Wazazi mbaroni kwa kuozesha wanafunzi
polisi mkoani Mwanza inawashikilia wazazi wawili kwa tuhuma za kuwaozesha kwa wanaume watoto wao wa kike waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.Hatua ya kukamatwa kwa wazazi hao, Josefine Benjamin na Athuman Haruna wakazi wa Kata ya Igogo jijini hapa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga kwa watendaji wa kata zote kufanya tathmini ili kubaini wanafunzi ambao hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa.
Mtendaji wa Kata ya Igogo, Joseph Rulamye alisema uchunguzi uliofanywa kwenye kata hiyo ulioshirikisha walimu wakuu, ofisi ya kata na mratibu elimu ulibaini kuwa kuwapo kwa wanafunzi ambao wameozeshwa kwa wanaume baada ya wazazi wao kupokea mahari.
“Tuliwasaka na kuwatia mbaroni wazazi hawa ili watusaidie kuwapata watoto hao na wanaume waliowaoa,” alisema Rulamye.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi, kuwatafuta watoto hao na kuwasaka ‘waume’ zao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Akizungumzia tuhuma za kumuoza binti yake, mmoja wa wazazi, Athuman Haluna alidai hakushiriki njama hizo, badala yake akamtupia lawama bibi wa mtoto huyo akidai ndiye aliyesuka mipango ya mjukuu wake kuolewa badala ya kuendelea na masomo.
“Mtoto huyu anaishi na bibi yake, mimi nilikuwa najua tayari ameripoti shuleni. Bibi yake ndiye mhusika mkuu wa tuhuma hizi,” alidai Haruna.
Mratibu wa Elimu Kata ya Igogo, Charles Kialiga alisema ofisi yake kwa kushirikiana na mamlaka nyingine inaendelea kufuatilia taarifa za watoto wengine ambao hawajaripoti kwenye shule za umma walizopangiwa ili kubaini iwapo wamejiunga na shule binafsi au la.
Katika kikao chake na wakuu wa shule, waratibu elimu kata na watendaji wa kata zote za wilaya hiyo, Konisaga aliagiza uongozi wa kata kufuatilia taarifa za watoto wote waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari, lakini hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa.
Pia, aliwataka viongozi hao wa kata kwa kushirikiana na walimu wakuu wa shule za msingi na wenzao wa sekondari kubaini iwapo wanafunzi hao wako majumbani au wameozwa.
Serikali imeanza kutekeleza sera ya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari kwa kufuta ada na michango yote ili kutoa fursa kwa watoto wote kusoma bila kujali uwezo kiuchumi wa wazazi au walezi.
0 comments:
Post a Comment