Maalim Seif Shariff Hamad, Mgombea wa Urais wa Zanzibar katika
uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana kupitia Chama cha Wananchi (CUF),
amesema CUF haitashiriki uchaguzi wowote chini ya Tume ya Jecha Salim
Jecha, anaandika Josephat Isango.
Akizungumza na MwanaHALISI Online Hoteli ya Serena ambapo yupo kwa
mapumziko baada ya kulazwa, Maalim Seif amesema kuwa kama yatatokea
maridhiano yatakaoongozwa na kusimamiwa na taasisi huru za kidemokrasia,
bila vitisho vya majeshi na polisi, kuwa na vyombo huru vya habari na
tume huru sio hii iliyopo Zanzibar chini ya Jecha, hapo CUF kitaweza
kufikiri kushiriki uchaguzi.
Ameongeza kuwa harakati za kudai haki, zitaendelea kwa njia ya amani
ili marekebisho ya tume yafanyike kwani kwa utaratibu uliopo hata mwaka
2020 upinzani ukishinda Tanzania bara, Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kitang’gang’ania madaraka.
“CUF tunaamini katika amani, tusichafue amani, tusichafue nchi yetu,
tuendeleze mapambano kwa kutoitambua serikali iliyojiweka madarakani
katika uchaguzi haramu wa Machi 20 mwaka huu, wala hatutaipatia
ushirikiano wowote katika mambo yote” alisema.
Uchaguzi wa 20 Machi, sio halali. Jecha hakuwa na uwezo wa kisheria
wala kikatiba kufuta uchaguzi, mgogoro uliopo sasa umesababishwa na
Jecha, ukapewa baraka za CCM, sababu CCM hawataki kushindwa, na hawataki
wapinzani kuongoza. Kila CCM ikishindwa hutoa visingizio.
“Kabla Kikwete (Rais Mstaafu Jakaya Kikwete) hajaondoka madarakani,
aliniambia kuwa Maalim CCM wanakuogopa, wanajua ukishinda utaweza
kuvunja Muungano, lakini nilimwambia, CCM ndio wenye jeshi, wenyewe ndio
wenye dola mimi nitavunjaje Muungano? Hiyo ni hofu na visingizio tu ili
waendelee kukwapua madaraka.”Alisema.
Ameweka bayana kuwa kwa sasa CCM imewarejesha wananchi miaka 20
iliyopita, kwani uhasama wa watu kutengana kwenye shughuli za kijamii
kwa sababu za tofauti za kisiasa zimeanza kurejea baada ya CCM
kulazimisha kukwapua madaraka ya wananchi kwa kufuta uchaguzi wa 25
Oktoba mwaka jana.
Akizungumzia suala la Muungano kama ambavyo amekuwa akihusishwa
Maalim seif amesema kuwa sasa Muungano utavunjwa na CCM, sio CUF wala
yeye kama wanavyosingizia.
Ameongeza kuwa kwa sababu CCM ya bara ndio inalazimisha kuweka
viongozi waliokataliwa na wananchi wa Zanzibar na chama chao kwa kutumia
majeshi na polisi wao ndio husababisha wananchi wachukie Muungano.
Aidha kuhusu uchaguzi wa marudio wa Machi 20, Seif amesema kuwa CUF
imeshinda, kwani wananchi wa Zanzibar waliitikia wito wa CUF, wakasusa,
hawakujitokeza kupiga kura. Hizo zilizotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC) wanajua walipozipata wao na CCM.
“Mimi nilishasema tangu awali, kuwa matokeo yameshajulikana kabla ya
uchaguzi, sababu ni ya kupika, namhurumia Dk Shein kwa kujisifu kupata
kura ambazo hazipo, mawakala waliweka wao na wasimamizi na kuna taarifa
kuwa wapiga kura walikuwa wanapewa rundo la kura, wapige na kutumbukiza
ili kukidhi matakwa ya CCM.” Amesema Maalim Seif.
Maalim Seif amewatakia utulivu Wazanzibar wote, na kuwaarifu kuwa
afya yake ni imara, na atarejea Zanzibar wakati wowote kuungana nao.
Mar 25, 2016
CCM WANAKUOGOPA MAALIM SEIF; JAKAYA KIKWETE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment