Nov 30, 2013

Kuanguka Kwa Ghorofa DAR,Serikali Ilizembea-RIPOTI

Siri ya kuporomoka ghorofa Ilala hii hapa

Maporomoko ghorofa Kariakoo 
KUPOROMOKA kwa jengo la ghorofa  Mtaa wa Indira Gandhi jijini Dar es Salaam Machi 29 mwaka huu na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 36, kunadaiwa kutokana na  uzembe wa serikali.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti iliyotolewa Novemba 24 mwaka huu na taasisi isiyo ya kiserikali ya Twaweza, asilimia 87 ya watu waliohojiwa, iliitupia lawama serikali kwamba inahusika kwa kiasi kikubwa.

Asilimia  47 ya  watu waliotoa maoni yao juu ya kuanguka kwa jengo hilo, ilisema kuwa uzembe wa wakaguzi wa majengo wa serikali pia ni miongoni mwa chanzo kingine.

Pia ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 32 ya waliohojiwa walisema kuporomoka kwa jengo hilo kulisababishwa na kampuni ya ujenzi iliyokuwa ikishikilia dhamana ya ujenzi wake.

Aidha, ripoti hiyo ambayo imejikita katika mahojiano ya watu 333 katika wilaya zote tatu za Dar es Salaam, inaonyesha kuwa asilimia 18 ya maoni yaliyotolewa kuhusu sababu za kuporomoka kwa jengo hilo ni uzembe wa manispaa husika.

Mbali ya hayo, ripoti hiyo inaeleza kuwa  asilimia 57 hawafahamu chochote kama kuna fidia zilizokuwa zimelipwa kwa waathirika ama familia zao.

Ripoti hiyo ya utafiti ilikwenda mbali zaidi na kubainisha kuwa maoni juu ya suala la mgawanyo wa wajibu ni sehemu kubwa ya jukumu, ambapo asilimia 46 ilisema wahusika  hawafanyi  kazi kwa kuhakikisha kuwa sheria za ujenzi zinafuatwa badala yake imekuwa ni kinyume.

Asilima 32 ya waliohojiwa pia waliitupia lawama kampuni ya ujenzi kwa ajali mbaya wakati ni suala la wajibu binafsi, lakini pia asilimia 78 walikubaliana kwamba rushwa ni chanzo cha majanga kama hayo.

0 comments:

Post a Comment