Jun 28, 2014

Rouhani: Waislamu waungane Mwezi wa Ramadhani

Rais Hassan Rouhani Rais Hassan Rouhani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewatumia salamu za pongezi viongozi wa nchi zote za Kiislamu duniani kwa munasaba wa kuwadia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo amewataka wautangaze mwezi wa Ramadhani mwaka huu kuwa ni 'Ramadhani ya Amani na Rahma'. 

Aidha amewataka viongozi wa nchi za Kiislamu kujitahidi kuleta umoja na udugu miongoni mwa Waislamu kote duniani. Katika ujumbe wake huo, Rais Rouhani amesema Ramadhani ni mwezi wa saumu, kiyamu na rehma na ibada na hivyo viongozi wa Kiislamu wanapaswa kuchukua hatua za kuimarisha umoja wa Kiislamu. Katika sehemu ya ujumbe wake, Dkt. Rouhani ameseama:
 'Mwaka huu, Waislamu wanaukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani huku machafuko na misimamo mikali ikiusukuma ulimwengu wa Kiislamu katika hofu, ujahili, na ghadhabu mambo ambayo yanawaandalia maadui njia ya kutekeleza njama zao za jadi za kuwafarakanisha Waislamu sambamba na kuibua vita vya kimadhehebu na kikaumu." 

Rais wa Iran katika ujumbe wake ameongeza kuwa: "Katika mwezi huu wenye baraka ambao ni machipuo ya Qur'ani tunapaswa kustafidi na mafundisho ya Qur'ani na maadili mema ya Mtume wa Rahma SAW". 

Ameongeza kuwa ni jambo la dharura kwa nchi za Kiislamu kuongoza vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali sambamba na kubeba bendera ya amani, msamaha na rahma duniani. Rais wa Iran ameelezea matumaini yake kuwa nchi za Kiislamu zitapata fanaka katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani uliojaa neema na baraka.

0 comments:

Post a Comment