza kupiga Jamaraat la mbali na Makkah, (Jamaraat dogo) kisha la kati, kisha Kubwa (Jamarat al Aqaba). Kila moja piga kwa mawe saba huku ukisema: "Allaahu Akbar", kila unaporusha jiwe. Hii ni kwa siku tatu zilizobaki.

Nyakati za kupiga mawe

Siku ya An-Nahr – Sikukuu mosi, usipige mawe mpaka jua lichomoze:

((Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa Muzdalifah aliwatanguliza Minaa watu dhaifu na wazee na wanawake, akawaambia: “Musirushe mawe mpaka jua litoke”)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy]

Mwenye udhuru anaweza kuchelewesha mpaka kabla ya Magharibi, lakini ni vizuri kupiga mawe baada ya kutoka jua na kabla haijaingia Magharibi kwa asiyekuwa na udhuru. (Baadhi ya Maulamaa wanajuzisha kupiga mawe baada ya Magharibi kwa udhuru, lakini bora ujaribu kupiga kabla jua kuzama).

Wakati wa kurusha mawe kwa siku mbili zilizobaki au siku tatu kwa wale wasiotaka kuharakisha, ni baada ya Zawal (wakati wa adhuhuri pale jua linaposogea kidogo baada ya kuwa katikati).

Kuomba Du’aa

Ni vizuri kuelekea Qiblah na kuomba du’aa baada ya kumaliza kupiga kila Jamaraat isipokuwa Jamaraat la mwisho. Hadiyth iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy na Imam Ahmad inasema:

((Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akeshapiga kila Jamaraat kwa mawe saba akisimama na kuelekea Qiblah na kuomba du’aa, isipokuwa baada ya kulipiga Jamaraat la mwisho hakusimama.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Imam Ahmad]

Siku Ya Kuharakisha

Ikiwa unataka kubaki hapo kwa mda wa siku mbili tu, basi siku ya tarehe Kumi na mbili Dhul Hijjah ambayo hujulikana kama ni "Yawmul isti’ijaal" - Siku ya Kuharakisha – unapiga mawe na kuondoka Minaa kabla ya jua kuzama, na ikiwa utakawia kuondoka ukawepo hapo baada ya juwa kuzama itakubidi ubaki hapo siku moja zaidi. Ni vizuri kubaki usiku wa tatu ikiwa huna cha kukushughulisha.

Twawaaful Wida’a

Unapotaka kurudi nchini kwako baada ya kumaliza shughuli za Hijjah, unatufu Twawaaful wida’a, (Twawaafu ya kuaga) nayo ni kama ifuatavyo:

Unatufu Al-Ka’abah mara saba na kufanya kama ulivyofanya katika Twawaafu za mwanzo, lakini mara hii bila ya kufanya Sa’ay baina ya Swafaa na Marwah.


::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::

Fadhila Za Hajj Na 'Umrah Na Adabu Zake


Imekusanywa Na: Ukht Muznah Faraj

Alhamdulillahi Rabbil Alaamiyn Was swalatu Wassalaamu Alaa Nabiyyinaa Waalaa Aalihi Waswahbihi Waman Tabiahum bi’ihsaani ilaa yaumid’diyn. Amma Ba’ad,
1- Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((Na Allaah Amewawajibishia watu wafanye hajji katika nyumba hiyo; (Al-Ka’abah) Yule awezae kufunga safari kwenda huko. Na atakae kanusha (asende, hali kuwa anaweza) basi Allaah simuhitaji kuwahitajia walimwengu))
[Qur-aan: 3:97]

2- Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Kufanya umrah hadi umrah  hufutiwa madhambi baina yake, na Hajj (Mabruur) yenye kukubaliwa haina malipo isipokuwa pepo))
{Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim}

3- Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Atakayehiji ikawa hakufanya maovu (kwa vitendo wala kwa maneno) na wala hakuvunja amri za Allaah (Subhaanahu Wata’ala) atasamehewa madhambi yake yote atakuwa kama siku aliyozaliwa na Mama yake))
[Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]

4- Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Chukueni Hajj kutoka kwangu))
[Imepokewa na Muslim]
- Ni wajibu wa kila mwenye kuhiji na kufanya umrah awe mali anayofanyia ibada hizo iwe ni ya halali ili Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) aikubali, kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Hakika Allaah Mtukufu ni mzuri na hakubali isipokawa kizuri))
[Imepokewa na Muslim]

6- Kwa hakika hajji ni kongamano kubwa kwa waislamu linalo wakutanisha waislamu, kwa sababu kunapatikana ndani yake kujuana, kupendana, na kusaidiana katika kutatua matatizo juu ya kila hali, na pia kushuhudia manufaa yanayopatikana humo ya dini na dunia. SubhaanAllaah!!!  Ametukuka Aliye Mbora wa viumbe.
Na Amesema Allaah Mtukufu:
((Na saidianeni kwa wema na uchaji Allaah wala msisaidaene katika madhambi na uadui))
[Qur-aan: 5:2]

7- Inajuzu kufanya umrah katika wakati wowote, lakini kufanya umrah katika mwezi wa Ramadhaan ni bora,  kwa kauli aliyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Kufanya 'Umrah katika mwezi wa Ramadhaan ni kama Hajj))
[Al-Bukhaariy na Muslim]

8- Swalah katika Msikiti mtukufu wa Makkah ni bora mara  laki moja kuliko Swalah katika Misikiti mingine. Kwa kauli aliyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Swalah katika Msikiti wangu huu ni bora katika Swalah elfu moja kuliko misikiti mingine iispokuwa Msikiti  mtukufu wa Makkah)) [Imepokewa na Muslim]
Swalah moja katika Msikiti wa Mtume Madiynah ni sawa malipo yake na Swalah elfu moja (1000).
Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Swalah katika Msikiti mtukufu wa Makkah ni bora kuliko Swalah katika Msikiti wangu huu kwa Swalah mia))
[Imepokewa na Ahmad]
Akimaanisha mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa swala moja ni sawa na swala mia, yaani 100*1000 = 100,000 .
Hii ni kuonyesha kuna fadhila kubwa sana na yoyote ambae amejaaliwa kufika huko basi na ajitahidi swala zake zote aziswali msikitini ili asikose thawabu hizi.

KWA UFUPI:
Hajj ni nguzo miongoni mwa nguzo za Kiislamu na ndani yake kuna fadhila nyingi ambazo nimezitaja kwa ufupi na manufaa  ya kidunia na Akhera.  Kwa mfano, unaweza kufanya biashara pindi umalizapo hajji na mengineyo ambayo tuliyataja hapo juu. Na manufaa ya akhera ambayo ni bora zaidi kuliko ya dunia.
Allaah Amesema:
((Na maisha (bora zaidi kabisa) ni ya Aakhirah yenye kudumu))
[Qur-aan: 87:17]

Basi ni juu ya kila muislamu ajitahidi kuendea njia hiyo pale atapo kuwa na uwezo wa kuifikia njia hiyo kabla hayajamfikia mauti hali yuko katika maaswi. Basi na ajihadhari kutokana na maovu, kuvunja amri za Allaah, mijadala isiyo ya hakki wala faida ndani yake na maaswi yote kwa ujumla.

ADABU ZA HAJJ NA UMRAH:
1- Itakase hajji yako iwe kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na sema kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
((Ee Mola ifanye Hajj yangu isiwe ya kujionyesha wala kusifiwa))
[Swahiyh Al-Bayhaqiy]
Kwani kuna baadhi ya watu matendo yao wanayafanya ili waonekane na wao wamekwenda au wamefanya hajji au wamesikilikana kwa kusifiwa kama Fulani pia amekwenda iwe ni matendo ya hajji au hata ibada zozote ilihali si kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hao matendo yao yatakuwa hayana malipo yoyote mbele ya Allaah Mtukufu.

2- Iwe hajji  imewafikiana na hajji aliohijji Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyo sema mwenyewe Bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Chukueni Hajj kutoka kwangu))
[Imepokewa na Muslim]

3- Jihadhari na  kutokufanya maovu na yaliyo katazwa, na maaswi, na mijadala iliyo baatili (iliyokatazwa) mpaka hijjah yako iwe ni maqbuul ( yenye kukubalika).

4- Jihadhari na kuomba duaa kwa asie kuwa Allaah Mtukufu. kuomba maiti mfano kwenye makaburi wakati unapo zuru makaburi ni kwa ajili ya kujikumbusha na mauti na kuwatakia rehma na maghfira sikuwaomba au kutaka msaada au kuokolewa  hiyo itakuwa ni shirki ambayo itabatilisha hajji na amali zako zote. Kama alivyo sema Allaah Mtukufu:
((Ikiwa utamshirikisha (Allaah ) bila shaka matendo yako yote yataruka patupu (hutazipatia thawabu japo ni matendo mazuri ) na lazima utakuwa miongoni mwa wenye khasara))
[Qur-aan 39:65]

5- Unatakiwa uwe mpole kwa walio karibu yako yaani walioko pembezoni mwako  wakati unapokuwa unafanya twawafu (kuizunguka al ka’abah) na unapo fanya saa’yi (kutembea kilima cha saffa na mar’wah) na wakati wa kutupa mawe katika minara ya jamaraati, wala msinyanyuwe sauti wakati wa kumtaja Allaah wala wakati wa Duaa na khasa pale mnapokuwa kwenye kundi kwani kunyanyuwa sauti kunawachanganya wengine kwakufanya hivyo hakuna dalili na hivyo kunyanyuwa sauti ni Bid’aa iliyozushwa.

6- Haifai kufanya zahma yaani kusukumana wakati wa kuliendea jiwe jeusi wala kusimama hapo kuwazulia wengine wakati unapo fanya tawaafu. Inavotakiwa ni kuligusa, kulibusu na huku unaomba nakuondoka si kusukumana.

7- Kusimama wakati wa Sa’yi kati ya Swaffa na Marwah pindi inapo nadiwa swala ya Jama'ah mpaka itapomalizika Swalah utatimiza palipobaki.

8- Kuhifadhi Swalah ya Jama'ah katika msikiti na khasa unapokuwa katika Msikiti wa Makkah, Kwani kuna fadhila kubwa kama tulivyotangulia kusema.

9- Usiwapitepite wenye kuswali ukawaudhi, kaa palipo karibu yako penye nafasi.

10- Jihadhari na kuwapita watu wanapo kuwa kwenye safu ya Swalah kati yako na mwenye kuswali hata kama ni katika msikiti mtukufu wa Makkah ili upite safu ya mbele ikiwa unataka kukaa mbele basi inakubidi uwahi na sio kuwakunja watu shingo ili upite mbele, kwani hayo ni matendo ya shaitwani, isipokuwa iwe kwa  dharura.
11- Kuzidisha kuizunguka al ka’abah kwani kufanya hivyo kuna malipo makubwa  kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Mwenye kuizunguka Al-Ka’abah mara saba atakuwa kama aliyemuacha huru Mtumwa))
[Imepokewa na Ibn Maajah]

12- Haifai kuchinja  kabla ya kufikia siku ya kuchinja wala haifai kutoa sadaka  kwa thamani yake.

13- Na katika alama za kukubaliwa hajji ni kubadilika katika hali iliyo nzuri ya aqidah yako (kutokumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika ibaada zako kushirikiana na Waislamu wenzio kwa wema na tabia njema na ni juu yako kumuomba Allaah wakati wote hii ni kipimo baada ya hajji kwani ikiwa hukubadilika katika 'Aqidah yako na tabia yako kwa ujumla itakuwa hajji yako ni matembezi tu na sio 'Mabruur'.
((Ee Mola Tukubalie hakika Wewe ni Mwenye kusikia na ni mjuzi))
“Aamiyn”

Allaah Atuwafiqishe na Atufanyie wepesi na ajaalie manufaa na kuyafanyia kazi yote na tufaidike nayo In sha Allaah. 

 ::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::

Fadhila Za Siku Ya 'Arafah Na Yawmun-Nahr (Siku Ya Kuchinja)

 ‘Arafah ni jabali ambalo alisimama Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwahutubia Maswahaba alipotekeleza Hijja ya kuaga. Na hapo ndipo wanaposimama Mahujaji kutimiza kilele cha ‘Ibaadah hii ya fardhi. Kusimama hapo ndio nguzo mojawapo kuu ya Hijjah bila ya kuweko hapo mwenye kuhiji atakuwa hakutimiza hijja yake kutokana na dalili  ifuatayo:

عن عبد الرحمن بن يعمر قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم:  ((الْحَجُّ عَرَفَة ، مَنْ جَاءَ قَبْلَ طُلُوعِ الْفَجْرِ مِنْ لَيْلَةِ جَمْعٍ فَقَدْ أَدْرَكَ الْحَجّ))  صحيح الجامع   

Kutoka kwa ‘Abdur-Rahmaan bin Ya’mur ambaye amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam: ((Al-Hajj ni ‘Arafah, atakayekuja kabla kutoka Alfajiri usiku wa kujumuika atakuwa ameipata Hajj)) [Swahiyh Al-Jaami’)



Fadhila Za Siku ya ‘Arafah:




1-Ni Siku Iliyokamilika Dini Yetu  

قال رجل من اليهود لعمر : يا أمير المؤمنين ، لو أن علينا نزلت هذه الآية : ((اليوم أكملت لكم دينكم وأتممت عليكم نعمتي ورضيت لكم الإسلام دينا)) لاتخذنا ذلك اليوم عيدا ، فقال عمر: "إني لأعلم أي يوم نزلت هذه الآية ، نزلت يوم عرفة ، في يوم جمعة"  البخاري

Kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Myahudi mmoja alimwambia: “Ewe Amiri wa Waumini, lau ingeliteremka kwetu sisi Aayah hii ((Leo Nimekukamilishieni Dini yenu na Nimekutimzieni Neema Zangu kwenu na Nimekuridhieni Uislamu kuwa ni Diyn yenu)) [Al-Maaidah (5: 3] tungeliifanya ‘Iyd siku hiyo. Akasema ‘Umar: “Hakika naijua siku gani imeteremka Aayah hii. Imeteremka Siku ya ‘Arafah siku ya Ijumaa” [Al-Bukhaariy)


Na ukamilifu wa dini siku hiyo ni kwa vile Waislamu hawakupata kutekeleza Hajj kabla ya hapo ya Kiislamu. Na kukamilika dini yao ni kukamilisha nguzo za Kiislamu zote.  


2-Kufunga Swawm ni kufutiwa madhambi ya miaka miwili:

Ni fadhila kubwa kwetu kujitakasa na madhambi tunayoyachuma kila siku kwani binaadamu daima ni mkosa.


عَنْ أَبِي قَتَادَةَ رضي الله عنه أن النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ :  ((صِيَامُ يَوْمِ عَرَفَةَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ وَالسَّنَةَ الَّتِي بَعْدَهُ )) أخرجه مسلم

Imetoka kwa Abu Qataadah (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Swawm ya 'Arafah nataraji (kwa Allaah) kufuta madhambi ya mwaka uliopita na wa baada yake.” [Muslim]

Umuhimu huo wa kufunga na msisitizo ni kwa wasiohiji, na walio katika Hajj wao hakuna msisitizo huo kwa dalili ifuatayo:


عن ميمونة بنت الحارث: أن الناس شكوا في صيام النبي صلى الله عليه وسلم يوم عرفة ، فأرسلت إليه بحلاب ، وهو واقف في الموقف ، فشرب منه والناس ينظرون" البخاري

Kutoka kwa Maymuunah bint Al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anhaa) kwamba watu walitia shaka na Swawm ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa  aalihi wa sallam) [kama alifunga] Siku ya ‘Arafah, nikampelekea maziwa, naye akiwa amesimama akayanywa na huku watu wanamtazama”  [Al-Bukhaariy]




3-Ni Siku Bora Kabisa Ambayo Wataokolewa Waja Kutokana Na Moto; Wataghufuriwa Madhambi Yao



عن  جابر  رضي الله عنه  عن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((مَا مِنْ يَوْمٍ أَفْضَلُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ يَوْمِ عَرَفَةَ، يَنْزِلُ اللَّهُ تَعَالَى إلَى سَمَاءِ الدُّنْيَا فَيُبَاهِي بِأَهْلِ الْأَرْضِ أَهْلَ السَّمَاءِ)) وروى ابن حبان
وفي رواية: ((إنَّ اللَّهَ يُبَاهِي بِأَهْلِ عَرَفَةَ مَلَائِكَتَهُ، فَيَقُولُ: يَا مَلَائِكَتِي، اُنْظُرُوا إلَى عِبَادِي، قَدْ أَتَوْنِي شُعْثا غُبْرا ضَاحِينَ))

Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa  aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna siku iliyo bora kabisa mbele ya Allaah kama siku ya ‘Arafah. Anateremka Allaah Ta’ala mbingu ya dunia (ya kwanza) kisha Anawafakhiri watu  ardhi  kwa watu wa mbingu.”


Na katika riwaaya nyingine: “Hakika Allaah Anawafakhiri watu ‘Arafah kwa Malaika Wake. Husema Husema Ee Malaika wangu, watazameni waja Wangu wamenijia wakiwa timtimu wamejaa vumbi …”

Pia,

 عن عائشة  رضي الله عنها عن النبي صلى الله عليه وسلم: ((ما من يوم أكثر من أن يعتق الله فيه عبيدا من النار من يوم عرفة ، وأنه ليدنو ، ثم يباهي بهم الملائكة فيقول : ما أراد هؤلاء ؟ اشهدوا ملائكتي أني قد غفرت لهم )) صحيح الترغيب

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakuna siku Anayoacha Allaah kwa wingi huru waja kutokana na moto kama siku ya ‘Arafah. Na huwa karibu kisha Anajigamba kwao kwa Malaika na Husema: Wametaka nini hawa? Shuhudieni Malaika wangu kwamba hakika Mimi Nimewaghufuria)) [Swahiyh At-Targhiyb]
  

عن جابر  رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم-(( ما من أيام عند الله أفضل من عشر ذي الحجة قال فقال رجل يا رسول الله هن أفضل أم عدتهن جهادا في سبيل الله قال: (( هن أفضل من عدتهن جهادا في سبيل الله وما من يوم أفضل عند الله من يوم عرفة ينزل الله تبارك وتعالى إلى السماء الدنيا فيباهي بأهل الأرض أهل السماء فيقول انظروا إلى عبادي جاءوني شعثا غبرا ضاحين جاءوا من كل فج عميق يرجون رحمتي ولم يروا عذابي فلم ير يوم أكثر عتيقا من النار من يوم عرفة))   الترغيب والترهيب - إسناده صحيح أو حسن 

Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna Siku iliyo bora kabisa kama siku kumi za Dhul-Hijjah, akasema mtu: “Ee Mjumbe wa Allaah, hizo ni bora au Jihaadi katika njia ya Allaah? Akasema: “Hizo ni bora kuliko Jihaad katika njia ya Allaah, na hakuna siku bora kabisa mbele ya Allaah, kama siku ya ‘Arafah, Anateremka Allaah Tabaaraka wa Ta’ala katika mbingu ya dunia kisha Anawafakhiri watu wa ardhini kwa watu wa mbinguni kisha Anasema: Tazameni waja Wangu wamenijia timtimu wamejaa vumbi wamekuja kutoka kila pembe ya mbali wanataraji Rehma Yangu na wala hawajaona adhabu Yangu. Na wala hakuona siku inayoachwa huru shingo kutokana na moto kama siku ya ‘Arafah.” [At-Targhiyb wat-Tarhiyb – Isnaad yake Swahiyh au Hasan]
  
  
4.    Siku Ya Kutakabaliwa Du’aa

Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa  aalihi wa sallam):

 ((خير الدعاء دعاء يوم عرفة، وخير ما قلت أنا والنبيون من قبلي: لا إله إلا الله وحده لا شريك له، له الملك وله الحمد وهو على كل شيء قدير)) روى الترمذي
  
“Du’aa bora kabisa ni du’aa katika siku ya 'Arafah, na yaliyo bora kabisa niliyosema mimi na Mitume kabla yangu ni: 'Laa Ilaaha Illa Allaah Wah-dahu Laa Shariyka Lahu, Lahul-Mulku Wa-Lahul-hamdu Wa Huwa 'Alaa Kulli Shay-in Qadiyr – Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah, Pekee Hana mshirika, ufalme wote ni Wake, na Sifa njema zote ni Zake, Naye ni Mweza wa kila kitu daima.” [At-Tirmidhiy]




6-     Siku Ambayo Allaah Ameiapia

Allaah Ameiapia siku hii ya ‘Arafah ambayo inajulikana kwa ‘Siku ya Kushuhudiwa’. Hii kutokana na kauli Yake Subhaanahu wa Ta’ala:
بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ  ((وَالسَّمَاء ذَاتِ الْبُرُوجِ))  (( وَالْيَوْمِ الْمَوْعُودِ))   ((وَشَاهِدٍ وَمَشْهُودٍ))
((Naapa kwa mbingu yenye Buruji!))  ((Na kwa siku iliyoahidiwa!)) ((Na kwa shahidi na kinachoshuhudiwa!)) [Al-Buruuj 85: 1-3]

Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: “Siku ya kuahidiwa ni siku ya kufufuliwa. Siku ya kushuhudiwa ni siku ya ‘Arafah, na Siku ya kinachoshuhudiwa ni Siku ya Ijumaa)) [At-Tirmidhiy na imepewa daraja ya Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]

7-Siku Ambayo Allaah Amechukua Fungamano (ahadi) Kutoka Kizazi Cha Aadam

Imesimuliwa kwamba Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: “Allaah Amechukua fungamano kutoka mgongo wa Aadam katika Na’maan yaani ‘Arafah. Akalete mbele mgongo wake kizazi chake chote na akawatandaza mbele Yake.. Kisha Akawakabali kuwauliza:
 ((أَلَسْتَ بِرَبِّكُمْ قَالُواْ بَلَى شَهِدْنَا أَن تَقُولُواْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَذَا غَافِلِينَ)) (( أَوْ تَقُولُواْ إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِن قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً مِّن بَعْدِهِمْ أَفَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ الْمُبْطِلُونَ))
((Je, Mimi si Mola wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia. Msije mkasema Siku ya Qiyaamah sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo)) ((Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walioshirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao. Basi Utatuangamiza kwa sababu ya waliyoyafanya wapotovu?)) [Al-A’araaf 7: 172-173] [Imesimuliwa na Ahmad na imepewa daraja ya Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]


Kutokana na fadhila hizo, ndio ikawa ni siku tukufu kabisa na siku ambayo ruknu ya Hajj kuu inatimizwa na bila ya mtu kusimama ‘Arafah inakuwa hakutekeleza Hajj.

Fadhila Za Yawmun-Nahr – Siku ya Kuchinja:
Siku kuu ya ‘Iydul-Adhw-haa na ndio inajulikana pia kwa Yawmun-Nahr.

Kasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): 

((إن أعظم الأيام عند الله يوم النحر، ثم يوم الق))  أبي داود

“Siku iliyo tukufu kabisa kwa Allaah ni siku ya kuchinja, kisha siku ya kutulia”  (yaani siku ya kukaa Mina)  [Abu Daawuud]
Sababu ya kuchinja ni kufuata Sunnah ya baba yetu Nabii ‘Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) alipotaka kumchinja mwanawe Ismaa’iyl na Allaah Akamteremshia badala yake kafara ya mnyama.

*****************************************

Kuchinja - Fadhila, Hikmah Na Hukmu Zake



Anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala):
((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))

((Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako)) [Al-Kawthar: 2]

Kuchinja ni moja ya ibada za Kiislam ambayo inatukumbusha Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Baraka Zake kwetu, pamoja na kutupa mafunzo ya utiifu wa baba yetu Ibraahiym kwa Mola wake na kumpwekesha Allaah. Hivyo ibada hii ya kuchinja ni muhimu sana kwa Muislam, na inatupasa tuizingatie kwa makini na kuitekeleza.


UBAINIFU WAKE
Ni kuchinja kondoo, ngamia au ng'ombe siku ya 'Iydul-Adhwhaa na siku za Tashriyq (siku ya 11, 12, 13 Dhul-Hijjah) ili kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).


KUWAJIBIKA KWAKE
Kuchinja ni waajib katika familia ya kila nyumba ya Muislamu, ambayo watu wake wanao uwezo wa kuchinja. Hii kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))
((Basi Swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako)) [Al-Kawthar: 2]

 ((وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ))

((Na ngamia wa sadaka tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Allaah; kwa hao mna kheri nyingi)) [Al-Hajj: 36]

Na uthibitisho wa Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
 (( ضحى بكبشين أملحين أقرنين ذبحهما بيده وسمى وكبر)) رواه البخاري ومسلم 
((Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja kondoo wawili walionona, walio na pembe, aliwachinja kwa mikono yake akataja jina la Allaah, Akamtukuza kwa kusema BimiLLaah Allaahu Akbar)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Aliulizwa Shaykh Muhammad bin 'Uthaymiyn kama masikini inampasa achinje. Akajibu "Ikiwa anao uwezo wa kuchinja basi achinje ili apate kheri hizi na kama hana uwezo basi haimpasi" 
Maoni ya wanachuoni wengi kuhusu Fadhila, Hukmu na Hekima za Hajj ni kama yafuatayo:


FADHILA ZAKE
Kuna ushahidi kwamba ibada ya kuchinja ina fadhila kubwa kwa sababu ya kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
 عن عائشة رضي الله عنها أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((ما عمل ابن آدم يوم النحر عملاً أحبُّ إلى الله من إراقة الدم، وإنه ليؤتى يوم القيامة بقرونها، وأظلافها، وأشعارها، وإن الدم ليقع من الله عز وجل بمكان قبل أن يقع على الأرض، فطيبوا بها نفساً))
Kutoka kwa mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu anhaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna kitendo cha mwana Adam kilichokuwa ni kipenzi kabisa kwa Allaah siku ya kuchinja kama kumwaga  damu (kuchinja). Atakuja (huyo mnyama) siku ya Qiyaamah na pembe zake, kucha zake na nywele zake. Damu yake itamwagika mahali fulani Allaah Anapajua kabla ya kumwagika katika ardhi. Hivyo zipendezesheni nafsi kwayo)) [At-Tirmidhiy]
Na kauli yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa:
ما هذه الأضاحي؟ " قال : ((سنة أبيكم إبراهيم)) ، قالوا : "مالنا منها؟" قال)) : بكل شعرة حسنة ، قالوا : فالصوف ؟ قال : ((بكل شعرة من الصوف حسنة))  رواه أحمد وابن ماجة .
"Nini hivi vichinjo?" akajibu: ((Ni Sunnah ya baba yenu Ibraahiym)). Wakasema, "Nini umuhimu wake kwetu? Akasema: ((Katika kila unywele kuna jema moja)) Wakasema: "Na sufi?" Akasema: ((Katika kila unywele wa sufi kuna jema moja)) [Ahmad na Ibn Maajah]


HIKMAH YAKE
1.    Kujikurubisha Kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama Anavyosema katika kauli Yake: 
((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))
((Basi Swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako)) [Al-Kawthar: 2]

Anasema pia:
((قُلْ إِنَّ صَلاَتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ))
 (( لاَ شَرِيكَ لَهُ وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَاْ أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ))

((Sema: Hakika Swalah yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Allaah Mola wa viumbe vyote)) 

((Hana mshirika Wake. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu)) [Al-An'aam: 162-163]. 

((لَن يَنَالَ اللَّهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَكِن يَنَالُهُ التَّقْوَى مِنكُمْ كَذَلِكَ سَخَّرَهَا  لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ))
        
((Nyama zao hazimfikii Allaah wala damu zao, lakini unamfikia uchaji Allaah wenu. Namna hivi Tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Allaah kwa Alivyokuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema)) [Al-Hajj: 37].

Na kafara ni kuchinja kwa kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)

2.    Kuihuiisha Sunnah Mojawapo Ya Tawhiyd, wakati Allaah Alipompa wahyi Ibraahiym (alayhis-salaam) amchinje mwanawe Ismaa'iyl. Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akampa fidia ya kondoo, akamchinja badala yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
((وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ))
((Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu)) [Aswaaffaat: 107]          

3.    Muislam Kuweza Kuwalisha Nyama Familia Yake Pamoja Na Jamaa Zake Siku Ya 'Iyd na kueneza Rahma miongoni mwa masikini na mafakiri.
 
4.    Kutoa Shukurani Kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  kutujaalia kuwa na wanyama wafugwao kama Anavyosema:
((وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ كَذَلِكَ سَخَّرْنَاهَا لَكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ))
 (( لَن يَنَالَ اللَّهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَكِن يَنَالُهُ التَّقْوَى مِنكُمْ كَذَلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ))
((Na ngamia wa sadaka Tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Allaah; kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Allaah juu yao wanaposimama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na walisheni waliokinai na wanaolazimika kuomba. Ndio kama hivi Tumewafanya hawa wanyama dhalili kwenu ili mpate kushukuru))

((Nyama zao hazimfikii Allaah wala damu zao, lakini unamfikia uchaji Allaah wenu. Namna hivi Tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Allaah kwa Alivyokuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema)) [Al-Hajj: 36-37]



HUKMU ZAKE
Umri Wake:                            
Kondoo wawe ni kondoo jike ambao wamekamilisha umri wa mwaka mmoja takriban. Mbuzi wawe wamekamilisha umri wa mwaka mmoja na kuingia mwaka wa pili. Ngamia wawe wamekamilisha umri wa miaka minne na kuingia wa tano. Ng'ombe wawe wamekamilisha miaka miwili na kuingia mwaka wa tatu, kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((لا تذبحوا إلا مسنة إلا أن تعسر عليكم فتذبحوا جذعة من الضأن)) رواه مسلم
((Msichinjie ila mnyama mwenye makamo isipokuwa ikiwa ni shida kwenu, hivyo mchinje kondoo (japo wa chini ya umri wa mwaka lakini awe zaidi ya umri wa miezi sita)) [Muslim] 

Usalama Wake:
Asiwe na kasoro yoyote kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi   wa aalihi wa sallam) amesema:
((أربع لا تجوز في الأضاحي: العوراء  البيّن عورها، والمريضة البيّن مرضها،  والعرجاء  البيّن ظلعها ،  والعجفاء  التي لا تنقي))  
((Mambo manne (kasoro nne) hayapasi katika kuchinja; mwenye jicho chongo lenye kudhihirika, mnyama mgonjwa mwenye kudhihirika ugonjwa wake, kilema mwenye kudhihirika kuchechemea kwake na aliyedhoofika ambaye hana nyama katika mifupa yake)) [Swahiyh Al-Jaami']  
 
Wakati Wa Kuchinja:
Kuchinja asubuhi ya siku ya 'Iyd baada ya Swalah. Hairuhusiwi kuchinja kabla ya Swalah kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
حديث أنس  رضي الله عنه- قال: قال رسول الله -صلى الله عليه وسلم  ((من ذبح قبل الصلاة فإنما ذبح لنفسه، ومن ذبح بعد الصلاة فقد تم نسكه وأصاب سنة المسلمين)) البخاري ومسلم
Kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu 'anhu kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayechinja kabla ya Swalah atakuwa amejichinjia kwa ajili yake mwenyewe. Na Atakayechinja baada ya Swalah atakamilisha kafara (kichinjo) yake na atapata   (atatekeleza) Sunnah ya Waislam)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Anaweza kuchinja siku ya pili ya 'Iyd au kuchelewesha hadi siku ya mwisho ya Ayyaamut-Tashriyq (siku za Tashriyq) ambayo ni siku ya kumi na tatu Dhul-Hijjah.           
  (... وفي كل أيام التشريق ذبح))  
((...siku zote za Tashriyq ni siku za kuchinja)) [Ahmad]


YANAYOPENDEKEZEKA KATIKA KUCHINJA 
Kumpwekesha Allaah:
Inapendekezeka kumuelekeza mnyama Qiblah wakati wa kumchinja na kusoma:
 ((إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ حَنِيفًا وَمَا أَنَاْ مِنَ الْمُشْرِكِينَ)) 
((Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa Aliyeziumba mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina))[Al-An'aam:79]
((إِنَّ صَلاَتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ))     ((لاَ شَرِيكَ لَهُ وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَاْ أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ))
((Hakika Swalah yangu, na kichinjo changu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Allaah, Mola wa viumbe vyote)) 
((Hana mshirika Wake. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu)) [Al-An'aam: 162-163]. 

Anapoanza Kuchinja Aseme:
((بسم الله والله اكبر، اللهم هذا منك ولك))
((BismiLLaah, wa Allaahu Akbar, Ewe Allaah hii ni kutoka Kwako na kwa ajili Yako))
Kuchinja mwenyewe ni bora zaidi:
Inapendekezeka Muislamu achinje mwenyewe na akimuwakilisha mtu kumchinjia pia inaruhusiwa hakuna ikhtilaaf katika jambo hili baina ya Maulamaa.   


KUGAWA NYAMA  
Inapendekeza kuigawa nyama sehemu tatu. Ya kwanza wale familia yake, sehemu ya pili kugawa sadaqah na sehemu ya tatu kuwagawia marafiki, jirani n.k. kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((لِيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَى مَا رَزَقَهُم مِّن  بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ))
((Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Allaah katika siku maalumu juu ya nyama hao Aliowaruzuku. Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri)) [Al-Hajj: 28]

((وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ))
((Na ngamia wa sadaka Tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Allaah, kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Allaah juu yao wanaposimama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na walisheni waliokinai na wanaolazimika kuomba)) [al-Hajj: 36]

Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
((كلوا وأطعموا وادخروا)). رواه البخاري
((Kuleni, lisheni na mbakishe [akiba])) [Al-Bukhaariy]

Na usemi mwengine kutoka kwa Muslim kutoka kwa mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa)
عن عائشة رضي الله عنها أن النبي صلى الله عليه وسلّم قال: ((كلوا وادخروا وتصدقوا)) رواه مسلم.
 ((Kuleni, bakisheni na mtoe sadaka)) [Muslim]

Inaruhusiwa pia kuigawa nyama yote sadaqah na Inaruhusiwa kubakisha sehemu.  


HAIFAI KUMPA CHOCHOTE KATIKA NYAMA MCHINJAJI KAMA UJIRA
Hairuhusiwi kumlipa mchinjaji aliyewakilishwa kuchinja baadhi ya nyama kama ujira wake kutokana na Hadiyth ifuatayo: 
عن علي قال‏:‏ أمرني رسول الله صلى الله عليه وسلم أن أقوم على بدنه وأن  أتصدق بلحومها وجلدها وأجلتها ‏(‏وأجلتها‏:‏ أي لباسها الذي يقيها البرد‏. )  وأن لا أعطي الجزار منها شيئا، وقال‏:‏ نعطيه من عندنا‏.
Kutoka kwa 'Aliy (Radhiya Alalhu 'anhu):"Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliniamrisha kuchinja? Na kutoa nyama, ngozi na kile kinachomfunika kumhifadhi na baridi kuvitolea sadaqah na nisimpe chochote katika nyama hiyo. ((Tutampa kitu tulichonacho)) [Al-Bukhaariy na Muslim]


Ufafanuzi Zaidi:
Ukichinja AL-HADYI, mchinjaji hapewi katika nyama alioichinja lakini anapewa ujira wake. AL-HADYI ni kuchinja na wewe upo katika Hajj.

Ukichinja UDHWHIYAH, mchinjaji anaweza akapewa katika nyama hiyo aliyoichinja kama sadaka ikiwa ni masikini, na atapewa pamoja na ujira wake. UDHWHIYAH ni kichinjo kwa wale wasiokuwa katika Hajj. Walio katika Hajj kichinjo kinaitwa AL-HADYI. 

MNYAMA MMOJA ANATOSHELEZA FAMILIA NZIMA
Kuchinja mnyama mmoja anatosheleza katika kila familia japo kama kuna watu wengi katika familia kutokana na kauli ya:
  أبي أيوب -رضي الله عنه- لما سئل: كيف كانت الضحايا على عهد رسول الله؟  فقال: "كان الرجل يضحي بالشاة عنه وعن أهل بيته"  (الترمذي)
Abu Ayyuub (Radhiya Allaahu 'anhu) alipoulizwa: "Uchinjaji ulikuwa vipi zama za Mjumbe wa Allaah?" Akajibu: "Mtu alikuwa anachinja kondoo mmoja kwa ajili yake na familia yake" [At-Trimidhiy]


YANAYOMPASA KUFANYA MWENYE KUTAKA KUCHINJA
Baada ya kutia Niya ya kuchinja, asikate mtu nywele wala kucha mpaka amalize kuchinja kama tulivyoamrishwa katika Hadiyth ifuatayo:
عن أم سلمة رضي الله عنها، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال:  (( إذا رأيتم هلال ذي الحجة وأراد أحدكـم أن يضحّي فليمسك عــن شعره وأظفاره))  ، وفي راوية (( فلا يأخذ من شعره ولا من أظفـاره حتى يضحّي  )) مسلم
Imetoka kwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu 'anhaa)    kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  ((Ukiandama mwezi wa Dhul-Hijjah na ikiwa  yuko anayetaka kuchinja basi azuie (asikate) nywele zake na kucha zake))

Na katika riwaya nyingine ((Asikate nywele wala kucha mpaka atakapomaliza kuchinja)) [Muslim na wengineo]
         

MWENYE UWEZO WA KUCHINJA ZAIDI YA MMOJA
Mwenye uwezo wa kuchinja zaidi ya mmoja na akipenda achinje kama alivyochinja Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya Ummah wa Kiislam wote. Hivyo Muislam asiye na uwezo wa kuchinja naye atapata fadhila hizi za kuchinja, naye mchinjaji atachuma thawabu za Waislam wote wasio na uwezo. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya hivyo:
وعن أبي رافع رضي الله عنه «أن النبي صلىالله عليه وسلّم كان يضحي  بكبشين أحدهما عنه وعن آله، والاخر عن أمته جميعاً»، رواه أحمد
Kutoka ka Abu Raafi' (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba:  Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akichinja kondoo wawili; mmoja kwa ajili yake na familia yake na wa mwengine kwa ajili ya Ummah wake wote)) [Ahmad]

Kutoka kwa Jaabir kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akichinja kwa ajili ya Ummah akisema:
 (( بسم الله والله أكبر. اللهم هذا عني وعمن لم يضح من أمتي))  رواه أحمد وأبو داود والترمذي.
((BismiLLaah, wa Allaahu Akbar, Ee Allaah hii kwa ajili yangu na kwa ajili ya wasio na uwezo katika Ummah wangu)) [Ahmad, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy]
 

 *******************************************

MAAJABU YA MAJI YA ZAM ZAM

Utafiti wa maji uliofanywa na Tariq Hussain,
Mhandisi wa kutoa chumvi katika maji
Imefasiriwa na Ummu Ummu Ayman

Tumekuja hapa tena kutekeleza Umrah, na nimekumbushwa na maajabu ya Zamzam.
Kisima cha Zamzam ni kisima ambacho Allaah amekichimbua huko Makkah kwa ajili ya mke wa Mtume Ibraahiym na kwa mtoto wake mkubwa Ismail, (amani iwe juu yao wote). Niruhusu nirudi nyuma kuona mambo yalianzaje. Katika mwaka 1971, Daktari wa kimisri aliandika katika European Press, barua inayosema kuwa maji ya Zamzam hayafai kwa matumizi ya kunywa.
Kwa haraka nilifikiria kuwa hii ilikuwa ni aina ya njama dhidi ya Uislam na kuwa kwa kuwa hoja zake ziliegemea katika dhana ya kuwa kwa kuwa Ka’abah ni pahala pafupi (chini ya usawa wa bahari) na ipo katikati ya mji wa Makkah, maji machafu ya mji yanayojikusanya katika mitaro yanaangukia katika kisima cha maji hayo (yaani Zamzam).
Kwa bahati njema, habari hii ilimfika  Mfalme Faysal ambae alikasirika sana na kuamua kupingana na maneno ya uchokozi ya Daktari huyo wa kimisri. Haraka aliamrisha Wizara ya Kilimo na Raslimali ya Maji kuchunguza na kupeleka sampuli za maji ya Zamzam katika maabara za Ulaya kwa ajili ya kuchunguza ubora wa maji hayo.
Wizara baaadae iliielekeza Jeddah Power and Desalination Plants kuifanya kazi hii. Hapo ndipo nilipoajiriwa kama mhandisi wa utoaji wa chumvi majini (mhandisi wa kemikali katika uzalishaji wa maji ya kunywa kutoka katika maji ya chumvi). Nilichaguliwa kuifanya kazi hii.
Kufikia hapo, nakumbuka kuwa sikuwa na fununu yoyote kuhusu kilivyo kisima chenye maji. Nilikwenda Makkah na kuripoti kwa viongozi wa wahusika ili kuelezea madhumuni ya ziara yangu. Walinitengea mtu maalum kunipa msaada wowote ule utaohitajika.
Tulipofika kisimani, ilikuwa vigumu kwa mimi kuamini kuwa, bwawa la maji kama kidimbwi kidogo, kama futi 18 kwa 14, ndio kisima chenye kutoa mamilioni ya magaloni ya maji kila mwaka kwa mahujaji tokea kilipoanza wakati wa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam), karne nyingi zilizopita.
Nilianza uchunguzi wangu na kuchukua vipimo vya kisima hicho. Nilimtaka yule mtu anioenyeshe kina cha kisima hicho. Kwanza alikoga na kuzamia katika maji. Kisha akasimama sawa sawa. Niliona kuwa kina cha maji kimefikia kiasi cha usawa wa mabega yake. Urefu wake ulikuwa  kama futi tano na nchi 8. Kisha akaanza kwenda kutoka kona moja hadi nyengine ndani ya kisima (akiwa amesimama wakati wote kwani hakuruhusiwa kuzamisha kichwa chake ndani ya maji) akijaribu kutafuta paipu inayoingiza maji kisimani ili kuona maji hayo yanakotokea. Hata hivyo, mtu huyo aliripoti kuwa hakuweza kuipata paipu yoyote ndani ya kisima hicho.
Nikapata mawazo mengine. Maji yanaweza kutolewa kwa haraka kwa kutumia pampu kubwa iliyokuwa imewekwa kwa ajili ya kujaza tangi la maji ya Zamzam.  Kwa njia hii, kina cha maji kitapungua na kutuwezesha kupata sehemu yanayoingilia maji. Kwa mshangao, hakuna kilichoonekana wakati wa kuyavuta maji, lakini nilijua kuwa hii ndio njia pekee ya kuweza kuipata sehemu ya kuingilia maji katika kisima. Kwa hivyo niliamua kurejea tena njia hiyo. Lakini mara hii nilimuelekeza yule mtu atulie pahala pamoja na aangalie kwa uangalifu chochote kitachojitokeza ndani ya kisima ambacho si cha kawaida.
Baada ya muda, ghafla alinyanyua mkono wake na kusema kwa nguvu, Alhamdulillah! Nimepaona! Mchanga unacheza cheza chini ya miguu wakati maji yanachimbuka katika sehemu ya chini ya kisima”.
Kisha alikizunguka kisima wakati wa kuvutwa maji na akahisi vile vile katika kila sehemu ya chini ya kisima. Ukweli ni kuwa uchimbukaji wa maji katika kila pahala ulikuwa sawa sawa, kwa hivyo kufanya kina cha maji kiwe kimetulia. Baada ya kumaliza uangalizi wangu nilichukua sampuli za maji kwa ajili ya uchunguzi katika maabara za Ulaya. Kabla ya kuondoka Ka’abah, Niliwauliza wahusika kuhusu visima vyengine vya Makkah. Niliambiwa kuwa visima hivyo karibu vyote vimekauka.
Nilipofika ofisini kwangu Jeddah niliripoti ugunduzi wangu kwa mkuu wangu ambae alinisikiliza kwa hamu kubwa lakini akatoa maoni yake yasiyopendeza kuwa kisima cha Zamzam kumeungana chini kwa chini na Bahari Nyekundu. Itawezekana vipi wakati Makkah iliyo kilomita 75 mbali na bahari, visima vilivyopo kabla ya mji kwa kawaida huwa vikavu.
Matokeo ya sampuli (vielelezo) zilizopimwa katika maabara ya Ulaya na zile ambazo tulizozipima sisi katika maabara yetu yalionekana kuwa karibu ni sawa sawa. Tofauti baina ya maji ya Zamzam na maji ya visima vyengine (maji ya mjini) yalikuwa ni katika viwango vya chumvi za chokaa (calcium) na magnesi (magnesium). Viwango nya chumvi hizi vilikuwa ni vikubwa kidogo katika maji ya Zamzam. Hii inawezekana ikawa ni sababu ya maji haya huwaondoshea uchovu (kuwachangamsha) mahujaji. Lakini kilichojitokeza zaidi, ni kuwa maji hayo yalikuwa na floridi (fluorides) ambayo inaathiri vijidudu.
Zaidi ya hayo, maelezo ya maabara za Ulaya yalionyesha kuwa maji hayo yanafaa kwa kunywa. Kwa hivyo maneno yaliyowekwa na Daktari wa Kimisri yalishuhudiwa kuwa ni ya uongo.
Yaliporipotiwa mambo hayo kwa Mfalme Faysal alifurahi mno na akaamrisha tofauuti za kupingana kati ya ripoti hizo zitolewe katika jarida la European Press.
Kwa njia hiyo, imekuwa ni baraka kuwa uchunguzi huo ulifanyika ili kuonyesha kemikali zilizomo katika maji hayo. Kwa kweli, kadri unavyopekuwa zaidi, ndivyo maajabu yake yanavyojitokeza zaidi na unajikuta mwenyewe unaamini kikamilifu miujiza ya maji hayo ambayo Allaah Amejaalia kuwa zawadi kwa wacha Mungu wanaokuja katika ardhi yenye jangwa kutoka masafa ya mbali kwa ajili ya hija.
Niwache nifupishe baadhi ya maumbile ya maji ya Zamzam
·  Kisima hichi hakijawahi kukauka. Na badili yake daima kimekuwa kinatosheleza mahitaji ya maji.

·  Daima kiwango chake cha chumvi na ladha kinabaki sawa sawa tokea kimekuwepo.

·  Ubora wake kwa kunywa daima  umetambuliwa kimataifa kwa vile mahujaji kutoka duniani kote wamekuwa wakiitembelea Ka’abah kila mwaka kwa ajili ya Hijja na Umra, lakini hakuna alielalamika kuhusu ubora huo. Badili yake, wamekuwa daima wakiyafurahia maji hayo ambayo yanawaondoshea uchovu.

·  Maji huwa na ladha tofauti katika pahala tofauti. Kupendwa kwa maji ya Zamzam kumekuwa ni kwa kimataifa.

·  Maji haya hayajawahi kutibiwa kwa kemikali yoyote au kutiwa klorini kama ilivyo kawaida ya maji yanayopelekwa mijini. Kuota kwa njia ya kibaiolojia (biological growth) vimelea na majani ni kawaida katika visima karibu vyote. Hii inasababisha maji kuwa si mazuri (kwa kunywa) kutokana na kuota kwa mwani (algae) unaoharibu  ladha na harufu. Lakini katika kesi ya kisima cha Zamzam, hakuna dalili yoyote ya kuota kwa vitu hivyo.

·  Karne nyingi zilizopita, Bibi Hajra (‘Alayhas Salaam) alitafuta kwa mfadhaiko maji katika vilima vya Swafaa na Marwa ili kumpa mtoto wake aliekuwa ndio kwanza anazaliwa Nabii Isma’iyl (‘Alayhis Salaam). Alipokuwa anakimbia huku na kule kutafuta maji, mtoto wake alipiga piga miguu yake chini mchangani. Bwawa la maji likachimbuka, kwa rehma za Allaah, yakajifanya kuwa kisima ambacho kimekuja kuitwa Maji ya Zamzam.


**********************************************************************************

Makosa Ya Mahujaji




Tawakkal Juma Husayn


YAJUE MAKOSA MBALIMBALI YAFANYIKAYO KATIKA IBADA YA HIJJA

Sifa zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, na Rehema na Amani zimwendee kipenzi chetu Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) Muhammad na wakeze na sahaba zake na watakaowafuata kwa wema hadi siku ya mwisho, wabaad.

Ndugu yangu katika Uislamu unayekusudia kufanya ibada ya Hijja mwaka huu;

Awali ya yote yakupasa umshukuru Allaah kwa kukupa Tawfiyq ya kuiendea nyumba yake tukufu na kongwe iliyoko Makkah ili kuitimiza nguzo hii ya tano ya Uislamu. Hongera, lakini angalia kuwa ibada ya Hijja siku hizi imetawaliwa sana na makosa ya kinamna ya kuyafanya matendo mbalimbali ya ibada hii. Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kawaamuru watu wachukue matendo na ibada ya Hijja kutoka kwake.

Katika makala hii nakutahadharisha juu ya makosa mbalimbali ya Hijja ambayo hupunguza thawabu na tija ya ibada hii tukufu.


IHRAMU NA MAKOSA YAKE

Imethibiti katika Sahihul Bukhari na Muslimu kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) amewapangia waislamu wa sehemu na pembe mbalimbali za dunia sehemu zao za kuhirimia wanapotaka kufanya ibada ya Hijja au Umrah. Sehemu hizo ni kama zifuatazo:

1.    Dhul Hulayfah kwa watu wa Madiynah
2.    Juh’fa kwa watu watokao Shamu
3.    Qarnul Manaazil kwa watu wa Najd
4.    Yalamlam kwa watu watokao Yemen

Kisha akasema: “Sehemu hizo ni kwa ajili ya wakazi wa sehemu hizo na kwa ajili pia ya wapitao sehemu hizo wasiokuwa wakazi wa sehemu hizo miongoni mwa wanaotaka kufanya ibada ya Hijja au ‘Umrah”. Kwa maana kuwa wewe mfano unatoka Afrika Mashariki sehemu yako ya kuhirimia ni Yalamlam kama unaelekea Makkah moja kwa moja, lakini ikiwa mathalani unakwenda Madiynah kwanza kwa ajili ya kuzuru Msikiti wa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kama ilivyo kwa misafara yetu mingi ya Hijja ndiyo baadaye uje uende Makkah kwa ajili ya Hijja hapo sehemu yako ya kuhirimia itakuwa ni ile ya watu wa Madiynah yaani Dhul Hulayfah na si ile ya kwako ya kawaida uliopangiwa yaani Yalamlam.

Kimsingi sehemu hizi ameziweka Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) na ni mipaka ya kishari’ah haifai kuiruka pasina kuhirimia wala haifai kuibadili kwa yeyote anayetaka kufanya ibada ya Hijja au ‘Umrah. Mwenye kwenda kuhiji anatakikana kuhirimia katika sehemu hizi ni mamoja awe anasafiri kwa njia ya nchi kavu, bahari au anga. Kwa bahati nzuri vyombo vya anga siku hizi huwatangazia Mahujaji kuwa sasa wamefika katika eneo la kuhirimia au Miyqaat. Na ni lazima Mahujaji wahirimie kabla ya kulipita eneo hilo. Ila ikiwa Mahujaji wanasafiri kwa ndege yawapasa wafanye haraka sana katika kuhirimia kwa kuwa, kwa mwendo kasi wake ndege huchukua muda mfupi sana kulipita eneo la Miyqaat au la kuhirimia.

Kosa hapa ni kuwa baadhi ya Mahujaji wanaokwenda moja kwa moja Makkah badala ya kuhirimia katika sehemu hizo wakiwa katika ndege au katika usafiri wowote walionao na si kusubiri hadi wateremke uwanja wa ndege wa Jiddah ndipo wahirimie. Haya ni makosa na ni kukhaalifu amri ya Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama). Ni juu ya viongozi wa Hijja kuweka wazi kama wanakwenda moja kwa moja Makkah au wanapitia kwanza Madiynah ili watu wajue wanatakiwa kuhirimia wapi. Kimsingi kosa hili linapotokea hadi anayekwenda kuhiji akawa ameshuka kiwanja cha ndege cha Jiddah ni juu ya Hujaji huyo kurudi hadi sehemu yake ya kuhirimia kama ataweza la sivyo Wanachuoni wengi wanaonelea kuwa analazimika atoe fidia ya kuchinja mnyama akifika Makkah na awagawie masikini wa Makkah wala hataruhusiwa yeye kumla mnyama huyo wala kuwapa matajiri kwa kuwa ni mnyama wa kafara ambaye anatakikana aliwe na masikini tu.


MAKOSA YA KIVITENDO YANAYOAMBATANA NA KUTUFU AU KUZUNGUKA AL-KA’ABAH.

Ilivyothibiti ni kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) alianza kuzunguka Al-Ka’abah akianzia katika sehemu lilipo jiwe jeusi au Hajarul Aswad katika nguzo inayoitwa Ruknul Yamaani. Pia imethibiti kuwa aliitufu Al-Ka’abah nje ya eneo linaloitwa Hijr, na pia  alikwenda mwendo wa haraka kidogo sawa na kukimbiakimbia pasina kunyanyua miguu sana. Mwendo huu unaitwa Raml na ilikuwa ni katika mara tatu tu za kwanza za kuizunguka Al-Ka’abah pale alipoingia Makkah na pia alikuwa wakati akitufu akiashiria, akiligusa jiwe jeusi na kulibusu na pia imethibiti kuwa aliishiria jiwe kwa Miijani naye akiwa katika mnyama wake na akawa anaibusu Miijani au fimbo yake hiyo na akawa kila akipita pahala pa jiwe anashiria kwa mkono wake na pia imethibiti kuwa alikuwa akiigusa Ruknul Yamaani kwa mkono wake.

Kimsingi kinamna na kisifa pana utofauti katika sifa na namna ya kufanya unapokuwa umefika sehemu ya Hajarul Aswad au jiwe jeusi, na hii inaashiria kuwa paangaliwe wepesi, ikiwa mtu itamuwia wepesi hadi kulifikia jiwe jeusi pasina mikiki basi na alishike na kulibusu. Pia ifahamike kuwa kuliashiria au kulishika na kulibusu si kwa jingine zaidi ya kumwabudu Allaah na kumtukuza wala si kwa kuitakidi kuwa jiwe hilo linadhuru au linaleta manufaa. Katika Sahihul Bukhari na Muslimu kutoka kwa ‘Umar kuwa yeye alikuwa akilibusu jiwe huku akisema; “Hakika mimi najua kuwa wewe hudhuru wala hunufaishi na lau kama si kumuona Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) akikubusu nisingalikubusu”. Kuna makosa  ambayo baadhi ya Mahujaji hufanya yakiambatana na sehemu hii nayo ni;

1.    Kuanza kuzunguka Al-Ka’abah kabla ya kufika sehemu ya jiwe jeusi, na kwa sasa kuna alama ya mstari maalumu inayoonyesha lilipo jiwe jeusi na kama ni usiku kuna taa ya rangi maalumu taa ya kijani yenye kuonyesha lilipo jiwe jeusi. Kuanza kuzunguka Al-Ka’abah kabla ya kufika lilipo jiwe jeusi aidha ni kutokujua au ni Mubalaa katika dini na ni kama kama kutanguliza kufunga Swawm ya Ramadhaan kwa kuanza kufunga siku mbili kabla. Baadhi ya Mahujaji hudai kuwa wao wanafanya hivi ili wasije wakakosea. Madai haya hayakubaliki kishari’ah kwani tunatakiwa tumfuate Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) haki ya kumfuata wala haifai kutanguliza kauli au kitendo mbele ya Allaah na Mtume Wake.

2.    Kutufu ndani ya eneo linaloitwa Hijr kutokana na msongamano mkubwa wa watu. Kimsingi hili ni kosa kubwa kwa kuwa eneo la Hijr kishari’ah liko ndani ya Al-Ka’abah na tawafu inatakiwa iwe nje ya Al-Ka’abah na sio ndani ya Al-Ka’abah. Kwa hiyo kwa kupita ndani ya Hijr unapotufu unakuwa umetufu katika sehemu ya Al-Ka’abah na si Al-Ka’abah yote ambayo ndiyo inayotakiwa.

3.    Kukimbia kimbia katika Tawafu zote saba.

4.    Kusongamana na kupigana vikumbo kwa ajili ya kulifikia jiwe jeusi ili kulibusu, jambo ambalo mara nyingine husababisha watu kurushiana matusi na hata kupigana na kwa kufanya hivyo wakawa wanaivunjia heshima nyumba tukufu ya Allaah. Kutufu kwa namna hii kunapunguza daraja ya kutufu bali  mara nyingine hata kuipunguza tija ibada nzima ya Hijja. Amesema Allaah: “Hija ni miezi maalumu na anayekusudia kufanya Hijja katika miezi hiyo basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika hiyo Hijja” (2:197). Misongamano kama hii haina ulazima bali inaondoa makusudio makubwa ya kutufu kwa kuondoa unyenyekevu na kumtaja Allaah ambayo ni miongoni mwa makusudio matukufu kabisa ya kutufu.

5.    Itikadi ya baadhi ya Mahujaji kuwa jiwe jeusi linanufaisha au linadhuru kwa dhati yake hivyo utawakuta pindi wanapoliamkua wanajipangusa katika viwiliwili vyao au wanawapangusa watoto wao walionao katika ibada ya Hijja au ‘Umrah. Na yote haya ni kutokana na ujinga na ni upotevu wa wazi. Manufaa na Madhara yanatoka kwa Allaah peke Yake, na imekwishatangulia kauli ya ‘Umar juu ya jiwe jeusi kuwa yeye alisema wakati akilibusu: “Hakika mimi najua kuwa wewe hudhuru wala hunufaishi na lau kama si kumuona Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) akikubusu nisingalikubusu”.

6.    Baadhi ya Mahujaji kung’ang’ania nguzo zote za Al-Ka’abah na mara nyingine wakawa wanazishika kuta zote za Al-Ka’abah na hata mara nyingine kuing’ang’ania sana Al-Ka’abah kwa kila sehemu au wakawa kila wakiigusa Al-Ka’abah wakawa wanajipangusia. Na huu ni ujinga na upotevu wa wazi. Maamkuzi ya jiwe jeusi ambalo liko katika Ruknul Yamaani upande wa Mashariki wa Ka’bah tukufu,  au kuiamkua Ruknul Yamaani ya upande wa Magharibi ni ibada na Utukuzo kwa Allaah (Subhaanahu Wata’ala) hivyo inatupasa tufanye kama vile alivyokuwa akifanya Mtume wetu (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama). Katika kitabu cha Musnad cha Imaam Ahmad kutoka kwa Mujaahid, kutoka kwa Ibn ‘Abbaas  (Allaah Amuwie Radhi yeye na Mzazi wake) kuwa yeye alizunguka Al-Ka’abah akiwa na Mu’aawiyah Allaah amuwie Radhi akawa Mu’aawiyah akiziamkua nguzo zote, Ibn ‘Abbaas akamuuliza Mu’aawiyah kwa kusema; kwa nini unaziamkua nguzo zote wakati Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama)  alikuwa hafanyi hivyo? Mu’aawiyah akasema hakuna cha kuachwa katika nyumba hii tukufu; Ibn ‘Abbaas akamwambia kwa hakika tuna sisi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kiigizo chema, Mu’aawiyah akamwambia hakika umenena kweli.


MAKOSA YA KIMATAMSHI YANAYOAMBATANA NA KUTUFU AU KUZUNGUKA AL-KA‘ABAH

Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kuwa yeye alikuwa akileta Takbira au akisema Allaahu Akbar kila alipolifikia jiwe jeusi; na alikuwa akisema anapokuwa kati ya Ruknul Yamaani na jiwe jeusi; “Rabbanaa Aatinaa fiy Dun’ya hasanatan wafiyl Aakhirati hasanah” (2:201).
Na akasema pia; “Hakika si vingine kumefanywa kutufu Al-Ka’abah, na kuzunguka Swafa na Mar’wa na kutupa mawe Jamaraat kuwa ni kwa ajili ya kusimamisha utajo wa Allaah”.
Miongoni mwa makosa yanayofanywa na baadhi ya watu wanapotufu Al-Ka’abah ni kuwa na du’aa maalumu kwa kila mzunguko, pasina kuomba du’aa nyingine, mpaka mara nyingine hufikia anapomaliza mzunguko kabla ya kumaliza du’aa huiacha du’aa hiyo hata kama limebaki neno moja tu katika du’aa hiyo basi hatolileta maadamu amemaliza mzunguko huo; hivyo atalikata neno hilo moja ili alete du’aa nyingine kwa ajili ya mzunguko mwingine. Na ikiwa atakuwa amekamilisha du’aa kabla ya kukamilisha mzunguko atanyamaza. Haikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kuwa yeye aliweka du’aa maalumu kwa ajili ya kila mzunguko wa Al-Ka’abah. Amesema Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah (Allaah Amrehemu): “Hakuna katika kutufu dhikri (utajo) au du’aa maalumu kutoka kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama); si kwa amri yake wala kauli yake wala mafunzo yake, bali anachotakiwa mtu ni kuomba kwa du’aa mbalimbalimbali na kile kitajwacho na watu wengi kuwa kuna du’aa maalumu hilo za kuzungukia Al-Ka’abah halikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama).” Kwa hiyo basi atakiwalo mtu anayezunguka Al-Ka’abah ni kuomba cha kheri akitamanicho miongoni mwa  kheri za Dunia na Akhera, na amtaje Allaah kwa du’aa yoyote ile iliyothibiti kishari’ah iwe ni Tasbihi au Tahmidi au Tahlili au Takbira au kusoma Qur-aan.

Na miongoni mwa makosa ambayo wanafanya Mahujaji wakati wa kutufu ni kuwa na vijitabu vya du’aa ili waombe kwa du’aa hizo japo hawajui maana yake. Na mara nyingine huwa kuna makosa ya uchapishaji au ya kunakili ambayo hubadili maana nzima ya du’aa hiyo na kuwa mtu badala ya kuomba manufaa akawa anaomba madhara pasina yeye kujua. Lau angeomba mwenye kutufu anachokitaka na anachokijua na akakusudia maana yake ni bora zaidi na hili lina manufaa zaidi na ni ndiko hasa kumuiga Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama)  na kumfuata.

Na miongoni mwa makosa yanayotokea wakati wa kutufu ni watu au kikundi cha watu kuwa chini ya mtu mmoja mwenye kuwaimbisha du’aa mbalimbali kwa sauti ya juu na wengine wakawa wanaitikia hivyo zikawa sauti ziko juu na ikawa ni vurugu mtindo mmoja, jambo ambalo hutokea kuwapa tashwishi Mahujaji wengine na wakawa wanashindwa waseme nini. Na hili huondoa unyenyekevu na kuleta maudhi kwa waja wa Allaah katika pahala hapa patukufu. Ilishawahi kutokea kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) aliwatokea watu fulani waliokuwa wakiswali na huku kila mmoja akisoma kwa sauti, akasema Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama): “Kila mmoja wenu anamnong’oneza Mola wake, basi msidhihirishiane sauti” (Imepokewa na Imaam Maalik katika kitabu chake cha Muwatwwaa). Ni uzuri ulioje lau huyu muongozaje wa watu Hijja angeliwatangulia watu wake na akawaambia fanyeni hivi au vile, ombeni kimya kimya kadri mtakavyo na akawa akitembea nao ili asipotee mmoja wao na kwa kufanya hivyo wakatufu kwa unyenyekevu na utulivu huku wakimuomba Mola wao kwa kuogopa na kutumai wanachokipenda na wanachokijua maana yake na hivyo watu wengine wakawa wamesalimika na maudhi yao.


MAKOSA YANAYOFANYIKA KATIKA RAKAA MBILI BAADA YA KUTUFU

Imethibiti kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kuwa alipomaliza kutufu alielekea Maqaamu Ibraahiym kisha akasoma sehemu ya Aayah ya 125 ya Suratul Baqarah. “Wattakhidhuu min maqaami Ibraahiyma muswallaa”. Kisha akaswali Rakaa mbili nyuma ya Maqaamu Ibraahiym. Akasoma katika Rakaa ya kwanza Alhamdu (Suratul Faatihah) na Qul yaa ayuuhal kaafiruna (Suratul kaafiruna), na katika Rakaa ya pili akasoma Alhamdu (Suratul Faatihah) na Qul HuwAllaahu ahad (Suratul Ikhlaas).

Na miongoni mwa makosa ambayo baadhi ya watu huyafanya ni ile dhana yao kuwa ni lazima kuswali Rakaa hizo mbili karibu na sehemu ya Maqaamu, jambo ambalo huwapelekea kusababisha misongamano, kulundikana, kuudhiana na hata watu wengine wanaozunguka Al-Ka’abah kukosa njia ya kupitia. Kimsingi Rakaa hizi mbili baada ya mtu kumaliza kutufu zinaweza kuswaliwa sehemu yoyote katika Msikiti wote wa Makkah na pia mwenye kuswali anaweza akaswali nyuma ya Maqaamu hata kwa mbali na hili litamwepusha na maudhi; hatoudhi wala kuudhiwa na ataweza kuswali kwa unyenyekevu zaidi na utulivu.

Na miongoni mwa makosa vile vile ni kule baadhi ya wanaoswali nyuma ya Maqaamu Ibraahiym baada ya kumaliza kutufu kuswali zaidi ya Rakaa mbili pasina sababu yoyote hali wanajua kuwa kuna ndugu zao wamemaliza kuzunguka Al-Ka’abah nao wanataka kuja kuswali hapo.

Na miongoni mwa makosa vile vile ni kule baadhi ya wenye kutufu wanapomaliza kutufu kiongozi wao huwasimamisha akawa akiwaombea kwa sauti ya juu, wakawa kwa kufanya hivyo wakiwasumbua Mahujaji wengine wanaoswali nyuma ya Maqaamu Ibraahiym na kuwakera. Allaah Amesema; “Muombeni Mola wenu hali ya kunyenyekea na kuogopa, kwa hakika Yeye Hawapendi wenye kuchupa mipaka” (Al ‘Aaraf: 55)


KUSA‘I KATI YA SWAFFAA NA MAR-WA NA MAKOSA YAKE

Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kuwa alipokuwa akikaribia Swaffaa alikuwa akisoma:
“Inna Sswafaa wal Mar-wata min sha‘aairi LLaah” (2:158).
Kisha akapanda kilima cha Swaffaa hadi akawa anaiona Al-Ka’abah hapo huielekea na kunyanyua mikono yake akimhimidi Allaah na akiomba atakacho, akimpwekesha, akimtukuza na akisema: “Laa ilaaha illa Llaahu wahdahu laa shariyka lahu, lahul Mulku walahul Hamdu wa Huwa ‘alaa kulli shay’in Qadiyru, laa ilaaha illa Llaahu Anjaza wa‘adahuu, wa Naswara ‘Abdahu, wa Hazamal ahzaaba wahdahuu”. Akiyasema maneno hayo mara tatu. Kisha akashuka kutoka katika kilima cha Swaffaa. Kisha akatembea hadi alipofika sehemu ambayo kwa sasa kuna alama mbili za kijani alikimbia kimbia katikati ya alama moja hadi nyingine. Alipofika katika alama ya pili alianza tena kutembea kama kawaida. Na akitoka Mar-wa kuelekea Swaffaa alifanya mithili ya vile alivyofanya alipokuwa akielekea Mar-wa kutoka Swaffaa.

Na miongoni mwa makosa yafanywayo na baadhi ya wenye kusa‘i ni pale wanapopanda Swaffaa au Mar-wa na kuelekea Al-Ka’abah na wakaleta Takbira tatu na wakaashiria Al-Ka’abah kwa vidole vyao kama wafanyavyo wakati wa kuswali kisha baada ya hapo wao hushuka kutoka kwenye Swaffaa au Mar-wa. Na hii ni kinyume na mafundisho ya Mtume wetu Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama).

Na miongoni mwa makosa ya Kusa‘i pia ni kule watu kukimbia sehemu zote za Swaffaa na Mar-wa. Na hili ni kinyume na mwendo wa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kwani yeye alikuwa akikimbia katikati ya alama mbili za kijani tu na sehemu nyingine akawa anatembea tu. Huenda hili linasababishwa ima na ujinga na kutofahamu au mtu kutaka amalize haraka Kusa‘i.


MAKOSA YA KUSIMAMA KATIKA VIWANJA VYA ‘ARAFAH

Imethibiti kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) alikaa siku ya ‘Arafah katika viwanja vya ‘Arafah katika sehemu inayoitwa Namirah. Alikaa hapo hadi wakati wa Adhuhuri. Kisha akapanda mnyama wake hadi alipoteremka na kuswali Adhuhr na Al‘Asr kwa Rakaa mbili mbili kila moja kwa Adhana moja na Iqaama mbili. Kisha akapanda mnyama wake kwa mara nyingine akaenda naye hadi sehemu alipotaka kusimama na hapo akasema: “Nimesimama hapa lakini ‘Arafah yote ni pahali pa kusimama”. Hapo Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama)  akawa akinyanyua mikono yake akiwa ameelekea Qiblah na kuomba hadi hadi Magharibi ikaingia na hapo akaanza kuelekea Muzdalifah.

Na miongoni mwa makosa watu wanyofanya katika viwanja vya ‘Arafah ni;

1.     Kufika mapema katika sehemu viliko viwanja vya ‘Arafah lakini wakawa nje ya Viwanja vya ‘Arafah hadi jua likazama. Kisha wakaondoka kwenda Muzdalifah hali ya kuwa hawajasimama katika Viwanja vya ‘Arafah. Na hili ni kosa kubwa ambalo linapotokea mtu anakuwa ameikosa Hijja kwani kusimama katika viwanja vya ‘Arafah ndiyo nguzo kubwa ya Hijja ambayo Hijja ya mtu haiswihi hadi mtu awe amesimama katika viwanja vya ‘Arafah. Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama)  amesema kuwa: “Hijja ni ‘Arafah, atakayekuja usiku wa baada ya Mahujaji kusimama ‘Arafah lakini kabla ya kuchomoza Alfajiri ya tarehe 10 atakuwa ameidiriki ‘Arafah na Hijja yake itakuwa sahihi”. Na sababu inayosababisha kosa la baadhi ya Mahujaji kutoidiriki ‘Arafa nao wakiwa karibu kabisa na viwanja hivyo ni kule wao kudanganyana wao kwa wao wakadhani kuwa wameshafika katika viwanja vya ‘Arafah kumbe kishari’ah wako nje ya viwanja hivyo vya ‘Arafah. Kimsingi Mahujaji hawana udhuru wa kuikosa ‘Arafah katika mazingira haya kwani kwa sasa kuna Mabango makubwa sana yenye kuonyesha Mipaka ya ‘Arafah kwa Kiarabu, Kingereza na lugha zingine. Yanaonyesha wazi wapi ni ndani ya ‘Arafah na wapi ni nje ya ‘Arafah. Pia kuna watu ambao huwaambia Mahujaji kuwa hapo walipo ni nje ya viwanja vya ‘Arafah kama wako nje ya ‘Arafah kimakosa.

2.     Kuondoka kwao katika viwanja vya ‘Arafah kabla ya kuzama jua. Na hii kosa kubwa tena ni haramu kwa kuwa kufanya hivyo ni kukhalifu amri ya Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama)  kwani yeye Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) alikaa katika viwanja vya ‘Arafah hadi jua likazama na giza likaanza kuingia ndipo akaondoka kuelekea Muzdalifah. Ama kuondoka kabla ya jua kuzama hii ni katika vitendo vya kijahiliya alivyokataza Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama).

3.     Baadhi ya Mahujaji kuelekea Jabal ‘Arafah wakati wa kuomba du’aa hata kama kwa wao kufanya hivyo wanakipa Qiblah mgongo au kinakuwa upande wa kulia au wa kushoto. Na hili ni kinyume na mwendo wa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama), kwani Sunnah wakati wa kuomba du’aa hapo ni kuelekea Qiblah na si Jabal ‘Arafah au kilima cha ‘Arafah.


KUTUPA MAWE NA MAKOSA YAKE

Imethibiti kuwa kutoka kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kuwa yeye alipiga Jamratul ‘Aqabah ambayo ni ya mwisho na inaelekea Makkah. Alipiga mawe na akachinja katika siku ya kuchinja. Akawa analeta Takbira au akisema Allaahu Akbar kwa kila kijiwe alichopiga. Vijiwe vyenyewe vinatakikana viwe saizi ya punje za karanga, kinyume cha hivyo kwa mfano kutupa mawe makubwa ni kuchupa mipaka katika katika dini, jambo ambalo hupelekea watu kuumizana na ni jambo ambalo liliwaangamiza waliokuwa kabla yetu kama alivyosema Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama). Wengine hufikia hadi kuipiga minara ile kwa kanda mbili na mawe makubwa!!!. Huku ni kuchupa mipaka ya Kishari’ah.

Miongoni mwa makosa yanayofanywa na Mahujaji katika kupiga mawe ni;

1.     Baadhi ya watu kuitakidi kuwa ni lazima wachukue vijiwe kutoka Muzdalifah tu. Kwa itikadi yao hiyo wakawa wanajikalifisha na kuzichosha nafsi zao kwa kufanya hivyo. Hufikia hata inapotokea mmoja wao akawa amedondosha jiwe moja kwa bahati mbaya huwa ni mwenye kuhuzunika sana na akawa anawaomba alionao wampe mawe ya ziada waliyonayo kutoka Muzdalifah. Na hili ni jambo ambalo halina mashiko kwani Mtu anaweza kuyachukua mawe hayo kutoka sehemu yeyote ile, bali mtu anaweza kwenda nayo hata kutoka nyumbani kwao alikotoka. 

2.     Itikadi yao kuwa wanapopiga minara ile ya Jamarati wanakuwa wanampiga Shetani. Hivyo mara nyingine utawasikia wakisema kuwa tumempiga Shetani mkubwa au mdogo au tumempiga baba wa Mashetani wakimaanisha ule mnara mkubwa yaani Jamaratul ‘Aqabah na mfano wa hivi. Na mingi ya mifano ambayo haifai katika sehemu hii tukufu. Mara nyingine utawaona wakitupa mawe kwa nguvu sana, kwa vurugu, kelele na mara nyingine hata wakawa wanatukana wanapoipiga minara hiyo na kudhani kuwa wanamtukana Shetani. Mara nyingine hufikia hata wakawa wanavua viatu au wakawa wanaivurumishia minara ile mawe makubwa kabisa tena kwa hasira na kwa kufanya hivyo wakaweza hata mara nyingine kuwaumiza watu wengine. Hiki ni kituko na kichekesho, na kwa hakika chanzo cha mambo haya ya kuchekesha na kuhuzunisha ni watu kuwa na ‘Aqiydah mbovu za kibid’ah na kutokuelewa ibada hizi zinatakiwa zifanywaje.

3.     Kutupa mawe makubwa, viatu na hata miti. Hili ni kosa kubwa na linalokhalifu mafundisho ya Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) ya kauli na vitendo. Kama tulivyokwisha kusema sababu ya mambo haya ni khulluu au kuchupa mipaka katika dini na kuitakidi kuwa wanampiga Shetani hasa badala ya kufanya kama vile Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) alivyoamrisha.

4.     Kuziendea sehemu za kupiga mawe kwa vurugu na papara bila hata kuwahurumia waja wengine wa Allaah, jambo ambalo husababisha maudhi kwa Waislamu wengine na hata mara nyingine kutukanana na kupigana au hata vifo. Hali hii hugeuza sehemu hizi tukufu na kuwa kama sehemu za vurugu, kutukanana na mapambano.

5.     Kuacha kwao kuomba baada ya kutupa mawe mnara wa kwanza na wa pili katika yale masiku yanayoitwa Ayyaamu Ttashriyq au masiku matatu ya kutanda nyama. Ilivyothibiti ni kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) alikuwa pindi akimaliza kupiga mawe minara miwili ya kwanza alikuwa akisimama baada ya kupiga kila mmoja ya minara hii miwili ya mwanzo akielekea Qiblah na kunyanyua mikono yake na kuomba du’aa ndefu. Na miongoni mwa sababu za kuacha watu kufanya hivi ni ujinga au kupupia kwao kutaka kumaliza haraka kupiga mawe kutokana na msongamano wa kutisha. 

6.     Kutupa mawe yote kwa mkupuo mmoja. Na hili ni kosa kubwa sana. Wanachuoni wanasema kuwa ikiwa mtu atatupa mawe yote kwa mkupuo mmoja basi hiyo itahesabiwa kuwa ametupa jiwe moja.

7.     Kuzidisha kwao du’aa wakati wa kutupa mawe, yaani du’aa ambazo hazikuthibiti wakati wa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama)  kama kusema kwao; “Ee Mwenyezi Mungu yajaalie mawe hayo kuwa ni radhi kwako na ni ghadhabu kwa Shetani”. Mara nyingine wao huacha Takbira iliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama). Na haya ni makosa kishari’ah. 

8.     Watu wengine kutaka kutupiwa mawe hata kama hawana udhuru wa kishari’ah. Hii inaweza kuwa ni kwa sababu ya kukwepa zahma na misongamano. Na hili linakuwa ni kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) na alivyoagiza. Linalotakiwa ni kuwa kila mwenye uwezo na afya njema akatupe mawe mwenyewe pasina kuwakilishwa na Mtu. Watu wafahamu kuwa Hijja ni moja kati ya aina za Jihadi ambayo ni lazima mwenye kuhiji akabiliane na tabu mbalimbali na lazima aikamilishe ibada hii kama alivyoamrisha Allaah na Mtume Wake.


MAKOSA YA TWAWAFU YA KUIAGA AL-KA’ABAH (TWAWAAFUL WIDA‘I)

Imethibiti katika Sahihul Bukhari na katika Sahihu Muslimu kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Allaah Amuwie Radhi) kuwa yeye amesema: “Watu waliamrishwa kuwa liwe jambo lao la mwisho wanapotaka kuondoka na kurudi makwao iwe ni kutufu nyumba ya Allaah isipokuwa wanawake walio katika siku zao wamekhafifiwa au kusamehewa hilo”.
Kuhafifishiwa wanawake walioko katika siku zao hapa inamaanisha kuwa wao wanaruhusiwa wakiwa katika hali hiyo ya hedhi kuondoka kurudi makwao ikiwa hakutakuwa na muda wa kutosha kwao kusubiri hadi watwaharike ndipo watufu na kuondoka.

Na miongoni mwa makosa wanayofanya Mahujaji yanayohusiana na ibada hii ya Twawaaful Wida‘i ni:

1.    Kuondoka Minaa wakaenda Makkah na wakafanya Twawaaful Wida‘i kisha wakarudi tena Minaa kumalizia kutupa mawe ndipo baadaye waondoke. Na hili halifai kwa kuwa ni kinyume na alivyofanya Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama). Na hapa utaona inakuwa ni kama kutupa mawe ndiko kumekuwa jambo lake la mwisho kufanya kabla ya kuondoka na hii ni kinyume na alivyoagiza Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kwani kaagiza kuwa jambo la mwisho kwa Mahujaji liwe ni kutufu Twawafu ya kuaga Al-Ka’abah.

2.    Kukaa kwao kitambo Makkah baada ya kutufu Twawafu ya kuaga, jambo ambalo linawafanya wazingatiwe kuwa jambo lao la mwisho walilofanya si kutufu. Na hili pia ni kinyume na amri ya Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kwani Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) alikuwa akifanya Twawaful Wida‘i kisha anaondoka na hivi ndivyo walivyokuwa wakifanya Maswahaba zake. Isipokuwa wanachuoni wameruhusu mtu kubakia kidogo baada ya kuiaga nyumba tukufu kama kuna dharura kubwa kama ya kuingia wakati wa Swalah au kuswalia jeneza au jambo lenye kuambatana na safari yake kama kununua kitu au kusubiri kidogo wenzake. Ama yule ambaye atakaa Makkah baada ya Twawaaful Wida‘i pasina dharura atalazima airudie Twawaafu baadaye.

3.    Kutoka katika milango ya Al-Ka’abah hali ya kuwa wanapiga piga vichogo vyao wakidhani kuwa kwa kufanya hivyo wanaitukuza Al-Ka’abah kumbe wanazua katika dini na hivyo kumaliza ibada hii tukufu kwa kufanya bid’ah.

4.    Kuilekea kwao Al-Ka’abah wakiwa mlangoni wamemaliza kutufu Twawafu ya kuaga na wakawa wanaomba dua zao kama wenye kuiaga Al-Ka’abah. Na jambo hili halikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama).


La lazima ni watu kufanya Ibada kama alivyoagiza Allaah na Mtume wake (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama). Ibada ni Tawqiyfiyah yaani ni mambo ambayo Shari’ah inamlazimu mtu ayafanye kwa jinsi, namna, viwango, na wakati kama ilivyofundishwa na Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) wala haifai kupunguza wala kuongeza mambo. Muislamu unayehiji uliza kama hujui, ni mwiko kufanya ibada kwa mazoea au kubahatisha. Tena kuna watu wazuri zaidi wa kuwauliza haya nao ni wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu vya Makkah na Madiynah kwani wengi wao wanaifahamu vizuri ibada ya Hijja kinadharia na kivitendo.


*********************************************************************************
 TARATIBU ZA HIJJAH;
SHEIKH Muhammad Bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn 
AlhamduliLLaah, Sifa na shukurani zote Anastahiki Mola wa ulimwengu.  Swalah na salaam zimfikie Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم Mtume wa mwisho pamoja na Ahli zake na Maswahaaba zake. 

Hajj ni mojawapo ya aina ya ibada bora kabisa na ni amali tukufu kabisa kwani ni mojawapo ya Fardhi za Kiislamu ambazo Allaah سبحانه وتعالى Amemtuma Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kutuongoza. Dini ya mja wa Kiislamu haikamiliki bila ya Hajj. Ni ibada inayokubaliwa pindi yafuatayo yatahakikishwa:


Mtu ataifanyia bidii ya dhati kuwa ni kwa ajili ya Allaah سبحانه وتعالى Pekee na kwa kutamani Akhera na haitowezekana kufanyika kwa ajili ya kumuonyesha mtu au kwa ajili ya maslahi ya mambo ya dunia.
Inampasa mtu anapotenda ibada yake afuate mfano wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kwa maneno na vitendo na hii haiwezekani kutimia ila kwa kujifunza na kupata elimu ya mafundisho ya Sunnah.
       

AINA ZA HAJJ

Kuna aina tatu za Hajj; Tamattu'u, Ifraad na Qiraan.
TAMATTU'U

Hujaji anavaa Ihraam ya 'Umrah tu wakati wa miezi ya Hajj (anapokwenda Makkah mapema) ambayo inamaanisha kwamba anapofika Makkah atafanya twawwaaf na Sa'ayi ya 'Umrah. Kisha atanyoa au kukata nywele. Siku ya Tarwiyyah ambayo ni siku ya nane Dhul-Hijjah, atavaa nguo zake za Ihraam kwa ajili ya Hajj tu na atatekeleza yote yanayompasa kufanya.

IFRAAD

Hujaji atavaa Ihraam kwa ajili ya Hajj pekee. Atakapofika Makkah atafanya twawwaaf pamoja na Sa'ayi ya Hajj. Hana haja kunyoa au kukata nywele zake kwani hatoki kwenye Ihraam yake. Bali atabakia katika Ihraam mpaka amalize kupiga mawe katika Jamrah Al-'Aqabah siku ya 'Iyd. Anaruhusiwa kuchelewesha Sa'yi yake ya Hajj mpaka amalize twawwaaf ya Hajj.

QIRAAN

Hujaji anavaa Ihraam ya zote mbili; 'Umrah na Hajj au anavaa kwanza Ihraam ya 'Umrah, kisha anatia Nia ya Hajj kabla ya twawwaaf ya Hajj. Wajibu wa anayefanya Ifraad ni sawa sawa na anayefanya Qiraan, isipokuwa tu mwenye kufanya Qiraan inampasa achinje na mwenye kufanya Ifraad haimpasi kuchinja


Aina ya Hajj iliyo bora kabisa katika hizi ni ya Tamattu'u ambayo ndio Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alisisitiza wafuasi wake waitekeleze.

Hata kama Hujaji akitia Nia ya kufanya Qiraan au Ifraad, anaruhusiwa kubadilisha Nia yake kuingia katika Hajj ya Tamattu'u. Na anaweza kufanya hivi hata kama baada ya kufanya twawwaaf na Sa'ayi kwa sababu Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipofanya Twawwaaf na Sa'ayi mwaka wa Hijjah ya Widaa' (Hajj ya kuaga) pamoja na Maswahaba zake, aliamrisha wote ambao hawakuleta mnyama kwa ajili ya kuchinja, wabadilishe nia zao za Hajj na kutia Nia ya 'Umrah, wakate nywele zao, na wavue Ihraam mpaka Hajj. Akasema:

(("لولا أني سقت الهدي لفعلت مثل الذي أمرتكم به))   البخاري

"Ingelikuwa sikuleta mnyama ningelifanya hivyo nilivyokuamrisheni mfanye" [Al-Bukhaariy]  

 
HUU NI MASJIDIN NABAWIYY ULIOPO MADINA NA HII NI SEHEMU YA NJE KAMA INAVYO ONEKANA NYAKATI ZA USIKU.

'UMRAH
Akipenda Hujaji kuwa katika Twahaara ya 'Umrah, akoge kama josho la janaba. Mwanamume atie manukato mazuri kabisa na apake mafuta mazuri kichwani. Hakuna ubaya harufu ikibakia baada ya Ihraam.

Kukoga ili kuingia katika Ihraam ni Sunnah kwa mwanamume na mwanamke pamoja na wanawake wenye hedhi na wale wenye Nifaas (Damu ya uzazi). 
 
Baada ya kukoga na kujitayarisha, Mahujjaaj wote isipokuwa wanawake wenye hedhi au nifaas wataswali Swalah za fardhi inapowadia wakati wake kama kawaida. Na ikiwa sio wakati wa Swalah ya fardhi basi ataswali Raka'ah mbili ambazo ni vizuri mtu kuswali kila anapotia wudhuu.

Atakapomaliza kuswali atasema Talbiyah hii:

لبيك عمرة، لبيك اللهم لبيك، لبيك لا شريك لك لبيك، إن الحمد والنعمة لك والملك لا شريك لك.


Labbayka 'Umrah, Labbayka-Llaahumma Labbayk. Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk. Innal-Hamda Wan-Ni'imata Laka Wal-Mulk Laa Shariyka Lak.

"Nimekuitikia Ee Allaah 'Umrah, Nimekuitika Ee Allaah nimekuitika, nimekuitika Huna mshirika Wako nimekuitika, hakika Sifa njema na Neema na Ufalme ni Vyako Huna mshrika"


Mwanamume atasema kwa sauti na mwanamke atasema kiasi cha kumsikia wa pembezoni mwake. (Wanawake wenzake).

Anatakiwa mtu kusema Talbiyah kila mara khaswa anapofika na kubadilisha kituo. Mfano anapopanda na kushuka kipando wakati wa safari au wakati wa usiku unapoingia na asubuhi kunapopambazuka. Pia Amuombe Allaah سبحانه وتعالى Ridhaa Yake ya kupata Pepo na aombe kujikinga kwa Rahma ya Allaah سبحانه وتعالى kutokana na moto. 

Anatakiwa mtu aseme Talbiyah wakati wa 'Umrah tokea anapovaa Ihraam yake hadi anapoanza Twawwaaf. Wakati wa Hajj aseme Talbiyah kutokea mwanzo wakati anapovaa Ihraam yake mpaka anapoanza kupiga mawe Jamarah ya 'Aqaba siku ya 'Iyd.

Hujaji anapoingia msikitini atangulize mguu wake wa kulia na kusema:

(( أعوذ بالله العَظيـم وَبِوَجْهِـهِ الكَََرِِيـمِ وَسُلْطـانِهِ القََدِيـمِ مِنَ الشّيْـطانِ الرَّجِـيمِ، [ بِسْـمِ الله، وَالصَّلاةُ] [وَالسَّلامُ عَلى رَسولِ الله]، اللّهُـمَّ افْتَـحْ لي أَبْوابَ رَحْمَتـِكَ))

((A'uwdhu BiLLaahil-'Adhwiym, Wa Biwajhihil-Kariym Wa Sultwaanihil-Qadiym Minash-shaytwaanir-rajiym, BismiLLaah Was-Swalaatu Was-salaam 'Alaa Rasuli-LLaah, Allaahuumaf-tah-liy Abwaaba Rahmatik))

 “Najilinda na Allaah  Aliye Mtukufu, na kwa uso Wake, mtakatifu, na kwa utawala Wake wa kale, kutokana na shetani aliyeepushwa na Rahma za Allaah, (kwa Jina la Allaah, na Rahma) (Na amani zimfikie Mtume wa Allaah ) Ee Allaah  nifungulie milango ya Rahmah Zako"

Anakaribia Hajar Al-Aswad (jiwe jeusi) na kuligusa kwa mkono wake wa kulia na kulibusu. Ikiwa hii haiwezekani, basi aelekeze tu uso wake kuelekea kwenye Hajar Al-Aswad na kuashiria kwa mkono wake. (Usibusu mkono wako!) Haifai kusukuma na kusababisha madhara kwake na kwa watu.  

Anapoligusa au kuliashiria Hajar Al-Aswad anatakiwa aseme hivi:

  بسم الله والله أكبر، اللهم إيماناً بك، وتصديقاً بكتابك، ووفاء بعهدك، واتباعاً لسنة نبيك محمد صلى الله عليه وآله وسلم

BismiLLaahi Wa-Allaahu Akbar, Allaahumma Iymaanam-Bik,  Wa Taswdiyqam-Bikitaabik, Wa Wafaa-am-Bi'ahdik, Wat-tibaa'al-lisunnati Nabiyyika Muhammad Swalla Allaahu 'Alayhi Wasallam.

Kwa jina la Allaah, na Allaah ni Mkubwa, Ee Allaah kwa iymani Kwako, na kwa kuamini kitabu Chako, na kwa kutekeleza ahadi yako, na kufuata Sunnah ya Nabii Wako Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم. (Tanbihi: Pamoja na Shaykh kutaja ziada ya du'aa baada ya 'BismiLLaahi Wa-Allaahu Akbar' (Kwa jina la Allaah, na Allaah ni Mkubwa),  maelezo yaliyofuatia pamoja na kwamba yananasibishwa na Maswahaba 'Aliy bin Abi Twaalib, Ibn 'Abbaas na Ibn 'Umar, lakini Wanachuoni wengi wa Hadiyth miongoni mwao Ibn Hajr na Al-Albaaniy wameeleza kuwa hazijathibiti kutoka kwao.)

Mwenye Kuhiji  lazima atembee huku Ka'abah liko kushotoni mwake. Anapofika Rukn Al-Yamaani aiguse lakini asibusu bali atakapokuwa baina yake na Hajar Al-Aswad aseme:



 رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الاَخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ 

((Rabbanaa Aatinaa Fid-Duniyaa Hasanataw-Wafil- Aakiharati Hasanataw-Waqinaa 'Adhaaban-Naar)).

"Mola wetu, Tupe duniani mema, na Aakhirah mema, na Utulinde na adhabu ya Moto"

((اللهم إني أسألك العفو والعافية في الدنيا والآخرة))

Allaahumma Inni As-alukal-'afuw Wal-'aafiyata Fid-Duniyaa Wal-Aakhirah

"Ee Allaah Nakuomba msamaha na 'afya duniani na Aakhirah"

Kila mara akilipita Hajar Al-Aswad anatakiwa aseme "Allaahu Akbar"

Katika kufanya Twawwaaf zilizobakia anaweza kusema anachopenda katika Du'aa, kumtaja Allaah سبحانه وتعالى, kusoma Qur'aan. Hii kwa sababu twawwaaf, Sa'ayi na kupiga mawe Jamrah imekhusiwa kwa ajili ya kumtaja Allaah سبحانه وتعالى .  

Katika Twawwaaf hii anahitajika mwanamume afanye vitu viwili: 


Aweke Al-Idhwtwiba'a kutoka mwanzo wa Twawwaaf mpaka mwisho. Al-Idhwtwiba'a ina maana kwamba ni kuweka sehemu ya katikati ya vazi (ridaa) chini ya kwapa lake la kulia na kipande cha ridaa akipitishe juu ya bega la mkono wa kushoto. Anapomaliza kufanya Twawwaaf anaweza kurudisha ridaa yake katika hali yake ya mwanzo kwa sababu wakati wa Idhwtwiba'a ni wakati wa Twawwaaf tu.


Kufanya Ar-Raml katika Twawwaaf tatu za mwanzo. Ar-Raml ina maana kwamba kuzunguka kwa mwendo wa haraka kwa  hatua ndogo ndogo. Kisha anatakiwa atembee mwendo wa kawaida katika Twawwaaf zake nne za mwisho.
 

Atakapomaliza mizunguko saba ya Twawwaaf, atakaribia Maqaamu Ibrahyim na atasoma:

((وَاتَّخِذُواْ مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى))

((Na alipokuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kuswalia)) [Al-Baqarah: 125]


Ataswali Raka'ah mbili fupi, akiwa karibu kiasi iwezekanavyo na nyuma ya Maqaamu Ibrahiym. Katika Raka'ah ya mwanzo atasoma Suratul-Kaafiruun na Raka'ah ya pili atasoma Suratul-Ikhlaas. Atakapomaliza Raka'ah mbili atarudi kuligusa Hajar Al-Aswad kama itawezekana.   Atakwenda Al-Mas'aa, atakapofika karibu na As-Swafaa atasoma:

((إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَآئِرِ اللّهِ))

((Hakika vilima vya Swafaa na Marwah ni katika alama za Allaah)) [Al-Baqarah: 158]


Atapanda (mlima wa) Swafaa mpaka aweze kuona Ka'abah. Aelekee Ka'abah na anyanyue mikono yake, amtukuze Allaah سبحانه وتعالى na aombe Du'aa apendayo. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliomba:

 لا إِلهَ إلاَّ  اللهُ وَحْدَهُ  لا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ المُلْكُ وَلَهُ الحَمْدُ وهُوَ عَلى كُلِّ شَيءٍ قَديرٌ، لا إِلَهَ إلا اللهُ وَحْدَهُ أَنْجَزَ وَعْدَهُ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ وَهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ

Laa Ilaaha Illa-Allaah Wahdahu Laa Shariyka Lah, Lahul-Mulku Walahul-Hamd Wa Huwa 'Alaa Kulli Shay-in Qadiyr. Laa Ilaaha Illa-Allaah Wahdahu, Anjaza Wa'dahu Wanaswara 'Abdahu Wahazamal-Ahzaaba Wahdahu.

 “Hapana Mola Apasae kuabudiwa kwa haki ila Allaah, hali ya kuwa peke Yake, wala Hana mshirika Wake, ni Wake Ufalme na ni Zake sifa njema Naye juu ya kila kitu ni Muweza.  Hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allaah hali ya kuwa peke Yake, Ametekeleza ahadi Yake, na Amemnusuru mja Wake, na Amevishinda vikosi peke Yake”


Atasema mara tatu akiomba Du'aa baina yake.


Atateremeka As-Swafaa na kuelekea Al-Marwah kwa mwendo wa kawaida mpaka anapofika katika alama ya kijani, hapo atakimbia mpaka alama ya kijani nyingine.  Ataendelea kuelekea Al-Marwah kwa mwendo wa kawaida. Atakapofikia ataupanda (mlima) na kuelekea Qiblah, atanyanyua mikono na kurudia kusema kama alivyosema alipokuwa As-Swafaa. Atateremka Al-Marwah kuelekea As-Swafaa, akihakikisha anatembea sehemu zinazohusika na kukimbia katika sehemu zinazohusika.


Ataendelea kufanya hivyo hivyo mpaka amalize mizunguko saba. Kutoka As-Swafaa kwenda Al-Marwah ni mzunguko mmoja na kurudi ni mzunguko mwingine. Wakati wa Sa'ayi anaweza kusoma anachotaka kama Du'aa, Qur'aan na kumtaja Allaah سبحانه وتعالى.


Anapomaliza Sa'ayi atanyoa nywele. Mwanamke atakata nywele kiasi cha urefu wa ncha ya kidole. Inapendekezeka kunyoa nywele zote, na kunyoa ni bora kuliko kukata kwani Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwaombea du’aa walionyoa mara tatu na waliokata mara moja. Isipokuwa ikiwa Hajj iko karibu na hakuna wakati wa kutosha kwa nywele kurudi kukua, basi ni bora kukata ili nywele zibakie kwa ajili ya kunyoa wakati wa Hajj, kwa sababu Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwaamrisha Maswahaba kukata nywele katika 'Umrah kwani walifanya asubuhi ya tarehe nne ya Dhul-Hijjah.

Baada ya hapo 'Umrah itakuwa imemalizika na Hujaji atakuwa huru kuvaa nguo nyingine, kutia manukato (mwanamume) na kurudia hali ya ndoa (kujimai na mkewe) na kadhalika.




***************

 


HAJJ

Siku Ya Tarwiyyah, Tarehe 8 Dhul-Hijjah 



Siku ya tarehe 8 Dhul-Hijjah, Hujaji atajitoharisha tena kwa kukoga kama alivyofanya kabla ya 'Umrah mahali hapo anapokaa.  Atavaa Ihraam yake na kusema:

 لَبَّيْكَ حَجّاً  لَبَّيْكَ اللَّهُمَّ لَبَّيْكَ ، لا شَرِيكَ لَكَ لَبَّيْكَ ،إنَّ الْحَمْدَ ،وَالنِّعْمَةَ ،لَكَ وَالْمُلْكُ ، لا شَرِيكَ لَكَ  

Labbayka Hajja Labbayka-Allaahumma Labbayk, Labbayka, Laa Shariyka Laka Labbayk, Innal-Hamda Wan-Ni'mata Laka Wal-Mulk, Laa Shariyka Lak

"Nimekuitikia Ee Allaah Hajj, Nimekuitika Ee Allaah nimekuitika, nimekuitika Huna mshirika Wako nimekuitika, hakika Sifa njema na Neema na Ufalme ni Vyako Huna mshirika Wako"


Ikiwa atakhofu kuwa jambo litamzuia kukamilisha Hajj yake basi atie Nia kwa kusema:

 وإن حبسني حابس فمحلي حيث حبستني

"Ikiwa nitazuiliwa na kizuizi chochote sehemu yangu ni popote nilipozuiliwa" 

Ikiwa hana khofu kama hiyo basi hana haja kujishurutisha hivyo.  

Kisha Hujaji atakwenda Mina na huko ataswali Swalah ya Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, 'Ishaa na Al-Fajiri na kufupisha Swalah za Raka'h nne kuwa mbili mbili kila moja bila ya kuziunganisha. (Yaani kuswali kila moja vile kwa wakati wake ila ziwe fupi tu) kwani Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akiswali Qaswran (kufupisha) na sio Jam'an (kujumuisha). 


 
Tarehe 9 Dhul-Hijjah – Siky YA ‘Arafah


Jua litakapochomoza  siku ya pili ambayo ni tarehe 9 Dhul-Hijjah, atakwenda 'Arafah na huko ataswali Adhuhuri na Alasiri kwa kuunganisha wakati wa Adhuhuri na kufupisha mbili mbili. Atabakia katika msikiti wa Namirah mpaka jua litakapokuchwa. Atamkumbuka Allaah سبحانه وتعالى  hapo 'Arafah na kuomba Du'aa nyingi sana awezavyo huku akielekea Qiblah na sio kuelekea Mlima wa 'Arafah.

Ikiwa atakuwa hakujaaliwa kuweko katika msikiti wa Namirah karibu na Jabali la 'Arafah basi popote alipokuweko kwani Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alisimama katika jabali la 'Arafah na akasema:

((وقفت هاهنا وعرفة كلها موقف، وارفعوا عن بطن عرنة))

((Nimesimama hapa na 'Arafah yote ni kisimamo (cha 'Arafah) na msisimame katika bonde la 'Uranah))

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akiomba:

 لا إِلَهَ إلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَريكَ لَهُ، لَهُ المُلْكُ ولَهُ الحَمْدُ وهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَديرٌ.

 Laa Ilaaha Illa-Allaah Wahdahu Laa Shariyka Lah, Lahul-Mulku Walahul-HamdWa Huwa 'Alaa Kulli Shay-in Qadiyr

 “Hapana Mola Apasae kuabudiwa kwa haki ila Allaah hali ya kuwa peke Yake, Hana mshirika Wake, ni Wake Ufalme na ni Zake sifa njema, Naye juu ya kila kitu ni Muweza”

Atakapochoka anaruhusiwa kuzungumza na wenzake au kusoma vitabu vyenye faida khaswa vile kuhusu Ukarimu na zawadi kubwa za Allaah سبحانه وتعالى kwetu ili apate kuzidi kupata matumaini kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى. Kisha arudi kuendelea kuomba Du'aa na kuhakikisha kuwa anatumia wakati wake wa mwisho wa siku hiyo katika Du'aa nyingi na nzito kwa sababu Du'aa zilizo bora kabisa ni Du'aa za siku ya 'Arafah. 

 Muzdalifah

Jua litakapozama ataondoka 'Arafah kwenda Muzdalifah na huko ataswali Magharibi, 'Ishaa na Al-Fajiri Ikiwa atachoka au ana uchache wa maji, anaruhusiwa kuunganisha Magharibi na 'Ishaa.  Ikiwa atakhofu kuwa hatofika Muzdalifah mpaka baada ya usiku wa manane, basi aswali kabla ya kufika huko kwani hairuhusiwi kuchelewesha Swalah mpaka usiku wa manane. 

Atabakia huko Muzdalifah akiomba Du'aa na kumtaja Allaah سبحانه وتعالى mpaka Alfajiri, ataswali Alfajiri mapema kwa adhaan na Iqaamah, kisha ataelekea Mash'aril-Haraam (sehemu tukufu) na atafanya tahliyl, yaani atasema "Laa Ilaaha Illah Allaah"  pia "Allaahu Akbar" na ataomba Du'aa mpaka kupambazuke vizuri. Ikiwa hakujaaliwa kwenda Mash'aril-Haraam, ataomba hapo hapo alipo kutokana na kauli ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

((وقفت هاهنا وجمع كلها موقف)) 

((Nimesimama hapa na kote hapa ni kisimamo (cha Muzdalifah)) [Muslim]

Na atakuwa akiomba Du'aa kwa kuelekea Qiblah na huku akinyanyua mikono. 


      
Minaa – Ar-Ramiy (Kupiga Mawe) Katika Jamrah



Ikiwa ni mtu dhaifu na hawezi kustahamili  zahma za watu wakati wa Ar-Ramiy (kupiga mawe), (kama mwanamke na mtu mzima), basi anaruhusiwa kwenda Mina mwisho wa usiku huo kupiga Jamrah kabla ya zahma ya watu kuwa kubwa.  



Tarehe 10 Dhul-Hijjah



Karibu na jua kuchomoza Hujaji ataondoka Muzdalifah kuelekea Mina. Atakapofika atafanya yafuatayo:



Atatupa mawe saba moja moja katika Jamrah ya 'Aqabah ambayo iko karibu na mnara wa Makkah na kusema :
الله أَكْبَر

Allaahu Akbar

Kwa kila jiwe analotupa.


Atachinja mnyama, na kula baadhi ya nyama na atatoa nyingine kuwapa masikini. Kuchinja ni fardhi kwa wale wanaofanya Hajj ya Tamattu'u na Qiraan. (Kwa hali ilivyo sasa huwa haiwezekani kufanya hivi, hivyo anaweza kutekeleza kama anavyoamrishwa yaani kulipa na kuacha jukumu hili kwa serikali ifanye kazi ya kuchinja) 

  

Atanyoa au kukata nywele. Inapendekezwa kunyoa kuliko kukata (kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika maelezo ya 'Umrah hapo juu). Mwanamke atakata nywele zake urefu wa ncha ya kidole.


Mambo matatu hayo yafanywe kama ilivyo taratibu yake ikiwezekana, lakini hakuna kikwazo au sharti ikiwa mtu atatanguliza kitendo chochote kabla ya chengine.

Akimaliza hayo mambo matatu anaruhusiwa kujitoa katika Ihraam. Na anaweza kuvaa nguo zake za kawaida na kufanya kila jambo la halali ila kuingia katika kitendo cha ndoa.   

Atakwenda Makkah kufanya Twawwaaful-Ifaadhwah na Sa'ayi kwa ajili ya Hajj. Ni Sunnah kujitia manukato kabla ya kwenda Makkah (kwa wanaume) kutokana na kauli ya Bibi 'Aishah رضي الله عنها kwamba:

((كنت أطيب النبي صلى الله عليه وسلم لإحرامه قبل أن يحرم، ولحله قبل أن يطوف بالبيت )) البخاري و مسلم

((Nilikuwa nikimpaka manukato Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kabla ya kuingia katika Ihraam na na baada ya kutoka katika Ihraam kabla ya kutufu Ka'aba)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Atakapomaliza Twawwaaf na Sa'ayi, Hujaji anaruhusiwa kufanya kila kitu kilicho halali hata tendo la ndoa. 




Tarehe 11 na 12 Dhul-Hijjah



Baada ya kufanya Twawwaaf na Sa'ayi atarudi Mina kulala huko usiku wa tarehe kumi na moja na wa kumi na mbili Dhul-Hijjah.

Atarusha mawe Jamrah tatu jioni zote za siku ya tarehe kumi na moja na kumi na mbili Dhul-Hijjah. Ataanza kwanza Jamrah ya kwanza ambayo iko mbali na Makkah, kisha ya katikati, kisha ya mwisho Jamrah Al-Aqabah. 

Katika kila moja ya Jamrah atarusha mawe saba moja moja na huku atasema Takbiyr kwa kila jiwe analorusha.

Atasimama baada ya kurusha mawe Jamrah ya kwanza na ya katikati kufanya Du'aa akielekea Qiblah akiwa amenyanyua mikono na kuomba Du'aa ndefu akiweza kufanya hivyo, au asimame kadiri atakavyoweza. Wala haimpasi kuacha kuomba Du'aa kwani ni Sunnah na watu wengi sana hawatekelezi hivi aidha kwa kutokujua au kupuuza. Na kila inapokuwa Sunnah haitekelezwi huwa kutangazika kwake kwa watu na kutendeka huenda ikaachwa kabisa na kupotea. 
  
Hairuhusiwi kurusha mawe kabla ya Adhuhuri katika siku mbili hizi. 

Ni bora kabisa kutembea kwenda kurusha mawe, ingawa kipando kinaruhusiwa. 

Ikiwa mtu ana haraka baada ya kurusha mawe siku ya kumi na mbili Dhul-Hijjah, anaweza kuondoka Mina lakini iwe kabla ya jua kuzama. Lakini akipenda kuzidisha makazi yake, ambayo ni bora zaidi, basi alale Mina usiku wa kumi na tatu na arushe mawe jioni kama alivyofanya siku ya kumi na mbili.



Twawaaful-Widaa’a (Twaaf Ya Kuaga)


Atakapokuwa tayari kurudi kwao, atafanya twawwaaful-Widaa' ambayo ni mizunguko saba katika Ka'abah kutokana na kauli ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم:

((لا ينفر أحد حتى يكون آخر عهده بالبيت ((مسلم

((Asikimbie mtu (asiondoke zake) mpaka iwe shughuli yake (kitendo chake cha mwisho) katika Nyumba (Ka'abah)) [Muslim]

Wanawake wenye hedhi na nifaas hawana lazima kufanya Twawwaaful-Widaa'i kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:

((أمر الناس أن يكون آخر عهدهم بالبيت إلا أنه خفف عن الحائض)) البخاري و مسلم


((Aliamrisha watu iwe shughuli zao za mwisho ni Ka'abah isipokuwa waliruhusiwa (wanawake) wenye hedhi)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

Ikiwa baada ya twawwaaful-Widaa'i umebakia wakati wa kusubiri wenzake au kipando chake au kununua kitu njiani hakuna neno juu yake, wala hana haja ya kurudia kufanya twawwaaful-Widaa'i isipokuwa akitia Nia ya kuchelewesha safari yake, mfano akitaka kuondoka mwanzo wa siku akatufu Ka'abah, kisha akachelewesha safari yake hadi mwisho wa siku, basi itamlazimu arudie kufanya Twawwaaf ili kiwe kitendo chake cha mwisho ni Ka'abah.



****************




Kutemebele Msikiti Wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم)  




Mwenye kuhiji atakwenda Madiynah kabla au baada ya Hajj kwa Nia ya kutembelea msikiti wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na kuswali humo na sio  kwa nia ya kutembelea kaburi kutokana na Hadiyth ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم:

((لا تشد الرحال إلا إلى ثلاثة مساجد: المسجد الحرام، ومسجدي هذا، والمسجد الأقصى)) البخاري ومسلم

((Msifanye ziara ila kwa misikiti mitatu; Masjidul-Haraam [wa Makkah], na Msikiti wangu [wa Madiynah], na Masjidul-Aqswaa [wa Palestina])) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Swalah moja humo ni bora kuliko Swalah elfu mahali pengine isipokuwa msikiti wa Makkah.


Anapofika msikitini atatanguliza mguu wa kulia na kusema:

 أعوذ بالله العَظيـم وَبِوَجْهِـهِ الكَرِيـمِ وَسُلْطـانِهِ القَدِيـمِ مِنَ الشّيْـطانِ الرَّجِـيمِ،[ بِسْـمِ الله، وَالصَّلاةُ] [وَالسَّلامُ عَلى رَسولِ الله]، اللّهُـمَّ افْتَـحْ لي أَبْوابَ رَحْمَتـِكَ

A'uwdhu BiLLaahil-'Adhwiym, Wa Biwajhihil-Kariym Wa Sultwaanihil-Qadiym Minash-shaytwaanir-rajiym, BismiLLaahi Wasw-Swalaatu Was-Salaam 'Alaa Rasuli-LLaah, Allaahuumaf-tah-liy Abwaaba Rahmatik.

 “Najilinda na Allaah  Aliye Mtukufu, na kwa uso Wake, mtakatifu, na kwa utawala Wake wa kale, kutokana na shetani aliyeepushwa na Rahma za Allaah, (kwa Jina la Allaah na Rahmah) (Na amani zimfikie Mtume wa Allaah) Ee Allaah  nifungulie milango ya Rahmah Zako"

Anatakiwa aswali Raka'ah mbili za Sunnah ya kuamkia msikiti au aswali Swalah za fardhi ikiwa ameingia katika wakati wake.


