Mar 28, 2016

ASKOFU: KANISA LINAPASWA KUJICHUNGUZA NA KUJIREKEBISHA KUTOKANA NA UOZO.


Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino Mokiwa.

Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino Mokiwa amewaonya wakristu dhidi ya mambo ambayo yanaelekea kulibomoa kanisa. Ameyasema hayo leo kwenye Ibada ya Pasaka ya kitaifa iliyofanyika Kanisa la Mtakatifu Albano Upanga jijini Dar es Salaam ambako pia Mkuu wa Mkoa Paul Makonda amehudhuria.

Askofu Mokiwa ameyaita mambo hayo yanayolibomoa kanisa kama mawe na kuyataja kuwa ni pamoja na mashindano miongoni mwa madhehebu ya kikristo. 


Amesema kanisa linapaswa kujichunguza na kujirekebisha kutokana na uozo unaofanyika. Alisema madhehebu yanashindana katika kumiliki vitu kama vile shule au hospitali baada ya kumuhubiri Kristo.

Ameyataja mambo mengine ambayo yanatishia uhai wa kanisa ni kitendo cha maaskofu, wachungaji mapadre na waumini kupgina vita. Amesema baadhi ya watumishi hao wa Mungu wamekosa utii na hawafuati taratibu za kanisa badala yake wamejenga tabia ya kusemana vibaya, kutukanana na kupanga mapinduzi ya kupindua wengine.

“Kusemana, kusingiziana na kusema uongo yamekuwa mambo ya kawaida, na ukiwaita wahusika ili myazungumze wanakimbia na hawako tayari kufanya hivyo, nguvu ya makundi ndani ya kanisa inatisha kiasi kwamba chuki ni kubwa na watu hawapendani,” alisema Askofu Mokiwa.

Aidha ameonya nguvu ya fedha kutumika kulivuruga kanisa. Amehoji kama watu wana fedha kwa nini hawaendi kusaidia watoto yatima au kuchangia uenezaji wa Injili badala ya kutumia fedha hizo kulivuruga kanisa? Amesema watu wanafanyabiashara kanisani badala ya kuhubiri Injili.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaonya waumini wenye tabia ya kumpigia simu na kuomba apeleke polisi kanisani kwa sababu ya vurugu. 


Makonda amesema mtu atakayefanya hivyo kuanzia sasa atashughulika naye kwa sababu kanisa lina taratibu zake za kushughulikia migogoro na siyo kupeleka polisi, kwani ni mambo ya aibu

0 comments:

Post a Comment