Mar 22, 2016

Salma said: Hivi ndivyo nilivyotekwa

Pg 3NA WAANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MWANDISHI wa habari wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani  (DW) na Mwakilishi wa Mwananchi Communications, Salma Said Humud, jana aliibuka na kusimulia jinsi alivyotekwa na watu wasiojulikana alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam akitokea Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Baraza la Habari Tanzania (MCT) jana, Salima alisimulia mkasa mzima ulioghubika kutekwa kwake.

Akionekana mwenye huzuni muda wote, alisema waliomteka walimpiga na kumsababishia maumivu makali kwenye mwili wake.

“Nilitekwa saa chache baada ya kuteremka kwenye ndege nikitokea Zanzibar saa 8:00 mchana.  

Nilimtafuta dereva wangu kwa simu   aweze kunipeleka hospitali kwa ajili ya kupima afya yangu.

“Dereva hakupatikana kwa simu, lakini wakati natafuta gari jingine ndiyo ilitokea teksi na kunitaka niingie katika gari hiyo.

“Nilikataa ndipo walipoamua kunivuta ndani kwa nguvu na kumkuta kijana mmoja mfupi ambaye alinipiga kibao akinitaka kufunika macho yangu kwa baibui nililokuwa nimelivaa,”alisema Salma.

Katika simulizi hiyo, mwandishi huyo alisema baada ya kufunika uso wake hakujua alikopelekwa hadi alipojikuta yupo ndani ya jumba ambako alipigwa mateke na mabuti na kumsababishia maamivu makubwa   katika mwili wake.

Alisema wakati wakiendelea kumpiga, watekaji  wawili walimtaka kuacha kazi ya kuripoti matukio ya Uchaguzi wa Zanzibar.

Watekaji hao walikuwa wakimtajia matukio mengine yaliyowawahi kuwatokea watu wengine akiwamo  Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari 2006 Ltd, Absalom Kibanda   na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (Malt), Steven Ulimboka.

“Baada ya kunipiga sana walitoka nje ndipo nami nilichukua  simu yangu ya mkononi na kumtumia meseji mume wangu kumuarifu kuwa nimekamatwa na baada ya hapo nilipiga simu ofisini (DW) kuwaambia nipo mahali pabaya,” alisema.

Alisema watu hao waliporudi na kukuta akiwa na  simu mkononi walimpiga sana hadi akaishiwa nguvu.

“Waliniambia hawataki kuniua isipokuwa shida yao ni kutaka kunidhibiti nisiendelee kuripoti habari za uchaguzi wa marudio Zanzibar.

“Walinirudisha maeneo ya waliponichukua majira ya saa 11 alfajiri na kunitaka nijifunike uso hadi waondoke ndipo nijifunue.

“Nilijikuta nipo maeneo ya Uwanja wa Ndege, nilijikokota  hadi kituo cha daladala ambako nilikutana na mama mmoja aliyenihoji hali yangu na alinitaka nipumzike.  

Baadaye alinisaidia kusimamisha daladala kwenda hospitali ya Aghakan,” alisema.

Alisema baada ya kufika katika Hospitali ya Aghkan hakumkuta daktari wake wa moyo ambaye humtibu hivyo aliamua kwenda Hospitali ya Regency.

Baada ya kufanyiwa vipimo   baadaye aliwatafuta watu mbalimbali akiwamo Mratibu wa Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu,Onesmo ole Ngurumwa.

Akizungumzia hali ya Zanzibar,alisema kuna matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wananchi kukamatwa, kupigwa na kutupwa nje ya miji, vituko ambavyo  vimekuwa vikifanywa na vyombo vya usalama kwa kushirikiana na kundi liitwalo mazombi.

Alisema awali alikuwa akipokea simu za vitisho pamoja na ujumbe mara kwa mara lakini licha ya kuripoti vituo vya polisi hakuna jitihada zilizokuwa zikichukuliwa.

Naye Mratibu wa Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu,Onesmo ole Ngurumwa alisema baada ya kupata taarifa za kupotea kwa mwandishi huyo alimuarifu Msaidizi wa IGP   na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni lakini hakuna walichokifanya.

Regency wamkana
Hospitali ya Regency ambayo Salma alisema alitibiwa, jana  ilikana kumpokea mgonjwa mwenye jina la Salma.

Akizungumza na gazeti hili huku akiombwa asitajwe jina lake kwa kuwa si msemaji wa hospitali hiyo, muuguzi wa zamu aliwaambia waandishi wa MTANZANIA kuwa  hakukuwa na mgonjwa mwenye jina la Salma Said ambaye alidai kutekwa na watu wasiojulikana.

Alisema  idadi ya wagonjwa waliofika kwenye hospitali hiyo wameandikwa kwenye kitabu cha mapokezi pamoja na taarifa zao, hivyo aliwataka waandishi hao kukagua daftari hilo na kujiridhisha  kama mgonjwa huyo yupo.
 
 Mwandishi wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Salma Said akiwa ameshikiliwa na mwandishi mwenzake, Kelvin Matandiko alipokuwa akiondoka katika Kituo cha Polisi cha Kati baada ya kuhojiwa, juzi usiku

0 comments:

Post a Comment