Atakwenda katika kaburi la Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na atasimama mbele yake, atamsalimia kwa kusema:

 السَّلاَمُ عَلَيْكَ أَيُّها النَّبِيُّ وَرَحْمَةُ اللَّهِ وَبَرَكَاتُه  

Amani zishuke juu yako ee Mtume na rehema za Allaah na baraka Zake

 اللّهُـمَّ صَلِّ عَلـى مُحمَّـدٍ  وَعَلـى آلِ مُحَمَّد كَمـا صَلَّيْـتَ عَلـى آلِ إبْراهـيم  وَعَلـى آلِ إبْراهـيم إِنَّكَ حَمـيدٌ مَجـيد

   اللّهُـمَّ  بارِكْ عَلـى مُحمَّـدٍ  وَعَلـى آلِ مُحَمَّد  كَمـا بارِكْتَ عَلـى  إبْراهـيم وَعَلـى آلِ إبْراهـيم  إِنَّكَ حَمـيدٌ مَجـيد

Allaahumma Swalliy 'Alaa Muhammad Wa 'Alaa Aali Muhammad Kamaa Swallayta 'Alaa Ibraahiym Wa 'Alaa Aali Ibraahiym Innaka Hamiydum-Majiyd. 

Allaahumma Baarik 'Alaa Muhammad Wa 'Alaa Aali Muhammad Kamaa Baarakta 'Alaa Ibraahiyma Wa 'Alaa Aal Ibraahiym Innaka Hamiydum-Majiyd.

“Ee Allaah  Mrehemu Muhammad,  na aila ya Muhammad  kama Ulivyomrehemu Ibraahiym na aila ya Ibraahiym hakika Wewe Umesifika na Umetukuka"

"Ee Allaah Mbariki  Muhammad, na aila ya Muhammad,  kama ulivyombariki Ibraahiym na aila ya Ibraahiym, hakika Wewe Umesifika na Umetukuka.

أشْهَد أنَّكَ رَسُولُ الله حَقاً، وَأنَّكَ قَدْ بَلَّغْتَ الرِّسَالَةَ، وَأدَّيْتَ الأَمَانَةَ، وَنَصَحْتَ الأُمَّةَ، وَجَاهَدْتَ فِي اللهِ حَقَّ جِهَادِه، فَجَزاكَ اللهُ عَنْ أُمَّتك أَفْضَل ما جَزَى نَبِيَّا عَنْ أُمَّتِه.

Ash-hadu Annaka Rasuulu-Allaah Haqqan, Wa Annaka Qad Ballaghtar-Risaalat, Wa Addaytal-Amaanah, Wa Naswahtal-Ummah, Wa Jaahadta Fiy-Llahi Haqqa Jihaadih, Fa-Jazaaka-Allaahu 'An Ummatika Afdhwal Maa Jazaa Nabiyyan 'An Ummatih

"Nashuhudia kwamba wewe hakika ni Mjumbe wa Allaah, Na kwamba umefikisha ujumbe, na umefikisha amana. Na umenasihi Ummah, na umefanya jihaad kwa njia ya Allaah ipasavyo hakika, basi Allaah Akulipe kwa Ummah wako bora kuliko Alivyomlipa Mtume (yeyote) kwa Ummah wake"

Kisha atasogea hatua moja au mbili upande wa kulia kujiweka mbele ya Abu Bakar na kumsalimia kwa kusema :

 السَّلاَمُ عَلَيْكَ
Assalaamu 'Alayka

"Amani zishuke juu yako"

Na akipenda amuombee Du'aa munaasib kama kusema:

رَضِيَ اللَّهُ عَنْكَ وَجَزَاكَ اللَّهُ  عَنْ أُمَّة مُحَمَّد  أَفْضَل جَزَاء

Radhiya-Allaahu 'Anka Wa Jazaaka-Allaahu 'An Ummati Muhammad Afdhwal Jazaa

"Allaah Aridhike na wewe na  Akulipe malipo bora kwa niaba ya Ummah Wa Muhammad" 

Kisha asogee hatua moja au mbili upande wa kulia kidogo na kuelekea kwa 'Umar na kumsalimia kwa kusema:

السَّلاَمُ عَلَيْكَ

Assalaamu 'Alayka

"Amani zishuke juu yako"

رَضِيَ اللَّهُ عَنْكَ وَجَزَاكَ اللَّهُ  عَنْ أُمَّةَ مُحَمَّد  أَفْضَل جَزَاء

Radhiya-Allaahu 'Anka Wa Jazaaka-Allaahu 'An Ummati Muhammad Afdhwal Jazaa

"Allaah Aridhike na wewe na  Akulipe malipo bora kwa niaba ya Ummah Wa Muhammad"

Haifai mtu kujikurubisha kwa Allaah سبحانه وتعالى kwa kugusa ukuta wa chumba cha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  au kufanya twawwaaf (kuzunguka). Pia haelekei mtu huko bali anaelekea Qiblah wakati wa kuomba Du'aa.  Kwa sababu kujikurubisha kwa Allaah سبحانه وتعالى  haiwi ila kama Alivyotuwekea sheria Yeye pamoja na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم, na ibada zinatakiwa zifuatwe sio zianzishwe.

Na mwanamke haimpasi kuzuru kaburi la Mtume صلى الله عليه وآله وسلم wala kaburi la yeyote mwingine kwa sababu Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amelaani wanawake wanaozuru makaburi. Lakini aswali na kumsalimia mahali hapo hapo alipo kwani zinamfikia salamu kama alivyosema:

)) صلوا علي فإن صلاتكم تبلغني حيث كنتم" وقال: "إن لله ملائكة سياحين في الأرض يبلغوني من أمتي السلام((  النسائي و أحمد

((Niswalieni kwani Swalah zenu zinanifikia popote mlipo. Na akasema: ''Hakika Allaah Anao Malaika wanazunguka katika ardhi na kunitumia salamu kutoka kwa ummah wangu'')) [An-Nasaaiy na Ahmad]


Akiwa Katika hali ya Twahaarah atakwenda kuswali katika msikiti wa Qubaa.


Atakwenda Al-Baaqiy'i kutembelea kaburi la 'Uthmaan رضي الله عنه atasimama mbele yake na kumsalimia kwa kusema:

السَّلاَمُ عَلَيْكَ
Assalaamu 'Alayka

"Amani zishuke juu yako"

رَضِيَ اللَّهُ عَنْكَ وَجَزَاكَ اللَّهُ  عَنْ أُمَّةَ مُحَمَّد  أَفْضَل جَزَاء

Radhiya-Allaahu 'Anka Wa Jazaaka-Allaahu 'An Ummati Muhammad Afdhwal Jazaa

"Allaah Aridhike na wewe na  Akulipe malipo bora kwa niaba ya Ummah Wa Muhammad" 

Kisha atawasalimia Waislamu wengine waliofariki waliopo hapo makaburini Al-Baaqiy'i kwa kusema:

السَّلامُ عَلَـيْكُمْ أَهْلَ الدِّيارِ مِنَ المؤْمِنيـنَ وَالْمُسْلِمينَ، وَإِنّا إِنْ شاءَ اللهُ بِكُـمْ لاحقون، ( وَ يَرْحَمُ اللَّهُ الْمُسْتَقْدِمِينَ مِنَّا وَالْمُسْتَأْخِرِينَ) نَسْـاَلُ اللهَ لَنَـا وَلَكُـمُ العَـافِيَةَ.

Assalaamu 'Alaykum Ahlad-Diyaari Minal-Muuminiyna Wal-Muslimiyn, Wa Insha-Allaah Bikum Laahiquun, Wayarhamu-Llahul-Mustaqdimiyna Minnaa Walmusta-akhiriyn) Nas-alu-Llah Lanaa Wa Lakumul-'Aafiyah

Amani ishuke juu yenu watu wa nyumba za waumini na Waislamu, nasi Apendapo Allaah tutakutana nanyi, tunamuomba Allaah Atusamehe, sisi na nyinyi.  [Na Allaah Awarehemu wa mwanzo na wa mwisho] namuomba Allaah  Atupe sisi nanyi afya njema.”



Atakwenda Uhud na kutembelea kaburi la Hamzah رضي الله عنه,  pamoja na mashahidi waliozikwa hapo.  Atawatolea salamu na kuwaombea hivyo hivyo Du'aa ya kuzuru makaburi.


Tanbihi Muhimu  



Zifuatazo ni Tanbihi muhimu kwa mwenye kufanya Hajj au 'Umrah


1
Ajishurutishe katika fardhi za Allaah سبحانه وتعالى za dini zinazompasa kama kuswali kwa wakati wake na kuswali Jama'ah

2
Ajiepusha na yote yaliyoharamishwa kama uchafu, dhulma, utovu wa adabu kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى  :

((الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلاَ رَفَثَ وَلاَ فُسُوقَ وَلاَ جِدَالَ فِي الْحَجِّ))

((Hija ni miezi maalumu. Na anayekusudia kufanya Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika Hija)) [Al-Baqarah: 197]

3
Ajiepushe na kuwadhuru Waislamu wenziwe kwa maneno au vitendo katika sehemu tukufu na kwengine kote.


4
Ajiepushe na  yote aliyozuiliwa kufanya katika  Ihraam kama yafuatayo:


Kwa Hujaji wa kiume na wa kike

a) Asikate nywele Hapana ubaya kukuna kichwa au kuchana nywele na ikiwa zitatoka kwa ajili hiyo hakuna ubaya. 

b) Asikate kucha. Ikikatika kucha na ikiwa inamuudhi hakuna ubaya kuikata.

c) Asijitie manukato mwilini, au katika nguo zake baada ya kuingia katika Ihraam. Ama kabla ya Ihraam inafaa (kama ilivyoelezwa mwanzo). Vile vile katika chakula kama kutia zaafarani kwani zaafarani ni katika harufu nzuri. Vilevile ajiepushe na kuoga sabuni iliyo na manukato. Hakuna ubaya ikiwa manukato aliyotia kabla ya Ihraam yamebakia katika nguo zake.

d)  Asimguse na kumbusu mke/mume wake kwa hamu na baya zaidi asifanye naye jimai (kitendo cha ndoa).

e) Asifunge Nikaah (Ndoa) au kupeleka posa kwa mwanamke kwa ajili yake au mwenzake.

f)  Asivae glavu, lakini hakuna ubaya kufunika mikono yake kwa nguo yake.


Tanbihi kwa mwanamume pekee:



a) Asivae nguo zilizoshonwa kama fulana, shati, suruwali, soksi, viatu na kadhalika ila tu ikiwa hakuweza kupata Izaar na makubadhi au malapa ndio anaweza  kuvaa suruwali na viatu.   Anaruhusiwa kuvaa saa, miwani visaidizi vya kusikia au kuzungumzia.
b) Haifai kujifunika kichwa kama kuvaa kofia, kilemba, ghutra na kadhalika. Ama kujifunika mwavuli kwa ajili ya kujihifadhi jua hakuna ubaya. Pia hakuna ubaya akibeba begi lake kichwani.



Tanbihi kwa mwanamke pekee:



a)    Asivae niqaab na glavu. Kuna Maulamaa waliosema kuwa haifai kujifunika uso wake kwa niqaab au chochote kingine ila kama kuna wanaume karibu yake, basi inambidi ajifunike uso wake (kuepusha fitna) na hatakiwi kulipa fidia akifanya hivyo.



Rahmah na Amani Zimshukie Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Na Ahli Zake  na Maswahaba Zake.





FAHARASA



Al-Baaqiy'i
Sehemu Madiynah ambako kuna makaburi ya Maswahaba

Al-Idhwtiba'a
Kuweka sehemu ya katikati ya shuka (Ridaa) Chini ya kwapa ya mkono wa kulia na ncha zake juu ya bega la mkono wa kushoto katika twawwaaf

Al-Ikhlaas
Surah Namba 112 katika Qur'aan yaani 'Qul-Huwa-Llahu Ahad'

Al-Kaafiruun
Surah Namba 109 katika Qur'aan yaani 'Qul Yaa Ayyuhal-Kaafiruun'

Al-Marwah

Jina la mlima ambako Muislamu anaanza Sa'ayi
Ar-Raml
Kwenda mwendo wa mbio mbio kwa hatua ndogo ndogo katika mizunguko mitatu ya mwanzo kwenye twawwaaf

'Arafah
Sehemu muhimu kabisa ya kusimama katika Hajj iliyoko baada ya Muzdalifah

Ar-Ramiy
Kurusha Mawe

As-Swafaa
Jina la mlima ambako Muislamu anamalizia Sa'ayi yake ya mwisho

Dhul-Hijjah
Mwezi wa kumi na mbili katika kalenda ya Kiislamu
Hajar Al-Aswad
Jiwe Jeusi lililoko pembeni mwa Kaa'bah

Al-Haaj
Mwanaume mwenye kutekeleza fardhi ya Hijjah huko Makkah

Al-Hajah
Mwanamke mwenye kutekeleza fardhi ya Hijjah huko Makkah

Hamzah
'Ami yake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliyekufa  Shahiyd katika vita vya Uhud.

Hedhi
Damu anayopata mwanamke kila mwezi

Ifraad
Aina ya Hajj ya iliyo pekee

Ihraam
Hali ya kuingia katika tendo la kufanya ibada ya Hajj, au pia nguo za Hajj zinaitwa hivyo.

 Jamrah

Mnara katika Mina
Jamrah Al-Aqabah
Mnara ulio karibu na Makkah

Ka'abah

Nyumba tukufu iliyoko katika msikiti mtukufu wa Makkah
Maqaamu Ibrahiym
Jiwe alilokanyaga Nabii Ibrahiym na kusimama kuomba Du'aa baada ya kujenga Ka'abah

Mas'aa
Sehemu iliyonyooka baina ya Swafaa na Marwah

Mina
Bonde karibu na Makkah na mahali patukufu wanapokwenda kulala wanaofanya Hijjah kutekeleza baadhi ya vitendo vya fardhi vya (za) Hijjah.

Muzadalifah
Sehemu tukufu wanapolala waislamu katika ibada ya Hijjah, ipo baina ya 'Arafah na Mina

Namirah
Msikiti uliopo 'Arafah.  

Nifaas

Damu ya uzazi
Niqaab
Kifuniko cha uso wanachovaa wanawake waislamu

Qiraan

Aina ya Hajj ya  kusindikizwa
Qubaa
Msikiti wa mwanzo waliojenga waislamu walipoingia Madiynah kutoka Makkah pamoja na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم 

Ridaa
Sehemu ya nguo  (shuka) ya juu wanayovaa wanaume katika Ihraam

Rukn Al Yamaani
Pembe katika Ka'abah inayoelekea Yemen.

Sa'ayi

Kutembea baina ya Swafaa na Marwah
Sunnah
Mwenendo wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika kauli na matendo, au pia Hadiyth za Mtume. 

Takbiyr

Kusema Allaahu Akbar (Allaah Mkubwa)
Talbiyah
Du'aa ya Muislamu anayosema anapoingia katika Ihraam baada ya kutia Nia.

 Tamattu'
Aina ya Hajj  ya kustarehe (mapumziko)

Tarwiyyah
Tarehe nane ya Dhul-Hijjah

Twawwaaf
Mzunguko katika Ka'abah

Twaaful-Ifaadhwah
Twawwaaf ya Hajj ambayo ni moja ya fardhi katika taratibu za Hijjah.

Twawwaaful-Widaa'
Twawwaaf ya kuaga

Uhud
Mlima ulioko Madiynah umeitwa hivyo kutokana na vita vilivyotokea hapo.

'Umrah
Hijjah ndogo inayofanywa kwa twawwaaf na Sa'ayi pekee.






 *******************************************************************************

Hajj: Hatua Kwa Hatua

1 – 7 Dhul-Hijjah – Makkah au Madiynah
Kuzuru Msikiti wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  au kuweko Makkah kufanya 'Umrah (kwa Wanaofanya Hajjut-Tamattu'u) na kuendelea kuswali hapo Masjidul-Haraam.

Madiynah

Kuswali Masjidun-Nabawiy na wanaume kuzuru kaburi la Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
  
Makkah


Kufanya Twawwaaf  Kuzunguka Ka'abah mara 7
Kuswali Raka'ah mbili Maqaam Ibraahiym



Sa'yi  -  Swafaa  Na Marwah
Kuanza Kilima cha Swafaa kwenda kilima cha Marwah mara saba.

Wakimaliza 'Umrah watabakia Makkah na kuswali katika Masjidul-Haraam kupata fadhila zake


8 Dhul-Hijjah – Mina


Asubuhi Wanaondoka Makkah kuelekea Minaa.

9  Dhul-Hijjah – Siku ya 'Arafah

Wanaondoka kutoka Minaa asubuhi kuelekea 'Arafah na kubaki hadi jua litakapozama. 
Ni siku ya kutekeleza fardhi kubwa miongoni mwa taratibu za Hajj. Siku ya kuomba Du'aa sana. Na ndiyo siku iliyokamilika Dini yetu tukufu aliposimama Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika mlima wa 'Arafah na kutoa khutbah yake ya mwisho. Na ni siku ambayo wengi wetu wataachiwa huru na moto.

Hapa wataswali Swalah ya Adhuhuri na Alasiri 'jam'an wa Qaswran' (kujumuisha na kufupisha Rakaah mbili mbili). Watasikiliza khutbah (watakaojaaliwa kuweko karibu na Masjidun-Namirah).  Wasiokuwepo huko siku hiyo watafunga Swawm ya 'Arafah ambayo Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kasema inafuta madhambi ya mwaka uliopita na ujao.


Jua likizama, wataelekea Muzdalifah.

10  Dhul-Hijjah – Muzdalifah – Mina - Makkah
Watafika Muzdalifah usiku na wataswali Magharibi na 'Ishaa  'jam'an wa Qaswran' (kujumuisha na kufupisha Rakaah tatu Magharibi kawaida na kufupisha rakaa mbili 'Ishaa)
Watabakia Muzdalifah usiku mzima kwa kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى sana na kuokota vijiwe vya kurusha katika Jamaraat.
Asubuhi – Yawmun-Nahr (siku ya kuchinja) kwa Mahujaji, na kwa wasiokuwepo huko ni siku ya 'Iyd. Wataelekea kutekeleza vitendo vifuatavyo vya fardhi za Hajj:
1) Kurusha vijiwe katika Jamaraat
2) Kutufu Twaaful-Ifaadhwah
3) Kunyoa nywele  
4) Kuchinja
(vyovyote watakavyotanguliza  katika vitendo hivi inajuzu)
 

Kurusha mawe katika Jamaraat 
  
11 – 12 Dhul-Hijjah – Ayyaamut-Tashriyq
(Siku ya kwanza na ya pili ya Tashriyq)
Watarudi Minaa na kwa ajili ya kurusha mawe katika Jamaraat.
Ni siku za kula na kunywa na kumkumbuka sana Allaah سبحانه وتعالى  

13 Dhul-Hijjah  (Siku ya mwisho ya Tashriyq)
Wanaopenda kubakia Mina watabakia kisha watarudi Makkah na ikiwa safari imewadia watafanya Twawwaaful-Wida'a (Twawwaaf ya kuaga)

********************************************************************************
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

  ((وَالَّذِينَ صَبَرُواْ ابْتِغَاء وَجْهِ رَبِّهِمْ وَأَقَامُواْ الصَّلاَةَ وَأَنفَقُواْ مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلاَنِيَةً وَيَدْرَؤُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ أُوْلَئِكَ لَهُمْ عُقْبَى الدَّارِ)) ((جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا وَمَنْ صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ وَالمَلاَئِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍ)) ((سَلاَمٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ))


((Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao na wakashika Swalah, na wakatoa, kwa siri na kwa uwazi, katika Tulivyowapa; na wakayaondoa maovu kwa wema. Hao ndio watakaopata malipo ya Nyumba ya Akhera))  ((Nayo ni Bustani za milele, wataziingia wao na waliowema miongoni mwa baba zao, na wake zao, na vizazi vyao. Na Malaika wanawaingilia katika kila mlango))  [Wakiwaambia] ((Assalaamu 'Alaykum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyosubiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera)) [Ar-Ra'ad: 22-24]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اسْتَعِينُواْ بِالصَّبْرِ وَالصَّلاَةِ إِنَّ اللّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ))
 ((Enyi mlioamini! Takeni msaada kwa subira na Swalah. Hakika Allah Yu pamoja na wanaosubiri)) [Al-Baqarah: 153]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 (( وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ))
 ((Na anayesubiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa)  [Ash-Shuuraa:  43]

Fadhila za subira zimetajwa sana katika Qur-aan na Hadiyth, na subira inahitajika katika kila vitendo vyetu, ikiwa ni vya ibada au vya nje ya ibada. Katika kuswali, kufunga, Hajj, kutoa mali kwa njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika maafa, maradhi, vifo vya watu wetu, katika kufanya da'awah, katika kuishi na wenzetu hasa inapokuwa kuna baadhi yetu tuna tabia nzito, katika kuishi katika mazingira tunapokuwa ugenini n.k.  
Muislam anapokumbwa na mitihani asihisi kuwa kaonewa, bali ni neema kwake kwani hivyo ni kuletewa adhabu duniani na kufutiwa dhambi kwa ajili ya mitihani hiyo ili kupunguziwa adhabu za Qiyaama. Vile vile ni dalili ya kupendwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama zinavyosema Hadiyth zifuatazo:
Anapendelewa kheri na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
وعن أنس قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم ((إذا أراد الله بعبده الخير عجل له العقوبة في الدنيا وإذا أراد الله بعبده الشر أمسك عنه بذنبه حتى يوافي به يوم القيامة)) الترمذي
Kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Anapompendelea kheri mja Wake, Humharakishia adhabu duniani. Na Anapomtakia shari mja Wake, Huzuia dhambi zake ili Amlipe siku Ya Qiyaama)) [At-Tirmidhiy]
Hadiyth zifuatazo zinatuthibitishia kuwa mja anapopatwa na msiba hufutiwa madhambi yake:
 وعن أبي هريرة  رضى الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم ((ما يزال البلاء بالمؤمن والمؤمنة في نفسه وولده وماله حتى يلقى الله تعالى وما عليه خطيئة))  رواه الترمذي
Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) amesema: ((Muumini mwanamume na Muumini mwanamke huendelea kupata mitihani katika nafsi yake, na mtoto wake na mali yake hata anakutana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) akiwa hana dhambi)) [At-Tirmidhiy)
عن أبي سعيد و أبي هريرة رضي الله عنهما عن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((ما يصيب المسلم من نصب ولا وصب ولا هم ولا حزن ولا أذى ولا غم حتى الشوكة يشاكها إلا كفَّر الله بها من خطاياه )) رواه البخاري و مسلم
Abu Sa'iyd na Abu Huraryah (Radhiya Allaahu 'anhumaa) wamepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema: ((Muislam hatopatwa na tabu, wala maradhi wala hamu wala huzuni wala udhia wala ghamu (sononeko) mpaka mwiba unaomdunga isipokuwa Allaah Humfutia dhambi zake kwa sababu ya hayo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ni dalili pia ya mapenzi ya Allah kwa mja Wake:
عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قال  رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ((مَنْ يُرِدْ اللَّهُ بِهِ خَيْرًا يُصِبْ مِنْهُ))    صحيح
البخارى
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anayependelewa na Allaah (basi Allaah) Humpa msiba)) [Al-Bukhaariy]



 و قال النبي صلى الله عليه وسلم: (( إن عظم الجزاء مع عظم البلاء، وإن الله تعالى  إذا أحب قوما إبتلاهم، فمن رضي فله الرضا ، ومن سخط فله السخط))     رواه الترمذي
Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Malipo makubwa yako pamoja na balaa kubwa. Hakika Allaah Anapowapenda watu, Huwapa mitihani. Atakayeridhika basi atapata Radhi (Za Allah) na atakayechukia atapata Ghadhabu)) [(At-Tirimidhy]
Faida za kukumbwa na mitihani:
·         Kufutiwa dhambi na maovu,
·         Kupandishwa daraja kwa kuzidishiwa imani yake mja kwa kuridhika kwake na mitihani,
·         Sababu ya kumfungulia mja milango ya kuomba tawbah kwa kumkumbuka Mola wake Aliyempa mitihani,
·         Kuimarisha mawasiliano na Allaah na kujikurubisha zaidi kwa Allaah kwa kumkumbuka na kumuomba Amuondelee mitihani hiyo na  Amlipe mema,
·         Kuzidi imani mja kwa kuamini yanayatokea ni Qadhwaa na Qadar ya Mola wake na sio kulalamika na kukufuru bali kushukuru na kuamini kuwa hakuna mwenye kuweza kumnufaisha au kumdhuru isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
·         Kuwafikiria walio chini yake wenye mitihani mikubwa zaidi.
Yote hayo na zaidi ya hayo ni mafunzo ya mitihani katika kusubiri kwani hivyo ndivyo Anavyotaka Mola wetu kutujaribu Atuone nani katika sisi atakayeweza kusubiri Amlipe kheri zake, nani mkweli nani mnafiki, na nani mwenye imani ya kuamini Qadhwaa na Qadar ya Mola Wake:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ  ((الم ))  ((أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ))   ((وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ))
Kwa Jina la Allaah, Mwingi Wa Rehma, Mwenye Kurehemu daima
((Alif Laam Miym)) ((Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe?))   ((Hakika Tuliwajaribu waliokuwa kabla yao, na kwa yakini Allaah Atawatambulisha walio wa kweli na Atawatambulisha walio waongo)) [Al-'Ankabuut: 1-3]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kuwa na subira katika kila mitihani Yake ili Atulipe hayo yote tuliyoahidiwa katika kauli Zake na za Mjumbe Wake Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam

*********************************************************************************

Nini Baada Ya Ramadhaan? 

Tumeshauaga mwezi wa Ramadhaan Mtukufu, mwezi  wenye Baraka na Rehema, tumeziaga siku zake za  mchana tukiwa katika subira ya Swaum, na siku zake za usiku zenye ladha ya ‘Ibaada. Tumeuaga mwezi wa Qur-aan, mwezi wa Taqwa, mwezi wa Jihaad, mwezi wa Maghfirah, Mwezi wa Du'aa kutakabaliwa,  na mwezi wa kuepushwa na moto. Amefaulu aliyetimizia Swaum ilivyopaswa akachuma mema mengi na akajitahidi kufanya ‘Ibaada zaidi na amekhasirika aliyepuuza Swaum na hukmu zake na asichume mengi, na akafanya uvivu asiyejitahidi kufanya ‘Ibaada zaidi.
Kwa hiyo kila Muislamu aliyeingia katika mwezi wa Ramadhaan atakuwa ameingia katika madrasa ya Taqwa. Na mtu anapoingia katika madrasa yoyote hutoka humo akiwa amepata shahada yake ya lile somo alilolisoma, na baada ya hapo huitumia ile elimu aliyoisoma aidha kuifanyia kazi au kumsaidia katika kuendesha maisha yake yamuongoze katika uhusiano wa tabia yake pamoja na familia yake, mujtamaa wake na watu wote kwa ujumla.
Na huendelea kuitumia hiyo elimu katika maisha yake yote hadi kufa kwake. Na ni hivyo hivyo ndivyo shahada ya Taqwa inayopatikana katika mwezi huu, elimu yake humuongoza Muislamu katika uhusiano wake pamoja na Mola wake, familia yake na watu wote kwa ujumla. Kwa hiyo inampasa Muislamu aendelee kuitumia elimu hii ya Taqwa hadi atakapoonana na Mola wake kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):     
(( وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّى يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ))
[Na muabudu Mola wako mpaka ikufikie Yakini [Maana yake hadi yakufukie mauti]  [Al-Hijr: 99]
Na hii ndio maana ya Istiqaamah (kunyooka au kuendelea kuthibiti) kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):   
((فَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ وَمَن تَابَ مَعَكَ وَلاَ تَطْغَوْاْ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ))
[Basi, simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa, wewe na wale wanaoelekea kwa Allaah pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo] [Huud: 112]
((فَاسْتَقِيمُوا إِلَيْهِ وَاسْتَغْفِرُوهُ))
(Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na muombe maghfirah) [Fusswilat: 6]
 Kunyooka katika ‘Ibaada vile vile ametufundisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ifuatayo:
 عن أبي عَمْرو، وَقِيلَ: أبي عَمْرَةَ، سُفْيَانَ بْنِ عَبْدِ اللهِ الثّقَفيِّ رَضيَ اللهُ عَنْهُ قَال: قُلْتُ: يا رَسُولَ الله، قُلْ لي في الإِسْلاَمِ قَوْلاً، لاَ أَسْأَلُ عَنْهُ أَحَداً غَيْرَكَ. قَال: (("قُلْ: آمَنْتُ باللهِ ثُمَّ اسْتَقِمْ")).
Kutoka kwa Abu 'Amr, vile vile (anajulikana kama) Abu 'Amra Sufyaan bin Abdillaah (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Nilisema: Ewe Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu, niambie kitu kuhusu Uislamu ambacho siwezi kumuuliza mtu yeyote ila wewe.  Akasema (Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Sema; Namuamini Allaah, kisha kuwa mwenye kunyooka. (kwa kuendelea kufanya ibada na kuwa na msimamo madhubuti katika dini)) [Imesimuliwa na Muslim]
Kuthibitika katika  ‘ibaada ya Ramadhaan au msimu wowote wa ‘ibaadah ni alama ya kukubaliwa vitendo vya ‘ibaadah alivyovifanya Muislamu humo na kupotoka na kuingia katika maasi baada ya kutoka kwenye Taqwa ni alama ya kuviharibu vitendo vyake vyema. Na inampasa Muislamu anapotoka katika mwezi wa Ramadhaan, hali yake ya twa'a na Mola wake iwe bora zaidi kuliko ilivyokuwa kabla. Na kuhakikisha hali hii, jiulize na ujibu maswali haya:
1.      Je, Umekufikia mchana mmoja kama mchana wa Ramadhaan ukiwa katika Swaum?      
2.      Je, Umekufikia usiku mmoja kama usiku wa Ramadhaan ukiwa katika Qiyaamul-Layl?
3.      Je, Umeburudika na kusoma Qur-aan kama ulivyoburudika katika Ramadhaan?
4.      Je, Umeuburudisha moyo wako kwa dhikr, istighfaar, du'aa kama ilivyokuwa hali yako katika Ramadhaan?
5.      Je umetokwa na machozi kwa kukumbuka madhambi yako na kumkumbuka Mola Mtukufu na adhabu Zake?
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anapenda vitendo vya mwanaadamu anavyoviendeleza japo kuwa kama ni kidogo vipi, kuliko vitendo vingi kisha asiviendeleze:
قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( أحب الأعمال إلى الله أدومها وإن قل))  متفق عليه
Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Vitendo Anavyovipenda Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) zaidi (kuliko vyote) ni vile vinavyodumishwa japokuwa ni vidogo)).  [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kwa hiyo nyooka ewe ndugu Muislamu kwa kujiendeleza kufanya vitendo vyema na ibada katika miezi mingine yote kama ulivyokuwa ukifanya katika mwezi wa Ramadhaan nazo ni: 
Swaum:
Funga siku sita za mwezi wa Shawwaal ili ujipatie thawabu za kufunga mwaka mzima kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):    
 ((من صام رمضان ثم أتبعه ستاً من شوال كان كصيام الدهر)) رواه مسلم و الترمذي وابن ماجه, أبو داود و أحمد 
(Yeyote atakayefunga mwezi wa Ramadhaan, kisha akafuatia kwa kufunga siku sita za mwezi wa Shawwaal, basi atapata ujira wa aliyefunga mwaka mzima). [Imepokewa na Maimaam Muslim, At-Tirmidhy, Ibn Maajah, Abu Dawuud na Ahmad]  
Vile vile kuna Swaum za Jumatatu na Alkhamiys, siku tatu katika mwezi, (Ayaamul-Biydh), Swawm ya Arafat, Swawm ya 'Ashuraa na zote zimetajwa fadhila zake katika mada inayopatikana katika AL HIDAAYA kwenye kiungo hiki kifuatacho:
Qiyaamul-Layl (kisimamo cha kuswali usiku)
Ni Swala ya Sunnah iliyo bora kabisa baada ya Swala ya Faradh kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:
((أفضل الصلاة بعد الفريضة صلاة الليل))  رواه مسلم.
(Swalah iliyo bora kabisa baada ya Fardh ni Swalah ya usiku) [Muslim]
Ikiwa ulikuwa ukitoa sadaqa katika Ramadhaan kwa wingi, basi endelea kutoa sadaka japo kidogo kidogo miezi mingine katika milango mingi ya Jihaad fiy Sabiyli-LLaah (Jihaad katika njia ya Allaah). Sadaka ni kinga kubwa ya kumuepusha Muislamu na maovu mengi, kama uhasidi, huwa ni kinga hata kwa adui zake, na pia ni kumtoharisha mtu moyo wake na kuuweka uwe safi kutokana na maradhi ya moyo kama uhasidi, chuki, ufidhuli n.k.  Na juu ya hivyo humzidisha kheri na baraka nyingi katika mali yake, umri wake, humpa mtu siha nzuri, na ni kumuepusha na moto pia.  
Kulisha Masikini:
Ni jambo Analolipenda Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Amelisisitiza katika Qur-aan na kuwasifu wenye kulisha maskini na wengineo kwamba ni waja wema na jaza yao ni Pepo:
((إِنَّ الْأَبْرَارَ يَشْرَبُونَ مِن كَأْسٍ كَانَ مِزَاجُهَا كَافُورًا   ((عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا عِبَادُ اللَّهِ يُفَجِّرُونَهَا تَفْجِيرًا ))
(( يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا))    ((وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَى حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا))
 (( إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاء وَلَا شُكُورًا ))  (( إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوْمًا عَبُوسًا قَمْطَرِيرًا ))
 (( فَوَقَاهُمُ اللَّهُ شَرَّ ذَلِكَ الْيَوْمِ وَلَقَّاهُمْ نَضْرَةً وَسُرُورًا ))  (( وَجَزَاهُم بِمَا صَبَرُوا جَنَّةً وَحَرِيرًا ))  
5. Hakika watu wema watakunywa katika vinywaji vilivyochanganyika na kafuri,
6. Ni chemchem watakaoinywa waja wa Allaah wakiifanya imiminike kwa wingi.
7. Wanatimiza ahadi, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana,  
8. Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa.  
9. Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Allaah. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani.  
10. Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu hiyo siku yenye shida na taabu.  
11. Basi Allaah Atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha.
12. Na atawajazi Bustani za Peponi na maguo ya hariri kwa vile walivyosubiri. [Al-Insaan: 5-12]

Kutenda Wema Na Ukarimu:
Ikiwa Ramadhaan ilikubadilisha tabia yako ukawa unatenda wema kwa wazazi, ndugu, jamaa, jirani na marafiki, basi kutenda wema huko kuendelee miezi yote mingine.
Na vitendo vingi vyenginevyo inampasa Muislamu aendelee navyo siku zote wakati wote.     
Tunatoa Nasiha za dhati kwa ndugu Waislamu waliofunga Ramadhaan ipasavyo, kuendelea kuthibiti katika Taqwa na kumshukuru na kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akusaidie kuwa katika hali hiyo bila ya kurudi nyuma.  Wala usiwe kama yule aliyeshona nguo yake akaipenda sana kisha akaiharibu kwa kuivuta uzi bila ya sababu kama mfano wa mwanamke mmoja aliyekuwa Makkah ambaye alikuwa akifuma uzi na kuufanya madhubuti kisha kila ukiwa madhubuti huufumua, naye Amemtaja Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):     
((وَلاَ تَكُونُواْ كَالَّتِي نَقَضَتْ غَزْلَهَا مِن بَعْدِ قُوَّةٍ أَنكَاثًا))
(Wala msiwe kama mwanamke anayeuzongoa uzi wake baada ya kwisha usokota ukawa mgumu) [An-Nahl: 92]
Hii ni kama hali ya mwenye kurudia katika maasi baada ya kutoka katika Ramadhaan na akaacha kuwa na twa'a na kufanya mema, akawa badala ya kuitumia neema ya kuwasiliana na Mola wake na kuwa karibu Naye, akarudi katika madhambi. Waovu walioje watu wanaomtambua Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Ramadhaan pekee. 
Alipofariki Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Maswahaba walikuwa katika vilio  na huzuni kubwa za ajabu hadi wengine walipigwa  na bumbuwazi, na 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) alifika hadi kusema "Atakayesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefariki nitamuua". Walivunjikwa moyo sana hadi hali ikawa sio ya kupendeza, ndipo Abu Bakar (Radhiya Allaahu 'anhu) akawaambia:
"من كان يعبد محمد فمحمد قد مات ومن كان يعبد الله فان الله باقي حي لا يموت"
"Yeyote aliyekuwa anamuabudu Muhammad, basi Muhammad amefariki na yeyote aliyekuwa anamuabudu Allaah, basi Allaah Anabakia, Yu hai Hafi"
Hali kadhalika tunasema 'aliyekuwa anaabudu Ramadhaan, basi Ramadhaan inapita na aliyekuwa anamuabudu Allaah, basi Allaah Anabakia, Yu hai Hapiti kuondoka (Hafi)"
Kutokuwa katika istiqaamah baada ya Ramadhaan kunadhihirika kwa njia kama zifuatazo:

Kupuuza Swala:
Kutokuswali Swala za Faradhi, au kutokuziswali kwa wakati wake au kutokuziswali kwa kwa utulivu kama ipasavyo.

Kuacha Kuswali Jamaa Misikitini:
Swala ya Jama'ah ni jambo liliosisitizwa sana na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) sio Ramadhaan tu, bali siku zote za kawaida. Lakini utaona misikiti inajaa watu siku za Ramadhaan khaswa katika Swalah ya Tarawiyh ambayo ni Sunnah, wakati Swalah za fardhi ndizo muhimu zaidi. Na fadhila nyingi zimetajwa katika Sunna anazozipata Muislamu kuswali Jama'ah.
Kuacha Kusoma Qur-aan Na Kujua Maana Yake:
Wengine  huijua Qur-aan katika Ramadhaan tu, ikimalizika Ramadhaan, misahafu inarudishwa katika kabati ijae vumbi hadi Ramadhaan nyingine, wakati Qur-aan ni uongofu kamili wetu, na ina manufaa makubwa sana katika maisha yetu kwa kila upande kwani imekusanya neema zote humo zenye manufaa kwetu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):    
((يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاء لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ))
((قُلْ بِفَضْلِ اللّهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَلِكَ فَلْيَفْرَحُواْ هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ))
((Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uongofu, na Rehma kwa Waumini))
(Sema: Kwa fadhila ya Allaah na Rehma Yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya) [Yuunus: 57-58]
Vile vile ni muhimu sana Muislamu ajue maana ya maneno ya Mola wake ili atambue maamrisho na makatazo yake, sheria zake anazozihitaji katika maisha yake, na vile vile Qur-aan ni kipumbazo cha moyo kwani humo kuna visa vya Mitume na watu wa kale ambavyo vina mafundisho mazito kwetu na masimulizi ya kuburudisha nyoyo.
Kurudia Katika Mambo Ya Upuuzi:
Inampasa Muislamu aendelee kujiepusha na mambo ya upuuzi kama kutazama michezo ya televisheni, kusikiliza nyimbo, kukaa barazani kupiga soga, kusengenya katika simu, kusoma vitabu visivyo vya elimu na haswa elimu ya dini ya Kiislamu na kadhalika, na badala yake anatakiwa ajitahidi autumie wakati wa thamani katika kutafuta elimu ya dini yake tukufu na kuutumia wakati wake wote katika yale yenye kumridhisha Mola wake tu. Kujiepusha na mambo ya upuuzi ni moja wa sababu ya kumrithisisha Muislamu Pepo ya Firdaws kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Aayah ifuatayo:
          ((وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ))
 ((Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi))  [Al-Muuminuun: 3]
Ndugu Muislamu, endelea kunyooka katika Taqwa siku zote, wakati wote, kwani hujui lini Malaika wa kuchukua roho atakuwa mgeni wako. Jihadhari kukutana naye wakati uko katika maasi na jitayarishe uwe katika wale ambao wanapofikiwa na Malaika wa roho uambiwe:
((يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ))   ((ارْجِعِي إِلَى رَبِّكِ رَاضِيَةً مَّرْضِيَّةً))     ((فَادْخُلِي فِي عِبَادِي))    ((وَاد ْخُلِي جَنَّتِي))
   ((Ewe nafsi iliyotua))  ((Rejea kwa Mola wako  umeridhika, na umemridhisha))  ((Basi ingia miongoni mwa waja wangu))       ((Na ingia katika Pepo yangu)) [Al-Fajr: 27- 30]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atutakabalie amali zetu zote tulizozifanya katika Ramadhaan na Atuhidi kutuendeleza kunyooka katika Taqwa na wenye kuzidisha kufanya vitendo vyema siku zote, wakati wote hadi tutakapokutana Naye Mola wetu Mtukufu tuwe miongoni mwa wale walioamini na Atuingize Peponi kama Alivyotuahidi katika kitabu chake Kitukufu:
((إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُوْلَئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ))
 ((جَزَاؤُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا رَّضِيَ اللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ذَلِكَ لِمَنْ خَشِيَ رَبَّهُ))
 (Hakika walioamini na wakatenda mema, hao ndio bora wa viumbe))
((Malipo yao kwa Mola Wao  ni Bustani za daima, zipitazo mito kati yake. Wakae humo milele. Allaah Yu radhi nao, na wao waradhi Naye. Hayo ni kwa anaye mwogopa Mola wake ) [Al-Bayyinah: 7-8]
Du'aa ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ya kututhibitisha nyoyo zetu katika Dini yetu tukufu.
 اَللَّهُمَّ يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِك
Allaahuuma Yaa Muqallibal-Quluub Thabbit Qalbiy 'Alaa Diynik
(Allaahuumma, Ewe Mgeuza nyoyo, thibitisha  moyo wangu katika Dini Yako(
اّللَّهُمَّ ياَ مُصَرِّفَ الْقُلُوب صَرِّف  قُلُوبَناَ عَلَى طَاعَتِك         
Allaahuumma Ya Muswarrifal-quluub Swarrif Quluubana 'Alaa Twaa'atik
(Allaahumma, Ewe Muelekezaji wa nyoyo, Elekeza nyoyo zetu katika Twa'aa Yako) 
Na Allaah Anajua Zaidi


---------------------------*********************------------------------------------*********************

Mambo Matatu Yanayofuatia Ramadhan: 1)Zakaatul-Fitwr, 2)'Iddul-Fitwr  3)Swaum Ya Sittatush Shawwaal

Tunakaribia kumaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhaan na mambo matatu yafuatayo ya muhimu yanayotukabili yanapasa kuzingatiwa ili tukamilishe Swawm zetu ipasavyo na tupate fadhila zake.

1- ZAKAATUL-FITWR  
Inaitwa Zakaatul-Fitwr (Zakaah ya Kufuturu au Kufutari) kutokana na kumalizika Swaum ya Ramadhaan. Imefaridhiwa mwaka wa pili wa Hijrah katika mwezi wa Ramadhaan.
Hikma Yake
Ni kutwaharisha Swaum ya Muislamu kutokana na maneno machafu, ya upuuzi wakati alipokuwa amefunga kwa kulisha maskini chakula ili nao wapate chakula kizuri siku ya ‘Iyd. Ndio maana kutolewa kwake kunakuwa kabla ya kuswali Swalaah ya ‘Iddul-Fitwr. Dalili ifuatayo inathibitisha:
عَنْ ابْنِ عَبَّاس ٍقَالَ فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ طُهْرَةً لِلصَّائِمِ مِنْ اللَّغْوِ وَالرَّفَثِ وَطُعْمَةً لِلْمَسَاكِينِ مَنْ أَدَّاهَا قَبْلَ الصَّلاةِ فَهِيَ زَكَاةٌ مَقْبُولَةٌ وَمَنْ أَدَّاهَا بَعْدَ الصَّلاةِ فَهِيَ صَدَقَةٌ مِنْ الصَّدَقَاتِ . " رواه أبو داود  بِإِسْنَادٍ حَسَنٍ .

Kutoka Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambaye amesema: “Mtume amefaridhisha Zakaatul-Fitwr kuwa ni twahaara ya mwenye kufunga kutokana na maneno ya upuuzi na machafu, na kulisha masikini. Atakayeitoa kabla ya Swala basi hiyo ni Zakaah iliyotakabaliwa, na atakayeitoa baada ya Swala basi hiyo ni miongoni mwa sadaka” [Abu Daawuud kwa isnaad iliyo nzuri].
Na ndio kusudio ya kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
((قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّى))   ((وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّى))
((Hakika amekwishafanikiwa aliyejitakasa)) ((Na akakumbuka jina la Mola wake Mlezi, na akaswali)) [Al-A’laa: 14-15]

‘Umar bin ‘Abdul-Aziyz alikuwa akiamrisha watu kutoa Zakatul-Fitwr na huku akisoma Aayah hizo tukufu. 
Wakati Unaowajibika Kutoa
Kuanzia Magharibi ya siku ya mwisho ya Ramadhaan hadi Asubuhi kabla ya Swala ya ‘Iddul-Fitwr. Inaweza pia kutolewa siku mbili tatu kabla. Mtoto atakayezaliwa siku hiyo kabla ya kuzama jua imewajibika kutolewa Zakaatul-Fitwr.
Anayewajibika Kutoa Zakaatul-Fitwr Na Kitu Gani Cha Kutoa
 عَنْ ابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَال فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ صَاعًا مِنْ تَمْرٍ أَوْ صَاعًا مِنْ شَعِيرٍ عَلَى الْعَبْدِ وَالْحُرِّ وَالذَّكَرِ وَالأُنْثَى وَالصَّغِيرِ وَالْكَبِيرِ مِنْ الْمُسْلِمِينَ وَأَمَرَ بِهَا أَنْ تُؤَدَّى قَبْلَ خُرُوجِ النَّاسِ إِلَى الصَّلاةِ . صحيح البخاري   

Kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma): "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameifanya Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa mtumwa na aliye huru, mwanamume na mwanamke, mdogo na mkubwa miongoni mwa Waislamu kwa kutoa swaa'* moja ya tende kavu au swaa’ moja ya shayiri, na akaamrisha kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali (Swalaatul-'Iyd)" [Al-Bukhaariy] 

  • swaa’ moja = kilo mbili na nusu hadi tatu au (mteko) viganja viwili vya mkono vya mtu wa wastani vilivyojaa mara nne.

Kinachotolewa Ni Chakula Kinachotumika Na Watu Katika Nchi:

عن  أبي سَعِيدٍ الْخُدْرِيَّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ "ُكُنَّا نُعْطِيهَا فِي زَمَانِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ صَاعًا مِنْ طَعَامٍ أو صَاعاً من الشعير, أو صاعاً من تَمر, أو صاعاً من زَبيب، أو صاعاً من أقِط    البخاري  
Abu Sa'iydil-Khudriyy (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: "Tulikuwa tukitoa zama za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) swaa’ moja ya chakula, au swaa’ ya shayiri au swaa’ ya tende au swaa’ ya zabibu au swaa’ ya aqit" (mtindi mkavu) (ambacho ndicho kilichokuwa chakula chao zama za hizo) [Al-Bukhaariy Na Muslim]
Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho  kuhusu mas-alah mbali mbali ya Zakaatul-Fitwr:
2- ‘IDDUL-FITWR  
Inaitwa ‘Iddul-Fitwr (‘Idd ya kufuturu au kufutari) kutokana na Waislamu kumaliza funga ya Ramadhaan. Hivyo haifai kufunga Swaum siku ya ‘Idd, bali ni sikukuu ya Waislamu ya kusherehekea, kufurahi kwa kila njia zilizomo katika mipaka ya Dini.
a)  Apasayo Kufanya Muislamu Yaliyo Sunnah
Kuoga Kabla Ya Kutoka Kwenda Kuswali
فقد صح في الموطأ وغيره أَنَّ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عُمَرَ كَانَ يَغْتَسِلُ يَوْمَ الْفِطْرِ قَبْلَ أَنْ يَغْدُوَ إِلَى الْمُصَلَّى
Imethibitika katika Muwattwaa na vitabu vinginevyo kwamba ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alikuwa akioga siku ya ‘Iydul-Fitwr kabla ya kwenda Muswallaa.
Kujipamba Na Kuvaa Nguo Nzuri
وعن جابر رضي الله عنه قال : كان للنبي صلى الله عليه وسلم جبة يلبسها للعيدين ويوم الجمعة . صحيح ابن خزيمة   
Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Mtume alikuwa ana jubbah akilivaa siku za ‘Iyd mbili na siku ya Ijumaa” [Swahiih Ibn Khuzaymah]    
Na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alikuwa akivaa nguo zake nzuri kabisa siku ya ‘Iyd.
Kwa hiyo inapasa kujipamba kwa nguo nzuri, na manukato mazuri. Ama wanawake hawapasi kujipamba na kudhihirisha mapambo yao ikiwa ni mavazi au kujipaka vipodozi na pia hawapaswi kujitia manukato na kutoka nje. Wanaweza kudhihirisha yote hayo mbele ya Maharimu zao tu.
Kula Tende Kabla Ya Kutoka Kwenda Kuswali

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لا يَغْدُو يَوْمَ الْفِطْرِ حَتَّى يَأْكُلَ تَمَرَاتٍ .. وَيَأْكُلُهُنَّ وِتْرًا . البخاري  
Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hatoki kwenda kuswali Swalah ya ‘Idd ila baada ya kula tende… na akila kwa hesabu ya witr. [Al-Bukhaariy]
Hii ni kwa sababu haifai kufunga siku hii ya ‘Idd. Asiyepata tende anaweza kula kitu chochote.
Ama katika 'Iydul-Adhwhaa ni Sunnah kutokula kabla ya kwenda Msikitini, na anaposhuka baada ya Swala ni bora kitu cha kwanza kula ni ile nyama ya Udhwhiyah (mnyama aliyechinjwa) ikiwa itapatikana.

Kuleta Takbiyrah Kwa Sauti
Sunnah kuu katika ‘Iyd kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ((
((na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Allaah kwa kuwa Amekuongoeni ili mpate kushukuru)) [Al-Baqarah: 185]

Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akileta Takbirah mpaka anamaliza Swalah. [Silsilat Al-Ahadiyth As-Swahiyhah - Shaykh Al-Albaaniy]
Matamshi Ya Takbiyrah
الله أكبر الله أكبر لا إله إلا الله والله أكبر الله أكبر ولله الحمد
Allaahu Akbar Allaahu Akbar, Laa Ilaaha Illa Allaah, WAllaahu Akbar Allaahu Akbar wa Lillaahil Hamdu  
Wakati wa Takbiyrah
Unaanza usiku wa ‘Iyd mpaka anapoingia Imaam kuswalisha Swalah ya ‘Iyd


Kupongezana  
Ni vizuri kupongezana siku ya ‘Iyd baina ya Waislamu, kuzidisha mapenzi baina yao. Na ilivyo Sunna ni kusema kama walivyokuwa wakiambiana Maswahaba wanapokutana siku ya ‘Iyd ni kusema:
'Tuqubbila Minna wa Minka’ au ‘Taqabbala Allaahu Minnaa wa Minkum’.

Kuelekea Katika Muswallaa Kwa kutembea Na Kurudi Kwa Njia Nyingine
  
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا كَانَ يَوْمُ عِيدٍ خَالَفَ الطَّرِيقَ . رواه البخاري    

Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambaye amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akibadilisha njia siku ya ‘Iyd” [Al-Bukhaariy]

Hikmah yake ni kwamba njia hiyo itashuhudia siku ya kiyama na ardhi itazungumza yote ya kheri na shari anayotembelea mja juu yake. Pia kudhihirsiha Uislamu katika njia mbili, pia kukutana na watu tofauti na kuwasaidia kwa njia yoyote.


Kuswali Swalah ya ‘Iyd Katika Muswallaa
Ni Sunnah bali, ni waajib kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliamrisha watu wote watoke kwenda kuswali:

 عَنْ أُمِّ عَطِيَّةَ رضي الله عنها قَالَتْ "أَمَرَنَا تَعْنِي النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ نُخْرِجَ فِي الْعِيدَيْنِ الْعَوَاتِقَ وَذَوَاتِ الْخُدُورِ وَأَمَرَ الْحُيَّضَ أَنْ يَعْتَزِلْنَ مُصَلَّى الْمُسْلِمِينَ"  مسلم
Kutoka kwa Ummu ‘Atwiyyah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) kwamba: “Ametuamrisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tutoke katika ‘Iyd mbili vijana na vikongwe na kaamrisha wanawake wenye hedhi wajitenge katika Muswallaa” [Muslim] 
b)  Yaliyo Bid’ah Katika ‘Iyd
Kuleta Takbiyrah Kwa Pamoja Katika Misikiti Na Muswallaa
Inavyopasa ni kila mtu kuleta Takbiyrah pekee.
Kutembelea Makaburi 
Imekuwa ni ada ya baadhi ya watu kutembelea makuburi siku za ‘Idd. Jambo hili halikufanywa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wala Maswahaba zake. Mtu anaweza uzuru makaburi siku yoyote na si kutenga siku ya ‘Idd kwa jambo hilo na hadi kugeuka kuwa ni katika Sunna za ‘Idd hivi leo.
Maamkizi Ya Kuiga Makafiri
Kupelekeana kadi na zawadi kama wafanyavyo makafiri, haipasi kuwaiga kwani ni jambo tulilokatazwa katika dini na tuwe na fakhari na mila na desturí zetu.
c)  Yaliyo Maasi
Kunyoa Ndevu
Kunyoa ndevu hasa kwa makusudi ya kukusudia ‘Idd kwa kudhani mtu anapendeza akifanya hivyo ilihali anavunja sharia na kupingana na Sunna za Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Wanawake Kutokutimiza Hijaab zao za kisharia na kudhihirisha mapambo yao mbele ya wasio Maharimu wao.
Sherehe Za Maasi
Kuchanganyika wanawake na wanaume (party) na kuwekwa muziki, vyakula na vinywaji vya haraam na kupeana mikono wanawake na wanaume.
((لأَنْ يُطْعَنَ فِي رَأْسِ أَحَدِكُمْ بِمِخْيَطٍ مِنْ حَدِيدٍ خَيْرٌ لَهُ مِنْ أَنْ يَمَسَّ امْرَأَةً لا تَحِلُّ لَهُ))
Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Ni bora kwa mwanaume kupigwa sindano katika kichwa chake kuliko kuushika mkono wa mwanamke ambaye si halali yake.” [Silsilat Al-Ahadiyth As-Swahiyhah - Shaykh Al-Albaaniy] 
Wanawake wanaruhusiwa kuimba Nashiid siku za ‘Idd wakiwa peke yao au mbele za Maharimu wao.
Kufanya Israaf ya chakula na mali badala ya kuwasaidia masikini na mafakiri
3- SWAUM YA SITATUSH SHAWWAAL   
Swaum hii inafuatia moja kwa moja baada ya mwezi wa Ramadhaan na siku ya 'Idd ul Fitr. Ni Sunnah iliyo na fadhila kuu kwani thawabu zake ni sawa na thawabu za mtu kufunga mwake mzima kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
(( من صام رمضان ثم أتبعه ستًّا من شوال كان كصيام الدهر)) أرجه مسلم في صحيحه،

((Atakayefunga Ramadhaan kisha akafuatiliza na siku sita za mwezi wa Shawwaal itakuwa kama ni funga ya mwaka)) [Muslim]

Hesabu ya kuwa mwaka mzima ni kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((مَن جَاء بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا وَمَن جَاء بِالسَّيِّئَةِ فَلاَ يُجْزَى إِلاَّ مِثْلَهَا وَهُمْ لاَ يُظْلَمُون))

((Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na afanyae ubaya hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa)) [Al-An'aam:160]

Na kauli ya Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((إن الله كتب الحسنات والسيئات , ثم بين ذلك , فمن هم بحسنة فلم يعملها كتبها الله له عنده حسنة كاملة فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له عنده عشر حسنات , إلى سبعمائة ضعف , إلى أضعاف كثيرة , ومن هم بسيئة فلم يعملها , كتبها الله عنده حسنة كاملة , فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له سيئة واحدة )) متفق عليه ،

((Allaah Ameandika mema na mabaya. Kisha Akayabainisha. Basi atakayetia nia kutenda jema kisha asilifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapofanya hima na akalitenda, ataandikiwa mema kumi hadi kuzidi mia saba na ziada nyingi. Na atakayetia nia kufanya kitendo kibaya kisha asikifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapokifanya  ataandikiwa dhambi moja)) [Al-Bukhaariy ya Muslim]

Maulamaa wanachambua sababu ya kulipwa mja ujira wa mwaka mzima kwa atakayefunga Ramadhaan na siku sita hizo za Shawwaal, kwa kusema: Jambo zuri hulipwa ujira mara kumi, kwa hiyo mtu akifunga siku 30 za Ramadhaan atapata ujira mara kumi; nazo zitakuwa 300, ukijumlisha na siku sita za Shawwaal ambazo zikilipwa mara kumi, huwa 60. Kwa hivyo 300 + 60 = 360, mtu atapata hesabu ya mwaka mzima.
Kwa mantiki hii, tunaona kuna umuhimu na ubora mkubwa wa kuifunga Swawm hii ndugu zangu. 
Tunawaombea Waislamu wote wajaaliwe kumaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhaan kwa kheri na mafanikio, watakabaliwe Swawm zao, na madhambi kughufuriwa, waweze kutoa Zakaatul-Fitwr za kutakasa Swawm, Wawe na ‘Iyd ya furaha na uwezo wa kufunga Sitatush Shawwaal.
Taqabballa Allaahu Minna wa Minkum


******************************************
Laylatul-Qadr- Vipi Uweze Kuupata Usiku Huu?
Tumeingia   kumi la mwisho, kumi ambalo ndani yake kuna siku tukufu, siku ya Laylatul-Qadr, ambayo ibada yake ni bora kuliko ibada ya miezi elfu.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):  
﴿ بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ ﴾
((إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ)) (( وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ)) (( لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ))  ((تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ)) ((سَلَامٌ هِيَ حَتَّى مَطْلَعِ الْفَجْرِ))
BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym
((Hakika Sisi Tumeiteremsha Qur-aan katika Laylatul Qadr,  (Usiku wa Makadirio[Majaaliwa]). Na nini kitachokujuulisha nini Laylatul Qadr?)) ((Laylatul-Qadr ni bora kuliko miezi elfu)) ((Huteremka Malaika na Roho (Jibriyl) katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo)) ((Amani usiku huo mpaka mapambazuko ya alfajiri))  [Al-Qadr: 1-5]

Vile vile dalili katika Hadiyth mbali mbali zimethibiti kuhusu Fadhila za usiku huu mtukufu, na jinsi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa hali yake katika siku hizi kumi za mwisho za Ramadhaan.
Baada ya kuzijua fadhila zake usiku huu mtukufu inakupasa Muislamu ujikaze katika siku kumi hizi za mwisho kuacha mambo yote yanayokushughulisha ya dunia na utumbukie katika ibada tu ili uweze kuupata usiku huo mtukufu, yaani ukukute wewe ukiwa katika ibada ili zihesabiwe ibada zako kama kwamba umefanya ibada ya miezi elfu.

Tukifanya hesabu miezi elfu hiyo ni sawa na umri wa miaka 83!  
1000 ÷ 12 = 83.3 yaani miaka themanini na tatu na miezi mitatu takriban.
Hivyo ikiwa Laylatul-Qadr imekukuta katika ibada ya aina yoyote, ikiwa ni Swalah (Qiyaamul-Layl), kusoma Qur-aan, kufanya aina za dhikr, kutoa sadaka, kulisha chakula, kuwasiliana na jamaa, kujielimisha au kuelimisha, kufanya wema kwa watu, yote hayo utaandikiwa kama umefanya hayo kwa umri wa miaka 83! Na juu ya hivyo ibada hiyo ya usiku mmoja tu ni bora zaidi kuliko ibada utakayoweza kufanya miaka 83 na miezi mitatu. Subhaana Allaah!
Jihadhari ndugu Muislamu usije ukakukuta usiku huu mtukufu ukiwa katika maasi au katika sehemu ukiwa  umeghafilika na ya dunia kama sokoni, magenge ya soga au michezo ya kupoteza wakati au kwenye televisheni ukiangalia misalsalaat, mipira na sinema zikakupita kheri zote za usiku huu. Utaona siku hizi Waislamu wengi wanashughulika kwenda madukani kutafuta nguo za 'Iyd khaswa kina dada wakiacha masiku haya yawapite wakiwa humo badala ya kuwa majumbani mwao au misikitini kufanya ibada na kutegemea kuupata usiku huu.   
Ni siku chache tu ndugu Waislamu ambazo zinakimbia kama upepo. Je, nani basi katika sisi atakayepuuza asiupate usiku huo? Na Nani katika sisi atafanya hima kuupata usiku huo? Kwani hatujui kama tutakuweko duniani mwakani kuzipata siku hizi au hata hatujui kama tutaikamilisha Ramadhaan hii. Basi tujitahidi kwa kukesha  siku kumi hizi na kuamsha familia zetu ili iwe kheri yetu kukutana na usiku huo mtukufu tuweze kupata fadhila zake hizo ambazo ni sawa na kulipwa malipo ya umri mrefu kama tulivyoona hapo nyuma hata kama hatutoruzukiwa umri huo.

Mwenye Kuukosa Usiku Huu Amekula Khasara Kubwa
Hakika mwenye kuukosa usiku huo atakuwa amenyimwa kheri zake na itakuwa ni khasara kuukosa usiku huu mtukufu kama anavyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):   
عَنْ أَبِي هُرَيْرَة رَضِيَ اللَّه عَنْهُ قَالَ : لَمَّا حَضَرَ رَمَضَان قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: (( قَدْ جَاءَكُمْ شَهْرُ رَمَضَان شَهْرٌ مُبَارَكٌ اِفْتَرَضَ اللَّهُ عَلَيْكُمْ صِيَامَهُ تُفْتَح فِيهِ أَبْوَاب الْجَنَّة وَتُغْلَق فِيهِ أَبْوَابُ الْجَحِيم وَتُغَلُّ فِيهِ الشَّيَاطِين فِيهِ لَيْلَة خَيْرٌ مِنْ أَلْف شَهْر مَنْ حَرُمَ خَيْرهَا فَقَدْ حُرِمَ)) رَوَاهُ النَّسَائِيّ
Kutoka kwa Abu Huraryah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba ilipofika Ramadhaan, amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, ni mwezi wa Baraka. Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni Fardh, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi elfu.  Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa haswa)) [An-Nasaaiy]

Siku hiyo ni siku iliyoteremeshwa Qur-aan kutoka mbingu ya saba hadi mbingu ya kwanza kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala):
﴿ بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ ﴾
((حم)) ((وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ))  (( إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ))  ((فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ))   
BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym
((Haa Miym)) ((Naapa kwa Kitabu kinachobainisha)) ((Hakika Tumekiteremsha katika usiku uliobarikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji)) ((Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima)) [Ad-Dukhaan: 1-4]

Aya ya nne inayosema 'Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikma' kuwa kuna makadirio ya mwaka huo na yote yatakayotokea katika mwaka mzima. Kwa maana kwamba, siku ya Laylatul-Qadr, makadirio yote yaliyomo katika Al-Lawhum-Mahfuudhw (Ubao uliohifadhiwa) na huteremshwa haya makadirio na Malaika ambao wanaandika makadirio ya mwaka unaokuja yakiwa ni kuhusu umri wetu wa kuishi, rizki zetu, na yatakayotokea yote hadi mwisho wake. [Imesimuliwa na Ibn 'Umar, Mujaahid, Abu Maalik, Adh-Dhwahaak na wengineo katika Salaf – Ibn Kathiyr: 8:671]
Kujikaza kufanya ibada
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa inapoingia kumi la mwisho akijikaza kwa kufanya ibada kuliko siku zozote zingine:
عن عائشة رضي الله عنها قالت: كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يجتهد في العشر الأواخر ما لا يجتهد في غيره.  رواه مسلم

Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijitahidi katika kumi la mwisho kuliko alivyojitahidi katika siku nyingine zozote" [Muslim]

Na katika Swahiyhayn (Al-Bukhaariy na Muslim):  
عن عائشة رضي الله عنها، قالت: "كان رسول الله صلى الله عليه وسلّم إذادخل العشر شذ مئزره، وأحيا ليله، وأيقظ أهله  ( وفي رواية) "أحيا الليل،وأيقظ أهله، وجدّ، وشدّ المئزر" رواه البخاري ومسلم
Kutoka kwake pia Mama wa Waumini  'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha):  "Ilipokuwa inaingia kumi (la mwisho) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaza izaar (shuka) yake, akikesha usiku, na akiamsha ahli zake" (Na katika riwaaya nyingine) "Akikesha usiku, akiamsha ahli zake, akijitahidi na akikaza izaar yake" [Al-Bukhaariy na Muslim]

Kwa Nini Umeitwa Laylatul-Qadr?

Amesema Shaykh Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu-Llaah):

Kwanza: Kutokana na uwezo nao ni utukufu kama vile kusema “fulani mwenye uwezo mkubwa" yaani mwenye hadhi au utukufu.   

Pili: Ni usiku ambao una makadirio ya mwaka mzima na huandikwa yote yatakayotokea mwaka huo, na hii ni Hikma ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) na kuonyesha usanifu wa utengenezaji Wake na Uumbaji Wake.  

Tatu: Usiku huo una uwezo mkubwa kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):  
من قام ليلة القدر إيمانا واحتسابا غفر له ما تقدم من ذنبه)) متفق عليه

((Atakayesimama  usiku wa Laylatul-Qadr kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]  
  
Sababu Ya Kupewa Waislamu Laylatul-Qadr
Sababu ya kupewa Ummah huu wetu wa Kiislamu siku hii tukufu ya Laylatul-Qadr ni kwamba:

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliona umri wa Ummah za mwanzo ni mrefu, na umri wa Ummah wake ni mfupi akapewa usiku wa Laylatul-Qadr uwe ni bora kuliko miezi elfu. [Muwatwtwaa 1/321 (Muhammad Fuad 'Abdul-Baaqy]

Ibada Za Kufanya Masiku Kumi Haya Katika Kukesha

1-Qiyaamul-Layl (Kisimamo cha usiku kuswali)
((من قام رمضان إيماناً واحتساباً غفر له ما تقدم من ذنبه)) متفق عليه
((Atakayesimama (Kuswali) Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

2-Kuosma Qur-aan
Khaswa kwa vile usiku wa Laylatul-Qadr ndio usiku ulioteremeshwa Qur-aan kama tulivyoona katika Aayah hizo za juu katika Suratul-Qadr na Suratud-Dukhaan.
Vile vile Ramadhaan nzima inampasa Muislamu asome Qur-aan kwani ni mwezi ulioteremshwa Qur-aan kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ))
((Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi)) [Al-Baqarah: 185]

Na Jibriyl ('Alayhis-Salaam) alikuwa akimteremkia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila usiku wa Ramadhaan akimsomesha na kumsikiliza Qur-aan:
"كَانَ رَسُولُ اللَّهِ -صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ- أَجْوَدَ النَّاسِ وَكَانَ أَجْوَدُ مَا يَكُونُ فِي رَمَضَانَ حِينَ يَلْقَاهُ جِبْرِيلُ وَكَانَ يَلْقَاهُ فِي كُلِّ لَيْلَةٍ مِنْ رَمَضَانَ فَيُدَارِسُهُ الْقُرْآنَ"-  رواه البخاري
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni  mbora (mwenye matendo mema) wa watu, na alikuwa mbora zaidi katika Ramadhaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur-aan)) [Al-Bukhaariy]

3- I'tikaaf
Kutia nia kubakia msikitini kwa kufanya ibada tu humo kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya hivyo:
 عن عائشة – رضي الله عنها- قالت "كان النبي يعتكف في كل رمضان عشرة أيام؛ فلما كان العام الذي قبض فيه اعتكف عشرين يوماً - أخرجه البخاري    
Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba: Mtume (swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya I'tikaaf kila Ramadhaan siku kumi, ulipofika mwaka wake wa kuaga dunia alifanya I'tikaaf siku ishirini" [Al-Bukhaariy]

4-Kuomba Maghfirah
Kwani usipoghufuriwa madhambi yako basi ni hatari!
عَنْ أَنَس وَغَيْره أَنَّ النَّبِيّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لَمَّا صَعِدَ الْمِنْبَر ثُمَّ قَالَ  (( آمِينَ آمِينَ آمِينَ)) " قِيلَ يَا رَسُول اللَّه عَلَامَ مَا أَمَّنْت ؟
 قَالَ (( أَتَانِي جِبْرِيل فَقَالَ يَا مُحَمَّد رَغِمَ أَنْف رَجُل ذُكِرْت عِنْده فَلَمْ يُصَلِّ عَلَيْك قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ ثُمَّ قَالَ رَغِمَ أَنْف رَجُل دَخَلَ عَلَيْهِ شَهْر رَمَضَان ثُمَّ خَرَجَ فَلَمْ يُغْفَر لَهُ قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ ثُمَّ قَالَ رَغِمَ أَنْف رَجُل أَدْرَكَ وَالِدَيْهِ أَوْ أَحَدهمَا فَلَمْ يُدْخِلَاهُ الْجَنَّة قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ)) صحيح الترمذي وقال الشيخ الألباني حسن صحيح  

Kutoka kwa Anas na wengineo kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipopanda juu ya minbar aliitikia ((Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn)). Alipoulizwa kwa nini ameitikia hivyo akasema: ((Amenijia Jibriyl akasema: Ee Muhammad, ole wake yule ambaye unapotajwa hakuswalii, hivyo sema Aamiyn. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: ole wake yule ambaye umeingia mwezi wa Ramadhaan kisha akatoka bila ya kughufuriwa, kwa hiyo sema Aamiyn. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: ole wake yule ambaye amewakuta wazazi wake au mmoja wa wazazi wake lakini wasimuingize Peponi. Hivyo sema Aamiyn. Nikasema Aamiyn)) [Swahiyh At-Tirmidhiy na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa Hadiyth hiyo ina daraja ya Hasan Swahiyh]

5-Du'aa Ya Kuomba Maghfirah Katika Siku Kumi Hizi Zakaatul-Fitwr Mwisho

عن عائشة رضي الله عنها أنها قالت يا رسول الله أرأيت إن وافقت ليلة القدر ما أدعو قال: ((تقولين: اَللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌ تُحِبُّ الْعَفْو فَاعْفُ عَنِّي)) ابن ماجه و صححه الألباني
Kutoka kwa mama wa waumini bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba alisema "Ewe Mjumbe wa Allaah je, nitakapowafikiswha  usiku wa Laylatul-Qadr  niombe nini?" Akasema, ((Sema: Ewe Allaah Hakika Wewe Ndiye Mwenye Kusamehe Unapenda Kusamehe basi Nisamehe)) [Ibn Maajah na kaisahihisha Al-Albaaniy]  

Matamshi Yake
Allaahumma Innaka 'Afuwwun Tuhibbul-'Afwa Fa'afu 'Anniy

6-Kumkumbuka Allaah Kwa Aina Zozote Za Dhikr

Kwa Tasbiyh, Tahmiyd, Tahliyl, Takbiyr (kusema: Subhaana Allaah, Alhamdulillah,  Laa Ilaaha Illa Allaah,  Allaahu Akbar)

7- Kuomba Du'aa Na Haja Zako
Kwa vile ni mwezi wa kuomba Du'aa pia kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala Ameunganisha Aayah za kufaridhishwa Swawm na Aaya za kuhusu kuomba Du'aa:
((وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُواْ لِي وَلْيُؤْمِنُواْ بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ))  
((Na waja Wangu watakapokuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka)) [Al-Baqarah: 186]

Usiku Gani Khaswa Unapatikana Laylatul-Qadr? 
Hadiyth zimetaja siku kadhaa ambazo usiku huu mtukufu hutokea katika siku kumi za mwisho na haswa katika usiku wa witiri, zikiwa zimetajwa nyingine kuwa ni usiku wa siku ya ishirini na moja, au ishirni na tatu, au ishirni na tano au ishirini na saba kama ilivyokuja katika dalili zifuatazo:
وفي حديث عائشة رضي الله عنها أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((تحروا ليلة القدر في الوتر من العشر الأواخر)) رواه البخاري
Hadiyth kutoka Mama wa Waumini 'Aiashah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Utafuteni usiku wa Laylatul-Qadr katika siku za witiri kwenye siku kumi za mwisho)) [Al-Bukhaariy]

وفي حديث ابن عباس رضي الله عنهما أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((التمسوها في العشر الأواخر من رمضان ليلة القدر في تاسعة تبقى ، في سابعة تبقى ، في خامسة تبقى)) رواه البخاري

Hadiyth kutoka Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Utafuteni usiku wa Laylatul-Qadr katika siku kumi za mwisho za Ramadhaan, katika (usiku wa) tisa, saba, na wa tano utakaobakia [mwisho wa Ramadhaan])) [Al-Bukhaariy]
Imaam Ahmad amerikodi kutoka kwa 'Ubaydah bin Asw-Swaamit kwamba alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu usiku wa Laylatul-Qadr akasema: 
((فِي رَمَضَان فَالْتَمِسُوهَا فِي الْعَشْر الْأَوَاخِر فَإِنَّهَا فِي وِتْر إِحْدَى وَعِشْرِينَ أَوْ ثَلَاث وَعِشْرِينَ أَوْ خَمْس وَعِشْرِينَ أَوْ سَبْع وَعِشْرِينَ أَوْ تِسْع وَعِشْرِينَ أَوْ فِي آخِر لَيْلَة))
((Katika Ramadhaan, utafuteni siku kumi za mwisho, hakika umo katika siku za witiri, siku ya ishirini na moja, au ishirini na tatu, au ishirini na tano, au ishirini na saba, au ishirini na tisa, au usiku wa mwisho)) [Ahmad]

Alama Zinazobainisha Laylatul-Qadr
  1. Kwenye usiku huo kunakuwa na mwanga zaidi. 
  2. Upepo siku hiyo hutulia, yaani siku hiyo hautokei upepo mkali.
  3. Hali ya hewa huwa nzuri.
  4. Nyoyo siku hizo huwa na utulivu na unyenyekevu zaidi kuliko siku nyingine.
  5. Baadhi ya watu wema huoteshwa usiku kama walivyokuwa wakioteshwa Maswahaba na Salafus-Swaalih (wema waliotangulia) 


Asubuhi Yake
حديث أبي بن كعب رضي الله عنه أنه قال: "أخبرنا رسول الله صلى الله عليه وسلم أنها تطلع يومئذ ٍ لا شعاع لها" رواه مسلم
Hadiyth kutoka kwa Ubay bin Ka'ab (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba: "Ametuambia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa jua hutoka siku hiyo likiwa halina mishale (mikali)" [Muslim]

(( ليلة القدر ليلة طلقة  لا حارة ولا باردة ، تُصبح الشمس يومها حمراء ضعيفة)) صحيح ابن خزيمة
((Laylatul-Qadr usiku ulio katika hali ya ukunjufu, usio na baridi wala joto, asubuhi yake jua huwa jekundu na dhaifu)) [Swahiyh Ibn Khuzaymah]

ليلة القدر ليلة بلجة  (أي مضيئة) لا حارة ولا باردة ، لا يرمى فيها بنجم))  (أي لا ترسل فيها الشهب) رواه الطبراني  ومسند أحمد
((Laylatul-Qadr usiku wa kung'aa [yaani wenye mwanga] sio joto wala baridi, na vimondo (nyota za kufyatuliwa) hazitotumwa)) [At-Twabaraaniy na Ahmad] 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kukesha masiku haya kumi ili tujaaliwe kuupata usiku huu mtukufu tutoke katika Ramadhaan hii tukiwa tumeghufuriwa madhambi yetu yote na tumepewa fadhila za usiku huu mtukufu zinazolingana na kuongezewa umri wa miaka 83.  Aamiyn




*************************************************************************************************************

Nyakati Tatu Muhimu Za Kufanya Ibada – Zisikupite Katika Ramadhaan

Nyakati tatu hizi ni muhimu sana za kufanya ibada kutokana na fadhila zake kuu. Mwenye kupenda kuchuma thawabu nyingi asizikose khaswa katika mwezi huu Mtukufu Wa Ramadhaan ambao ni mwezi wenye malipo maradufu
1-Wakati wa mwanzo:  Baina ya Alfajiri na jua kuchomoza:
Usimulizi uliothibiti kutoka katika Swahiyh Muslim (564/1) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba walikuwa wakibakia macho wakati huo hadi jua kuchomoza kwani ni wakati mja anapogaiwa rizki yake, na ni wakati wenye kheri nyingi, unampa siha nzuri ya mwili binaadamu, na kwa ujumla ni wakati wenye baraka nyingi za kila aina kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba:  
((اللهم بارك لأمتي في بكورها))  الترمذي, أحمد, أبي داود, ابن ماجه 
((Ewe Allaah, wabarikie Ummah wangu nyakati za asubuhi mapema)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Abu Daawuud, Ibn Maajah na imethibitishwa kuwa ni Hadiyth Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]
Usimulizi huu umetoka kwa Maswahaba kadhaa ambao wameelezea kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipotaka kupeleka kikosi au jeshi aliwapeleka mwanzo wa asubuhi". Vile vile wamesimulia kwamba: "Swakhar alikuwa mtu tajiri ambaye alikuwa akipelekea biashara zake mwanzo wa asubuhi na matokeo yake ilikuwa ni kufuzu katika biashara na kupata faida kubwa sana".
Wamesimulia Salafus-Swaalih kwamba Ibn 'Abbaas naye alimkataza mtu kulala nyakati hizo alipomwambia:
   "قُم، أتنام في الساعة التي تقسَّم فيه الأرزاق؟"
"Inuka! Je, unalala katika saa ambayo rizki inagaiwa?"
Ikiwa basi wakati huo ni kama hivyo ilivyoelezwa juu, basi vipi Muislamu auache wakati huu umpite khaswa katika mwezi huu mtukufu wa Ramdhaan?
Ibnul-Qayyim (Rahimahu-Allaah) katika kitabu chake 'Zaad Al-Ma'aad' amesema: "Usingizi wa asubuhi unanyima rizki kwani huo ni wakati ambao Muumba anaombwa rizki na wakati wa kugaiwa rizki. Hivyo usingizi unanyima rizki isipokuwa kwa dharura. Usingizi wakati huo pia ni madhara kwa mwili…"   
Faida nyingine kubwa ya kubakia macho ukimdhukuru Allaah wakati huu
Si chini ya muda wa saa na nusu utakuwa umepata thawabu za Hajj na ‘Umrah kamilifu:
عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال  (( من صلى الفجر في جماعة ثم قعد يذكر الله  حتى تطلع الشمس ثم صلى ركعتين كانت له كأجر حجة وعمرة تامة تامة تامة) ) أخرج الترمذي  صححه الألباني .
Imetoka kwa Anas kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jama'ah kisha akakaa anamkumbuka Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]

Pindi ukifanya hivyo kwa mwezi mzima utakuwa umechuma thawabu za Hajj na ‘Umrah mwezi mzima. Hizo ni fadhila za siku za kawaida, seuze ukifanya mwezi mtukufu huu wa Ramadhaan? Jitahidi ndugu Muislamu kadiri uwezavyo kuchuma hizi thawabu kubwa ambazo zingelikukalifu mali, tabu za safari na mashaka ya kufika Makkah kutekeleza ibada hizo. Lakini kwa Rahma ya Allaah Ametujaalia tuweze kuzichuma tukiwa majumbani mwetu tena kwa wepesi kabisa. Wanaume thawabu zitazidi ikiwa watatekeleza wakiwa misikitini. Wanawake wanazipata fadhila hizo hata wakiswali majumbani mwao.  Hata hivyo, pamoja na ujira wote huu, tusisahau kuwa fadhila hizo hazivunji wala hazifuti fardh ya kwenda Hajj kwa mwenye uwezo, asije mtu akadhani kufanya hayo kutakuwa kumetengua wajiibu wake wa kuhiji au kufanya ‘Umrah.

2- Wakati wa pili: Kabla ya Jua kuzama (Magharibi): 
Huu ni wakati ambao bado Muislamu yuko katika Swawm na du'aa yake anayoiomba hairudi:
 قال صلى الله عليه وسلم: ((ثلاثة لا ترد دعوتهم: الصائم حتى يفطر والإمام العادل والمظلوم))  وروى الترمذي   بسند حسن
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (([Watu] watatu du'aa zao hazirudi; mwenye kufunga hadi afuturu/afutari, Kiongozi muadilifu na aliyedhulumiwa)) [At-Tirmidhiy kwa isnaad nzuri]
Kwa hiyo ni fursa ya kuitumia Muislamu aombe du'aa na haja zake wakati huu khaswa pia kwa vile ni wakati ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amehimiza Atukuzwe kama Anavyosema:
 (( وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ))   
((.. na mtakase kwa kumsifu Mola wako  kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa)) [Qaaf: 39]
 ((وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا وَمِنْ آنَاء اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَى)) 
((…Na umtakase Mola wako kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na nyakati za usiku pia umtakase, na ncha za mchana ili upate ya kukuridhisha)) [Twaahaa: 130].
 (( وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَار))  
((…Na omba msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako  kwa kumhimidi jioni na asubuhi)) [Ghaafir: 55]
   
3- Wakati wa tatu: Suhuur - Kabla ya Alfajiri

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewaaahidi Wacha Mungu Pepo kwa sababu sifa mojawapo yao ni kuomba maghfira kabla ya Alfajiri: 
 إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُون)) ((آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ))  ((كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ))  ((وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُون))

((Hakika wenye taqwa watakuwa katika Mabustani na chemchem)) ((Wanapokea Aliyowapa Mola wao. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema)) ((Walikuwa wakilala kidogo tu usiku)) ((Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfira)) [Adh-Dhaariyaat: 15-18]


Kisha wamesifiwa tena kwa sifa hiyo hiyo pamoja na nyinginezo:
((الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالأَسْحَارِ))  
((Wanaosubiri, wanaosema kweli, na watiifu, na wanaotoa sadaka, na wanaoomba maghafira kabla ya Alfajiri)) [Al-'Imraan: 17]
Muislamu asiache wakati huo umpite kwani ni wakati muhimu na wenye fadhila na faida kubwa kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka wakati huo kutoka mbingu ya saba na kuweko mbingu ya ardhi kutukidhia haja zetu:
 عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((ينزل ربنا تبارك وتعالى كل ليلة إلى السماء الدنيا حين يبقى ثلث الليل الآخر فيقول: من يدعوني فأستجيب له؟ من يسألني فأعطيه؟ من يستغفرني فأغفر له )) البخاري و مسلم
Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Nani miongoni mwetu asiyemhitaji Mola wake kumkidhia haja zake na kumuondeshea shida zake? Nani asiyekuwa na madhambi asiyemhitaji Mola wake kumghufuria? Hivyo usiache wakati huu ukakupita khaswa kwa vile mwezi huu Mtukufu ambao kila jambo ulifanyalo lina fadhila na thawabu marudufu.
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kudiriki nyakati hizo tatu na nyingine, tuwe katika ibada katika mwezi huu wa Ramadhaan na miezi yote mingineyo na Atujaalie kheri na Baraka nyingi, Atukidhie haja zetu, Atuondoshee shida zetu na Atughufurie madhambi yetu yote. Aamiyn.
 

