Dec 11, 2013

Wanawake wawatwanga waume zao. Polisi yasema wanajisikia aibu kuripoti

HUKU mataifa duniani yakiendelea na siku 16 za kupinga udhalilishaji wa kijinsia, mambo yamegeuka Zanzibar ambapo wanawake wanadaiwa kuwanyanyasa wanaume.
Kwa ilivyozoeleka wanawake ndio waathirika wakubwa wanaokabiliwa na vitendo vya udhalilishaji, lakini hapa Zanzibar kibao kimewageukia wanaume ambao kwa mujibu wa jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi zipo kesi kadhaa zilizoripotiwa.
Akizungumza Ofisini kwake Muembemadema, Mkuu wa Dawati hilo Staff Sagenti Zahor Faki, alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya wanawake wenye tabia ya kuwanyanyasa waume zao ikiwemo kuwapa vipigo.
Alisema dawati lake limepokea kesi tisa za wanawake kuwadhalilisha wanaume na kwamba kesi hizo zimeripotiwa kuanzia mwezi Januari mwaka huu hadi Oktoba.
Alisema wanawake wengi wenye kufanya vitendo vya udhalilishaji hasa vya kuwapiga waume zao, hufanya kwa kuvizia hasa wakiwa wanaume hao wamelala.
Mkuu huyo alisema sababu kubwa zinazopelekea waume hao kupigwa na wake zao zinatokana na wanawake wengi kuwa na wivu wa kupindukia katika ndoa zao pamoja na migogoro ya kugombani mali.
Aidha akizitaja sababu nyengine alisema zinatokana na watoto wakati wazazi wao wanapoachana huku mwanamke akizuia hati ya nyumba ambayo si haki yake bila kukaa kulitatua tatizo hilo.
"Sababu hii inatokana na mume alieachana na mke wakati wakiwa wameshazaa mwanamke huanza vurugu na kuzuia hati ya nyumba wakati si haki yake na husema hatoi mpaka apewe kitu fulani bila ya kukaa pamoja na kulitatua tatizo hilo", alifafanua Mkuu huyo.
Alifahamisha kuwa wanawake wengi wamekuwa wakiwavizia waume zao wakati wakiwa usingizini na kuwajeruhi sehemu mbalimbali za miili ikiwemo sehemu ya siri huku wakiwapa maneno makali.

0 comments:

Post a Comment