Jul 2, 2014

Watoto watumikishwa katika mizozo 23 duniani:

watoto waliotumikishwa kijeshi wakichora katika kituo cha UNICEF, Jamhuri ya Afrika ya Kati 

Mwaka 2013, watoto wametumikishwa, na kuuawa, kulemazwa ama kubakwa katika mizozo 23 tofauti duniani, kwa mujibu wa ripoti ya Katibu Mkuu illiyotolewa leo kuhusu watoto na mizozo.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo mjini New York, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na Mizozo, Leila  Zerrougui, amesema kumeripotiwa visa vya utumikishwaji wa watoto katika majeshi 7 ya kitaifa na vikosi 50 vya waasi.

Kikosi kipya kilichoorodheshwa mwaka huu ni Boko Haram, ambacho kimejihusisha na kushambulia shule na hospitali, kitendo kinachopiganiwa na Umoja wa Mataifa.

Leila Zerrougui ametaja sehemu nyingine ambazo zinamtia wasiwasi zaidi, zikiwemo Sudan Kusini, Iraq, Syria, Israel/Palestina na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Hata hivyo amesema, matumaini yanakuwepo, akitaja nchi ya Chad ambayo imetekeleza mpango wa kusalimisha watoto wote waliojiunga na jeshi, na kufanikiwa kushiriki katika jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa.

Ameongeza kwamba, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya "Watoto si wanajeshi",

 Machi mwaka jana, nchi zote saba ambazo zinaajiri watoto jeshini zimeahidi kuandaa mpango wa kusalimisha watoto hawa, yaani Sudan Kusini na Sudan, Somalia, Yemen, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afghanistan na Myanmar. Tunahitaji kuona ahadi zigeuzwe kuwa vitendo, amesema, akiongeza:

"Tunasisitiza kwamba njia nzuri zaidi ya kusitisha utumikishwaji wa watoto kwenye mizozo ni kupambana ipasavyo kwa kutumia mbinu zipasazo na ukwepaji wa sheria. 

Pia, ni kuhakikisha kwamba watoto wanarejeshwa ipasavyo kwenye maisha ya kawaida, pengine, wasipokuwa na ulinzi, na kamanda aliyewaajiri asipopewa adhabu, basi utumikishwaji utaendelea."

0 comments:

Post a Comment