Oct 12, 2013

POLISI Wadaiwa Kutoa Siri



WANANCHI  wa kijiji cha Murugwanza, wilayani Ngara,  mkoani  Kagera, wamelituhumu jeshi la polisi wilayani humo kuwa baadhi ya askari wamekuwa na tabia ya kutoa siri wanazopewa na raia kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu na kusababisha dhana ya polisi jamii kutoweka.

Wananchi  hao walitoa tuhuma hizo dhidi ya jeshi la polisi   kwenye mkutano wa  uzinduzi wa dhana ya elimu ya polisi jamii katika tarafa ya Nyamiaga  uliofanyika  katika kijiji cha Murgwanza  katika mamlaka ya mji mdogo wa Ngara.

Mkutano huo  ulioitishwa na maafisa wa jeshi la polisi kitengo cha polisi jamii kutoka ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi wilayani Ngara (OCD), ili kutoa elimu ya ulinzi shirikishi katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao.

Akizungumza kwa niaba ya  wakazi  wa kijiji hicho, Edwin Bitwale,  alisema kitendo cha baadhi ya polisi  kupewa taarifa kuhusiana na wahalifu  na ndani ya  muda mfupi  taarifa hizo husambaa mitaani, hali ambayo inakatisha tamaa wananchi na kukosa  imani kwa  jeshi hilo.

“Tuna hofu   kwamba  maisha yetu yako hatarini  kwani mhalifu  aliyetajwa anaanza kumtafuta aliyetoa taarifa hizo polisi na anaweza kuunda kikosi cha kummalizia mtoa siri,” alisema Bitwale.

Alisema  polisi hawawajibiki kulinda  na kutetea viapo wanavyoapa katika mafunzo na kusababisha taifa kuwa na askari wasio wazalendo.

Aliongeza  kuwa katika kuvujisha siri askari hao wanapewa hongo ili wawalinde wahamiaji haramu ambao wanaendelea  kuishi nchini kinyume cha sheria kwenye harakati za utekelezaji wa Operesheni  Kimbunga, awamu ya pili.

Kwa upande wake  afisa polisi jamii tarafa ya Nyamiaga  Respicius  John alisema ni kosa la jinai  kwa askari polisi kutoa siri za mteja  na kwamba kufanya hivyo  ni kuvunja  kiapo katika utumishi wake.

John  aliwataka  wananchi kutoa taarifa mara moja kwa viongozi wa ngazi za juu wa jeshi hilo ili polisi mvujisha siri aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

0 comments:

Post a Comment