Jul 2, 2014

Vifo kutokana na Ebola vyaongezeka hadi 467

Muuguzi akimuhudumia mgonjwa mwenye virusi vya Ebola. 

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema kuwa kufikia Juni 30, idadi ya vifo vilivyotokana na mkurupuko wa ugonjwa wa Ebola imepanda na kufikia watu 467, huku visa vya maambukizi ya virusi hivyo hatari katika nchi tatu zilizoathiriwa za Guinea, Liberia na Sierra Leone vikiwa sasa vimetimu 759.

Idadi kubwa zaidi ya vifo hivyo imetokea nchini Guinea, ambako watu 303 wamefariki dunia, huku Liberia ikishuhudia vifo 65 na vifo 99 kutokea Sierra Leone.

Kwa mujibu wa WHO, sababu tatu kubwa zinazochangia kuongezeka maambukizi katika ukanda huo utamaduni na imani za kijadi vijijini, idadi ya watu wengi katika maeneo yaliyo nje ya miji ya Conakry na Monrovia, pamoja na shughuli za kibiashara na kijamii zinazoendelea kwenye mipaka ya nchi hizo na watu kuvuka mipaka.

WHO imesema kudhibiti mkurupuko huo kunahitaji hatua thabiti katika nchi hizo, hususan kwenye maeneo ya mipaka. 

Kama njia moja ya kuitikia tatizo hilo, WHO inaandaa mkutano wa ngazi ya juu kwa ukanda huo kuanzia Julai 2-3 mjini Accra, Ghana, ili kutathmini hali, kutambua upungufu, kuunda mpango wa kuudhibiti ugonjwa huo, pamoja na kuongeza utashi wa kisiasa na ushirikiano mipakani baina ya serikali za ukanda huo.

0 comments:

Post a Comment