Oct 3, 2013

Mwandishi Akamatwe-ICC

Mahakama ya kimataifa ya ICC, imetoa kibali cha kukamatwa kwa raia Mkenya ambaye anatuhumiwa kwa kujaribu kuwahonga mashahidi ili wajiondoe kwenye kesi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya William Ruto.

Viongozi wa mashtaka walisema kuwa mshukiwa huyo Walter Osapiri Barasa ameshtakiwa kwa makosa matatu ikiwemo kutumia njia za ufisadi kumshawishi shahidi mmoja na mkewe kwa kumlipa shilingi milioni 1.4 au dola 16,200, ili wajiondoe kama mashahidi katika kesi hiyo.
Aidha mahakama inasema kuwa ni juu ya Kenya sasa kumkamata Barasa.

Kiongozi wa mashtaka Fatou Bensouda amesema kuwa ana ushahidi wa kutosha kuonyesha njama ya Barasa kutaka kuwahonga mashahidi ili wajiondoe katika kesi dhidi ya Ruto.
Bensouda amesema kuwa kuna mtandao wa watu wanaofanya kila wawezalo ili kuporomosha kesi dhidi ya Ruto.

Lakini Barasa ameambia BBC kuwa yuko tayari kujitetea mbele ya mahakama hiyo na kuonyesha kuwa hana hatia.
Naibu Rais Ruto na Rais Kenyatta wameshtakiwa kwa kupanga na kuongoza ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo watu 1,200 walifariki.

Mahakama ya kimataifa ya ICC italazimika kuwa na vikao virefu zaidi vya kusikiliza kesi dhidi ya Naibu rais wa Kenya William Ruto, kwa sababu ya muda uliopotea kutokana na Ruto kurejea Kenya kwa dharura.

Jaji anayeongoza kesi hiyo Chile Eboe-Osuji pia alisema kuwa mahakama itadurusu uwezekano wa kusikiliza kesi hiyo Jumatano siku ambayo wangepumzika ili kuruhusu kesi nyengine kusikilizwa ndani ya chumba hicho.

"kama tunavyojua sote tumepoteza muda katika kesi hii kwa sababu ya matukio ambayo hayangeweza kuepukika. Lazima tuweze kupata muda huo'', alisema jaji huyo.

Kesi dhidi ya Ruto iliakhirishwa Septemba 23 kutokana na shambulizi la kigaidi nchini Kenya ambalo liliwau watu zaidi ya sitini.

Hata hivyo jaji huyo alisisitiza kuwa kesi hiyo itaakhirishwa kwa muda ili kutoa nafasi kwa kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta Novemba tarehe 12 ambaye ni mshitakiwa mwenza wa William Ruto.

Kesi dhidi ya Ruto na mwenzake Joshua Sang, iliakhirishwa tarehe 23 Septemba, wakati mahakama ilipomruhusu Ruto kurejea Nairobi kushughulikia shambulizi la kigaidi la Westgate na athari zake.

0 comments:

Post a Comment