“Kwa miaka minne mfululizo maelfu ya tani za
mkaa wa mawe yamekuwa yanasombwa na maji kutoka katika Kijiji cha Ndumbi
hadi ndani ya Ziwa Nyasa, wananchi wanatumia maji hayo kwa ajili ya
kunywa,’’ anasema Mwenyekiti wa kijiji hicho wilayani Nyasa mkoani
Ruvuma, James Mbawala.
Anasema Kampuni ya Mkaa wa Mawe ya TANCOAL ambayo
inachimba mkaa wa mawe katika eneo la Ngaka wilayani Mbinga ndiyo
inayoitumia Bandari ya Ndumbi, Ziwa Nyasa kwa ajili ya kusafirishia mkaa
wa mawe kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Mbawala anasema katika bandari ya kijiji hapo ni
mahali pa kupitishia mkaa huo na kwamba kijiji hicho hakina huduma ya
maji ya bomba badala yake wananchi wanatumia maji ya Ziwa Nyasa kwa maji
ya kunywa na matumizi mbalimbali.
Ushirikishwaji katika EIA
Kwa kawaida Serikali inapokusudia kuanzisha miradi
mikubwa kama ya madini, katika tathmini ya mazingira yaani
Environmental Impact Assessment (EIA) inatakiwa Serikali kuwashirikisha
wananchi katika eneo husika ili kubaini iwapo mradi huo utakuwa na
madhara au laa, mwenyekiti huyo anadai kuwa Serikali haikuwashirikisha
ilipoamua kuitumia Bandari ya Ndumbi kwa ajili ya kusafirishia mkaa
wakati wa utafiti na sasa wakati wa uchimbaji na uuzaji.
Sera ya mazingira ya mwaka 1997 ambayo imetumika
kutunga sheria mama ya mazingira ya mwaka 2004 katika kifungu cha 4 (1)
na kifungu cha 5 (1) inaeleza wazi kuwa kila mtu Tanzania ana haki ya
kuishi katika mazingira safi, salama na afya njema hivyo hatua za
uchimbaji wa madini iwapo siyo salama inaweza kutumika sheria hii kudai
haki.
Mwanasheria na Mkurugenzi Mtendaji wa Lawyers
Environmental Action Team (LEAT), Dk Nshala Rugemeleza anasema sheria
mama ya mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 21 inaonyesha wazi miradi
yote mikubwa inayotakiwa kufanyiwa tathmini ya mazingira (EIA) miradi
ambayo inabadilisha asili ya umbile la eneo husika kama ilivyo kwa mkaa
wa mawe ambao umebadilisha asili ya umbile la Bandari ya Ndumbi.
Dk Nshala anasisitiza kuwa iwapo taratibu za EIA
hazikufuatwa wadau wanaweza kupeleka malalamiko yao mahakamani ili kudai
haki pia mwekezaji anatakiwa kurudishia mazingira aliyoyaharibu katika
Bandari ya Ndumbi baada ya mradi kwa kuyarekebisha ili kurejea katika
hali yake ya asili kabla hajaondoka.
Kulingana na Dk Nshala mfumo wa utoaji leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini, gesi na mafuta ni mbovu, hivyo uangaliwe.
Kulingana na Dk Nshala mfumo wa utoaji leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini, gesi na mafuta ni mbovu, hivyo uangaliwe.
0 comments:
Post a Comment