********************************************************

Mirungi  

(Historia, Madhara Na Mikasa)



بسم الله الرحمن الرحيم

Muhammad Baawazir
Historia Yake

Inaaminika kuwa Ethiopia ndio asli yake kuanzia karne ya 15, na ikaenea katika milima ya Afrika Mashariki na Yemen. Ingawa vilevile kuna wanaoamini kuwa ilianzia Yemen katika karne ya 13 kabla ya kuenea hadi Ethiopia na nchi za jirani.

Kutoka Ethiopia na Yemen, mti au mmea huo ulienea sehemu mbalimbali za Arabuni, Somalia, Sudan, Kenya, Tanzania, Uganda. Congo, Malawi, Zimbabwe, Zambia hadi Afrika ya Kusini.

Baadhi hudai kuwa matumizi yake yanarejea miaka ya nyuma sana tokea wakati wa Wamisri wa kale ambao inasemekana walikuwa wakiitumia kama madawa ya jadi kwa baadhi ya magonjwa.

Anaeleza mwandishi wa Kimalaysia ‘Abdullaah bin ‘Abdil-Qaadir kuwa alipokuwa Yemen mwaka 1854, aliona ada na tabia ya utafunaji Mirungi huko Al-Hudaydah. Anaeleza: “Niliona jambo la ajabu katika mji huu –kila mtu anatafuna majani kama mbuzi anavyokula akameza na kisha kucheua kisha hutafuna tena kile alichokicheua. Kuna aina ya tawi, si pana sana kiasi cha urefu wa vidole viwili, ngumu kiasi, watu hutumia aina hii ya tawi au jani na kutia mdomoni na hutumiwa na viambatanishio vingine kuila, tawi hili hutiwa lote mdomoni na kutafunwa. Wanapokuwa wengi na kula kwa pamoja, utaona mabaki ya majani hayo yamerundikana mbele yao. Wanapotema mate, mate yao huwa ya rangi ya kijani. Kisha nikawauliza kuhusu hicho wanachokula: ‘Ni faida gani mnayopata kwa kula majani hayo?’ Wakajibu, ‘Hakuna chochote, ni jambo tulilolizoea lenye kutugharimu ambalo tumekulia nalo’. Wale wanaokula majani haya inawabidi watumie sana mafuta na asali, kwani wasipofanya hivyo wanaweza kuugua. Hayo majani hujulikana kama Kad (Mirungi).”


Wasifu Na Kilimo Chake
Mirungi ni mti unaoota polepole ambao unakuwa kwa urefu wa mita 1.5 hadi mita 20, kutegemea na eneo kijiografia na pia hali ya mvua ya eneo. Likiwa na majani ya kijani yaliyokoza ambayo yana urefu wa sentimeta 5 hadi 10 na upana wa sentimeta 1 hadi 4.

Ina ladha ya uchachu mkali na utamu wa mbali kwa wakati mmoja. Hufungwa katika majani ya migomba ili kuhifadhi ubichi wake. Kawaida huvunwa asubuhi sana na kuuzwa mchana wake au usiku wake, kila inavyokaa sana hupunguza ubora wake kwa walaji na thamani yake. Na kwa sababu walaji wa Tanzania hutegemea zaidi Mirungi kutoka Kenya, huwa hawapati ule ubora unaotakikana kutokana na umbali na kutofika kwa haraka; ingawa walaji wa Arusha hupata haraka zaidi kwa ukaribu wake na Nairobi kuliko wale wa Dar na Zanzibar au miji ya bara ya mbali kama Mwanza na kwengineko.

Kwa hivyo, majani ya Mirungi yanapoanza kukauka, kemikali ile kali ya aina ya cathinone inakauka pia na inabakia ile ambayo sio kali: cathine, na ndio maana mirungi inaposafirishwa inawekwa katika mifuko maalum ya plastiki au kufunikwa na majani ya migomba ya ndizi ili ihifadhike vizuri.

Mirungi ni zao lenye kuwaingizia wakulima Yemen kipato kikubwa na ndio maana wengi wameanza kuacha kilimo cha kahawa, na hutumika asilimia 40 ya matumizi ya maji ya nchi nzima kwa kilimo chake, pamoja na uzalishaji wake kuongezeka kiasi cha asilimia 10 hadi 15 kila mwaka. Matumizi ya maji yamekuwa makubwa kiasi cha hifadhi ya maji ya San’aa mji mkuu wa Yemen kupungua na ikiendelea namna hii basi baada ya miaka kumi tu maji yatakauka na kwa hali hiyo imefikia serikali kugawa maeneo kwa kuwahamisha wakazi wa San’aa kwenda kuishi maeneo ya pwani ya Bahari nyekundu.

Shamba La Mirungi Huko Yemen

Matumizi ya Mirungi aghlabu hutumika katika maeneo yanayolimwa zaidi na maeneo ya jirani na yale ambayo hufika Mirungi haraka ingali bado mpya mbichi na safi kwa sababu ya mzimuo wake. Kila inavyokaa mzimuo wake na upandishaji wa ‘handasi’/ ‘nakhwa’ yake hupungua.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza ya kwamba zaidi ya masaa 14.6 milioni yanapotezwa kila siku katika ulaji wa Mirungi huko Yemen. Ripoti hiyo, iliotolewa katika tovuti ya WHO, inaonyesha ya kwamba asilimia 80 ya watu wazima (male adults) wanatafuna Mirungi kila siku kwa muda wa masaa matatu mpaka manne hadi matano wakati ambapo zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wamo pia katika tabia hii yenye hatari.

Mirungi ni kileo kinachotumika sana kama ‘mkusanyiko wa kijamii’ katika maeneo mengi, na huwajumuisha zaidi wanaume ingawa baadhi ya sehemu na kwa miaka ya karibuni wanawake wamevamia sana uraibu huo haswa maeneo ya pwani ya Afrika Mashariki kama Mombasa, Tanga na Dar-es-Salaam na mji kama Arusha ambao pia umekumbwa na ugonjwa huo kwa vijana wengi wa mjini. Na hupendelewa na madereva wa magari makubwa wanaosafiri safari ndefu, madereva wa abiria na hata wa magari ya kukodishwa kwa kuamini kuwa inawafanya wawe macho na makini. Vilevile hutumiwa na wanafunzi wakiamini kuwa inawafanya wasome muda mrefu na kukesha, kadhalika walinzi wa usiku huona inawasaidia kuwa macho usiku. Na baadhi ya watu hutumia kwa kisingizio cha kukesha kwa ajili ya kufanya ‘Ibaadah za usiku.

Nchi kama Tanzania, imepigwa marufuku lakini serikali kwa kutofuatilia kwa karibu kumefanya kuwe kunaliwa hadharani na bila woga wowote. Hufuatwa sheria pale maaskari wanapotaka kupata chochote kutoka kwa walaji na ni nadra kusikia mla Mirungi katiwa ndani, na akitiwa ndani basi hutolewa mara moja bila kufikishwa mahakamani.

Huko Somalia, waliposhika madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2006 na kuleta amani ambayo haikuwahi kuonekana Somalia, Baraza La Juu La Mahkama Ya Kiislam, walipiga marufuku kuliwa mwezi wa Ramadhaan na kusababisha maandamano na upinzani huko Kismayo. Na mwaka huo huo katika mwezi wa Novemba, Kenya ilipiga marufuku ndege kwenda Somalia wakitaja ni sababu za kiusalama, hali ambayo ilisababisha upinzani kutoka kwa walimaji Mirungi. Mbunge wa Ntonyiri, Meru ambayo ndio eneo lenye kutegemewa sana Afrika Mashariki kwa ulimaji wa Mirungi, alieleza kuwa imetengwa ardhi maalum ya kulimia Mirungi, ambapo tani 20 zenye thamani ya Dola Laki 8 ($800, 000) husafirishwa kila siku kuelekea Somalia na hivyo kizuizi cha serikali kitailetea taifa madhara ya kiuchumi na kipato kama hicho kwa siku.


Aina Zake

Alenle (yenye majani mapana mengi, na ni ghali) – Yemen, Ethiopia na Kenya
Kangeta – Kenya
Giza (ni aina ya mirungi iliyo ndogo ndogo) – Kenya
Mbaga (ni aina ya mirungi iliyo ndogo ya aina duni ambayo aghlabu ni ya bei ya chini -japo kuna baadhi ya mashamba machache sana hutoa aina yenye afadhali- na huliwa na wasiomudu kununua aina za ghali) – Tanzania




Madhara Yake

“Familia nyingi zinateketea, wake kukimbia waume zao, waume kutojali familia zao; hawataki kufanya kazi, jamii kujaa wavivu waombaji, wazazi na wakwe kulea wajukuu wasiongaliwa na wazazi wao, ulaghai na maasi kuzidi, ‘Ibaadah kupuuzwa, uchumi kuporomoka…”

Naam, tukiyaunganisha maneno hayo na tunavyoona hali ya walaji, hakika yana ukweli mtupu usiopingika kwa wanaojua hali hiyo katika jamii.

Tutajaribu kuyaorodhesha madhara mbalimbali yanayosababishwa na ulaji Mirungi.


Madhara Ya Kidini Na Kimaadili

  1. Kupitwa na vipindi vya Swalah au kutokuswali kabisa;

  1. Swawm haikamiliki – katikati ya mchana wa Ramadhaan watu huhangaika kutafuta Mirungi na kucheza bao, keramu, dhumna, kutazama mipira na sinema. Jambo la kwanza baada ya futari, watu huanza kusaga Mirungi. Hakuna Swalah za usiku, hakuna ‘Ibaadah nyingine yoyote, hata Swalah ya Alfajiri huwapita walaji wengi kwa sababu Shaytwaan wa Mirungi huwaambia wakalale muda mchache tu kabla ya Swalah ya Alfajiri! Kuamka kwao ni mchana au Alasiri, Ramadhaan inakuwa haina uzito wowote kwa maisha ya mla Mirungi;

  1. Mchanganyiko baina ya wanaume na wanawake;

  1. Uongo – hii ni kawaida kwa wengi ili wafikie malengo ya kupata wakitakacho; ima kudanganya wengine kwa kuwakopa pesa za kununulia Mirungi na kisha hawarejeshi madeni hayo. Na pia wanapokopa husingizia matatizo makubwa waliyonayo wao au jamaa zao kama maradhi, matibabu, ada za shule, n.k. ili waweze kukubaliwa kupata mikopo hiyo. Aghlabu wanapokopa hawasemi ukweli kuwa wanataka pesa za kununulia Mirungi; maana hakuna atakayewakopesha;

  1. Usengenyaji – vikao vingi vya walaji huwa ni mazungumzo ya kidunia, mipira, filamu, kujadili mambo ya siasa, jamii, na kujadili maisha ya watu, maingiliano ya kindoa, na wao kwa wao kutoa siri zao za ndani na kutaja maovu yao waliyowahi kuyafanya;

  1. Uropokaji, uchache wa adabu, ujuaji wa kila kitu, mlaji akiongelea siasa basi hakuna mwanasiasa kama yeye, akija kwenye mpira wa miguu na hususan ligi ya Uingereza, basi hakuna anayeichambua ligi hiyo kama yeye… na mtihani mkubwa na msiba ni kuwa hata mas-ala ya Diyn wao pia ni wataalam wakioongelea Taariykh na kwanini fulani aliuliwa na wangapi waliritadi baada ya Mtume na kwanini fulani walikuwa hawastahiki Ukhalifa walimdhulumu fulani n.k.!!

  1. Upungufu wa hayaa;

  1. Kupoteza muda mkubwa katika vikao hivyo;

  1. Kuomba omba – wengi huwa hawana uwezo wa kununua Mirungi kukidhi mahitaji ya uraibu wao, na hivyo kuwapelekea kuwa waombaji kwa wengine ima wa pesa za kununulia au uombaji wa Mirungi kwa walaji wenzao;

  1. Maasi – baadhi ya vikao vya Mirungi hutawaliwa na kutazamwa sinema za uchi ili kusukumia handasi zao. Hali hiyo ya uchafu wa maadili na kujitumbukiza katika uharamu, huwakutanisha wazee kwa vijana na matokeo kupoteza heshima baina yao, na pia nyumba hizo kupoteza hadhi katika jamii na nyakati nyinginezo kuwatukanisha wake za wenye nyumba hizo kwa machafu yanayoendelea hapo. Baadhi ya nyumba waume wamepoteza wake zao kwa marafiki zao kutokana na maingiliano huru yasiyo na mipaka baina ya wake kwa waume;

  1.  Kuharibiwa itikadi zao – mji kama Arusha, vijana wengi wamebadili itikadi zao za Diyn baada ya kujiunga na uraibu huo na kushiriki vikao vyake. Ndani ya vikao hivyo kuna kundi la wakongwe ambao wameweza kuwashawishi vijana kutoka katika itikadi waliyozaliwa nayo na kujiunga na itikadi ya kukufurisha na kulaani Maswahaba na wema waliopita. Imefikia hali ya kusikitisha sana kwa kuona kundi kubwa la watu likiwa limekaa barazani likicheza Dhumna (Domino) na huku Swalah ya Jama’ah ikiadhiniwa, kuqimiwa, na kuswaliwa ubavuni mwao kwenye Msikiti na wala hawana wasiwasi tena wakifanya zogo na kelele na kuzipigisha kete zao kwa nguvu kana kwamba wanashindana na sauti ya Mnadi Swalah. Maskini na wao wanajiona wako sawa kabisa kwenye haki! Na wanapotanabahishwa waache lahwu zao na waende kuswali, husema kuwa wao wanajumuisha Swalah kutokana na Itikadi yao. Ukweli wengi hata kuswali hawaswali;

  1.  Haki za kifamilia kukiukwa – haki za kinyumba; waume wanakuwa hawatoa haki zao ima kwa kukesha nje ya nyumba zao, au kwa kudhoofika nguvu zao za kiume na pia kumaliza haraka wanapofanya tendo la ndoa na hivyo kusababisha wake kukosa haki za msingi;

  1.  Talaka kuzidi – kwa sababu tulizotaja katika kipengele kilichotangulia, wake wengi hushindwa kuvumilia katika ndoa zao na kuamua kudai talaka;

  1.  Haki za watoto hazitekelezeki – kwa kuwa walaji wengi hawafanyi kazi, na wanaofanya kazi hutumia gharama nyingi kwenye ulaji, hivyo hakupatikani matumizi nyumbani au matumizi kubanwa na haki kutotimizwa. Walaji wengine hulelewa watoto wao na wakwe zao au wazazi wao;

  1.  Kutoka nje ya ndoa – baadhi ya walaji wanakuwa si waaminifu kwenye ndoa zao, kadhalika baadhi ya wake wanashindwa kuvumilia kuwa wapweke kila mara kwa kuwa waume zao hukesha nje ya nyumba zao, na wakirudi ni usingizi, wakiamka ni kutafuta Mirungi, na hivyo hupelekea wake hao kukosa uvumilivu na kwa kuzidiwa kwao na matamanio yao –na kwa uchache wa Iymaan- kunawapelekea wao kuyahamisha matamanio yao pengine.

  1.  Walaji wa uraibu huu hukesha kuorodhesha mambo watakayoyafanya siku ifuatayo, pasi na kuyatekeleza, na kuendelea katika hali hiyo kila mara bila ya mafanikio yoyote.

  1. Wengine husingizia eti wanakesha kwa ajili ya ‘Ibaadah, lakini ni aina gani ya ‘Ibaadah inayofanyika wakati mashavu yametuna kwa kujaa majani hayo?



Madhara Ya Kiafya

Matatizo na madhara ya Mirungi yaligunduliwa mwanzo katika mwaka 1935 na League Of Nations, Mwaka 1970 taasisi ya tiba ikaitenga madhara ya cathinone yanayopatikana katika Mirungi ambayo kikemikali inafanana na amphetamine, na hivyo katika mwaka 1971 ikaorodheshwa na United Nation kuwa ni miongoni mwa madawa ya kulevya.

Bwana mmoja kutoka Canada ajulikanaye kama Mathew Bryden aliyekuwa akifanya kazi na mashirika ya msaada kwa miaka mitatu huko Somalia anasema, “Watumiaji wengi wa Mirungi wamejikuta wakipambana na msisimko wake ili waweze kupata usingizi au hata kufanya kazi kisawasawa. Wanaelekea kwenye pombe au madawa ili kupata mapumziko au kupunguza hali ya wasiwasi. “Hali ilivyo Mogadishu ni watu kutawaliwa na nguvu za Mirungi, madawa au pombe,” Bwana Bryden anaendelea, “Unakuwa umevurugikiwa kabisa. Ima uharibikiwe kikamilifu au upoteze mwelekeo wa hali halisi.”



Utumiaji wa Mirungi husababisha madhara mbalimbali kiafya kama:

  1. Magonjwa ya vidonda vya tumbo (ulcers);

  1. Ukosefu wa haja kubwa (constipation);

  1. Utumiaji wa muda mrefu husababisha kuharibu utendaji kazi wa ini, na pia kusababisha ubadilikaji rangi meno, kudhoofika, na fizi kuuma na harufu ya mdomo;

  1. Upungufu wa msukumo wa kufanya jimaa (sex drive). Na pia kuwahi kumaliza haraka na kutoweza kudumu kwenye tendo la ndoa kwa muda mrefu;

  1. Kupatwa na ugonjwa wa futuru/futuri/bawasiri/baasili – nyama inayoota kwenye utupu wa nyuma;

  1. Upungufu wa usingizi;

  1. Humpelekea mlaji kutawaliwa nayo (Addiction);

  1. Walaji wengi huvuta na sigara, hata yule aliyekuwa havuti kabla ya kuanza kula Mirungi, hujikuta akizama kwenye uvutaji, na madhara huwa maradufu;

  1. Madhara ambayo bado kinamama walaji Mirungi hawajagundua ni kwamba mtoto anayezaliwa na mama mlaji Mirungi mara nyingi hukataa kunyonya titi la mama yake kwa sababu ladha ya maziwa inabadilika kwa ajili ya utumiaji wa madawa (pesticides) unaotumiwa na wakulima wa Mirungi kama inavyoeleza utafiti uliofanyika na Chuo Kikuu Cha Aden (Aden University). Utafiti huo unazidi kueleza ya kwamba aina ya madawa yanayotumiwa na wakulima ni zaidi ya 118 (na nyingi katika hizo ni katika zile zilizokatazwa kisheria [illegal pesticides]) na ambazo zinasababisha asilimia 70 ya ugonjwa wa saratani (cancer) huko Yemen.

  1.  Utafiti mwengine kule Ethiopia unatueleza ya kuwa mtoto wa mama mwenye kula Mirungi kwa wingi huwa hana uzito wa kawaida wakati wa kuzaliwa.

  1.  Ukosefu wa hamu ya kula chakula na mengi mengine.


Madhara Ya Kiuchumi Na Kijamii

  1. Kuwa na taifa la wavivu wapenda starehe wasiotumika;

  1. Jamii ya Kiislamu iliyo chafu kimaadili na isiyosimamisha ‘Ibaadah;

  1. Harakati za kunyanyua uchumi kuwa duni, harakati na juhudi zinazopatikana huwa ni za kuwazika na kutajika tu. Anapokuwa mtu amesha'khazin' fundo lake la Mrungi kwenye shavu lake linalovimba kama pulizo kwa kujaa ‘taksima’, hapo atakuwa anatoa mipango na mikakati mizito mizito ya kujenga maghorofa, kuanzisha miradi ya mamilioni..lakini yote ni mipango inayopangwa na ‘Handas’ na ‘Nakhwa’, baada ya kutemwa gomba, mipango yote iliyokuwa ikipangwa huyeyuka na kuwa kama ngano za Alinacha….hapo tena husubiriwa siku ya pili ya kusagwa na mipango yake mingine ya mamilioni ya kuwazika;

  1. Kulala mchana kutwa – kukosekana harakati na michakato ya utafutaji rizki;
  2. Kuzidi kwa omba omba – bila shaka ikiwa watu hulala mchana mzima na hawahangaiki kufanya kazi, kinachotarajiwa ni kuzidi kwa wanyanyua mikono na wainamisha vichwa wanaoongea kwa huzuni kama waliofiwa wakati wanatupa makombora yao ya maombi;

  1. Vijana wa mjini hawataki kuajiriwa – kwa sababu wanajiona ni ma-alwatwan, kwa hiyo –kwa mtazamo wao- haiwezekani kwao kutumwa au kuajiriwa! Matokeo yake uchumi wa wakazi wa mjini kuporomoka na mwisho wake ni wao kukodisha nyumba zao kwa wageni (wanaotoka miji ya mbali) zikawa maduka, na mwisho wake hufikia kuuza hizo nyumba zao ambazo wamerithi kutoka kwa wazee wao waliokuwa wakihangaika na kuchapa kazi;

  1. Huwapelekea baadhi yao kujidunisha na kuwatumikia mabwana wakubwa si kwa lingine ila kwa ajili ya kilo ya Mirungi.



Vituko Na Mikasa Vya Mirungi Na Walaji Mirungi

(Kama inavyoitwa petroli “dhahabu nyeusi,” Mirungi inaitwa na walaji wake “dhahabu ya kijani”).

Matukio yafuatayo hapa chini ni ya kweli yamewahi kutokea na hakuna kilichozidishwa; yanathibitishwa na walaji katika sehemu hizo:


1.     Mmoja wa wasagaji Mirungi alipohandasika alitundika koti lake pale alipo nzi ukutani akidhani ni msumari, na la kushangaza zaidi, ni pindi nzi yule aliporuka kuhamia kwengine, bwana yule alimfuata pale anapotua na kujaribu kutundika koti lake kwa mara ya pili.

2.     Mwengine alijigonga kwenye mti wa stima barabarani na kuuomba msamaha akidhani amemgonga mpita njia mwenzake.

3.     Na kuna tukio la kuhuzunisha huko Arusha na Mombasa, ni pale walipokuwa wakila Mirungi na kutazama sinema chafu, nyumba hiyo ambayo wamebandika Aayah za Qur-aan kwenye kuta –hali ya kuidhalilisha Qur-aan kuifanya ni mapambo na kupoteza lengo la kushushwa kwake-, baada ya kuwa wanatazama maasi yao, mmoja wao akashtuka na kusema ‘AstaghfiruLlaah!!’ na kukimbia kuigeuza ile fremu ya Aayah za Qur-aan kwa sababu aliona ni kuivunjia heshima! Na baada ya kumaliza maasi yao, wakaigeuza fremu ili zile Aayah zirejee kuonekana tena kama awali. Mwengine huko Mombasa alikuwa na gazeti lake la kufunika hizo Aayah pindi anapoanza kutazama balaa hizo, na akimaliza hutoa gazeti hilo ambalo huwa ni kwa kazi hiyo.

4.     Kuna mmoja wa walaji Mirungi alikamatwa huko Arusha na kupelekwa kituoni – kama tulivyosema awali ni tukio la nadra mtu kutiwa ndani kwa kula Mirungi- na wenzake waliposikia, wakamfuata kituoni kumtoa, lakini hawakukumbuka kuwa mashavuni mwao wamejaza taksima ya Mirungi na hali wako kituoni.

5.     Mlaji mmoja baada ya kupata ‘Nakhwa’ iliyomkolea, wakati walipomaliza kikao chao cha Mirungi akaondoka amevaa viatu vya mwengine; alipofika mbele ya safari na kutanabahi, tayari akabaki kwenye tahayuri ya kujiona kuwa atashukiwa kwa wizi na hali ilikuwa ni raha za ‘Nakhwa’.

6.     Dereva mmoja wa Taksi huko Arusha alikuwa amembeba abiria mzungu aliyekuwa akielekea kituo cha ndege cha KIA (Kilimanjaro International Airport) ambacho kipo katikati ya mji wa Arusha na Moshi, kwa kupandwa na ‘Handasi’, alijikuta akikipita kituo hicho na kufika Moshi mjini. Akaanza kuuliza kituo kiko wapi – pamoja na kwamba anakijua kilipo kituo ila ni ulevi wa Mirungi umempoteza-, akaulizwa ‘Kwani wewe umetokea wapi?’ Akajibu, ‘Arusha’, akaambiwa, ‘Mbona kituo umekipita huko nyuma kabla hujaingia Moshi?’…akachanganyikiwa na kuanza kurudi kwa kasi, hata alipofika kituoni, mzungu keshakosa ndege!!

7.      Na huko Australia: Bwana na Bibi McDavitt wa huko Perth (Australia) walipewa “zawadi” ya mmea na rafiki yao wa Kiafrika ili wauoteshe katika bustani yao kubwa nzuri iliyopo mbele ya nyumba yao. Mti ulikuwa mkubwa na mzuri wa kuvutia. Mti ulipokuwa mkubwa kiasi, rafiki yake wa Kiafrika aliomba apunguze (pruning) majani na matawi ya huo mti huo ili uendelee kuwa mkubwa na wa kuvutia. Mtindo huu uliendelea mara kwa mara na kila mara mti unapoanza kuchipuwa vizuri, yule rafiki Mwafrika akawa anakuja na kuomba kupunguza matawi na majani kama ilivyo kawaida yake. Lakini siku moja, Bwana na Bibi McDavitt walishtuka walipoona watu wengine wa Kiafrika (na sio rafiki yao wa kila siku) wakikata matawi bila ya rukhsa yao. Hapo ndipo walipopatwa na wasiwasi kuhusu mti huo. Na baadaye wakagundua ya kuwa mti huo ni mti wa Mirungi! Wakaamua kuukata.

8.     Na Djibouti: Tani kumi za Mirungi hupelekwa kila siku kwa ndege kutoka Ethiopia kuelekea Djibouti. Katika uwanja wa ndege, hakuna mgeni anayengojewa kwa hamu kama mgeni huyo (Mirungi). Zaidi ya magari 300 yanakuwa tayari kwenye kiwanja cha ndege kumpokea “mgeni” huyo wa thamani. Wafanya biashara wa Mirungi wanaitwa ‘Masultani wa Qaat.’ Ilitokea siku moja watu kushikwa na kiwewe kiwanja cha ndege walipopata habari ya kwamba huenda Mirungi isiwasili siku hiyo kwa sababu fulani fulani. Ilitokea fujo katika nchi na ilikuwa ni siku ya huzuni na watu waligoma kuondoka kiwanja cha ndege. Punde si punde, ndege iliwasili na watu walipopata habari hiyo, basi walikumbatiana kwa furaha na kupeana mikono kama vile ni Siku Kuu (‘Iyd). Djibouti imekataa kupiga marufuku mirungi kwa sababu inaingiza serikalini kila mwaka faida ya dollar 15,000,000.- Kwa hivyo, umefanya mkataba wa Kiserikali baina ya Djibouti na Ethiopia kuhusu kutochelewesha mirungi hata siku moja.

Hayo ni matukio machache kati ya matukio mengi yasiyo na idadi ambayo kurasa haziwezi kuorodhesha zote. Matukio yanayosemekana kutokea huko Yemen, Ethiopia, Kenya na Somalia yanawezwa kuandikwa vitabu kwa vitabu.

In shaa Allaah tutamalizia makala hii kwa kuona namna Wanachuoni mbalimbali walivyolieleza tatizo hili na kunyambua hukmu ya Uharamu wake kutoka katika viini vya Shari’ah ya Diyn yetu safi isiyo na nafasi ya uchafu na uraibu wowote wa kiwendawazimu.
 **********************************************************************************