Afisa mdhamini wa tume ya uchaguzi
Zanzibar (ZEC), Ali Mohamed Dadi amesema mshindi wa uwakilishi katika
jimbo la Ziwani ni Suleiman Ali wa CCM na si Asaa Hamad wa UPDP ambae
alitangazwa awali.
Dadi kutoka ofisi ndogo ya Pemba alisema jana kuwa msimamizi wa
uchaguzi katika wilaya ya Chakechake, Othman Khamis alikosea wakati wa
kujaza karatasi ya matokeo ya mshindi wa jimbo hilo.
“Nimezungumza naye na amesema kwamba alitoa ufafanuzi kuwa walifanya
makosa katika kuandika matokeo, hivyo aliyeshinda ni mgombea wa CCM,”
alisema.
Katika karatasi hiyo ya matokeo iliyokuwa imebandikwa ukutani, Asaa
Ali Hamad alionekana kuwa amepata kura 221 dhidi ya 121 za mgombea wa
CCM, lakini kwa ufafanuzi huo waZEC hakuna chama cha upinzani
kilichoshinda nafasi ya uwakilishi au udiwani.
Kwa matokeo hayo, CCM imeshinda majimbo yote ya uwakilishi Unguja na
Pemba na hivyo kuzidisha utata kwa rais mteule, Dk.Ali Mohamed Shein
anayeapishwa leo, kuunda serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) kwa mujibu
wa ibara ya 9 (3) ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 2010.
Awali, kulikuwa na uwezekano wa UPDP kutoa mteule wa nafasi ya makamu
wa kwanza wa rais kwa kuwa kilitangazwa kimakosa kupata kiti cha
uwakilishi baada ya CCM lakini baada ya ufafanuzi huo wa ZEC matumaini
hayo yameyeyuka.
Kuyeyuka kwa ndoto hiyo ya UPDP kunamaanisha kwamba hakuna chama
kilichoshika nafasi ya pili kwakupata kura asilimia 10 au zaidi, ambacho
kwa mujibu wa katiba hiyo kingekuwa na nafasi ya moja kwa moja kutoa
makamu wa kwanza wa rais na baadae mawaziri wa upinzani kuunda SUK.
Tangu Dk.Shein atangazwe kushinda urais katika uchaguzi wa marudio
baada ya matokeo ya ule wa awali kufutwa, mjadala mkubwa kwenye vyombo
vya habari na mitandao ya kijamii umekuwa ni jinsi gani atateua serikali
yake kukidhi matakwa ya katiba ya kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa
ili kuendeleza maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa baina ya CCM na CUF
kabla ya uchaguzi wa 2010.
Wakati naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai akisema rais
Shein atatumia busara zake kumpata makamu wa kwanza wa rais, baadhi ya
wanasheria wamesema hawaoni ufumbuzi wa moja kwa moja kutokana na
upungufu huo wa kikatiba.
Kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, rais atateua makamu wa kwanza wa
rais kutoka chama kilichoshika nafasi ya pili na mgombea wake wa urais
kupata asilimia 10 ya kura za urais, au nafasi ya makamu wa kwanza
itaenda kwa chama chochote cha upinzani kilichoshika nafasi ya pili kwa
wingi wa viti vya majimbo katika baraza la wawakilishi.
Mar 25, 2016
Ushindi wa UPDP Ziwani Pemba waota mbawa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment