WAZIRI wa Fedha, Mhe. Omar Yussuf Mzee, amesema watendaji wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) upande wa Tanzania Bara,wanasababisha mgogoro
wa makusudi kwa wafanyabiashara wa Zanzibar.
Akitoa ufafanuzi kuhusu hoja ya Mwakilishi wa Kikwajuni, Mhe. Mahmoud
Mohammed Mussa, kuhusu makontena ya Zanzibar yaliyozuiliwa bandarini
Dar es Salaam na kitendo cha kuletwa wafanyakazi saba wa TRA kufuatilia
makontena hayo wakati akichangia bajeti ya wizara ya Biashara, Viwanda
na Masoko, Waziri huyo alisema TRA Tanzania Bara wana tatizo lakini
hawalisemi, hali inayosababisha mgogoro mkubwa.
Hata hivyo, alisema wataendelea kutafuta kiini cha tatizo hilo kwa
mazungumzo na ikishindikana watatumia Kamati ya kero za Muungano.
Aidha alisema wizara inasubiri majibu kutoka TRA Zanzibar kuhusu
wafanyakazi wa TRA Tanzania Bara kutumwa kuchunguza makontena hayo,
baada ya kupokea malalamiko kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara,
Wenyeviwanda na Wakulima (ZNCCIA) kuhusu kitendo hicho cha TRA.
Mapema Mbunge huyo wa Kikwajuni, alisema wafanyakazi hao wa TRA
walitumwa kufuatilia makontena hayo na kuyapekuwa kujua kilichomo ndani
na kuripoti makao makuu na kuhoji utaratibu huo utaendelea hadi lini.
Alisema makontena hayo yalifika bandarini Dar es Salaam tokea Juni 5,
lakini yalikuwa yakizuiliwa na TRA kwa utashi wao tu na kwa lengo la
kudhoofisha biashara ya Zanzibar.
Wakichagia bajeti hiyo,Wawakilishi walieleza kusikitishwa kwao kufa
kwa viwanda vya ndani, hali iliyosababisha ukosefu mkubwa wa ajira kwa
vijana.
Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Mhe. Saleh Nassor Juma, alisema Zanzibar
ilikuwa na viwanda vingi muda mfupi baada ya mapinduzi, lakini vyote
vimekufa na kudhoofisha mfumo wa ajira kwa vijana.
Aidha aliitaka wizara hiyo kutafuta ufumbuzi wa moshi nzito unaotoka
katika kiwanda cha makonyo Wawi, ambao unasababisha athari za kiafya kwa
wananchi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo Tumbe, Mhe.Rufai Said Rufai, aliitaka serikali kuimarisha viwanda ili kukuza uchumi.
Akitoa majumuisho, Naibu Waziri wa Viwanda, Mhe. Thuwaiba Kisasi,
aliwataka wafanyabiashara kuwa na moyo wa huruma kwa wananchi katika
kipindi hichi wakijiandaa na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema serikali ilitoa msamaha wa kodi kwa wafanyabiashara wa
chakula, kwa lengo la kuuza bidhaa zao kwa wananchi kwa bei nafuu,
lakini misamaha hiyo hawaisaidii walaji na kuendelea kununua bidhaa kwa
bei ya juu.
Kuhusu kodi mara mbili, Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Nassor Ahmed
Mazrui, alisema bado tatizo hilo linaendelea kwa wafanyabiashara wa
Zanzibar.
Alisema wapo baadhi ya wafanyakazi wa TRA ambao kwa makusudi wanataka
kudhoofisha Muungano na kufanya ubaguzi baina ya wafanyabiashara wa
Zanzibar na Tanzania Bara jambo ambalo halifai kwani linaweza kuleta
athari kubwa siku za baadae.
Kuhusu kufungwa kiwanda cha kuzalisha vinywaji baridi cha Coca Cola
Zanzibar, alisema kiwanda hicho kimesitisha uzalishaji kutokana na
mitambo yake kuchakaa na hofu waliyonayo wamiliki wa kampuni hiyo kwamba
kikiachiwa kuendelea kuzalisha kinaweza kuzalisha bidhaa zisizo na
ubora.
Hata hivyo, aliwatoa hofu Wawakilishi kwamba serikali inaendelea
kuzungumza na uongozi wa kiwanda hicho na kwamba mitambo iliyopo ndani
ya kiwanda hicho ni mali ya kampuni lakini majengo ni ya serikali.
Hivyo, kama kampuni hiyo itashindwa kufanya uzalishaji, serikali itatafuta mwekezaji mwengine.
Wajumbe wa baraza hilo walichangia bajeti ya wizara hiyo baadae wakaipitisha.
Jun 27, 2014
‘TRA Bara wanasababisha mgogoro’
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment