Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kasi ya
uwekezaji nchini inaweza kuongezeka mara dufu iwapo wananchi
watazingatia zaidi uimarishaji wa mazingira hasa katika mtandao wa
mawasiliano.
Alisema wawekezaji wengi huvutika na hali ya mazingira safi
yanayowashawishi kupanua wigo wa mtandao huo ambao husaidia kupatikana
kwa huduma zote za msingi za mawasiliano kwa upande wa simu, posta na
utangazaji.
Balozi Seif alieleza hayo wakati akizindua mtambo maalum wa
usimamizi wa masafa ya mawasiliano Zanzibar hafla iliyofanyika katika
Ofisi ya Mamlaka ya mawasiliano Tanzania { TCRA } iliyopo Chukwani nje
kidogo ya Maji wa Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha mfuko wa
mawasiliano kwa wote ili kuunga mkono juhudi za wawekezaji binafsi na
washirika wa maendeleo katika ujenzi wa miundo mbinu ya mawasiliano
kwenye maeneo ya vijijini ambayo kibiashara bado hayajavutia wawekezaji.
Alieleza kwamba Serikali imefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010
na Dira ya Taifa ya Tanzania ya mwaka 2015.
Balozi Seif alisema ujio wa wawekezaji hao umesaidia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa gharama za mawasiliano ya simu na utangazaji ikiwa ni pamoja na kuongeza pato la Taifa.
“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefarajika kwa kutimiza wajibu
wenu na kuhakikisha kuwa Zanzibar pia inakuwa na uwezo wa kusimamia
masafa muda wote bila ya kusubiri mtandao kama huo kutoka Tanzania Bara
“. Alisisitiza Balozi Seif.
“ Nafurahi kuona Tanzania hivi sasa inajipanga kwenda kisasa zaidi “. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment