DARSA


DARSA YA ZAKKAH

Naam leo tunaanza darasa jipya ambalo ni nguzo ya TATU katika moja wapo ya nguzo  TANO za Kiislam nayo ZAKAAH.

       🔹UTANGULIZI🔹

Kutoa Zakaah ni nguzo ya tatu ya Islam. Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"Nguzo za Uislam ni tano. Shahada kuwa hapana Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa ALLAAH, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Kusimamisha Swalah, na Kutoa Zakaah, na Kufunga mwezi wa Ramadhan na Kuhiji Makka kwa mwenye uwezo wa kufika huko".


🔸Kufaridhishwa kwa Zakaah ni jambo muhimu na tukufu sana kwa Waislam kwa sababu ya wingi wa faida yake na kwa ajili ya haja kubwa ya kuwepo kwa jambo hilo, kutokana na masikini na mafakiri wanaohitajia sana msaada wa ndugu zao wenye uwezo, kwani katika Kutoa Zakaah uhusiano mzuri unajengeka baina ya Waislam matajiri na Waislam masikini, na hii ni kwa sababu siku zote moyo wa mtu huelekea na kumpenda yule anayemfanyia wema na ihsani. Zakaah inasaidia pia katika kuzisafisha na kuzitakasa nyoyo.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

● خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا


" Chukuwa Swadaqah katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Swadaqah zao)".
[ At-Tawbah: 103 ]


Katika kutoa Zakaah au Swadaqah kunaizoesha nafsi katika kuwapendelea kheri watu wenye haja na katika kuwaonea huruma na pia kunaipatia nafsi baraka nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Subhanaahu wa Ta’ala.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

● وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ

"Na chochote mtakachotoa, basi Yeye Atakilipa; naye ni Mbora wa wanaoruzuku".
[ Saba-a - 39 ].


Na Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema :-

" Mwenyezi Mungu Anasema :-  '' Ewe mwanadamu, toa na sisi tutakupa ".

Anasema Ibn Uthaymiyn:-

"Kutoa Zakaah ni jambo liliofaradhishwa katika Uislam, na ni nguzo muhimu sana baada ya SHAHADA MBILI na SWALAH, na dalili ya kuwajibika kwake imo ndani ya Qur-aan na pia katika mafundisho ya Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam), pamoja na ijmai ya Waislam, na yeyote anayeikanusha nguzo hii anakuwa Kafir aliyeritadi katika Uislam, na hukumu yake ni kutubishwa, na akitubu anasamehewa.
Ama akikataa kutubu na akaendelea kuikanusha basi hukmu yake ni kuuliwa.

Ama anayeifanyia ubakhili au akapunguza katika Zakaah yake, huyo anakuwa miongoni mwa madhalimu wanaostahiki adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

● وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ

"Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Mwenyezi Mungu, wape habari za adhabu inayoumiza inayowangoja.

Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahanamu, na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, (na huku wanaambia); "Haya ndiyo (yale mali) mliyojilimbikia (mliyojikusanyia) nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya."
[ At-Tawbah - 34 - 35 ]



● "Miongoni mwa faida za kutoa Zakaah anazozipata mtu katika dini yake" anaendelea kusema Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn, "Ni kuitimiza nguzo katika nguzo za Kiislam, jambo litakalomletea mtu furaha katika dunia yake na katika akhera yake, na pia inazidi kumkaribisha mja kwa Mola wake na kumuongezea Imani,kama ilivyo katika mambo yote ya kumtii Mwenyezi Mungu Subhanaahu wa Ta’ala."



🔹HUKMU YA ASIYETOA         ZAKAAH.


Kutoa Zakaah ni fardhi, na ni katika mambo waliyokubaliana maulamaa wote kuwa yeyote anayeikanusha fardhi hii anakuwa kesha toka katika dini akiwa ni kafiri aliyertadi, isipokuwa kama mtu huyo ni Muislam mpya, na kwa ajili hiyo husameheka kutokana na kutoelewa kwake.

Ama yule anayeacha kutoa Zakaah lakini wakati huo huo hakanushi kuwajibika kwake, huyo anapata dhambi ya kuacha kuitoa, lakini kuacha huko hakumtoi katika dini, isipokuwa ikiwa anaishi katika nchi inayohukumiwa na shari’ah ya Kiislam, basi anayehukumu atatakiwa aichukuwe Zakaah hiyo kwa nguvu.


🔸Ipo hitilafu baina ya maulamaa iwapo anayeacha kutoa Zakaah atozwe gharama kwa kuacha kwake huko kwa ajili ya kumtia adabu, na gharama yenyewe ni kuchukuliwa nusu ya mali yake, na hii inatokana na Hadiyth iliyotolewa na Imaam Ahmad na Annasaiy na Abu Daawuud na Al-Haakim na Al-Bayhaqiy kutoka kwa Bahza bin Hakim kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake kuwa amesema:-

"Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akisema:-

"…Atakayekataa (kutoa Zakaah) tutaichukuwa (kwa nguvu, na pia tutachukua) pamoja na nusu ya mali yake haki katika haki ya Mola wetu Mtukufu na watu wa Aali Muhammad si halali kwao kuchukuwa chochote katika hiyo (Zakaah)".

Amesema Imaam Ahmad kuwa isnadi ya Hadiyth hii ni sahihi na amesema Al Hakim kuwa hii ni Hadiyth sahihi.

🔸Hata hivyo wapo baadhi ya maulamaa walioidhoofisha Hadiyth hii na wengine wakasema kuwa hukmu hii ilifutwa baadaye, wakiegemea baadhi ya Hadiyth zinazoelezea juu ya baadhi ya watu waliochelewa kulipa Zakaah na Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) hakuwachukulia nusu ya mali zao.

Ama ikiwa watu watakataa kutoa Zakaah wakiwa wanaelewa kuwa ni jambo la wajibu, na ikiwa zipo nguvu za kuweza kupambana nao, basi watapigwa vita mpaka wakubali kuitoa. Na hii inatokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim kuwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya LLAAHU ‘anhu) amesema kuwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahada ya; LAA ILAAHA ILLA ALLAAH MUHAMMADAN RASULU LLAAH, na wasimamishe Swalah na watowe Zakaah. Wakishafanya hivyo, damu yao na mali yao zitakingika kwangu isipokuwa katika kulipa haki za Kiislam, na hesabu yao iko kwa Mwenyezi Mungu".


Imeelezwa na Abu Hurayrah (Radhiya LLAAHU ‘anhu) kuwa; Alipofariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) na Abu Bakr akawa (Khalifa), baadhi ya waarabu walikataa kutoa Zakaah, na Abu Bakr (Radhiya LLAAHU ‘anhu) alitayarisha jeshi la kupambana nao.

‘Umar akasema (kumuuliza Abu Bakr):-

"Vipi unataka kupigana vita na watu (Waislam), wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alisema:-

"Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahada ya; LAA ILAAHA ILLA ALLAAH na atakayetamka hayo itakingika kwangu mali
 yake na nafsi yake isipokuwa katika haki yake (anayodaiwa au kisasi kwa makosa aliyofanya), na hesabu yake iko kwa Mwenyezi Mungu?”

Abu Bakr (Radhiya LLAAHU ‘anhu) akasema:-

"WALLAAHI !! nitampiga vita yeyote atakayetenganisha baina ya Swalah na Zakaah, kwa sababu Zakaah ni katika 'haki yake' (shahada hiyo). WALLAAHI !! lau kama wataacha kunipa mbuzi mdogo (na katika riwaya nyingine 'Kamba') iliyokuwa ikilipwa wakati wa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam), ningewapiga vita kwa kukataa kwao kuitoa".

‘Umar (Radhiya LLAAHU ‘anhu) akasema:-

"WALLAAHI !! nilipoona kuwa Mwenyezi Mungu amemfungulia Abu Bakr kifua chake aamue kuwapiga vita, nikajuwa kuwa yuko katika haki".
[ Muslim - Abu Daawuud - na Attirmidhy na maImaamu wengine wa Hadiyth.]

 In Shaa ALLAAH Itaendelea.
[1:25 AM, 3/11/2016] Dr jimy: Assalaam 'Alaykum Warahmatul LLAAHI Wabarakaatuh.

Naam tunaendelea na Darasa letu la Zakaah Leo tukiwa Sehemu ya nne.


   🔸SEHEMU YA NNE🔸


🔹UMUHIMU WAKE
 ( KATIKA SUNNAH ).


Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema :-

"Mambo matatu naapa juu yake na nakuhadithieni Hadiyth muihifadhi (vizuri).

Mali haipungui kwa kutoka Swadaqah, na mtu anapodhulumiwa akasubiri, basi Mwenyezi Mungu humuongezea utukufu, na mtu anapojifungulia mlango wa kuombaomba, basi Mwenyezi Mungu humfungulia mlango wa ufakiri ".
[ (At-Tirmidhiy kutoka kwa Abi Kabshah Al-Anmaary (Radhiya LLAAHU ‘anhum) ]



Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya LLAAHU ‘anhu) amesema kuwa; Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema :-

"Hakika Mwenyezi Mungu anazikubali Swadaqah na anazipokea kwa mkono wake wa kuume na anailea kama mmoja wenu anavyomlea nyumbu wake mpaka tonge (anayoitoa Swadaqah) inafikia ukubwa wa jabali Uhud ".
[ Ahmad - At-Tirmidhiy na ameisahihisha ].


🔹Hadithi hii inatujulisha kuwa mtu anapotoa Zakaah au Swadaqah, basi Zakaah hiyo inaingia mikononi mwa Mwenyezi Mungu Subhanaahu wa Ta’ala kwanza, kabla haijaingia mikononi mwa masikini anayepewa, ikitufahamisha jinsi gani Mwenyezi Mungu anavyoitukuza ‘Ibaadah hii ya Kutoa Zakaah na jinsi anavyompenda mja wake mwenye kutoa Zakaah au Swadaqah hata akaipokea kwa mikono yake Mwenyewe Subhanaahu wa Ta’ala kwanza, akaizidisha jaza yake na kuifanya iwe na ukubwa wa Jabali Uhud.



🔸Anasema Waki’i:

"Hadiyth hii pia inasadikisha kauli yake Subhanaahu wa Ta’ala katika Qur-aan pale Aliposema:-

● يَعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ

"Je! Hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba za waja Wake na kuzipokea Swadaqah?"
[ At-Tawbah: 104 ].


Na Aliposema:-

● يَمْحَقُ اللّهُ الْرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ

"Mwenyezi Mungu huyafutia (baraka mali ya) riba, na huyatia baraka (mali inayotolewa) Swadaqah".
[ Al-Baqarah - 276 ].


Imepokelewa kuwa Anas (Radhiya LLAAHU ‘anhu) amesema:-

"Mtu mmoja kutoka katika kabila la Bani Tamim alimwendea Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) na kumwambia:-

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi nina mali nyingi na nina jamaa wengi na wageni huja kwangu kwa wingi. Kwa hivyo nijulishe nini nifanye na vipi nitowe ?"

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akamwambia :-

"Utoe Zakaah kutoka katika mali yako, kwa sababu hiyo ni tohara itakayokutahirisha, na uwaendee watu wako (ndugu zako wa nasaba), na uijue haki ya masikini na ya jirani na ya muombaji".
[ Ahmad ].


Na Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya LLAAHU ‘anha) kuwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"Mambo matatu naapa juu yake, Mwenyezi Mungu hawezi kumfanya aliye na sehemu yake katika Uislam akawa sawa na yule asiye na sehemu. Na sehemu za Uislam ni tatu. Swalaah, Funga na Zakaah. Na Mwenyezi Mungu Anapokuwa pamoja na mja wake hapa duniani, basi huko akhera hamuachi akawa na mwengine asiyekuwa Yeye. Na mtu anayewapenda watu hapa duniani, basi siku ya Qiyaamah Mwenyezi Mungu Atamjaalie awe pamoja nao…"
[  Ahmad  ].


Na kutoka kwa Jaabir (Radhiya LLAAHU ‘anhu) amesema:-

"Mtu mmoja alimuuliza Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam);

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu; Unasemaje juu ya mtu anayetoa Zakaah ya mali yake ?"

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akasema :-

"Atakayetoa Zakaah ya mali yake, kesha iondoa shari yake ".



🔸SEHEMU YA PILI🔸
     Darasa la Zakaah


🔹 KUFARADHISHWA ZAKAAH.


Zakaah imefaradhishwa wakati Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alipokuwa Makka katika siku za mwanzo za Uislam, lakini hapakuwekwa Nisaab, (kiwango cha mali ambacho mtu akiwa nacho kwa muda wa mwaka analazimika kuitolea Zakaah), wala kiasi cha kulipa, isipokuwa waliachiwa Waislam wenyewe kukisia kiasi cha kutoa.


Katika mwaka wa Pili baada ya Hijra, ilifaradhishwa kiasi chake katika kila aina ya mali na kubainishwa vizuri.


🔸SEHEMU YA SITA🔸
     Darasa la Zakaak.

🔹WASIOTOA  ZAKAAH
       ( Katika Sunnah )

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya LLAAHU ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Atakayepewa mali kisha asitoe Zakaah yake, basi mali hiyo Siku ya Qiyaamah itageuzwa kuwa joka dume lenye upara, mwenye madoa mawili machoni (kutokana na wingi wa sumu aliyonayo), atajizungusha katika mwili wa mtu huyo, kisha atamkaba shingoni huku akimwambia:

"Mimi ndiyo hazina yako uliyokuwa ukiikusanya, mimi ndiyo mali yako", kisha Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akaisoma aya hii:

وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ

"Wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubakhili huko)".
[ Al-Bukhaariy na Muslim ]



Na kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar bin Al-Khattwaab - Radhiya LLAAHU ‘anhuma amesema kuwa; "Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Enyi watu wa Madina, mambo matano mkija mkapewa mtihani juu yake na kuteremshiwa - Najikinga kwa Mwenyezi Mungu yasije yakakukuteni - Hautoenea uzinzi katika kaumu mpaka wakafikia kujitangazia, (isipokuwa) yatakuja kuenea kwao maradhi (aina mpya) ambayo hayajakuwepo kwa waliowatangulia, na hawatopunjwa watu katika vipimo na katika mezani isipokuwa wataletewa umasikini na shida ya kupatikana vitu, na dhulma ya ufalme. Na watakapoacha (watu) kutoka Zakaah ya malizao, watanyimwa mvua, na lau kama si kwa ajili ya wanyama, basi isingenyesha mvua. Na watakapovunja ahadi ya Mwenyezi Mungu na ahadi ya Mtume wake, watasalitishiwa adui asiyekuwa mwenzao achukuwe baadhi ya vilivyo mikononi mwao. Na ikiwa viongozi wao hawatahukumu kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi vitafanywa vita vyao viwe bainayao"
[ Ibn Maajah – Al-Bazaar na Al-Bayhaqiy ].



 🔸SEHEMU YA TATU🔸


🔹 UMUHIMU WAKE
 (   KATIKA QUR-AAN.   )

Katika Qur-aan tukufu na katika Mafundisho ya Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam), yamo mafunzo mengi yanayopendekeza Kutoa Zakaah na yanayowakemea wale wasioitoa.

Katika Qur-aan Mwenyezi Mungu Anasema :-

● خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

"(Ewe Mtume) Chukua Swadaqah katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Swadaqah zao)".
[ At-Tawbah: 103 ].



Na maana yake ni "Chukua ewe Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) Swadaqah maalum kutoka katika mali za Waislam na uwape wanaostahiki ili wenye mali 'wasafike' kutokana na uchafu wa ubakhili na tamaa, na kutokana na ubaya wa kuwanyima masikini haki zao na pia 'uwatakase' nafsi zao kwa Swadaqah hizo na wapate baraka za Mola wao ili waweze kupata furaha za hapa duniani na za huko akhera.



Na Akasema :-

● إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ. آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ. كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ. وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ. وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ

"Hakika wachamungu watakuwa katika Mabustani na chemchem.
Wanapokea Aliyowapa Mola wao.
Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema.
Walikuwa wakilala kidogo tu nyakati za usiku.
Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira.
Na katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba".
[ Adh-Dhariyaat: 15-19 ].



Katika Aayah hii Mwenyezi Anatuelezea juu ya wale atakaowaingiza katika bustani Zake na chemchem, kwa sababu walipokuwa huko duniani walikuwa wenye kulala muda mfupi sananyakati za usiku, na sehemu kubwa ya usiku, walikuwa wakiswali, na nyakati za kabla ya kuingia alfajiri walikuwa wakiomba maghfira huku wakijikurubisha kwake Subhanaahu wa Ta’ala.



Walikuwa pia watu wenye kutoa katika mali zao kuwapa fakiri na maskini, wenye kuomba na wasiyo omba huku wakiwaonea huruma.

Na Mwenyezi Mungu Akasema pia:-

● وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللّهَ وَرَسُولَهُ أُوْلَـئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللّهُ إِنَّ اللّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

"Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Swalaah, na hutoa Zakaah, na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu Atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima".
[ At-Tawbah - 71 ].



🔹SEHEMU YA KWANZA🔹

     🔸Maana Ya Zakaah.

Zakaah ni ile haki Aliyoifaradhisha Mwenyezi Mungu kwa Muislam katika mali yake anayotakiwa kuwapa wanaostahiki. Neno Zakaah, katika lugha (katika kamusi ya lugha ya kiarabu) maana yake ni 'Kujitakasa', kwa sababu anayetoa Zakaah anataraji kuitakasa mali yake, nafsi yake na kupata baraka kutoka kwa Mola wake.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

● خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

"Chukua Swadaqah katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Swadaqah zao)".
[ At-Tawbah: 103 ].


🔸Zakaah ni nguzo ya TATU ya Uislam iliyofaradhishwa katika Qur-aan tukufu na katika mafundisho ya Mtume mtukufu (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam), na kwa sababu ya umuhimu wake, Mwenyezi Mungu ameitaja mara themanini na mbili katika Qur-aan kwa kuifuatanisha pamoja na Swalaah.


Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya LLAAHU ‘anhu) kuwa amesema:

"Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alipomteua Muadh bin Jabal (Radhiya LLAAHU ‘anhu) kuwa gavana wa nchi ya Yemen na kadhi wao alimwambia:-

"Unakwenda katika nchi ya watu wa Ahlul Kitab, kwa hivyo (kwanza) walinganie katika shahada ya LAA ILAAHA ILLA ALLAAH na kwamba mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Mwenyezi Mungu amewafaradhishia Swalah tano mchana na usiku, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Mwenyezi Mungu amewafaradhishia Swadaqah (Zakaah) za mali zao, zichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na kurejeshewa masikini wao, na kama wakitii juu ya hilo, usije ukachukuwa mali zao zenye thamani, na uiogope dua ya aliyedhulumiwa, kwani hapana kizuizi baina yake (dua hiyo) na baina ya Mwenyezi Mungu".

Imesimuliwa na MaImaamu wote wa Hadiyth

Imesimuliwa pia na At-Twabaraaniy kutoka kwa ‘Aliy (Radhiya LLAAHU ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"Mwenyezi Mungu amewafaradhishia matajiri wa Kiislam katika mali zao kiasi cha kuwatosha masikini wao. Na (masikini) wasingepata tabu ya njaa na mavazi isipokuwa kutokana na ubakhili wa matajiri wao. Jueni kuwa Mwenyezi Mungu atawahesabia hesabu nzito sana na atawapa adhabu iumizayo".




 🔸SEHEMU YA TANO🔸
        Darasa la Zakaah


🔹WASIOTOA  ZAKAAT.
      ( KATIKA QUR-AAN )



Mwenyezi Mungu Anasema:-

● وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ

"Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Mwenyezi Mungu, wape habari za adhabu inyoumiza inayowangoja.
Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahanamu, na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, (na huku wanaambia); "Haya ndiyo (yale mali) mliyojilimbikia (mliyojikusanyia) nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya."
[ At-Tawbah: 34 - 35 ].



Na akasema:-

● وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُواْ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ

"Wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubakhili huko). La, ni vibaya kwao. Watafungwa kongwa (madude ya kunasa shingoni) za yale waliyoyafanyia ubakhili - siku ya Qiyaamah. Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ana khabari za yote mnayoyafanya."
[ Aali-‘Imraan - 180 ].



Katika aya hii, Mwenyezi Mungu Amesema'Sayutwawwaquwna' na maana yake ni (Watafungwa kongwa) badala ya 'Sawfa yutwawwaquwna'. (Watakuja kufungwa kongwa).

Ameacha kutumia neno ‘Sawfa’ akaiunganisha moja kwa moja kwa kusema:- 'Sayutwawwaquwna' kwa ajili ya kutujulisha ukaribu wa mtu kukumbana na adhabu hizo. Kwa sababu mtu akeshakufa tu Qiyaamah chake kishasimama, na kuanzia hapo mpaka siku ya Qiyaamah ataanza kukumbana na baadhi ya adhabu kutokana na yale maovu aliyoyatenda.



🔸Wangapi wametoka majumbani mwao kwa miguu yao wenyewe, wakarudishwa wakiwa wamebebwa. Wangapi walifunga wenyewe vifungo vya suruali zao, wakaja kufunguliwa na waoshaji maiti.

Mwanaadamu anapotafakari juu ya wale wanaobebwa juu ya majeneza kila siku na kupelekwa makaburini wakiacha mali zao nyingi nyuma yao, mali zitakazokuja kufaidiwa na warithi, ataona namna gani yeye alivyohangaika kuichuma mali hiyo na nani atakayekuja kufaidika nayo, na nani atakayehesabiwa juu ya mali hiyo.


Ikiwa mali imepatikana kwa njia zisizokuwa za halali au ikiwa mali hiyo haikutolewa ndani yake haki ya Mwenyezi Mungu, basi mali hizo watastarehe nayo warithi, na yule aliyechuma ndiye atakayeulizwa na Mwenyezi Mungu na kuhesabiwa.



Mwenyezi Mungu Subhanaahu wa Ta’ala Akamaliza Aayah hii kwa kusema:-

● وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ

"Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ana khabari za yote mnayoyafanya."


🔸Na maana yake ni kuwa hata kama utawaachia mali hiyo watu wako, wao pia watakuja kufa na watakaokuja baadaye nao watakufa, na mwisho kabisa hapana atakayebaki isipokuwa Mwenyezi Mungu Subhanaahu wa Ta’ala, siku atakayozirithi mbingu na ardhi na kila kilicho juu yake.


Naam tunaendelea na Darasa letu la Zakaah tuone Mali inazotolewa  Zakaah.


🔹MALI  INAYOTOLEWA ZAKAAH.

1.🔸 Dhahabu na Fedha

2.🔸Mazao na Matunda.

3.🔸Mali ya Biashara.

4. 🔸Wanayama wa kufugwa.


🔹DHAHABU NA  FEDHA.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ

"Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Mwenyezi Mungu, wape habari za adhabu inayoumiza inayowangoja.
Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahanamu, na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, (na huku wanaambia); "Haya ndiyo (yale mali) mliyolimbikia (mliyojikusanyia) nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya."
[ At-Tawbah: 34-35 ].


🔸Kwa hivyo mwenye kumiliki viwili hivyo (Dhahabu au Fedha) ikiwa ni katika mfumo wa pesa au mikufu au vipande (vinoo), ikitimia Niswaab yake na kukamilisha mwaka na akawa hana deni, wala shida yoyote inayokubalika, anawajibika kuitolea Zakaah yake.


● WAKATI WA MTUME.

Wakati wa Mtume Muhammad (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam), watu wa Bara Arabu walikuwa wakifanya biashara zao kwa njia ya kubadilishana bidhaa, na hawakuwa wakitumia pesa isipokuwa wachache sana walioweza kumiliki pesa za dhahabu na za fedha zilizokuwa zikitumika katika nchi za jirani.

Pesa zilizotengenezwa kwa dhahabu zilikuwa zikiitwa Dinari, na zilikuwa zikiletwa kutoka nchi za Warumi kama vile Byzantine na nyenginezo, na walikuwa pia wakitumia pesa zilizotengenezwa kwa fedha zilizokuwa zikiitwa Dirham na hizi zilikuwa zikitoka nchi ya Wafursi -Iran.

Kwa vile pesa hizo zilikuwa zikiwafikia zikiwa na uzito mbali mbali, na kiasi mbali mbali, nyengine ndogo ndogo na nyengine kubwa kubwa, na hazikuwa na kiasi maalum wala uzito maalum, kwa hivyo watu wa Makka hawakuwa wakizitumia kama zinavyotumiwa pesa za kawaida, bali walikuwa wakizipima na kuzipa thamani maalum waliyokubaliana.

● Miongoni mwa vipimo walivyokuwa wakitumia ilikuwa ratili, ambayo wakati huo ilikuwa na uzito wa wakia kumi na mbili na walikuwa pia wakitumia vipimo vya Mithqaal.

Kutokana na kipimo cha Mithqaal, Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akasema:-

"Haitolewi Zakaah ikiwa dhahabu haikutimia Mithqaal ishirini."



Karatasi za benki (Bank notes) zinazopigwa chapa na serikali tofauti ulimwenguni, hupigwa chapa kulingana na Dhahabu na Fedha inayomiliki serikali hizo, ama sivyo serikali yoyote masikini au yenye madeni ingelipiga chapa idadi ya noti yenye thamani kubwa kuliko dhahabu waliyo nayo na kuweza kulipa madeni yao na kujitajirisha.


 🔹 NISWAAB YAKE .

Dhahabu hailipiwi kitu mpaka ifikie Niswaab yake na imilikiwe (Niswaab hiyo) kwa muda wa mwaka (Mwaka wa Kiislam).

Niswaab ya dhahabu ni mithqaal 20 au gramu 92 au Tola 71/2 au wakia 3. (Baadhi ya maulamaa wanasema kuwa Niswaab yake ni gramu 85 au Tola 5 au wakia 2), na hii inatokana na ugumu wa kuweza kukisia bei ya vipimo vilivyokuwa vikitumika wakati wa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) na vinavyotumika wakati wetu huu. Hapana hitilafu juu ya kiwango cha Mithqaal 20 isipokuwa hitilafu ipo katika kuifasiri Mithqaal katika vipimo vya kisasa.

 Inapofikia kiwango hicho, na kubaki muda wa mwaka, unaichukua na kuipeleka kuipima kwa sonara au kwa wajuzi, na baada ya kuijua thamani yake unailipia 2.5% (mbili unusu katika mia) ya thamani ya dhahabu yote.


Niswaab ya dhahabu ndiyo Niswaab ya pesa za kawaida.

Kwa mfano katika nchi ya UAE, bei ya gramu tisini na mbili ya dhahabu ni Dh. 2575/-

Kwa hivyo hicho ndicho kiwango cha kuanzia kulipia Zakaah. Na dhahabu yako inapofikia kiwango hicho unailipia Dh. 64/- ambayo ni mbili unusu katika mia ya thamani hiyo. Dhabu inapozidi, na Zakaah yake inaongezeka.

Unailipia thamani ya dhahabu tu bila kuhesabu ujira wa mfuo au kazi ya mkono au thamani ya nakshi zake. (Gharama za ufulishaji hazimo).


 🔹 FEDHA

Niswaab ya fedha ni mithqaal 140 au Tola 36 au wakia 141/2.

Ikifikia kiwango hicho na ikamilikiwa muda wa mwaka, inalipiwa moja katika arubaini au mbili unusu katika mia ya thamani yake.



🔸SEHEMU YA 12🔸
    Darasa la Zakaah.


🔹 KUTOA  PANAPOWAJIBIKA.


Inawajibika kuitoa Zakaah wakati wake unapowadia, na haijuzu kuichelewesha isipokuwa kwa dharura inayokubalika.

Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya LLAAHU anha) amesema kuwa; Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"Haichanganyiki mali pamoja na Zakaah isipokuwa itaiangamiza", na katika riwaya nyingine;

"Inakuwa ishakuwajibikia katika mali yako kuitolea Zakaah, kisha usiitoe, kwa hivyo (malimali ya) halali".
[ Ash-Shaafi’iy na Al-Bukhaariy katika 'At-Taariykh' ].


🔸Kuitanguliza Zakaah.

Inajuzu kuitanguliza na kuitoa kabla ya kufikia wakati wake hata kabla ya miaka miwili.

● Anasema Ash-Shawkaaniy katika kitabu chake 'Naylul-Awtaar';:-

"Maulamaa wengi kama vile Az-Zuhriy na Al-Hassan Al-Baswriy na Maimaam Ash-Shaafi’iy na Ahmad na Abu Haniyfah wamejuzisha kuitanguliza Zakaah kabla ya kufikia wakati wake".



● Ama Imaam Malik na Sufyaan Ath-Thawriy na baadhi ya Maulamaa wengine wameona kuwa haijuzu kuitanguliza kabla ya wakati wake, wao wameziegemea zile Hadiyth zinazowajibisha kutoa Zakaah baada ya kukamilika mwaka.


Anasema Ibn Rushd:-

"Hitilafu iliyopo baina ya Maulamaa ni kuwa - Zakaah ni ‘Ibaadah au haki iliyowajibishwa kupewa masikini. Wanaosema kuwa Zakaah ni ‘Ibaadah, wao wameifananisha na Swalah na wakasema kuwa haiwezekani kutolewa kabla ya kufikia wakati wake.

● Ama wale wenye kuona kuwa ni haki iliyowajibika, wamejuzisha kuitoa kabla ya kufikia wakati wake ikiwa mtu mwenyewe amejitolea kufanya hivyo".


● Ama Imaam Ash-Shaafi’iy ameegema madai yake katika riwaya inayosema kuwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) aliwahi kuchukua katika mali ya Al-‘Abbaas (Radhiya LLAAHU ‘anhu) na kuitolea Zakaah kabla ya kufikia wakati wake.




    🔸SEHEMU YA TISA🔸
         Darasa la Zakaah.


🔹MTOTO NA MPUNGUFU WA AKILI.

 Inamuwajibikia aliyekabidhiwa mali ya yatima au ya mtu mwenye upungufu wa akili kuitolea Zakaah mali hiyo ikifikia kiwango chake.

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru (Radhiya LLAAHU ‘anhu), anasema kuwa; Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"Mwenye kumlea yatima mwenye mali, basi aifanyie biashara mali hiyo na asiiache mpaka ikamalizika kwa kuliwa na Swadaqah (Zakaah)".


Anasema Shaykh Sayid Saabiq katika Fiqhis Sunnah kuwa; Isnadi yake ina udhaifu ndani yake. Akaendelea kusema:-

“Anasema Al-Haafidh kuwa Hadiyth hii ina ushahidi kuwa ni 'Mursal' iliyorushwa moja kwa moja mpaka kwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) bila ya kutaja isnadi. Ama Imaam Ash-Shaafi’iy ameikubali (hadithi hii) kwa sababu zipo Hadiyth nyingi zinazoelezea juu ya kuwajibika kwa Zakaah katika mali yoyote ile. Anasema Imaam At-Tirmidhiy kuwa wanavyuoni wamekhitalifiana juu ya kuwajibika kuitolea Zakaah mali ya yatima,” amemaliza kusema Shaykh Sayid Saabiq.

 

  🔸 SEHEMU YA 15 🔸
      Darasa la Zakaah.


🔹ZAKAAH  YA  DENI .
       (Mwenye Kudai)


MAULAMAA wameigawa deni katika hali mbili.

1.🔸 Ikiwa anayedaiwa ni mtu tajiri au mtu muaminifu , deni hilo litachukuliwa mfano wa pesa zilizowekwa dhamana katika benki ambapo wakati wowote mtu anaweza kuzipata au ana uhakika wa kulipwa deni lake.

🔹Katika hali hii zipo rai tatu.

a)  ● Ya kwanza ni kuwa mwenye kudai anatakiwa ailipie mali hiyo Zakaah yake, juu ya kuwa halazimiki kuilipia mpaka pale atakapozipata na wakati huo atailipia pamoja na Zakaah ya siku zote za nyuma.

b) ● Ya pili ni kuwa analazimika kuilipia Zakaah yake kila unapotimia mwaka, kwa sababu pesa hizo zitahesabiwa mfano wa pesa zilizowekwa benki, na hii ni kwa sababu aliyekopeshwa ni mtu tajiri au muaminifu kiasi cha kuwa ana uhakika wa kulipwa au wa kuzipata pesa zake hizo wakati wowote ule anapozitaka.

c) ● Rai ya tatu ni kuwa hazilipii mpaka pale atakapolipwa deni hilo, na hapo atazilipia Zakaah ya mwaka ule mmoja tu.

☆ Anasema Shaykh Muhammad bin Uthaymiyn:-

"Rai ya mwanzo, nayo ni kuilipia Zakaah ya miaka yote pale atakapozipata pesa zake ni bora zaidi na inakubalika zaidi".



2.🔸Ikiwa anayedaiwa ni mtu masikini au mtu asiyekuwa muaminifu, haimuwajibikii mwenye kudai kuzitolea Zakaah pesa hizo mpaka atakapozipata na kubaki nazo muda wa mwaka mzima kisha atazilipia Zakaah ya mwaka huo tu, ambao mali yake hiyo ilibaki kwake kama kawaida ya utoaji wa Zakaah.


☆ Anasema Shaykh Bin ‘Uthaymiyn:-

"Haijuzu kumdai au kumlazimisha mtu masikini au kumshitaki na hatimaye kumuingiza jela na kumtenganisha na watu wake ikiwa mtu huyo kweli hana uwezo wa kulipa deni, na ikiwa mtu huyo hafanyi ujanja wa kuchelewesha makusudi, na badala yake tunatakiwa tumsitahamilie mpaka pale Mwenyezi Mungu Atakapomfariji.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

وَإِن كَانَ ذُو عُسْرَةٍ فَنَظِرَةٌ إِلَى مَيْسَرَةٍ وَأَن تَصَدَّقُواْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ وَاتَّقُواْ يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللّهِ ثُمَّ تُوَفَّى كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لاَ يُظْلَمُونَ

"Na kama (mkopi) ana dhiki, basi (mdai) angoje mpaka afarijike, na kama nyinyi (mnaodai mkizisamehe deni zenu) mkazifanya Swadaqah, basi ni bora kwenu. Ikiwa mnajua haya (basi fanyeni).
Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha viumbe wote watalipwa kwa ukamili yote waliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa".
[ Al-Baqarah: 280-281]


Mtu akisema:-

"Pesa zangu kwanini nisizidai ?", Anaendelea kusema Shaykh Bin ‘Uthaymiyn,

"Tunamwambia:-
Ni kweli pesa zako, lakini wewe mwenyewe ndiye uliyemkopesha pesa hizo. Pale alipokujia kutaka kukukopa ungelimtafutia udhuru wowote ule, kisha ukampa kiasi chochote cha mali ikiwa kama ni msaada (Swadaqah) tu kutoka kwako, basi yasingekukuta haya. Lakini umemkopeshe na hali unajuwa kuwa mtu huyu ni masikini, kisha akishindwa kukulipa ukamshitaki, umtie jela na kumtenganisha na mke na watoto wake, jambo hilo ni haramu kabisa na haijuzu kwa Muislam kulitenda".

(Mwisho wa maneno ya Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn).


    🔸 SEHEMU YA 12 🔸
         Darasa la Zakaah


    🔹 ALIYEFARIKI .

Anasema Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah kuwa, katika madhehebu ya MaImaam Ash-Shaafi’iy na Ahmad na Abu Thawr, ni kuwa mtu akifarki na akaacha deni la Zakaah, basi inawajibika katika mali yake kwanza kutolewa deni la Zakaah, tena iwe kabla ya kutimizwa wasia alioacha na kabla ya urithi kugawiwa.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْنٍ

" Baada ya kutoa aliyoyausia au kulipa deni ".
[ An-Nisaa: 11 ]



Na Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"Deni la Mwenyezi Mungu linastahiki zaidi kulipwa".

Na Zakaah ni deni la Mwenyezi Mungu.



Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya LLAAHU ‘anhu) kuwa amesema:-

“Mtu mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akasema:-

"Mama yangu amefariki na anadaiwa saumu ya mwezi mzima, je nimlipie ?"

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akamuuliza :-

"Mama yako angelikuwa na deni ungemlipia ?"

Akasema :-

"Ndiyo, ningemlipia".

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akamwambia:-

"Basi deni la Mwenyezi Mungu linastahiki zaidi kulipwa".
[ Al-Bukhaariy na Muslim ].



    🔸 SEHEMU YA 17 🔸
        Darasa la Zakaah.


🔹ZAKAAH YA BIASHARA.

Hukmu Yake
Wapo baadhi ya maulamaa ambao ni wachache sana wanaosema kuwa hapana dalili ya kuwa mali ya biashara inatolewa Zakaah, lakini dalili zilizomo ndani ya Qur-aan na Sunnah zinaleta maana kinyume na rai zao.

Mwenyezi Mungu Anasema :-

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلاَتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ

"Chukua Swadaqah katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Swadaqah zao) na kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua. Hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu."
[ At-Tawbah - 103 ].


Aayah hii inaleta maana ya ujumla kuwa Zakaah inatakiwa itolewe kutoka katika mali zao (Matajiri), mali ya aina yoyote ile ikiwemo mali ya biashara, bila kufafanua aina ya mali hiyo.

Na Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema :-

"Ichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na kurudishiwa mafakiri wao".


Kwa hivyo dalili hizi zinatujulisha kuwa mali yeyote ile, ikiwemo mali ya biashara, lazima itolewe Zakaah, na kwamba Zakaah hiyo ichukuliwe kutoka kwa matajiri, na bila shaka wafanya biashara ni matajiri, na kwamba irudishwe kwa masikini. Muhimu mali hiyo iwe imekifikia kile kiwango cha kutolewa Zakaah (Niswaab) na imekamilisha muda wa mwaka.


 🔹NAMNA YA KUTOA  ZAKAAH  YA  BIASHARA.

Mwenye kumiliki mali ya biashara iliyofikia Niswaab, akisha kamilisha mwaka anatakiwa ahesabu mali yake yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya biashara.
Kama ni mfanya biashara wa nyumba, basi azihesabu nyumba zake (zile tu alizozitayarisha kwa ajili ya biashara), au ardhi au vyombo vya nyumbani, magari au nguo au biashara ya aina yoyote ile. Atavihesabu vitu alivyokuwa navyo kwa ajili ya biashara pamoja na kuzihesabu pesa zote alizonazo kwa ajili ya biashara kisha atazitolea Zakaah yake, nayo ni mbili unusu( 2.5 % ) katika mia au moja katika arubaini (1/40 ).

Atafanya hesabu hiyo bila kujali kama wakati wowote ule ndani ya mwaka ule pesa hizo zilipungua au kuongezeka.


  🔹 KUMBUKA .

Ikumbukwe kuwa vitakavyohesabiwa (katika Zakaah ya Biashara) ni vitu vilivyotayarishwa kwa ajili ya biashara tu.


Kwa mfano mtu anamiliki magari hata yakifikia idadi ya magari kumi au zaidi, au atataka kuuza gari lake mwenyewe kwa ajili ya kulibadilisha tu na kununua gari jengine au ardhi au nyumba au chochote kile, ikiwa anataka kuuza kwa ajili ya kutaka kununua kingine badala yake au kwa ajili ya mahitajio mengine yasiyokuwa ya kibiashara, basi mali hiyo haitolei Zakaah ya biashara, na hii ni kwa sababu Niyah ya kuviuza vitu hivyo si kwa ajili ya biashara.


🔸Kumbuka pia kuwa Zakaah inatolewa kutokana na asili ya chochote kilichoongezeka kutokana na mali hiyo wakati wowote ule katika mwaka. Ama kile kilichoongezeka kutokana na asili nyingine, basi mwaka wake unaanza kuhesabiwa kuanzia siku ile iliyoongezeka mali hiyo.


🔹Kwa mfano;
Mfanya biashara alikuwa akiendela kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha Shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa mwisho au hata katika siku ya mwisho kabla ya kutimia mwaka, akapata faida kiasi cha Shilingi laki saba, pesa zote hizo ZITAHESABIWA pamoja na Zakaah ya biashara ya mwaka huo, kwa sababu asili yake (faida iliyopatikana) inatokana na biashara hiyo anayoitolea Zakaah.


🔹Mfano mwingine :-

Mfanya biashara alikuwa akiendelea kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa kumi na mbili au katika siku ya mwisho au siku yoyote ile ndani ya mwaka huo kabla ya kuingia muda wa kulipa Zakaah ya mwaka ule, mtu huyo akarithi mali au pesa kutoka kwa jamaa yake aliyefariki kiasi cha Shilingi milioni moja.

Pesa hizo alizorithi HAZITOHESABIWA katika Zakaah ya mwaka huo, bali ataanza kuzihesabia mwaka wake mpya kuanzia siku ile alizozipata pesa hizo. Kwa sababu asili ya pesa hizo hazitokani na biashara ile anayoitolea Zakaah, bali inatokana na asili nyingine, ambayo ni urithi.

🔸WENYE  KUPOKEA
          MISHAHARA .

Kwa kawaida mwenye kupokea mshahara pesa zake huongezeka na kupungua katika miezi mbali mbali. Kwa vile itakuwa vigumu kwake kuweka hesabu ya kila mwezi pale zinapokamilisha Niswaab au kuongezeka pale zinapopungua, wanavyuoni wakasema kuwa mtu huyo ataanza kuuhesabu mwaka wake kuanzia siku ile aliyoweza kutimiza Niswaab, na kuanzia mwezi huo, atakuwa akiitolea Zakaah mali yake kila anapotimiza mwaka.



  🔸SEHEMU YA NANE🔸
       Darasa la Zakaak.

🔹WANAOWAJIBIKA KUTOA.

Ni Muislam anayemiliki Niswaab, nacho ni 'Kiwango maalum cha mali’ kilichowekwa na shari’ah katika aina yeyote ile ya mali inayowajibika kuitolea Zakaah.

·Niswaab hiyo lazima iwe ishatolewa ndani yake mahitajio ya dharura ya lazima kama vile chakula, mavazi, makazi, vyombo vya nyumbani, chombo cha usafiri na vyombo vyake vya kufanyia kazi, madeni nk.

· Lazima kiwango hicho kiwe kimemilikiwa kwa muda wa mwaka mzima (mwaka wa Kiislam) bila kupungua katika wakati wowote ule ndani ya mwaka huo, na kama kitapungua katika wakati wowote ule kabla ya kutimia mwaka, basi hesabu nyingine mpya itaanzwa kuanzia pale kinapokamilika tena Kiwango hicho.

🔸Amesema Imaam An-Nawawiy :-
" Madhehebu yetu na madhehebu ya Maimaam Malik na Ahmad na ya maulamaa walio wengi ni kuwa; Mali inayotolewa Zakaah kwa ajili yake, kama vile dhahabu, fedha na wanyama wa kufugwa, lazima kiwango chake kibaki kwa muda wa mwaka mzima bila kupungua. Na wakati wowote ule kitakapopungua, basi mwaka wake unakatika, na wakati wowote ule kitakapotimia tena, unaanza kuhesabiwa mwaka mwingine".


🔸Ama Abu Haniyfah anasema:-
"Kinachotakiwa ni kuwepo kwa Kiwango (Niswaab) mwanzo wa mwaka na mwisho wake, na haidhuru iwapo kitapungua katikati ya mwaka, hata kama mtu alikuwa nazo Dirham mia mbili kisha zikapotea zote katikati ya mwaka na akabakiwa na dhirham moja tu, au kama alikuwa na kondoo arubaini wakapungua na akabaki mmoja tu, kisha mwisho wa mwaka akaweza kumiliki (Dirham) mia mbili kamili au (kondoo) arubaini kamili, basi itawajibika Zakaah kwa vyote ".

●Tanbihi :-
Masharti haya hayahusiani na Zakaah za mazao na matunda, kwa sababu vitu hivyo Zakaah yake inatolewa siku ya mavuno.

● Mwenyezi Mungu Anasema:-

وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ

"Na toeni haki yake siku ya kuvuna kwake".
[ Al-An’aam - 141 ].



   🔸 SEHEMU YA 18 🔸
     Darasa la Zakaah.


🔹 ZAKAAH YA MAZAO .

Mwenyezi Mungu amewajibisha kuyatolea Zakaah mazao Aliposema:-

وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ جَنَّاتٍ مَّعْرُوشَاتٍ وَغَيْرَ مَعْرُوشَاتٍ وَالنَّخْلَ وَالزَّرْعَ مُخْتَلِفًا أُكُلُهُ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُتَشَابِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ كُلُواْ مِن ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ

"Naye (Mwenyezi Mungu) ndiye Aliyeiumba miti inayoegemezwa na isiyoegemezwa, na mitende na mimea yenye matunda mbali mbaIi, na (Akaumba) Mizaituni na Mikomamanga inayofananana na isiyofanana. Kuleni matunda yake inapotoa matunda na toeni haki yake siku ya kuvuna kwake ".
[ Al-An’aam: 141 ].



🔺Katika kuifasiri ayah hii amesema Ibn ‘Abbaas (Radhiya LLAAHU ‘anhu):-

'" Haki yake, ni Zakaah yake iliyofaradhishwa ".



Wakati wa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam), Zakaah ya mazao ilikuwa ikitolewa katika Mahindi, Ngano, Mtama, Tende na Zabibu na wengine wakaongeza 'Mchele' na wengine wakasema kuwa Zakaah ya mazao inatolewa katika chakula chochote kile kinachoweza kubaki muda mrefu kama vile mwaka au zaidi bila kuharibika.


Matunda, haya kuwa yakitolewa Zakaah isipokuwa Tende na Zabibu. Matunda mengine haya kuwa yakitolewa Zakaah isipokuwa kama matunda hayo ni kwa ajili ya biashara, basi hapo itatolewa Zakaah ya biashara na si Zakaah ya Mazao.

🔸Tanbihi :-
Zakaah ya Mazao inatolewa siku ya kuvuna na kabla ya kuuzwa wala kuliwa na si lazima itimie mwaka.


  🔹NISWAAB YA MAZAO

Mazao hayatolewi Zakaah mpaka yatimie WISKI TANO yakiwa safi bila magamba. Kama hayajasafishwa, basi lazima yatimie WISKI KUMI.


Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema :-

" Chini ya Wiski tano haitolewi Zakaah ".
[ Imaam Ahmad na Al-Bayhaqiy ].



WISKI 5 ni sawa na pishi 300, kwa sababu WISKI MOJA ni sawa na PISHI SITINI  kwa pishi iliyokuwa ikitumika wakati wa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam), na PISHI SITINI mara TANO ni sawa na PISHI MIA TATU.


🔺Kwa vipimo vya kisasa, anasema Ustadh Said ‘Abdullaah katika kitabu chake 'Kutoa Zakaah':

"Niswaab ya mazao ni Wisqi 5. Moja ni kilo 60 yaani kilo 300. Kilo moja ni ratili 13/4 (ratili mbili kasorobo) (300 mara 13/4 = ratili 525).

Kilo karibu ni sawa na pishi ya mbao (vibaba vinne)."

Mwisho wa maneno ya Ustadh Said ‘Abdullaah.



Kwa hivyo mazao yakifikia pishi 300 au ratili 525 yanakuwa yamefikia Niswaab yake (kiwango chake) na yatatolewa Zakaah yake ambayo ni moja juu ya kumi (one tenth), hii ikiwa mazao hayo yanapata maji yake bila kuyahangaikia, yaani kama vile kunyeshewa na mvua au maji ya mito au chemchem nk.


Ama ikiwa mkulima anayatilia maji yeye mwenyewe kwa kuyahangaikia maji hayo, basi Zakaah yake itapungua na itakuwa ni nusu ya moja juu ya kumi.

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema :-

"Kilichonyeshewa na mvua au maji yanayopita (waadi) au yaliyotwama (Zakaah yake ni) moja katika kumi na kilichomiminiwa maji nusu ya moja katika kumi".
[ Al-Bukhaariy na wengineo].



Mwenyezi Mungu Ameamrisha kuitoa Zakaah ya mazao; "Siku ya kuvuna kwake", na maana yake ni; kabla hakijaliwa wala kugawiwa chochote kile ndani yake, na ikiwa mtu amekwishafanya hivyo kwa kusahau, basi itambidi akisie kile alichotoa au alichouza na akitolee Zakaah yake.

Ama kile alichokula mkulima kabla ya kuvuna, hakimo katika hesabu.

Alipoulizwa Imaam Ahmad juu ya wanachokula wenye ardhi kabla ya mavuno alisema:-

"Hapana neno ikiwa atakula katika mazao yake kiasi anachohitajia".



Anasema Shaykh Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah:-

"Kauli hii pia imetamkwa na Imaam Ash-Shaafi’iy na Allayth na Ibn Hazm'.

🔹Ama Imaam Malik na Imaam Abu Hanifa wanasema:-

"Anachokula mtu katika mazao yake kabla ya mavuno atahesabiwa katika Niswaab"

Mwisho wa maneno ya Sayyid Saabiq.


🔹 TOENI  KATIKA  VIZURI.

Baadhi ya wenye kumiliki mitende walikuwa wakitoa Zakaah yao ya mazao katika tende au zabibu au mazao yasiyokuwa mazuri. Walikuwa wakichagua mazao yasiyokuwa mazuri na kuyatolea Zakaah, na yale mazuri walikuwa wakichukua wenyewe.

Mwenyezi Mungu Akasema:-

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَنفِقُواْ مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الأَرْضِ وَلاَ تَيَمَّمُواْ الْخَبِيثَ مِنْهُ تُنفِقُونَ وَلَسْتُم بِآخِذِيهِ إِلاَّ أَن تُغْمِضُواْ فِيهِ وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ

"Enyi mlioamini! Toeni katika vile vizuri mlivyovichuma na katika vile tulivyokutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya hali nyinyi wenyewe msingevipokea isipokuwa kwa kutoviangalia (Basi Mungu atapokea vibaya?). Basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkwasi na asifiwaye".
[ Al-Baqarah: 267 ].


🔺Anasema Imaam Ash-Shawkaaniy :-

"Hii ni dalili kuwa, haijuzu mtu kuwapa watu Zakaah katika yale mazao mabovu na yasiyokuwa mazuri."



  🔸SEHEMU YA 13🔸
    Darasa la Zakaah.


🔹KUOMBA DU’AA.

Inapendeza kumuombea dua mtoaji Zakaah, pale anapoitoa.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلاَتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ

"Chukua Swadaqah katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Swadaqah zao) na kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua. Hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu. "
[ At-Tawbah: 103 ].



🔸Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Abi ‘Awfiy amesema:-

“Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alikuwa anapoletewa mali ya Zakaah akisema: "ALlaahumma salliy ‘alayhim".

Na baba yangu siku moja alimpelekea mali ya Zakaah akasema :-
 "Allaahumma salliy ‘alaa aali Abi ‘Awfiy".
[ Ahmad na wengineo ].



Imepokelewa kutoka kwa Wail bin Hajar kuwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alimuombea mtu mmoja aliyeleta ngamia wa Zakaah akasema:

"Allaahumma Baarik fiyhi wa fiy ibilihi".(Mwenyezi Mungu mbariki yeye na katika ngamia wake)



🔹Anasema Imaam Ash-Shaafi’iy:

"Ni Sunnah kwa Imaam anapopokea mali ya Zakaah kumuombea dua mtoaji kwa kumwambia:- "Aajaraka ALLAAHU fiyma a’atwayta, wa baarik laka fiyma abqayta ".

" Mwenyezi Mungu akupe ujira mwema katika ulichotoa na akubarikie katika kilichobaki ".



🔸SEHEMU YA KUMI🔸
      Darasa la Zakaah.


🔹 MWENYE   DENI .



Mwenyezi kumiliki kiwango kinachomwajibisha kutoka Zakaah, na wakati huo huo anadaiwa, kwanza anatoa kiasi cha deni analodaiwa, kisha anailipia Zakaah mali iliyobaki ikiwa bado inafikia kiwango cha kutolewa Zakaah. Ama ikiwa maliiliyobaki haifikii kiwango, basi hatoi Zakaah, kwa sababu wakati huo anahesabiwa kuwa ni mtu fakiri, na Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) anasema:

"Hatoi Swadaqah (Zakaah) isipokuwa mtu tajiri".
[ Ahmad ].

Na amesema:-

"Ichukuliwa (mali ya Zakaah) kutoka kwa matajiri wao na kurudishiwa mafakiri wao".




   🔸SEHEMU YA 16🔸
       Darasa la Zakaah.


🔹ZAKAAH YA MAPAMBO.

Maulamaa wamekhitalifiana katika kuzitolea Zakaah dhahabu na fedha za mapambo.

Wapo waliosema kuwa dhahabu au fedha ya kujipamba inapofikia Niswaab yake lazima itolewe Zakaah yake,

🔸Na hawa wameegemeza Hadiyth ya Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) aliposema kumwambia mwanamke mmoja aliyemvisha mwanawe mkufu wa dhahabu akamwambia :-

" Unailipia Zakaah yake ?"
Akasema :-
" La, hatuilipii "
Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akamwambia :-
" Huogopi Mwenyezi Mungu akakuvalisheni mikufu ya Moto? Zilipie Zakaah yake ".
[ Imaam Ahmad ].


🔸Na pia Hadiyth iliyosimuliwa na Bibi ‘Aaishah (Radhiya LLAAHU anha) aliposema :-
" Aliingia chumbani kwangu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akaniona nimevaa pete za fedha. Akaniuliza :-

" Nini hiki Ewe ‘Aaishah ?"
Nikamwambia :-
" Nimezitengeneza ili nijipambe kwa ajili yako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ".
Akasema :-
" Unazilipia Zakaah yake ?"
Nikasema :-
" Hapana ."
Akasema :-
" Hiyo inatosha kwa (kukupatia adhabu ya) Moto ".
[ Abu Daawuud – Ad-Daaraqutniy na Al-Bayhaqiy].



🔹Ama wale wanaosema kuwa Dhahabu ya mapambo hailipiwi Zakaah, wao wameegemeza hoja zao katika Hadiyth iliyosimuliwa na Al-Bayhaqiy inayosema :-

"Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya LLAAHU ‘anhu) aliulizwa juu ya mapambo:-

" Yanatolewa Zakaah ?
Akasema :-
" La, hayatolewi "
Akaulizwa :-
" Hata kama thamani yake itafikia Dinari elfu moja ?'
Akasema:-
"Zaidi" (hata kama zaidi ya thamani hiyo).


🔹Na pia Hadiyth iliyomo katika Muwataa, kitabu cha Imaam Malik inayosema :-

"Bibi ‘Aaishah alikuwa akiwalea wana wa kaka yake mayatima na walikuwa na mapambo na hakuwa akiyatolea Zakaah .”


🔸Tanbihi :-
Atakayezichunguza Hadiyth hizi na zile, ataona kuwa zile zinazolazimisha kuitolea Zakaah dhahabu au fedha ya mapambo ndizo zenye nguvu zaidi na zenye uhakika zaidi kuliko zisizolazimisha - WaLLAAHU Taala Aalam.


Ndugu Zangu kuna Marekebisho hapo juu hiyo ni Darasa ya Kumi na Moja sio ya Kumi na Mbili kama nilivyoandika .Samahani katika hilo .

  🔸 SEHEMU YA 19 🔸
       Darasa la Zakaah.


🔹ZAKAAH YA WANYAMA WA KUFUGWA.

Wanyama wanaofugwa wanalazimika kutolewa Zakaah kwa masharti yafuatayo:-

1●Lazima watimie Niswaab.

2.● Wakamilishe mwaka.

3. ●Wawe wanyama wa kufugwa.


🔺Wanyama wasiokuwa wa kufugwa kama vile wa kupandwa au wanaotumiwa kwa kubeba mizigo au kwa kilimo n.k. Hawa HAWATOLEWI Zakaah.

🔺Wanyama WANAOTOLEWA  Zakaah ni Ngamia, Ng'ombe, Mbuzi na Kondoo.


🔹 ZAKAAH YA NGAMIA.

Ngamia hawatolewi Zakaah mpaka watimie WATANO. Wakitimia watano wa kufugwa hadi TISA na kutimiza mwaka chini ya milki ya mtu, basi atawatolea MBUZI MMOJA.


🔸 Note .
Wakitimia NGAMIA 10 mpaka 14 atawatolea MBUZI WAWILI.

Na hivyo hivyo kila wakizidi ngamia WATANO ataongeza MBUZI MMOJA.

🔺Wakitimia ngamia 25 mpaka 35 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha mwaka na kuingia mwaka wa pili au mtoto wa ngamia dume aliyekamilisha mwaka wa 2 na anaingia wa 3.

🔺Kuanzia ngamia 36 mpaka 45 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha miaka 2 na kesha ingia wa 3.

🔺Kuanzia ngamia 46 mpaka 60 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha miaka 3 na kuingia wa 4.


🔺Kuanzia ngamia 61 mpaka 75 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha miaka 4 na kuingia mwaka wa 5.

🔺Kuanzia ngamia 76 mpaka 90 atatoa watoto wa ngamia wawili jike waliokamilisha miaka miwili na kuingia wa tatu.

🔺Kuanzia ngamia 91 mpaka 120 atatoa watoto wa ngamia wa kike wawili waliotimia miaka 3 na kuingia mwaka wa 4.

🔺Wakizidi kuliko hapo, basi katika kila ngamia 40 atatoa mtoto wa ngamia wa kike aliyekamilisha miaka 2 na kuingia wa 3. Na katika kila ngamia 50 waliozidi kuliko hapo atatoa mtoto wa ngami wa kike aliyekamilisha miaka 3 na kuingia wa nne.


🔸Anasema Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah:-

"Hawatolewi Zakaah ngamia dume ikiwa wapo wa kike, lakini anatolewa mtoto wa ngamia wa kiume aliyetimia miaka miwili na kuingia wa tatu ikiwa hajapatikana wa kike aliyekamilisha mwaka na kuingia wa pili.


 🔹ZAKAAH YA NG’OMBE.

Ng'ombe hawatolewi Zakaah mpaka watimie 30 wa kufugwa. Wanapotimia 30 mpaka 39 wa kufugwa na kukamilisha mwaka, atatolewa ndama aliyekamilisha mwaka mmoja.

🔺Wakitimia ng'ombe 40 mpaka 59 atatolewa ndama asiyepungua umri wa miaka miwili.

🔺Wakitimia ng'ombe 60 mpaka 79 atatolewa ndama wawili wa mwaka mmoja.

🔺Kutoka hapo, kila wakizidi ng'ombe 30, ataongeza kutoa ndama wa mwaka mmoja.

🔺Na kila wakizidi ng'ombe 40 atawatolea ndama wa miaka miwili.

 
🔹ZAKAAH YA MBUZI.

Mbuzi hawatolewi Zakaah mpaka watimie 40, na wakitimia arubaini mpaka 120 wa kufugwa na kukamilisha mwaka kwa mwenye kuwamiliki, atawatolea mtoto wa mbuzi wa mwaka mmoja.

🔺Hatowatolea tena mpaka wafikie idadi yao mbuzi 121.

🔺Wakiongezeka na kutimia 121 mpaka 200, atawatolea mtoto wa miaka MIWILI.

🔺Kuanzia mbuzi 201 mpaka 300 atawatolea KONDOO WATATU.

🔺Wakizidi kuliko mbuzi 300, basi atawatolea KONDOO MMOJA katika kila MBUZI MIA  waliozidi.


🔸TANBIHI :-
Inaruhusiwa pia kutoa MBUZI badala ya KONDOO.



🔹 WANYAMA WENGINE .

Wanyama wengine wasiokuwa hawa kama vile farasi, nyumbu, punda na wengineo, hawatolewi Zakaah isipokuwa kama ni kwa ajili ya biashara.



  🔸SEHEMU YA  20 🔸
  Darasa la Zakaah


🔹ZAKAAH YA MADINI YA KALE .


Madini inayotolewa ardhini kama vile petroli, gesi, shaba, chuma n.k, hivi vyote havitolewi Zakaah, isipokuwa dhahabu na fedha tu na tushaelezea hapo mwanzo namna ya kutoa Zakaah yake. Ama vilivyobaki vinatolewa Zakaah ya biashara baada ya kuchimbuliwa au kutolewa na kuuzwa.




    🔺SEHEMU YA 23🔺
       Darasa la Zakaah.


🔹   WANAOSTAHIKI   🔹
      KUPEWA  ZAKAAH.

🔸Swadaqah ya kawaida, anapewa mtu yeyote hata akiwa si Muislam,

🔸Ama Zakaatul Fitwr wanapewa watu wa aina MBILI TU, nao ni MASIKINI na MAFAKIRI Waislam.

🔸ZAKAATUL MAAL (Zakaah ya mali), hii wanapewa aina 8 tu ya WAISLAM waliotajwa na Mwenyezi Mungu katika kitabu chake kitukufu Aliposema :-

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللّهِ وَاللّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

" Swadaqah hupewa (watu hawa) :-

1 ● MAFAKIRI

2.● MASIKINI

3.● WANAOZITUMIKIA .

4. ● WANAOTIWA NGUVU NYOYO ZAO (juu ya Uislam)

5. ● KATIKA KUWAPA UUNGWANA WATUMWA

6.● KATIKA KUWASAIDIA WENYE DENI 

7.● KATIKA (KUTENGENEZA) MAMBO ALIYOAMRISHA ALLAAH. 

8.● KATIKA (KUPEWA)
            WASAFIRI
( WALIOHARIBIKIWA ).

Ni faradhwi inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi (na) Mwenye hikima ".
[(  At-Tawbah: 60. )].


Atakayeichunguza ayah hii ataona kuwa Mwenyezi Mungu ametumia neno 'LIL' katika kuwataja watu aina NNE wa mwanzo wanaostahiki kupewa Zakaah. Na hii inaitwa LAAM YA TAMLIYK, na maana yake ni kuwa lazima kuwamilikisha watu wa aina NNE wa mwanzo (yaani kuwapa mikononi mwao) Zakaah yao.


Mwenyezi Mungu Anasema:-

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ

Ama katika aina NNE waliobaki, Mwenyezi Mungu ametumia neno 'FIY'. Na kwa kutumia neno hilo Mwenyezi Mungu hatulazimishi, kuwamilikisha kwa kuwapa Zakaah yao mikononi mwao.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ

Kwa hivyo katika aina NNE za mwisho, kwa mfano kama unataka kumsaidia mwenye deni, hulazimiki kumpa pesa hizo mkononi mwake, bali unaweza kwenda kumlipia deni hilo moja kwa moja bila ya kumkabidhi mdaiwa huyo pesa hizo mkononi mwake. Hata hivyo, ukitaka unaweza pia kumkabidhi mweyewe mkononi mwake.

Ukitaka kuzitumia pesa za Zakaah katika njia ya Mwenyezi Mungu, unaweza kununua kwa mfano silaha na kuwakabidhi wapiganaji 'Mujahidiin' au unaweza kuzitumia katika njia ya Mwenyezi Mungu bila ya kumkabidhi mtu pesa hizo mkononi mwake, wakati huo huo unaweza ukitaka kuwakabidhi wanaohusika au wajuzi ili ipate kutumika kwa usahihi zaidi.


 🔺    SASA TUANZE      🔺
KUCHAMBUA KUNDI MOJA
  BAADA YA MOJA KATIKA
          MAKUNDI HAYO.


🔹MAFAKIRI/ MASIKINI.🔹

Haya ni Makundi la kwanza na la pili ambao ALLAAH amewataja wanaostahiki kupewa Zakaatul Maal .
Juu ya kuwa watu wamehitalifiana juu ya nani masikini na nani fakiri, lakini kwa ujumla hawa ni watu ambao wanachokipata hakiwatoshi katika matumizi yao ya kila siku.

Mtu anaweza kuwa masikini hata kama anapata mshahara mkubwa lakini wakati huo huo ana watoto wengi au wazee na ndugu wanaomtegemea anaowajibika kuwatizama, au ana madeni kiasi ambapo juu ya kuwa anapata mshahara mkubwa, pesa hizo hazimtoshi kuwalisha watu wake hao.

Kwa ajili hiyo juu ya tofauti iliyopo baina ya masikini na fakiri katika sharhi yake, lakini katika kuhitajia kwao msaada, wote wawili wapo katika hali moja.

Zipo Hadiyth zinazotujulisha kuwa wapo baadhi ya masikini wenye kustahi kuombaomba juu ya shida kubwa walokuwa nazo. Waislam wanatakiwa wawachunguze watu wa aina hii na kuwasaidia na wasiwaache mpaka hali zao zikawa mbaya.

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) anasema:-

" Masikini si yule anayeomba akapewa tende moja au mbili akaondoka, au tonge moja au mbili, lakini masikini wa kweli ni yule anayejizuwia."

Someni Katika (kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo):-

التَّعَفُّفِ تَعْرِفُهُم بِسِيمَاهُمْ لاَ يَسْأَلُونَ النَّاسَ إِلْحَافًا

" Utawafahamu kwa alama zao hawawaombi watu wakafanya ung'ang'anizi ".


Anayepewa Zakaah ni Masikini au Fakiri Muislam tu, ama Masikini au Fakiri asiyekuwa Muislam hapewi katika mali ya Zakaah, na kama Fakiri asiyekuwa Muislam atahitajia msaada, basi atapewa katika mali ya Swadaqah na si ya Zakaah.


🔹WENYE KUZITUMIKIA🔹

 Hili ni Kundi la tatu ambalo ALLAAH amelitaja nao ni
Wanaozitumikia Zakaah ni wale waliopewa jukumu la kuipokea, kuikusanya kutoka kwa matajiri na wenye kazi ya kuihifadhi, waandishi, na wenye kuigawa, wakiwemo wachungaji wa wanyama wa Zakaah.

Ili waweze kupewa katika Mali ya Zakaah, watu hao lazima wawe Waislam, na wasiwe katika wale walioharamishwa kupokea Zakaah katika watu wa Ahlul Bayt ya Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) katika Banu Abdul Muttalib ambao tutawataja baadaye.

Katika wanaoitumikia Zakaah, hata akiwa mtu tajiri basi anastahiki kupewa katika mali hiyo, na ikiwa mtu wa aina hiyo amepewa na wakubwa wanaohusika na akawa hana haja nayo mali hiyo, basi aichukuwe na kuwagawia anaowataka au kumnunulia zawadi anayemtaka.

Imepokelewa kuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya LLAAHU ‘anhu) alipokuwa akifanya kazi ya kukusanya mali ya Zakaah, Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alimpa katika mali hiyo.

‘Umar (Radhiya LLAAHU ‘anhu) akasema:-

"Mimi najitolea tu na sina haja ya kulipwa, mpe mwenye kuzihitajia zaidi kuliko mimi ".

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akamwambia:-

"Alichokupa Mwenyezi Mungu katika mali hii bila ya wewe mwenyewe kuiomba, uichukuwe na uitumie au itolee Swadaqah."
[ Al-Bukhaariy na An-Nasaaiy ].



     🔸SEHEMU YA 22🔸
         Darasa la Zakaah.

          🔺 Swadaqah 🔺

Muislam anaipa mali yake mtazamo wa aina nyingine kabisa tofauti na asiyekuwa Muislam, kwani dini ya Kiislam inampa kila mtu haki ya kutafuta mali na kufanya biashara ya halali na kuwa tajiri anayeweza kumiliki mali nyingi. Isipokuwa baada ya kuimiliki mali hiyo, analazimika kuwapa maskini Zakaah, ambayo ni haki yao maalum waliyopangiwa na Mola wao Subhanaahu wa Ta’ala.

Wakati huo huo Muislam anatakiwa ajipatie thawabu nyingi zaidi na ajiepushe na shari nyingi pamoja na kuwasaidia ndugu na jamaa zake, na masikini waislamu wenzake wenye kuhitaji, kwa kutoa kiasi kingine katika mali zao kwa hiari yao wenyewe na kwa kiasi anachokitaka mwenyewe, na hii inaitwa 'Swadaqah'.

Kinyume na njia inayotumika katika nchi za kikoministi za kuwanyang'anya matajiri mali zao kwa nguvu na kuwapa masikini, kitendo cha dhulma na cha ufisadi, kwa sababu binaadamu kwa kawaida wanakhitalifiana katika ujuzi na katika jitihada zao, na kwa ajili hiyo lazima wahitalifiane katika ujira na mapato yao, kwani katika kuwafanya watu wote wawe sawa katika mapato, utakuwa unamweka katika daraja moja mvivu na mwenye kujitahidi, hodari na asiyekuwa hodari, mtaalamu na asiyekuwa mtaalamu.

Hii ikiwa mali hiyo wanayonyang'anywa matajiri wanapewa kweli masikini na wale wanaostahiki, na ikiwa watu wote watakuwa sawa kweli, lakini uhakika wa mambo umethithibitisha kuwa yanayotendeka ni kinyume kabisa na maneno yao, kwani wao huwanyang'anya mali matajiri na kuwapa viongozi wa vyama vyao pamoja na vibaraka wao.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

مَّا أَفَاء اللَّهُ عَلَى رَسُولِهِ مِنْ أَهْلِ الْقُرَى فَلِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ كَيْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاء مِنكُمْ

"Mali aliyoleta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya Mtume na jamaa na mayatima na masikini na msafiri aliyeharibikiwa, ili isiwe kinyang'anyiro baina ya matajiri wenu tu."
[ Al-Hashr: 7 ].

Mwenyezi Mungu katika ayah hii anatujulisha kuwa jamaa na mayatima na masikini na wasafiri walioharibikiwa wana haki zao katika mali zetu, na anawakataza matajiri wasiifanye mali ikawa kinyang'anyiro baina yao tu na kusahau haki za wengine.

Muislam pia anatakiwa aitumie mali yake katika kuijenga akhera yake na kujitayarishia Pepo yake.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّهُ الدَّارَ الاخِرَةَ وَلَا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّهُ إِلَيْكَ وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الاَرْضِ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ

"Na utafute kwa yale aliyokupa Mwenyezi Mungu - makazi mazuri ya akhera, wala usisahau sehemu yako ya dunia, na ufanye wema kama Mwenyezi Mungu Alivyokufanyia, wala usitafute kufanya ufisadi katika nchi, bila shaka Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi".
[ Al-Qaswas: 77 ].

Haya ndiyo mafundisho ya Kiislam yaliyo kinyume kabisa na mafundisho ya mafisadi wanaojishughulisha na kukusanya mali tu na kurimbika, na wakati huo huo yanatufundisha kuwa Musilam hatakiwi abaki msikitini tu akifanya ‘Ibaadah bila kujishughulisha na elimu pamoja na kufanya biashara, na kuwaachia makafiri peke yao katika uwanja wa elimu na biashara na viwanda, na kwa ajili hiyo wanapata nguvu ya kututawala kiuchumi na kielimu, bali Muislam anatakiwa asiisahau pia sehemu yake ya dunia.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

وَلا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّهُ إِلَيْكَ

"Wala usisahau sehemu yako ya dunia, na ufanye wema kama Mwenyezi Mungu alivyokufanyia".
[ Al-Qaswas: 77 ]

Dini ya Kiislam inatutaka tuwe msitari wa mbele katika kutoa, na Mwenyezi Mungu amewaahidi kheri nyingi wale wanaotoa katika njia Yake.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

مَّثَلُ الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللّهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنبُلَةٍ مِّئَةُ حَبَّةٍ وَاللّهُ يُضَاعِفُ لِمَن يَشَاء وَاللّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ

"Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyotoa mashuke saba; ikawa katika kila shuke pana punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, (zaidi kuliko hivi), na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa mkubwa (na) Mwenye Kujua".
[ Al-Baqarah: 261 ].


Na Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akasema:-

"Hakika ya Swadaqah inazima ghadhabu ya Mola  na inamuondolea maiti adhabu"
[ At-Tirmidhiy ].

Na akasema:-

"Haipiti asubuhi wanayoiamkia watu, ila Malaika wawili wanateremka. Mmoja wao anasema: "Mwenyezi Mungu muongezee mtoaji badala ya kile anachokitoa".Na mwengine anasema: "Mwenyezi Mungu mharibie mali yake (usiite baraka) aliyeacha kutoa ".
[ Muslim ].

 
🔸AINA ZA SWADAQAH 🔸

Swadaqah haina maana ya kutoa pesa tu au kumsaidia mtu, bali Swadaqah ziko aina nyingi sana.

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"Kila Muislam anatakiwa atoe Swadaqah".

Wakasema:-

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, asiyekuwa na mali (je) ?"

Akasema:

"Afanye kazi kwa mikono yake, ajisaidie nafsi yake kisha atoe Swadaqah".

Wakasema:-

"Ikiwa hajapata?"

Akasema:

"Amsaidie mwenye shida".

Wakasema:-

"Asipompata?"

Akasema:-

"Afanye mema na aache shari, kwani akifanya hivyo anaandikiwa (thawabu ya) Swadaqah".
[ Al-Bukhaariy na wengineo]


Na katika riwaya nyingine amesema:-

"Kila siku jua linapochomoza nafsi inaandikiwa juu ya kila inachotenda (katika thawabu ya) Swadaqah. Katika hayo ni kuwapatanisha wawili wanaogombana (anaandikiwa mtu thawabu ya kutoa) Swadaqah. Akimsaidia mtu kumnyanyua ili aweze kumpanda mnyama wake, anaandikiwa Swadaqah, akimnyanyulia mzigo wake, Swadaqah, kuondoa udhia barabarani, Swadaqah, neno jema, Swadaqah, na kila hatua anayokwenda msikitini Swadaqah".
[ Ahmad na wengineo ]


Na akasema:-

"Kati yenu kama yupo mwenye kuuogopa moto, basi atoe Swadaqah walau kwa nusu ya tende, na asiyepata, basi kwa neno jema”.
[ Ahmad na Muslim ].

Na akasema:-

"Siku ya Qiyaamah Mwenyezi Mungu Atasema:-

"Ewe mwanaadamu, niliumwa (kwa nini) hukunitembelea?"

Atasema (mwanadamu):

"Ee Mola, vipi nitakutembelea na wewe ni Mola wa Ulimwengu?"

Atasema:

"Hukujua kuwa mja wangu fulani alikuwa akiumwa na hukumtembelea? Ama ungelimtembelea, ungelinikuta kwake. Ewe mwanaadamu nimekuomba chakula na wewe hukunilisha?"

Atasema:

"Ee Mola wangu, vipi nitakulisha na wewe ni Mola wa ulimwengu wote?"

Atasema:

"Hukujuwa kuwa fulani alikuomba chakula na hukumpa. Huelewe kuwa ungelimpa chakula, ungelikikuta kwangu?

Ewe mwanaadamu, nilikuomba maji hukunipa".

Atasema:

"Ee Mola wangu, vipi nitakunywesha nawe ni Mola wa Ulimwengu wote?'

Atasema:

"Mtu fulani alikuomba maji, na wewe hukumpa. Ama ungelimpa ungeyakuta hayo kwangu".
[ Muslim ].


Na Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akasema pia:-

"Mtu hapandi kitu au halimi kitu kisha mwanadamu akala katika mazao hayo au mnyama au chochote ila ataandikiwa kwa ajili yake Swadaqah".
[ Ahmad na At-Tirmidhiy ]

Na akasema:-

"Kila wema ni Swadaqah, na katika wema ni kumkabili mwenzio kwa uso wa bashasha… (uso mkunjufu)."
[ Ahmad na At-Tirmidhiy ]



 🔺 SEHEMU YA 24  🔺
      Darasa la Zakaah.

Tunaendelea na Darasa letu tukiwa bado katika Mlango wa Zakaah , tuone Walio haramishwa Kupewa Zakaah.


🔹WALIOHARAMISHWA
KUPEWA ZAKAAH. 🔹
        


Walio haramishwa kupewa Zakaah ni hawa Wafuatao :-

1● KAFIRI .

Katika Hadiyth iliyotangulia, Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema :-

" Zichukuliwe kutoka kwa matajiri Wao na kurejeshewa masikini Wao "

Na maana yake ni kuwa:-

Zichukuliwe kutoka kwa matajiri wa Kiislam na kupewa masikini wa Kiislam.


2 ● BANI  HASHIM .

Nao ni watoto wa Aliy na Aqiyl na Jaafar na Al ‘Abbaas na Al Harith (Radhiya LLAAHU ‘anhum).

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

" Swadaqah haijuzu kupewa kwa watu wa Muhammad ".
[ Muslim ].


🔸Maulamaa wamekhatalifiana juu ya ukoo wa Bani Al Muttalib, iwapo nao pia hawapewi katika mali ya Zakaah au wanapewa.

🔺Imaam Ash-Shaafi’iy amesema kuwa hawa nao wasipewe katika mali ya Zakaah, na hii inatokana na Hadiyth iliyotolewa na Imaam Ash-Shaafi’iy na Imaam Ahmad na Imaam Al-Bukhaariy kutoka kwa Jubair bin Mut’am aliposema:-

" Siku ya Khaybar (baada ya kumalizika vita hivyo), Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) aliikusanya upande mmoja sehemu ya ngawira ya watu wa ukoo wake katika Bani Haashim na ya Bani Al-Muttwalib na akawaacha (watu wa kabila lake) katika Bani Nawfal na Bani ‘Abdu Shams. Tukamwendea mimi na ‘Uthmaan bin ‘Affaan na kumuuliza:-

" Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hawa ni Bani Haashim na sisi hatukanushi fadhila zao kutokana na daraja yako mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini vipi hawa ndugu zetu katika Bani Al Muttwalib, umewaingiza wao ukatuacha sisi wakati nasaba yao na yetu juu yako ni sawa sawa ?"

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akasema:-

"Sisi na Bani Muttwalib hatujafarikiana katika ujahilia wala katika Uislam, bali sisi na wao ni kitu kimoja". Akaviingiza vidole vyake vya mkono wa kulia ndani ya vidole vya mkono wa kushoto na kuvichanganya ."


Kutokana na ushahidi huu, baadhi ya maulamaa wakasema;

'Bani Muttwalib nao pia wanaingia katika kuharamishiwa kupewa katika Mali ya Zakaah ".

3 ●  BABA NA WATOTO .

Haijuzu mtu kumpa katika mali ya Zakaah baba yake, mama yake, watoto wake na babu zake, na hii ni kwa sababu mtoaji Zakaah anawajibika kuwatizama watu hao na kuwapa katika mali yake, na kwa ajili hiyo, watu hao wanalazimika kuwa matajiri kutokana na utajiri wake.


4 ● MKE .

Haijuzu mtu kumpa mkewe katika mali ya Zakaah, na jambo hili linakubaliwa na maulamaa wote na hii ni kwa sababu mtu anawajibika kumtizama na kumpa mkewe katika mali yake kama anavyowajibika kuwapa wazee wake wawili akiwa anao uwezo huo.

Anasema Ibnul Mundhir :-

"Isipokuwa kama mke ana deni, basi hupewa Zakaah katika ile sehemu ya kuwasaidia wenye madeni kwa ajili ya kulipa deni hilo".

Ama ikiwa mke ni tajiri mwenye uwezo wa kutoa Zakaah, basi yeye anarushusiwa kumpa mumewe katika mali ya Zakaah kutokana na kauli ya Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) aliposema:-

" Amesema kweli Ibn Mas’uud, mumeo na mwanao wanastahiki zaidi kuwapa Swadaqah ".
[ Al-Bukhaariy ].


5 ● Haijuzu kuitumia mali ya Zakaah kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kama vile kujenga misikiti, kununua misahafu, kununua vifaa vya kusaidia kuosha maiti nk. Na hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu kwa hekima yake keshazitaja na kuzisherehesha njia za kutoka Zakaah katika ayah iliyotangulia ya Surat At-Tawbah -60, na akaikamilisha ayah hiyo kwa kusema;

" Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi (na) Mwenye hikima ".




    🔺  SEHEMU YA 26   🔺
          Darasa la Zakaah.


🔹KUINUNUA  ZAKAAH.


Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amekataza mtu kuinunua Zakaah yake.

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya LLAAHU ‘anhu), amesema:-

"‘Umar (Radhiya LLAAHU ‘anhu) alimtoa farasi wake Swadaqah fiy sabiyli LLAAHI, kisha akamkuta farasi huyo anauzwa na akataka kumnunua. Akamuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) juu ya jambo hilo, akamwambia:-

"Usimnunue na wala usirudie (kutaka kuimiliki tena) Swadaqah yako"

Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo



Baadhi ya maulamaa wakasema kuwa kukataza huko ni kwa ajili ya kujiepusha tu, na si kwa ajili ya kuharamisha, wakiegemea Hadiyth nyingine inayoruhusu mtu kuipokea Swadaqah yake kamazawadi itokayo kwa masikini aliyempa.



Naam tunaendelea na Darasa letu tukiwa katika Mlango wa Zakaah, na tumeshaelezea Makundi Matatu (3) kati ya Makundi Nane (8) yanayoStahili  kupewa Zakaah Kutoka Zakaatul Maal , Kwahiyo tuendelee Kuona Makundi Mengine Matano (5) yaliyobakia.


🔹WENYE KUTIWA NGUVU🔹
Hawa ni watu wanaopewa katika mali ya Zakaah kwa ajili ya kulainishwa nyoyo zao na kutiwa nguvu kutokana na udhaifu wa nyoyo hizo, na wengine hupewa kwa ajili ya kuwaepusha Waislam na shari zao, au kuwavutia katika kuupenda Uislam na kuupa nguvu.

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiwapa wakubwa wa makabila ya Kiarabu na hasa makabila ya Kibedui kwa ajili ya kuwapendekeza katika Uislam.

Imepokelewa kuwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alimpa mtu mmoja aitwae Safwaan bin Umayyah ngamia wengi sana katika ngamia wa ngawira waliopatikana katika vita vya Hunain, na Safwan huyu alikuwa mkubwa wa kabila lake.

Safwaan alikuwa wakati huo bado hajasilimu, na alipopewa mali hiyo, akarudi kwa watu wake na kuwaambia:-

"Enyi watu wangu, ingieni katika dini ya Kiislam, kwani Muhammad anatoa utoaji wa mtu asiyeogopa ufakiri".


(Mwenye kuchunguza, ataona kuwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiwatendea makabila ya Kibedui tofauti na anavyowatendea watu wa mijini. Alikuwa akiwachukulia kwa akili zao. Na hii ni kwa sababu Mabedui ni watu wagumu sana kufahamu. Hata katika kuuliza masuali, Mabedui walikuwa wakimuuliza Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) masuali na kujibiwa, wakati masuali hayo hayo wangeuliza Maswahaba wanaokaa mjini (Radhiya LLAAHU ‘anhum), basi Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) angekasirika nayo masuali hayo).


Wakati wa ukhalifa wake Abu Bakr (Radhiya LLAAHU ‘anhu) alikuwa akiendelea kuwapa watu wa aina hii, lakini ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya LLAAHU ‘anhu) siku moja alikataa kutoa, akawaambia:-

"Hii Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alikuwa akikupeni kwa ajili ya kuzizowesha nyoyo zenu na kuzilainisha, lakini sasa Mwenyezi Mungu amekwishautukuza Uislam na hatuna haja nanyi tena, mkitaka ingieni katika Uislam, na kama hamtaki basi baina yetu na baina yenu ni panga. Mwenyezi Mungu Amesema:-

وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَن شَاء فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاء فَلْيَكْفُرْ

"Na sema; 'Huu ni ukweli ulotoka kwa Mola wenu, basi anayetaka na aamini na anayetaka na akufuru.”
[( Al-Kahf: 29 )].

Anasema Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah:-

"Abu Bakr (Radhiya LLAAHU ‘anhu) alikubaliana na ‘Umar (Radhiya LLAAHU ‘anhu) katika uamuzi wake huo, na hapana hata Swahaba mmoja (Radhiya LLAAHU ‘anhum) aliyepinga. Na hii ni katika Ijtihadi zake ‘Umar (Radhiya LLAAHU ‘anhu), na hata Makhalifa waliokuja baada yake, Uthmaan na Aliy (Radhiya LLAAHU ‘anhum) hawakuwapa tena watu wa aina hii katika mali ya Zakaah.

Hata hivyo," anaendelea kusema Shaykh Saabiq, " hii haimaanishi kuwa watu wa aina hii wasipewe, na Imaam yeyote yule atakayetawala na akaona kuwa ipo haja ya kuwapa watu wa aina hii, basi atawapa kwa sababu dalili ipo katika Qur-aan na Sunnah.”


  🔹KATIKA KUGOMBOA🔹

Uislam umeijaalia ‘Ibaadah hii ya kuwagomboa mateka na watumwa kuwa ni kitendo kinachompatia Mtu thawabu nyingi sana na kumuingiza katika Pepo za Mwenyezi Mungu Subhanaahu wa Ta’ala.

Kutoka kwa Al-Barra-a (Radhiya LLAAHU ‘anhu) amesema:-

"Mtu mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) na kumwambia:-

" Nijulishe juu ya amali (njema) itakayonikurubisha na Pepo na kunibaidisha na Moto ".

Akasema Mtume صلى الله عليه وسلم :-

" Waachie huru watu na wagomboe watumwa ".

Akauliza (tena):-

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, si yote hayo yanabeba maana moja tu?"

Akasema:-

"La, (sivyo), 'kuwaachia huru' ni kujihusisha peke yako katika kuwaacha huru, na 'kuwagomboa' ni kusaidia katika kulipa thamani ya kuwagomboa".
[( Ahmad na Ad-Daaraqutniy.)].


Wakati ule ilikuwa Mtumwa anaweza kuandikiana na kukubaliana kuwa atakapoweza kulipa malipo fulani katika muda fulani, ataachwa huru. Kwa hivyo Waislam walitakiwa wawasaidie watu wa aina hiyo kwa kuwalipia kiasi hicho ili waweze kujigomboa.


🔹KUMSAIDIA MWENYE🔹
                    DENI .

Hawa ni wale wenye madeni makubwa wakashindwa kuyalipa kutokana na kula hasara katika biashara zao nk. Sharti madeni hayo yawe katika mambo ya halali au yatokane na Maasi aliyotubu nayo mtu huyo.


Imepokelewa kutoka kwa Maimaam Ahmad na Abu Daawuud na Ibn Majah na At-Tirmidhiy, kutoka kwa Anas (Radhiya LLAAHU ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alisema:-

"Mas-ala (ya kuwasaidia wenye madeni), hayawi halali isipokuwa katika mambo MATATU; aliye fakiri sana, au mwenye deni zito sana, au mwenye kudaiwa damu (ya diya - fidiya).”

(Huyu ni mtu aliyejikuta amebebeshwa deni la diya kutokana na ndugu yake au jamaa yake aliyeuwa kwa bahati mbaya. Ikiwa hajalipa diya hiyo, basi ndugu yake huyo au jamaa yake atauliwa kwa ajili ya kulipa kisasi )


 🔹KATIKA KUTENGENEZA🔹

(Fiy sabiyli LLAAH), ni njia yoyote ile inayomfikisha mtu katika kumpatia radhi za Mwenyezi Mungu Subhanaahu wa Ta’ala, juu ya kuwa Maulamaa wengi wanasema kuwa haya ni mambo yanayohusiana na vita vya Jihadi tu pamoja na watu wanaopigana vita hivyo.



Hawa wana sehemu yao katika mali ya Zakaah wanayopewa hata kama askari mpiganaji Jihadi ni tajiri anayejiweza.

Anasema Sayyid Saabiq, katika Fiqhis Sunnah:-

"Maulamaa wengine wamesema kuwa inajuzu kuzitumia pesa hizo katika kutengeneza njia inayowapeleka watu Makka kwa ajili ya Hijjah na katika kuwanunulia maji ya kunywa na chakula ikiwa hapana mali nyingine inayoweza kutumiwa katika kazi hiyo. Inajuzu pia kuzitumia katika kuwasomesha na kuwatayarisha walingaNiyaji wa dini kwa ajili ya kuwapeleka katika nchi zisizokuwa za Kiislam kwa ajili ya kufanya da’awa nk."

Vitu vinavyonunuliwa kutokana na pesa za Zakaah kwa ajili ya vita, kama vile farasi, panga, nk. lazima virudishwe katika nyumba ya hazina ya Waislam (Baytul maal) baada ya kumalizika kwa vita.


  🔹  KATIKA KUPEWA  🔹
              WASAFIRI .

Msafiri aliyeishiwa na pesa akawa hana njia nyingine ya kupata pesa za matumizi, huyu anapewa katika mali ya Zakaah, sharti safari yake hiyo iwe katika mambo ya twa-a na si katika kumuasi Mola wake, hata akiwa msafiri huyo huko kwao alikotoka ni mtu tajiri mwenye mali nyingi.

Na hayo ndio Makundi nane (8) yanayopaswa kupewa Zakaah kutoka katika Zakaatul Maal .



🔺 WENYE KUSTAHIKI
ZAIDI  KUPEWA
SWADAQAH 🔺           
      .

Unatakiwa Uanze na watu wako, Mkeo na Watoto wako pamoja na ndugu zako wa nasaba ndio wanaoistahiki zaidi Swadaqah yako.

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"Mmoja wenu akiwa fakiri, basi ajitosheleze nafsi yake, kinachozidi awape watoto wake, kinachozidi, awape ndugu zake wa nasaba, na kikizidi basi atoe huku na kule".
[ Ahmad na Muslim ].


🔹TANBIHI:-
Hukumu ya Swadaqah inahitilafiana na ya Zakaah, kwani mali ya Zakaah haijuzu kupewa asiyekuwa Muislam, lakini Swadaqah anaweza kupewa asiyekuwa Muislam.


Mwenyezi Mungu Anasema:-

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَى حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا

"Na huwalisha chakula maskini na mayatima na wafungwa na hali ya kuwa wenyewe wanakipenda".
[ Ad-Dahar: 8 ].


Neno lililotumika kwa 'wafungwa', katika ayah hii ni 'Asiyran', na maana yake ni mateka wa kivita ambaye bila shaka ni kafiri aliyetekwa baada ya kupigana vita dhidi ya Waislam, lakini juu ya hivyo Mwenyezi Mungu anawasifia Waislam wanaowalisha chakula wafungwa hao.


 🔺     KUIHARIBU    🔺
           SWADAQAH
                  YAKO

Haijuzu kumsimulia au kumdharau anayepokea Swadaqah kwa sababu kilichomfanya akubali kuipokea Swadaqah hiyo ni umasikini wake, na mtu kumtakabaria masikini ni dhambi kubwa sana, na anapofanya hivyo thawabu zake zinapotea bure.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تُبْطِلُواْ صَدَقَاتِكُم بِالْمَنِّ وَالأذَى كَالَّذِي يُنفِقُ مَالَهُ رِئَاء النَّاسِ وَلاَ يُؤْمِنُ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ

"Enyi mlioamini! Msiharibu Swadaqah zenu kwa masimulizi na udhia kama yule anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamwamini Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho".
[ Al-Baqarah: 264 ].


🔺 KUTOA SWADAQAH  🔺
          KATIKA MALI YA
                HARAMU.

Mwenyezi Mungu haikubali Swadaqah ikiwa inatokana na mali ya haramu. Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema :-

"Enyi watu! Mwenyezi Mungu ni mzuri na hakubali isipokuwa kizuri tu ".

Imesimuliwa kuwa siku moja mtu mmoja aliiba tufaah kisha akaliuza, na pesa alizopata akawagawia masikini.

Habari zilipomfikia Qaadhi wa mji huo, akamwita na kumuuliza:-

"Kwa nini umeiba kisha ukazigawa Swadaqah pesa za mali ya wizi ?"

Yule mtu akajibu :-

"Kwa sababu Mwenyezi Mungu Anasema :-

مَن جَاء بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا وَمَن جَاء بِالسَّيِّئَةِ فَلاَ يُجْزَى إِلاَّ مِثْلَهَا

"Afanyae kitendo kizuri atalipwa mfano wake mara kumi. Na afanyae kitendo kibaya hatalipwa ila sawa nacho tu".
[ Al-An’aam: 160 ].

Kwa hivyo, akaendekelea kusema mtu Yule aliyeiba tufaah: ‘Kutokana na aya hii, mimi nilipoiba tufaah nilifanya kitendo kibaya nikalipwa dhambi moja tu sawa na tufaah moja nililoiba, lakini nilipowagawia masikini nilifanya kitendo chema nikalipwa mara kumi, na thawabu 10 nilizozipata kwa kuligawa tufaah lile, ukitoa ile dhambi moja ya kuiba, nitabakiwa na thawabu tisa"

Qaadhi akamwambia :-

"Lakini umesahau jambo moja ewe ndugu Muislam, (Mwenyezi Mungu ni mwema, na hakubali isipokuwa chema tu ).”



  🔺    KUWASAIDIA.     🔺
       WANYAMA PIA NI
           SWADAQAH.

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alisema kuwaambia Maswahaba (Radhiya LLAAHU ‘anhum):

"Mtu mmoja aliyekuwa akitembea, alishikwa na kiu, akaona kisima mbele yake, akateremka na kunywa maji ndani yake kisha akatoka. Alipokuwa akitoka alimuona mbwa akihema kwa kiu. Yule mtu akasema; "Bila shaka mbwa huyu ameshikwa na kiu kama nilivyoshikwa mimi. Akateremka (tena) kisimani, akajaza maji kiatu chake, kisha akamshika kichwa chake mbwa yule na kumnywesha.

Akashukuriwa na Mwenyezi Mungu na kughufuriwa".

Maswahaba (Radhiya LLAAHU ‘anhu) wakasema:

" Hata katika wanyama tunapata thawabu ?"

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akasema:

"Katika kila chenye uhai mna thawabu".
[ Al-Bukhaariy ].


  🔺  SWADAQATUN  🔺
             JAARIYAH .

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema :-

"Mwanaadamu anapokufa, amali zake zote zinakatika isipokuwa TATU. SWADAQATUN Jaariyah (Swadaqah inayoendela), au ELIMU yenye kunufaisha watu, au MTOTO mwema anayemuombea".
[ Ahmad na Muslim ].


🔺KUSHUKURU PIA NI🔺
           SWADAQAH .

Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"Atakayekufanyieni Wema mlipeni, na ikiwa hamna cha kumlipa, basi muombeeni dua mpaka muhisi kuwa mumemlipa".
[ Abu Daawuud na An-Nasaaiy ].


Imesimuliwa na IMAAM AHMAD kutoka kwa Al-Ash’ath bin Qays kuwa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

" Hamshukuru Mwenyezi Mungu yule asiyewashukuru watu ."
[ Ahmad ].

Na akasema :-

"Aliyetendewa jema, akasema kumwambia aliyemtendea: “JAZAAKA ALLAAHU KHAYRAN ', (Mwenyezi Mungu Akujaze kheri), huyo amekwisha shukuru kama inavyotakikana ".


    🔸 SEHEMU YA 20 🔸
        Darasa la Zakaah.


    🔹ZAKAATUL FITWR🔹

Imefaridhishwa katika mwezi wa Shaabani mwaka wa 2 baada ya Hijra (baada ya kuhamia Madina). Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alifaridhisha Zakaatul Fitwr ili iitakase saumu kutokana na dhambi ndogo ndogo zilizopatikana ndani ya mazungumzo na matendo. Na wakati huo huo Zakaah hiyo iwe msaada kwa mafakiri na wasiojiweza katika kuisherehekea Sikukuu.

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya ALLAAHU ‘anhu) kuwa amesema :-

"Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) alifaridhisha Zakaah ya Fitwr kwa ajili ya kumtakasa aliyefunga kutokana na dhambi ndogo ndogo za mazungumzo na matendo, na ili wafaidike masikini. Atakayeitoa kabla ya Swalaah (ya Idi) inakubaliwa kama Zakaah ya Fitwr na atakayeitoa baada ya Swalaah inakubaliwa kama Swadaqah ya kawaida ."
[ Abu Daawuud – Ibn Maajah na Ad-Daaraqutniy ]



Alikuwa (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) akitoa Zakaah ya Fitwr siku ya mwisho ya mwezi wa Ramadhan kabla ya Swalaah ya Idi kuswaliwa" .
[ Abu Daawuud na Ibn Majah na Al Hakim ].



Kila aliyefunga Mwezi wa Ramadhaan mwenye kumiliki chakula cha kumtosha kwa muda wa siku moja, inamwajibikia kutoa Zakaatul Fitwr, nayo ni pishi ya tende au pishi ya ngano au pishi ya shaiyri. Anatakiwa atowe kwa ajili yake na kwa ajili ya kila anayemtegemea kama vile wanawe, wakeze nk. na kuwapa masikini ili nao wapate kufurahi katika Siku ya Sikukuu.

Kwa vipimo vya kisasa, pishi moja ya mbao iliyokuwa ikitumika wakati wa Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) ni kiasi cha kilo 2.

🔺Zakaah hii ni wajibu kwa kila Muislam mdogo na mkubwa, mwanamume au mwanamke.

Ibn ‘Umar (Radhiya LLAAHU ‘anhu) amesema :-

"Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amefaridhisha kwa kila mtu kutoa Zakaatul Fitwr katika mwezi wa Ramadhaan, pishi ya tende (au) pishi ya shaiyri, ikiwa yeye ni mtumwa au mtu aliye huru, mwanamume au mwanamke, mdogo au mkubwa miongoni mwa Waislam".
[ Al-Bukhaariy na Muslim ].


  🔹  HIKMA  YAKE 🔹
     ZAKAATUL FITWR


Zakaatul Fitwr ilifaridhishwa katika mwezi wa Shaabani mwaka wa pili baada ya Hijra kwa ajili ya kumtwahirisha aliyefunga kutokana na makosa yoyote yale aliyotenda katika mwezi wa Ramadhaan pale alipokuwa amefunga, kama vile mazungumzo ya upuuzi au madhambi, na wakati huo huo Zakaah hiyo itawafaa masikini na wahitaji ili nao wapate kufurahi pamoja na Waislam wenzao siku ya Sikukuu.

Ibn ‘Abbaas (Radhiya LLAAHU ‘anhu) amesema:-

"Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amefaridhisha Zakaatul Fitwr kwa ajili ya kumtahirisha aliyefunga kutokana na maneno ya upuuzi au madhambi madogo madogo na ili masikini nao wapate chakula. Atakayeitoa (Zakaah hiyo) kabla ya Swalaah (ya Idi) inakubaliwa Zakaah yake, ama atakayeitoa baada ya Swalaah (ya Idi), itahesabiwa kama ni Swadaqah ya kawaida tu".
[ Abu Daawuud na Ibn Majah na Ad-Daaraqutniy ].



  🔺 MWENYE KUITOA 🔺
        ZAKAATUL FITWR.

Anayeitoa Zakaah hiyo ni mtu aliyefunga. Anajitolea yeye mwenyewe, mkewe na watoto wake wanaomtegemea na anawatolea pia wote wale wanaomtegemea wakiwemo watumishi wake.


      🔺  KIASI  CHAKE 🔺
        ZAKAATUL FITWR.

Iliyowajibishwa katika Zakaatul Fitwr ni pishi ya ngano au ya shaiyri au ya tende au zabibu au mchele au mahindi na vinginevyo vilivyo na mfano huo katika vyakula.

🔹Imaam Abu Haniyfah peke yake amejuzisha kutoa pesa zenye thamani hiyo badala ya kutoa nafaka panapo udhuru.


  🔺WAKATI WA KUITOA🔺
      ZAKAATUL FITWR.

Maulamaa wengi wamekubalina kuwa Zakaatul Fitwr itolewe katika Ramadhaan ya mwisho, lakini wamekhitalifiana juu ya wakati maalum unaowajibika kuitoa.

Wapo waliosema kuwa wakati unaowajibika kuitoa ni pale jua la Ramadhaan ya mwisho linapozama, na wengine wakasema kuwa wakati wake ni kuanzia baada ya kuingia alfajiri ya siku ya Sikukuu.

🔹Kutokana na hitilafu hii tunapata faida ya kuwajibika kumtolea Zakaah hiyo mtoto aliyezaliwa kabla ya kuingia alfajiri ya siku ya Sikukuu na baada ya jua kuzama, je mtoto huyo anatolewa Zakaah?

🔸Kwa wale wenye kufuata rai kuwa wakati wa kuitoa Zakaah hiyo ni pale jua la siku ya Ramadhaan ya mwisho kuzama, mtoto huyo hatolewi Zakaah kwa sababu amezaliwa baada ya kumalizika wakati wa kuwajibika, na kwa wenye kufuata rai ya pili, kwa sababu amezaliwa kabla ya wakati unaomwajibika.

       🔺  Kuitanguliza 🔺
         ZAKAATUL FITWR.

Maulamaa wengi wanakubali kuwa Zakaatul Fitwr inaweza kutangulizwa na kutolewa kabla ya wakati wake kwa siku moja au mbili.

Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya LLAAHU ‘anhu) inasema:-

"Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) ametuamrisha kuitoa Zakaatul Fitwr kabla ya watu kutoka msikitini (katika Swalaah ya ‘Iyd)".


Anasema Naafi’ (Radhiya LLAAHU ‘anhu):-

"Ibn ‘Umar (Radhiya LLAAHU ‘anhu) alikuwa akiitoa kwa siku moja au siku mbili kabla ya Siku ya Sikukuu".

🔺TANBIHI :-
Ama zaidi ya hapo, maulamaa wamekhitalifiana.

🔸IMAAM ABU HANIYFAH amesema:-
"Inaweza kutolewa wakati wowote ule katika mwezi wa Ramadhaan".

🔸IMAAM ASH-SHAAFI’IY amesema:-
"Inajuzu kuitoa (hata) katika siku za mwanzo za mwezi wa Ramadhaan ".

🔸IMAAM MALIK  amesema:-
"Inajuzu kutanguliza kwa siku moja au mbili kabla ya Sikukuu".

Lakini maulamaa wote wamekubaliana kuwa haijuzu kuiahirisha na kuitoa baada ya ‘Iyd.
.


  🔺 SEHEMU YA 25 🔺
       Darasa la Zakaah.


     🔹WATU  WEMA .

Zakaah anapewa Muislam anayeistahiki akiwa Muislam huyo ni mtu mwema au mtu asi, isipokuwa mtu asi hapewi katika mali ya Zakaah ikiwa itajulikana kwa uhakika kuwa atakuja kuitumia mali hiyo katika kuuendeleza uasi wake.

Ikijulikana kwa uhakika kuwa ataitumia mali hiyo katika kumuasi Mwenyezi Mungu, basi mtu huyo atanyimwa, ama ikiwa hayajulikani hayo, au ikijulikana kuwa ataitumia mali hiyo katika shida zake, basi hapo atapewa.



Hata hivyo ni bora kwa mtoaji Zakaah aihusishe mali hiyo kwa kuwapa watu wema au maulamaa wanaostahiki wanaoifayia kazi elimu yao, kwani Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"Walisheni chakula chenu wacha Mungu na mnaowajuwa katika walioamini (kweli) ".
[ Ahmad ].


🔺Anasema Ibn Taymiyah:-

"Asiyeswali hapewi katika mali ya Zakaah mpaka pale atakapotubu akawa anaswali."


🔺Anasema Sayyid Saabiq:-

"Katika kundi hilo  wanaingia pia wale wanaomuasi Mwenyezi Mungu bila kujali wala kuona haya, na kuendelea kuzama katika maasi huku nyoyo zao zikiwa ziAsh-Shaafi’iysidika na dhamiri zao zimekwisha haribika".


Hawa hawapewi katika mali ya Zakaah isipokuwa kama Zakaah hiyo itawasaidia katika kuwaongoza mwongozo ulio sahihi au itawasaidia katika kutoka hali yao hiyo.



   🔺  SEHEMU YA 27  🔺
        Darasa la Zakaah.


🔹KUISAFIRISHA ZAKAAH🔹
Mulamaa wengi wamekubali kuwa mali ya Zakaah (Zakaatul Maal - si Zakaatul Fitwr) inaweza kusafirishwa na kutolewa katika nchi nyingine kwa wanaoistahiki zaidi ikiwa watu wa mji anaoishi mtoaji hawaihitajii zaidi mali hiyo. Ama ikiwa katika nchi hiyo wapo wanaoihitajia, basi zipo Hadiyth zinazotujulisha kuwa Zakaah ya kila nchi wanapewa masikini wake.

Katika madhehebu ya Imaam Abu Haniyfah, wao wanasema:-

"Ni Makruuh kuisafirisha mali ya Zakaah isipokuwa ikiwa kwa ajili ya kumsaidia ndugu wa nasaba mwenye kuihitajia, na hii inatokana na umuhimu wa kuunganisha undugu huo, au pia kwa ajili ya watu wenye shida sana katika watu wa nchi yake, au kwa ajili ya kuiondoa kutoka nchi ya kikafiri na kuipeleka katika nchi ya kiislam."



🔹Madhehebu ya Imaam Ash-Shaafi’iy yanasema:-

"Haijuzu kuisafirisha mali ya Zakaah na inawajibika kutolewa katika nchi iliyochumwamali hiyo isipokuwa pakikosekana wenye kuihitajia Zakaah hiyo katika nchi hiyo".



Mu’aadh bin Jabal (Radhiya LLAAHU ‘anhu) alipewa ugavana wa nchi ya Yemen na Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam), na alipotawala ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya LLAAHU ‘anhu) alimuacha Mu’aadh aendelea kuwa gavana wa nchi hiyo. Lakini Mu’aadh (Radhiya LLAAHU ‘anhu) alipompelekea ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya LLAAHU ‘anhu) theluthi ya mali ya Zakaah, ‘Umar (Radhiya LLAAHU ‘anhu) alikataa kuzipokea akamwambia:-

"Sikukupeleka uwe mchotaji (wa mali) wala mpokeaji wa kodi, bali nimekupeleka kwa ajili ya kuchukua mali (ya Zakaah) kutoka kwa matajiri wao na kuzirudisha kwa masikini wao".

Mu’aadh (Radhiya LLAAHU ‘anhu) akasema:-

"Nisingekuletea ila kwa sababu sikumpata (masikini) anayezistahiki kuzichukua".



 🔺SEHEMU YA 28🔺
    Darasa la Zakaah.


🔹 KUIDHIHIRISHA 🔹
             ZAKAAH.


Inazuju kwa mtoaji kuidhihirisha au kuitoa kwa siri Zakaah yake, yote sawa ikiwa anachokitowa ni Swadaqah ya kawaida au Zakaah ya mali, ingawaje kuitoa kwa siri ni bora zaidi.

Mwenyezi Mungu Anasema:-

إِن تُبْدُواْ الصَّدَقَاتِ فَنِعِمَّا هِيَ وَإِن تُخْفُوهَا وَتُؤْتُوهَا الْفُقَرَاء فَهُوَ خَيْرٌ لُّكُمْ

"Kama mkitoa Swadaqah kwa dhahiri ni vizuri, nakama mkitoa kwa siri na kuwapa mafakiri, basi huo ni ubora zaidi kwenu".
[ Al Baqarah - 271 ].



Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wa sallam) amesema:-

"(Watu aina) Saba Mwenyezi Mungu Atawaweka chini ya kivuli chake siku ambayo hapatokuwa na kivuli isipokuwa kivuli chake:- Imaamu muadilifu, na kijana aliyekulia katika kumuabudu Mwenyezi Mungu, na mtu ambaye moyo wake umeshughulika na misikiti, na watu wawili waliopendana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, walikutana kwa ajili Yake na wakafarikiana kwa ajili Yake, na mtu aliyetoa Swadaqah kwa siri akaificha hata (mkono wake wa) kushoto usijuwe nini kimetolewa na wa kulia, na mtu aliyemtaja Mwenyezi Mungu akiwa peke yake mpaka akatoka machozi, na mtu aliyeitwa na mwanamke aliye na cheo (kikubwa) na mali (nyingi) akimtaka kwa ajili ya nafsi yake (akimtaka azini naye), akasema (mtu huyo); "Mimi namuogopa Mwenyezi Mungu".
[ Al-Bukhaariy - Muslim na Imaam Ahmad ]

 Na hapa ndio mwisho wa Darasa letu la Zakaah .

     🔹         MWISHO         🔹
           DARASA ZAKAAH


*********************************************************************************
*********************************************************************************

JE INARUHUSIWA KUTAZAMA PICHA ZA NGONO KWA AJILI YA KUJIANDAA NA NDOA



SWALI: 
Kanijia mtu kisha akaniuliza swali.
ANASEMA KUWA YEYE HAJAWAHI KUFANYA UCHAFU WA ZINAA, NA ANATARAJIA KUFUNGA NDOA MWEZI WA SABA, ANAWEZA KUANGALIA PICHA ZA EX KWA AJILI YA KUJIANDAA, ILI ASIJEKUPATWA NA AIBU WAKATI ATKAPOKU NDANI NA MKE WEKE, KWA SABABU HAJUI HILI WALA LILE KWA UPANDE WA MWANAMKE, KWA HIVYO NDIO ANAULIZA SWALI  INAFAA? 


JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mas-ala ya ngono wakati wa Nikaah. Kuhusu kuangalia picha za uchi au picha chafu zozote kwa sababu yoyote ile haifai katika Uislamu. Hili hata kimantiki haliingii akilini kwani wale ambao utakuwa ukiwaangalia watakuwa katika hali ya uchi ambayo imekatazwa na Uislamu. Picha hizo zinamtia mwanamme ashiki ya bure na hivyo kumkaribisha yeye na zinaa.

Jambo ambalo anafaa kufanya ni kupata vitabu vya Kiislamu ambavyo vinaelezea suala hilo kwa muono unaofaa kidini. Pia anaweza kukaa na mashaykh ambao watamfunza kwani mas-ala hayo ya ngono hasa usiku wa kwanza yameelezewa na Uislamu. Na tendo la ndoa limeezewa kinaganaga katika Qur-aani na Sunnah, kwa nini sisi tutafute njia nyingine mbaya? 

Mwambie ndugu yetu asitie wasiwasi kwani hilo si jambo zito bali ni jambo la kawaida kabisa na ni suala la kimaumbile na unapofika wakati ataliona kuwa ni jepesi na rahisi kufahamika.

Ikiwa hukupata vitabu hivyo wala Sheikh ambaye anaweza kukupatia muongozo kuhusu hilo basi inafaa ukae na mtu uliye karibu naye ambaye tayari ameoa naye atakupa nasaha na maelezo yanayofaa.

 

***********************************************************************************************

Inafaa Kufunga Swaum Za Sunna Kabla Ya Kulipa Deni La Ramadhaan?



SWALI:

Asalam alaykum. Inafaa kufunga swaum za sunna kama ya arafah na nyinginezo ikiwa hujalipa deni la swaum ya Ramadhan? Kwa mfano Arafah imefika na ninataka kufunga, lakin nina deni la Ramadhan kama siku 5, je ninaweza kufunga Arafah, halafu hilo deni nitafunga siku nyengine?



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Baadhi ya Maulamaa wameona kwamba haipasi kutekeleza ‘Ibaada za Sunna kabla ya kutimiza za fardhi. Kwa sababu faradhi ni deni na isipotekelezwa huwa ni dhambi. Ama asipotekeleza ibada ya Sunna mtu huwa hapati dhambi. Hivyo basi ni vyema kwanza kutekeleza faradhi kwani hakuna uhakika wa uhai, huenda mtu akaondoka duniani na kubakisha deni.  

Hata hivyo, atakayefunga Swaum za Sunna kabla ya kulipa deni, Swaum yake itasihi InshaAllaah madamu atakuwa anao muda wa kulipa deni, kwani deni linaweza kulipwa hadi kabla ya Ramadhaan inayofuatia.

Na ikiwa mtu atalipa deni pamoja na kutia Niya kufunga Sunna kama za ‘Arafah, ‘Aashuraa basi atakuwa ametimiza deni lake na atapata pia thawabu za kufunga Sunna.  

Lakini kuunganisha deni la Ramadhaan na Swaum ya Sunna ya Sita ya Shawwaal haifai kwani hilo hukumu yake tofauti kabisa kutokana na dalili zake.

 

-------------------*************--------------------

Anajitegemea Mwenyewe, Anachangia Katika Futari, Je Anawajibika Kutoa Zakaatul-Fitwr?

SWALI:
salam alaykum.
Swali langu ni kwamba. Mimi nataka kutoa zaka ni msichana ninae jitegemea lakini nimekua nafturu kwa ndugu tofauti mwezi mzima. Na pia huko ninako enda kufuturu nachanigia kitu katika ftar. Je zakaah yangu niitoe vipi?
Waaleykum saam.




JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kufuturu kwa watu au kuchangia futari haihusiani na hukmu ya kutoa Zakaatul-Fitwr kwani hikma ya kutoa Zakaatul-Fitwr ni kuitwaharisha Swawm ya mwenye kufunga kutokana na maneno maovu, machafu ambayo ameyatamka. Vile vile ili kuwapatia masikini nao chakula kizuri siku ya 'Iyd nao wafurahi. Dalili ifuatayo ni uthibitisho:
عَنْ ابْنِ عَبَّاس ٍقَالَ فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ طُهْرَةً لِلصَّائِمِ مِنْ اللَّغْوِ وَالرَّفَثِ وَطُعْمَةً لِلْمَسَاكِينِ مَنْ أَدَّاهَا قَبْلَ الصَّلاةِ فَهِيَ زَكَاةٌ مَقْبُولَةٌ وَمَنْ أَدَّاهَا بَعْدَ الصَّلاةِ فَهِيَ صَدَقَةٌ مِنْ الصَّدَقَاتِ . " رواه أبو داود  بِإِسْنَادٍ حَسَنٍ .

Kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambaye amesema: "Mtume amefaridhisha Zakaatul-Fitwr kuwa ni twahara ya mwenye kufunga kutokana na maneno ya upuuzi na machafu, na kulisha masikini. Atakayeitoa kabla ya Swalah basi hiyo ni Zakaah iliyotakabaliwa, na atakayeitoa baada ya Swalah basi hiyo ni Sadaqah miongoni mwa Sadaqah" [Abu Daawuud kwa isnaad iliyo nzuri].

Kwa hiyo  ni waajib wako kuota Zakaatul-Fitwr maadam una uwezo na unajitegemea mwenyewe.

 *****************************************************************************

Alifanya Jimai (Kitendo Cha Ndoa) Bila Ya Kujua Kwamba Alfajiri Imeingia



SWALI:

Mume alifanya Jimai (Kitendo cha Ndoa) na mkewe katika masaa ya mwisho ya usiku akidhania kuwa wakati wa Alfajiri bado haujaingia. Lakini, baada ya kumaliza, katoka chumbani na kutambua kuwa amefanya kitendo hicho baada ya Alfajiri kuingia. Amesikitika na akaendelea kufunga.  Lakini anahisi kuwa amefanya dhambi na anauliza nini kinachompasa kufanya kuhusu kufanya kitendo hiki baada ya Alfajiri kuingia?

JIBU:

Kama hali ilikuwa kama ilivyotajwa, basi anatakiwa alipe siku hiyo na kama ana hakika kuwa alifanya kitendo cha Jimai baada ya kutakiwa ajiepushe na mambo yanayovunja Swawm baada ya kuingia Alfajiri. Na akishalipa siku hiyo, anatakiwa aache huru mtumwa mmoja aliye muumin na ikiwa hawezi basi afunge miezi miwili mfululizo (bila ya kupumzika) na ikiwa hawezi basi alishe masikini 60 au watu wanaohitaji kwa sababu ya dharau yake ya kufanya kitendo hicho bila ya kuhakikisha wakati kama Alfajiri imeingia. Na mke naye anatakiwa kulipa hivyo hivyo isipokuwa ikiwa alilazimishwa kufanya kitendo hicho na mumewe.

Na kwa Allaah سبحانه وتعالى  ndio yako mafanikio yote na Rahma na Amani zimfikie Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na Swahaba zake.

 

Halmashauri ya kudumu ya Utafiti Wa Kiislaam Imejumuisha:

Kiongozi Mkuu: Shaykh 'Abdul 'Aziyz ibn 'Abdullaah  ibn Baaz

Msaidizi Kiongozi Mkuu: Shaykh ‘Abdullaah ibn Ghudayyaan

Mwanachama: Shaykh 'Abdullaah Ibn Ghudayyan

Fataawa Ramadhaan - Mjalada 2, Ukurasa  615, Fatwa Namba 612;
Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah lil-Buhuuth al-'Ilmiyyah wal-Iftaa. - Fatwa Namba 10676

 ********************************************************************************

Hukmu Ya Kutenda Kitendo Cha ndoa Mchana Wa Ramadhaan




SWALI:

Nini hukmu ya aliyetenda Jimai (kitendo cha ndoa) na mke wake mchana wa Ramadhaan?

JIBU:

Ikiwa wote walikuwa wako katika udhuru wa kutokufunga mfano, kama walikuwa safarini, hakuna ubaya hivi hata kama wote walikuwa wamefunga. Lakini ikiwa walikuwa katika hali ya kuwapasa kufunga, basi ni HARAAM kwao wote na wanatakiwa walipe siku hiyo, na juu yake (wafanye 'kafara’) nayo ni kuachia huru mtumwa, na kama hawawezi basi wafunge miezi miwili mfululizo (bila ya kukatiza), na ikiwa hawawezi kufanya hivi basi walishe masikini 60 au watu wanaohitaji. 

Kufanya hivyo inawapasa wote wawili kila mmoja afanye sehemu yake. Lakini kama mke alilazimishwa kufanya kitendo hicho basi yeye haimpasi kulipa 'kafara'.

 

Shaykh Ibn 'Uthaymiyn
Fataawa Ramadhaan – Mjalada 2, Ukurasa 606, Fatwa Namba 597
Fataawa Shaykh Ibn 'Uthaymiyn –Mjalada 1, Ukurasa  541-542


 **********************************************************************************

Hakulipa Siku Zake Za Swawm Za Ramadhaan Alipokuwa Katika Hedhi Miaka Yote Iliyopita


SWALI: 
Bibi mtu mzima mwenye umri wa miaka 60 alikuwa hajui hukumu ya kulipa Swawm alizokuwa hafungi wakati alipokuwa katika hedhi miaka mingi.  Miaka yote iliyompita hakulipa siku zake za Swawm za Ramadhaan akifikiri kwamba kulikuwa hakuna haja ya kuzilipa.  Hivi ni kutokana na alivyosikia kutoka kwa watu.
JIBU:
Inampasa aombe maghfirah na tawbah kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى  kwa kutokuuliza (Waislamu) wenye elimu.  Kisha alipe siku zote alizokuwa hakufunga na alipe kafara kwa kulisha maskini mmoja kibaba kimoja cha shayiri au tende au mchele au chakula chochote kinachotumika (sana) katika nchi anayoishi. Hivyo ni kama anao uwezo, na ikiwa hana uwezo wa kulisha maskini basi inamtosha kulipa tu siku alizokuwa hakufunga.
Na kwa Allaah سبحانه وتعالى  ndio yako mafanikio yote na Rahma na Amani zimfikie Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na Swahaba zake.
 
Halmashauri ya kudumu ya Utafiti Wa Kiislaam Imejumuisha:
Kiongozi Mkuu: Shaykh 'Abdul 'Aziyz ibn 'Abdullaah  ibn Baaz
Msaidizi Kiongozi Mkuu: Shaykh ‘Abdullaah ibn Ghudayyaan
Mwanachama: Shaykh 'Abdullaah Ibn Ghudayyan
Mwanachama: Shaykh ‘Abdullah ibn ‘Awd
Fataawa Ramadhaan - Mjalada 2, Ukurasa  583, Fatwa Namba 567;
Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah lil-Buhuuth al-'Ilmiyyah wal-Iftaa. - Fatwa Namba 1790

 *****************************************************************************

Je, Mke Anatakiwa Kulipa Kafara Ikiwa Alifanya Jimai (Kitendo Cha Ndoa) Na Mumewe mchana wa Ramadhaan?



SWALI:

Mtu alifanya jimai (kitendo cha ndoa) na mkewe katika siku ya Ramadhaan na kwa hivyo akafunga kafara ya miezi miwili mfululizo. Sasa mkewe anatakiwa kufanya lolote?  Allaah Akulipeni.

JIBU: 

Kwa jina la Allaah, na Sifa zote anastahiki Allaah سبحانه وتعالى Pekee. Yale yale yanayompasa yeye mke ni sawa na yanayompasa mumewe ikiwa alifanya kitendo hicho kwa pendekezo lake mwenyewe na hakulazimishwa. Na ikiwa ni shida kwake kufunga miezi miwili mfululizo, basi alishe masikini 60 au wanaohitaji, kila mmoja amlishe kibaba kimoja. Lakini kama alilazimishwa na kupigwa basi hatakiwi kulipa lolote na dhambi zitakuwa ni za mume pekee. Lakini kama alifanya kwa mapendekezo basi anatakiwa afanye kafara sawa sawa na mumewe.

 

Shaykh Ibn Baaz
Fataawa Ramadhaan – Mjalada  2, Ukurasa 610, Fatwa Namba 605
Majmu'u Fataawa libni Baaz - Mjalada 3, Ukurasa 200



 *****************************************************************************

Hukmu Ya Aliyeacha Kufunga Miaka Ya Nyuma




SWALI:  

Nini hukmu ya Muislamu aliyekuwa hafungi miaka ya nyuma ingawa alikuwa akitimiza Fardhi nyingine, na kutokufunga huko kulikuwa bila ya kizuizi au sababu yoyote? Je, Inampasa alipe funga hizo hata baada ya kutubu?

JIBU:

Iliyokuwa sahihi ni kwamba haimpasi kulipa funga za nyuma zilizompita alizokuwa hazifungi baada ya kutubu. Hii ni kwa sababu  vitendo vyote vya 'ibada kwa Waumini vimewekwa    katika muda wake mahsusi uliotajwa.  Kwa hiyo ikiwa mtu atawacha kufanya 'ibada hiyo au kuichelewesha na muda upite bila ya sababu yoyote, Allaah سبحانه وتعالى  Hatapokea kitendo hicho, na kutokana na hayo, hakuna maana kulipa yaliyompita.  Lakini, inampasa atubu kikweli  kwa Allaah سبحانه وتعالى  na azidishe sana vitendo vyema (kama Sunnah za Swalah, Swawm) na yule mwenye kuomba msamaha kwa Allaah سبحانه وتعالى, basi Allaah  Atamsamehe.

Shaykh Ibn 'Uthaymiyn
Fataawa Ramadhaan - Mjalada 2, Ukurasa 556, Fatwa Namba 539;
Fataawa  Shaykh Muhammad Swaalih Al-'Uthaymiyn – Mjalada  1, Ukurasa  536

 

*****************************************

Kutoa Damu Hakubatilishi Swawm

SWALI:

Assalamu  'allykum,
Je, kutoa damu kidogo yakufanya check up wakati umefunga inafaa? JAZAKA ALLAHU KHEIR 





JIBU:
AlhamduliLlaah,  Waswalaatu Was-Salaam 'alaa Rasuli-Llaah, Amma ba'ad,
Kutoa damu ya kufanya matibabu wakati umefunga haibatilishi Swawm.   

Yafuatayo ni mambo yanayobatilisha na yasiyobatilisha Swawm:

YANAYOBATILISHA (YANAYOHARIBU) SWAWM
1.     Kula na kunywa kwa makusudi. Na sio kwa kusahau wala kwa bahati mbaya au kwa kulazimishwa, katika mchana wa Swawm.
2.     Kujitapisha kwa makusudi. Kuwe kujitapisha huko kwa kutia kidole mdomoni au kunusa kitu kitachopelekea kutapika.
3.      Mume kumuingilia Mke wake. Na pia kumkumbatia au kumchezea hadi yakamtoka manii.
4.     Kujichua (kuyatoa manii) kwa makusudi ima kwa mkono au kwa kuchezewa na Mkeo au kwa njia yoyote ile. Ama manii hayo yakitoka kwa kuota (ndoto) au kutazama (bila kukusudia) basi haiharibu Swaumu.
5.     Kupatwa na Hedhi au Nifasi kwa Mwanamke. Hata kukiwa kutokea huko kuwa ni wakati wa kukaribia kufuturu.
6.     Mwenye kutia Nia ya kula wakati amefunga, kwa sharti kuwa kaazimia tendo hata hakulitekeleza.kamahilo
7.     Kudhania kuwa jua lishazama magharibi au bado hakujapambazuka (yaani haujaanza wakati wa kufunga), kisha akala ,akanywa au akamuingilia mke wake.

   YASIYOBATILISHA (YASIYOHARIBU) SWAWM
1.     Kula au kunywa kwa kusahau, kimakosa au kulazimishwa.
2.     Kuingia maji ndani ya matundu ya mwili bila kukusudia, kwa mfano wakati wa kuoga.
3.     Kudungwa sindano mwilini wakati wa maradhi.
4.     Dawa ya maji idondoshewayo machoni.
5.     Kuoga na kujimwagia maji mwilini wakati wa joto kali.
6.     Kuonja chakula kwa mpishi kwa sharti asimeze kile akionjacho.
7.     Kumbusu au kumkumbatia mkeo, kwa sharti awe mtu ana uwezo wa kujizuia na kudhibiti matamanio yake.
8      Kupiga chuku (cupping), ikiwa kupika chuku huko hakutomfanya huyo mtu adhoofike. Ingawa kuna baadhi ya Maulamaa wanaona kuwa haifai na hali kadhalika kutoa damu.
9     Haitobatilika swawm ya mtu atakayeamka na janaba au atakayeota mchana wa swawm akatokwa na manii.
10     Kuingia harufu ya manukato au udi puani mwake. Ingawa baadhi ya Maulamaa wanasema ni vizuri kujiepusha moshi usiingie hadi kufika tumboni.
11     Kupiga mswaki, kusukutua au kusafisha pua kwa kutia maji puani bila kuzidisha.

Na Allaah Anajua zaidi


 

********************************

Je, Inafaa Kusogea Kumpisha Mtu Katika Swalah?

SWALI:
Haifai wakati wa kusali kumpisha mtu badala yako kama mfano ni mtu mzima?


JIBU:

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shaykh ibn 'Uthaymiyn يرحمه الله   amesema kwamba msingi wa sheria katika mas-ala ya kusogea (kufanya harakaat) katika Swalah ni makruuh (jambo la kuchukiza) isipokuwa imefanyika kwa sababu na akagawanya hizo sababu katika aina tano:
  1. Harakaat (mishughuliko) iliyowajibika
  2. Harakaat zilizoharamishwa
  3. Harakaat za mustahabbah (zinazopendekezeka)
  4. Harakaat zinazoruhusiwa
  5. Harakaat zilizokuwa ni makruuh (kuchukiza)

Harakaat zilizizowajibika
Ni zile ambazo zinategemea kuswihi kwa Swalah yenyewe. Kwa mfano mtu akiona najsi katika kofia yake, aivue kofia. Hii ni kwa sababu Jibriyl عليه السلام alikuja kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipokuwa akiswalisha watu, na akamwambia kuwa kuna uchafu katika kiatu chake. Hivyo Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akakivua na huku anaswali na akaendelea kuswali. [Imesimuliwa na  Abuu Daawuud na ikiwa ni sahihi kutoka kwa Shaykh Albaaniy katika Al-Irwaa]
Vile vile ikiwa mtu ameambiwa kuwa hakuelekea Qiblah basi ageuke na kuelekea Qiblah.
Harakaat zilizoharamishwa
Hizi ni zile ambazo ni kila mara zinazofanyika bila ya sababu, kwa sababu aina ya harakaat hizi zinabatilisha Swalah, na chochote kinachobatilisha Swalah hakifai kutendeka kwani ni kama kufanya mzaha na alama za Mwenyezi Mungu.
Harakaat zinazopendekezeka (Mustahabbah)
Hizi ni zile zinazotendeea kwa ajili ya kufanya vinavyopendekezeka katika Swalah, mfano kama mtu kusogea kuunga swaff (mstari) au anapoona mtu kuna uwazi katika mstari wa mbele, atasogea kujaza uwazi huo kwani hivyo ni kuifanya Swalah iwe bora zaidi na imekamilika. Ibn 'Abbaas رضي الله عنه aliposwali na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alisimama kushoto kwake, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimvuta kwa kumshika kichwa chake kwa nyuma na akamfanya asogee kusimama kulia kwake. [Al-Bukhaariy na Muslim]
Harakaat zilizoruhusiwa
Ni zile ndogo ndogo zinazotokana na sababu fulani au harakaat kubwa penye kuhitajika. Harakaat ndogo kama mfano Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipokuwa akiswali na huku amembeba Umaamah, mjukuu wake  kutoka kwa mwanawe Zaynab. Alipokuwa akisimama alikuwa akimbeba na alipokuwa akienda kusujudu alikuwa akimuweka chini. [Al-Bukhaariy na Muslim] 

Harakaat zinazochukiza (Makruuh
Hizi ni zote nyinginezo ambazo zisizokuwa aina ya hizo zilizotajwa juu. Na hii ni sheria ya msingi kuhusu harakati (kusogea) kwenye Swalah.

Hivyo tunaweza kusema kuwa kumpisha mtu mzima itakuwa ni katika harakaat za mustahabbah (zenye kupendekezeka) kwa hiyo inafaa kufanya hivyo. 
Jambo la kuzingatia ni kuhusu idadi ya harakaat hizo:
Amesema Shaykh ibn 'Uthaymiyn kuwa "Zikiwa ni harakaat nyingi itakuwa ni kama mtu asiyeswali. Kwa hiyo harakaat hizo zitabatilisha Swalah. Na ndio maana wataalamu wameeleza maana yake kuwa ni kutokana na al'urf (mazoea) na wakasema: "Ikiwa harakaat zitakuwa ni nyingi na za kuendelea basi Swalah itabatilika", bila ya kutaja idadi ya harakaat. Baadhi ya Maulamaa wametaja idadi ya harakaat kuwa ni tatu, lakini hii inahitaji dalili kwa sababu kuweka idadi yoyote lazima iweko dalili au sivyo itakuwa ni kuzua fikra mpya". [Majmuu' Fataawa al-Shaykh, 13/309-311]

Dalili kuwa harakaat ndogo ndogo au za kuendelea kuwa haziharibu Swalah ni ripoti kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimfungulia Bibi 'Aishah رضي الله عنها mlango uliofungwa kwa kusogea inavyosemekana kuwa ni zaidi ya harakat tatu. [Abu Daawuud, An-Nasaaiy, At-Tirmidhiy, Ahmad ikiwa ni Sahiyh kutoka kwa Sh Albaaniy]
Vile vile ripoti tuliyotaja juu alipombeba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  mjukuu wake wakati wa kuswali na kumuweka chini alipokuwa akisujudu.
Na Allah Anajua zaidi.
  *************************************************************

Ndugu muislamu na ndugu yetu msomaji wa blog hii.

Ukiwa na maswali tafadhali tuulize kwa anuani zifuatazo;-

muniiramadrasa@yahoo.com

au

jumarashidmusa@yahoo.com

Tutayapeleka maswali yako kwa masheikh

wenye utaalam kwa fani munasaba na swali lako,kisha swali na majibu yako tutayaingiza katika blog hii kwa faida ya wasomaji wote.

Tafadhali tunaomba ushirikiano wako mwema kwa kutaraji Radhi za ALLAH S.W

**************************************************************

SWALI NO 06:

ANATAKA KUZINI KABLA YA RAMADHAAN. (VUNJA JUNGU) JE SWAUM YAKE ITAKUBALIWA?

SWALI:
Assalam alaykum,
swali: siko katika ndoa, na ninafahamu kuwa sitakiwi kuzini.Je, ni kweli kwamba nikiingiliana na mwanamume mfano siku tatu kabla ya Ramadhan,funga yangu hata pokelewa mpaka siku thelathini zipite?


JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukurani kwa swali lako hili la mtu kuzini kabla ya Ramadhaan.
Ni makosa, makubwa, bali ni dhambi Muislamu kuukaribisha mwezi wa Ramadhaan kwa maasi badala ya vitendo vyema. Tunaona kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuwekea mwezi mtukufu wa Rajab, kisha mwezi wa Sha'abaan ambayo yote ni faida kwetu kujitayarisha na vitendo vyema kuupokea mwezi wa Ramadhaan. Lakini ni jambo la kusitikisha sana kuona kwamba ndugu zetu wengine hufanya kinyume chake; wengine kuukaribisha kwa kama inavyojulikana 'vunja jungu', na humo wengine ima huingia katika mambo ya munkaraat kama michanganyiko wa wanawake na wanaume kwenda mandarini (picnics), wengine kufanya maparty ya muziki na wengine hufika hadi kutenda maasi ya kulewa au kuzini kama ilivyo hali ya muulizaji.
Ikiwa jambo hili limekwishatokea, hivyo linaulizwa tu kuhusu funga ya mtu huyo, naye akarudi kutubu kwa Mola wake, basi funga hiyo itakuwa sahihi na Allaah ni Mwingi wa Msamaha. Lakini ikiwa jambo hilo umelitilia nia, tunakupa nasaha za dhati ujiepushe nalo haraka kwa kubadilisha nia yako na badala yake uukaribishe mwezi wa Ramadhaan kwa vitendo vyema, kwa sababu, binaadamu hatuna uhakika kama tutaishi hadi kufika Ramadhaan, au mwezi kabla yake, au wiki, au siku au hata saa moja. Je, umewaza ndugu kuwa huenda mauti yakakuta wakati uko katika maasi hayo? Je, hutambui kwamba mja hufufuliwa akiwa katika hali aliyoondokea? Je, hufikiri kwamba huenda mauti yakakufika na huku umetia nia hiyo? 
Tunakupa nasaha ujiepushe kabisa na jambo hilo na mche Mola wako. Bbadilisha nia yako hiyo na  weka nia ya kutenda vitendo vyema vya kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhaan.

 SWALI NO 05;

Ndoa Ya Siri Inafaa?


SWALI:
Asalam aleikum, Mimi ni mwanamke wakiisilamu ambae nimeolewa wasunatillah warasuloh (SAW) lakini ni ndoa ya siri.
Swali. Jee ndoa hii yaswihi au haiswihi kulingana na sharia za kiisilamu ingawa ndoa yetu ilifungwa msikitini mbele ya imam na mashahidi wawili na watoto wangu? Shukran wa jazakumullah kheir, 



JIBU:
 Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum)   na walio wafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran dada yetu kwa swali lako hilo zuri. Kwa hakika kama tulivyojibu mara nyingi kuhusu masuala ya ndoa ni kuwa ndoa katika Uislamu ina nidhamu yake na masharti yake ambayo yakipatikana basi ndoa hiyo inakuwa ni halali. Miongoni mwa masharti ni:
     1.      Kupatikana walii wa binti.
2.      Kusiwepo na vizuizi kwa wenye kuoana vya kuwazuia kuuoana, kama undugu wa damu n.k. 
     3.      Kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu.
     4.      Kuwepo na Iyjaab na Qubuul, yaani walii kusema, nimekuozesha bint yangu...., na kujibu mume (muoaji), nimekubali kumuoa .....

Ikiwa ndoa ilifungwa Msikitini na kukawa na mashahidi wakiwemo watoto wako huwa si siri tena hiyo na ndoa hiyo imeswihi na ni ya sawa sawa. Kwa hakika ikiwa ni siri kabisa ambapo hakuna mashahidi wala walii ndoa hiyo kisheria haitakuwa ni yenye kusihi.
Na Allah Anajua zaidi.
*******************************************************************

 SWALI NO 04:

MGONJWA WA PUMU ANATUMIA DAWA YA KUPULIZA MDOMONI JE, INABATILISHA SWAUM?

 SWALI:
Mimi ni mgonjwa wa Pumu, na kila mara  au kila siku zinanijia, na zinaponijia inanibidi nitumie dawa ili nipate nafuu, dawa ninayotumia sio ya vidonge wala sindano natumia dawa ya kupuliza mdomoni ile hewa inayotoka ndio nikimeza natapa nafuu. swali langu lipo hapa je? nikitumia dawa hiyo nitakuwa sina swaum.


JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Swaum yako ni sahihi In shaa Allaah, kwani hiyo dawa ya kupuliza inaingia katika mapafu na sio chakula kinachoingia tumboni, kwa hiyo kuitumia sio miongoni mwa vitu vinavyobatilisha Swaum.Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo ya mambo yanayobatiilisha na yasiyobatilisha Swaum.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

*********************************************************
SWALI NO 03;KUVAA VIDANI:

Assalaam alaykum,

Natumai hali zenu nyote ni nzuri, nimefurahi sana waislam kupata blog hii inayotupa mafunzo mbalimbali ya dini yetu. Swali langu ni kwenu mashekh ni kuhusu vidani vya madini ya silver ambavyo vijana wengi wa kiislam wanavivaa, je ni halali kuvaliwa? Na ikiwa ni halali je,tunaruhusiwa kuswali navyo? Au kuna uzito Fulani (grams) ambao ina kuwa ni ruhusa?




JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Rehma na salamu zimfikie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliotangulia katika wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunakushukuru ndugu yetu kwa kuuliza swali muhimu hasa kwa zama hizi.
Swali lako ni kuhusu kuvaa vidani wanaume.
Vidani aina yoyote ile kama ni dhahabu, fedha, shaba na kadhalika havifai kwa mwanamme kwani hayo ni mapambo kwa wanawake. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza pamoja na kuwalaani wanaume wote wanaojifananisha na wanawake na kinyume chake. Mbali na hivyo uvaaji wa vidani ni ‘amali ya makafiri ambao pia sheria imetutaka tuwe tofauti nao.

Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake na wanawake wanaojifananisha na wanaume” (al-Bukhaariy, Abu Dawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

Hivyo, ni vyema kabisa kwa Muislamu mwanamme aachane na kuvaa vidani. Kwa hiyo, haifai kuvivaa katika Swalah au wakati mwingine wowote.

Na Allaah Anajua zaidi


*************************************************************

 Swali no 02;Nini Hukumu Ya Kujichua Sehemu Za Siri Au Kujisaga?

SWALI  LA KWANZA:
NAULIZA KWAMBA...DINI INASEMAJE KUHUSU KUPIGA PUNYETO KWA KIJANA AMBAYE BADO HAJAOA;NA HANAUWEZO  WA KUOA.
SWALI LA PILI:
as kum,  naomba kuuliza juu ya baadhi ya vijana wa kike na wa kiume,wanapofikia umri fulani au baada ya kubaleghe hujiwa na matamanio ya kujamii(sexual desires) hivyo wengine huamua kutoa manii kwa kutumia mikono yao na kwa wanawake huamua kujitia kitu chochote kinachoweza kuleta hisia na kupunguza matamanio yao.
 swali ni kwamba,je hadithi na quran inalizungumziaje swali hili.  natumai majibu mazuri.
SWALI LA TATU:
Assalam aleikum!                                  
 swali ni kuwa kujitoa
manii(nyeto) ni haramu au ni makuruu?kwani kwa fikra zangu naona ni vizuri kwani unapunguza matatamanio kwa wanawake na hasa kufanya tendo la zinaa kabla ya ndoa.






JIBU:
BismiLLaah wa AlhamduliLLaah wasw-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  ‘Aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba’ad
Hili ni swali muhimu kwa kuwa linagusa tatizo sugu linalowakabili vijana wengi wa Kiislam, ambao bado hawajaoa, na wanaokabiliana kwa hali ya juu kabisa na vishawishi vilivyowazunguka katika jamii mbalimbali wanazoishi ndani yake. Kujichua wanaume au kujisaga wanawake ni jambo linalokubalika na kufanyika sana katika jamii zisizo za Kiislam kwa idadi kubwa ya watu: vijana wa kiume na kike, makapera, wazee na hata waliooa/kuolewa.

Lakini hali hiyo katika Uislam ni kinyume. Kwani katika Uislam kujichua au kujisaga (punyeto) ni haraam kwa mwanamme na mwanamke, kwa dalili zifuatazo:
Kwanza, dalili kutoka katika Qur’aan:
((وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ))

 ((إِلَّا عَلَى أَزْوَاجِهِمْ أوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ))

 (( فَمَنِ ابْتَغَى وَرَاء ذَلِكَ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ))

((Na ambao wanazilinda tupu zao))
((Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa))
((Lakini anayetaka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka)) [Al-Muuminuun:5-7]
Aayah hii inakataza waziwazi vitendo vyote vya tendo la ndoa (ikijumuisha punyeto) isipokuwa kwa wake, na yeyote anayejipelekea kwenye matendo kinyume na hayo yaliyoruhusiwa, basi ni katika warukao mipaka.
وَلْيَسْتَعْفِفِ الَّذِينَ لَا يَجِدُونَ نِكَاحًا حَتَّى يُغْنِيَهُمْ اللَّهُ مِن فَضْلِهِ  
((Na wajizuilie na machafu wale wasiopata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu Awatajirishe kwa fadhila Yake)) [An-Nuur:33]
Ayah hii vilevile inaamrisha wazi kwa yule asiye na uwezo wa kimali kwa ajili ya kuoa, basi anatakiwa ajiweke katika hali ya kujidhibiti  na machafu na kujihifadhi kimwili na awe na subira ya kuweza kukabiliana na vishawishi mbalimbali ikiwemo kupiga punyeto, hadi Mwenyeezi Mungu Atakapomruzuku kwa fadhila Zake.

Vilevile Wanachoni wa Fiqh (Fuqahaa) wamechukulia hukumu kutoka katika ayah hii kuwa ni haraam kupiga punyeto kwa sababu mbili: Ya kwanza: Katika ayah hii, Allaah سبحانه وتعالى  Anaamrisha kujizuia na machafu, na kutokana na kanuni za ki-Fiqh, maamrisho  yanaashiria ulazima (uwajibu) wa jambo. Hivyo kubaki katika hali ya usafi (kujizuia na machafu) ni wajibu na panapokuwa kujizuia na machafu ni wajibu, basi kujizuia na yale yote yanayopelekea kufanya machafu ni wajibu zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba kujizuia na machafu au kubaki safi kutapatikana pale mtu anapojizuia na vile vyenye kusababisha hayo machafu.

Sababu ya pili, kwamba katika ayah hiyo Allaah سبحانه وتعالى    Ameamrisha Usafi (kutofanya machafu) kwa wale wasio na uwezo wa kuoa. Hapa Allaah سبحانه وتعالى Hajadhihirisha uhusiano wa kujizua na machafu na ule wa kuoa. Hivyo kunahesabika kuwa kujichua ni haraam. Na kama kungekuwa ni halaal, basi hapa ndipo pahala pake palipokuwa panatakikana kutajwa. Kwa kutotajwa uhalali wa kujichua katika ayah hii ambapo ndipo pahali muwafaka wa kuelezwa hilo, kunadhihirisha kuwa jambo hilo ni haraam, Kwani ‘kunyamazwa katika sehemu ya kuelezwa kunaashiria makatazo.’ Tazama pia tafsiri ya Imaam Qurtubiy katika ayah hiyo.

Pili, dalili kutoka katika Sunnah:
Anasema ‘Abdullaah ibn Mas’uud رضي الله عنه, “Tulikuwa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na hali bado ni vijana na hatuna uwezo wa mali. Basi Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  akatuambia: ((Enyi vijana! Mwenye kuweza kuoa na aoe, kwani kuoa kunamsaidia yeye kuinamisha macho yake (kutotazama ya haraam) na kuhifadhi tupu yake (kutofanya zinaa na uchafu mwingine), na yule asiye na uwezo wa kuoa, afunge, maana funga hupunguza matamanio ya kimwili)) Al Bukhaariy
Hadiyth hii inamuamrisha mtu asiye na uwezo wa kuoa, afunge, japokuwa kuna ugumu wa kufanya hivyo kila wakati anapozidiwa na matamanio, ili asitumbukie katika vitumbukizo vikiwemo punyeto, pamoja na urahisi na mvuto wa kulifanya jambo hilo. Na kama kungekuwa ni halali kupiga punyeto, basi hapa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  angeliruhusu kwa sababu ni jambo rahisi na lenye kustarehesha na asingesema watu wafunge kwani hilo ni jambo gumu na zito kulifanya. Na kama tunavyofahamu, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakuletwa kutufanyia ugumu na uzito.

Wema waliopita kama Sa’iyd ibn Jubayr رضي الله عنه anasema kuhusiana na punyeto, “Mwenyeezi Mungu Atawaadhibu watu kwa sababu walikuwa wakichezea sehemu zao za siri.” Naye ‘Atwaa  رحمه الله  anasema, “Baadhi ya watu watafufuliwa na hali mikono yao ina mimba, Nadhani ni wale waliokuwa wakipiga punyeto.”

Ingawa baadhi ya Maimam wanalijuzisha jambo hilo kwa sababu mbalimbali, kama; ikiwa mtu anaogopa kutumbukia katika zinaa, au kufanya huko ni kwa sababu tu ya kutoa matamanio yaliyozidi na wala si kwa ajili ya kujistarehesha n.k.. Hata hivyo, rai hizo hazina dalili yoyote zilizoambatana nazo, kwa hivyo ni bora mtu kujiepusha na tendo hilo kutokana na dalili zilizotangulia kutajwa.

Tunawanasihi ndugu zetu wenye kukabiliwa na vishawishi hivyo, wafuate nukta hizi ili ziwasaidie kupambana na hali hiyo inayowasumbua wale walio katika hali ya ukapera (kutokua na mke/mume):
1-    Jambo la mwanzo na muhimu kuliko yote ili kuepukana na mtihani huu wa kutumbukia katika tabia hiyo, ni kujitahidi kufuata maamrisho ya Allaah سبحانه وتعالى na kuogopa  adhabu Zake.

2-      Kuwa safi na machafu (Kujizuia na machafu), kwa kujiweka daima katika hali ya kufikiria adhabu ya moto, na kuamini kuwa kujihifadhi huko kwa kufanya machafu ni sababu ya kuipata pepo.

4-    Kuinamisha macho yako (kutotazama yale ya haraam kama picha za uchi, sinema, au kukaa majiani na kutazama maumbo ya wanawake wapitao). Kujizuia huko kutazama ya haraam, kutakusaidia sana kutoamsha hamu zilizorundikana ambazo zikishaamka, basi kufanyika haraam kunakuwa ni jambo lisiloepukika kirahisi. Mwenyezi Mungu سبحانه وتعالى Ameamrisha wanaume na wanawake katika ayah mbili zifuatazo:
((قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ذَلِكَ أَزْكَى لَهُمْ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ))

  ((وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ ))
((Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu Anazo khabari za wanayoyafanya))
((Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao….)) [An-Nuur:30-31] 
Naye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  anasema: ((Usifuatilize mtazamo (kuangalia kwa kutokusudia (vile vilivyoharamishwa) kwa mtazamo mwingine))[At-Tirmidhiy]
Huu ni mwongozo kutoka kwa Mtume wetu صلى الله عليه وآله وسلم wa kujizuia na yale yote yanayoweza kuchochea matamanio ya kimwili ambayo yanaweza kumpelekea mtu kufanya yaliyokatazwa.

5-    Ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo ni kukimbilia kuoa haraka pale tu unapokuwa tayari kiuwezo, kama tulivyoona katika hadiyth ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   

6-   Kufunga. Jizoeshe kufunga kila unapohisi matamanio yanaanza kufumuka. Nako huko kufunga kunasaidia sana kwa mengi zaidi ya hilo. Jizoeshe kufunga kila Jumatatu na Alkhamiys, masiku meupe (tarehe 13, 14 na 15 za Kiislam, kila mwezi), na ukiona matamanio yako ni mengi na ya mara kwa mara basi funga Swawm ya Nabii Dawuud عليه السلام   ya kila baada ya siku moja.
        Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  amesema:
))يَا مَعْشَرَ الشَّبَابِ مَنْ اسْتَطَاعَ الْبَاءَةَ فَلْيَتَزَوَّجْ فَإِنَّهُ أَغَضُّ لِلْبَصَرِ وَأَحْصَنُ لِلْفَرْجِ وَمَنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَعَلَيْهِ بِالصَّوْمِ فَإِنَّهُ لَهُ وِجَاءٌ((  البخاري ومسلم
((Enyi vijana, anayeweza kuoa basi na aoe kwani ni kuinamisha macho na ni stara ya uchi, Na asiyeweza basi afunge (Swawm) kwani ni kinga (ya matamanio).[Al-Bukhaariy na Muslim]

7.    Kuutumia muda wako usio na la kufanya, kwa kufanya ibada zaidi na kujisomea na kutafuta elimu ya dini; kwa kusikiliza mawaidha au kutazama.

8.    Kujiepusha na kutumia baadhi ya vyakula, vinywaji n.k. ambavyo vinachochea hamu na kusababisha mshawasha na muibuko wa matamanio.

9.    Daima fikiria madhara yanayoweza kusababishwa na tendo hilo; kama ya kudhoofisha nguvu za macho, nguvu za mishipa, nguvu za uume (kwa mwanamme) au uti wa mgongo. Na muhimu zaidi, ni kule kuwa na hisia za dhambi na usumbufu utakaopatikana baada ya kufanya kitendo hicho kama vile, kuweza kupoteza Swalah ya faradhi kwa kukubidi kuchukua muda wa kwenda kuoga kila baada ya tendo hilo.

10.   Fanya Tawbah, muombe Allaah سبحانه وتعالى  msamaha kila wakati, kufanya hivyo na pia kutenda matendo mema na kutokata tamaa na Rahma za Allaah سبحانه وتعالى   kunaweka karibu zaidi na Allaah سبحانه وتعالى na kukufanya kumuogopa zaidi na kufikiria kila tendo unalotaka kulifanya kwanza.

11.   Jua kuwa Allaah سبحانه وتعالى ni Mwingi wa Kusamehe na daima Humkubalia du’aa za yule anayemtaka msaada. Hivyo basi, kumuomba Allaah سبحانه وتعالى msamaha ni jambo lenye kupokelewa Naye, na hilo linatupa nguvu kumuomba Yeye daima na kutaraji msamaha Wake.

12.  Kujishughulisha na mambo ya muhimu na ya faida; yakiwa ni ya akhera au ya kilimwengu ili usipate nafasi ya kuwa na faragha na ukaanza kufikiria kufanya tendo hilo ambalo hakika ni ada iliyo ngumu kuepukika.

13.   Fanya mazoezi mbalimbali ya kukuchosha, mwili ukishachoka matamanio yanazama.

14.  Usile sana, au kula kila wakati. Kwani unaposhiba mambo mengine yanachemka na kutaka haki zake.

Hayo ndio machache katika mengi ambayo yanaweza kumsaidia mtu kujiweka mbali na tendo hilo linalowasumbua wengi haswa vijana na wajane.

Wa Allaahu A’alam
 

***************************************

JE,NI MUDA GANI WA KUTWAHARIKA NA DAMU YA NIFASI?

 
SWALI
Mie nilikuwa naomba kutolewa katika utata huu,kuna watu wanaosema mtu akijifungua basi mwisho siku 60 kama bado hajasafika na akoge na kuswali,kwani hiyo itakuwa sio damu ya nifasi tena.
Na kuna mwengine ameniambia kuwa hapana ni siku 10 tu ukisafika usisafike wewe ukoge na uanze kuswali kwani ndio walivyofanya wake na watoto wa mtume (s.a.w).
hapa shekhe nilikuwa naomba kuwekewa sawa ipi kweli na ushahidi wake.kwani imekuwa tunachangwa akili sie tuliokuwa hatuna elimu ya kutosha.
JazakaAllaahul kheir.



 JIBU:
AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

Shukrani ndugu yetu kwa swali lako hilo kuhusu damu ya nifasi. Hakika ni kuwa nifasi ni damu inayotoka katika tupu ya mbele ya mwanamke baada ya kuzaa, wala hapana mpaka wa uchache wake, kwani wakati wowote atakapoona mwenye nifasi twahara, ataoga na ataswali na hata kuingiliwa na mume wake.

Kwa hiyo, muda wako mfupi inawezekana baada ya masaa ya kuzaa kwake ikiwa damu hiyo itakatika. Ama muda wake mrefu ni siku 40 kulingana na Jamhuri ya wanazuoni ingawa kuna waliosema siku 60. Amesema at-Tirmidhiy: “Wamekubaliana wanazuoni kuanzia kwa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Tabiina na waliokuja baada yao kuwa mwenye nifasi anaacha Swalah kwa siku 40 ila akitwahirika kabla ya hapo. Ikiwa ni hivyo atajitwahirisha na kuswali (Sunan at-Tirmidhiy). Mj. 1, uk. 258). 

Pia ipo Hadiyth iliyopokewa kuwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) alisema: “Alikuwa mwanamke mwenye nifasi anakaa siku arobaini”. 

Na amesema nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) muda gani anakaa mwanamke pindi akizaa? Akasema: “Siku arobaini ila atakapoona twahara kabla ya hapo” (at-Tirmidhiy, na ameisahihisha al-Haakim). 

Ikiwa damu yenyewe itapita siku 40 basi hiyo itakuwa ni damu ya ugonjwa inafaa mwenye kuona hivyo baada ya muda huo aoge na ni lazima kwake kufunga na kuswali.

Na Allaah Anajua zaidi

 

JE,NDANI YA SWALA INAFAA KUOMBA DUA KWA LUGHA YOYOTE ?


SWALI:
Je inafaa kuomba dua katika SIJDA kwa lugha yeyote kwenye Swalah ya SUNNAH?





JIBU 

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa swali lako zuri kuhusu mas-ala ya 'Ibadah na hasa ile ya Swalah ambayo ni nguzo muhimu na ya pili baada ya Shahada. Mtume Muhammad (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: "Swalini kama mulivyoniona mimi nikiswali" (Al-Bukhaariy). Hivyo, 'Ibadah zote ni tawqiifiyyah, yaani kufuata kama alivyofanya Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au kutuelekeza.
Rai yenye nguvu ni kuwa Swalah za fardh haifai kusoma Du'aa ndani ya Swalah kwa lugha isiyo ya Kiarabu! Ama Swalah za Sunnah, wametofautiana Wanachuoni; wengine wanasema inatakikana kusomwa kwa Kiarabu vilevile na baadhi wamesema kuwa inawezwa kusomwa kwa Du'aa ndani ya Swalah kwa lugha isiyo ya Kiarabu kwa asiyeweza kabisa kusoma kwa Kiarabu au asiyejua. Hata hivyo asijiache mtu  kutokufanya bidii ya kujifunza Du'aa hizo kwa Kiarabu na akawa tu ametosheka kwa lugha yak kwani ni imemwajibikia kila Muislamu kujifunza lugha ya Kiarabu kwa kuwa ni lugha Aliyoichagua Allaah Subhaanahu wa Ta'ala kuwa ni lugha ya Qur-aan.

Na Allah Anajua zaidi