Feb 16, 2015

CUF wapuliza kipenga, urais wasubiri Ukawa

wafuasi-cuf

Chama cha Wananchi (CUF), kimepuliza kipenga kwa wanachama wake kikiwataka wajitokeze kuchukua fomu za kugombea uongozi katika nafasi za udiwani, ubunge, uwakilishi na urais unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Kadhalika, chama hicho kimeweka hadharani ratiba ya uchukuaji fomu, kura ya maoni, vikao vya kuchuja majina ya wagombea wenye sifa na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa ajili ya kufanya uteuzi wa wagombea uwakilishi, ubunge na urais.

Hata hivyo, ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu kwa nafasi ya urais kiporo.


Akizungumza na Waandishi wa Habari, jana jijini Dar es Salaam jana, Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Shewaji Mketo, alisema nafasi hizo zipo wazi kwa wanachama wote wenye sifa wanaotimiza masharti ya Katiba ya nchi na chama kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania.

“Chama kinatangaza kuwa kutakuwa na zoezi la kura za maoni kwa ajili ya kuwapata wagombea wa udiwani, ubunge, uwakilishi na urais…uchaguzi huu utafanyika ili kukidhi matakwa ya Katiba ya chama Ibara ya 91,92 na 93 pamoja na marekebisho yake,” alisema.

Mketo alisema pamoja na chama hicho kuweka ratiba, malengo yao kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) yapo pale pale na kwamba kila chama kitatafuta wagombea katika ngazi zote na baadaye kuchambuliwa na vyama vya Ukawa ili kuona nani anastahili kupewa wapi ya kuwa mwakilishi wa Ukawa.

Vyama vinavyounda Ukawa ni CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.

RATIBA
Mkurugenzi huyo aliweka bayana ratiba hiyo kuwa ni Machi 1 hadi 10, mwaka huu, wanachama kuchukua na kurejesha fomu kwa nafasi ya udiwani.


Machi 11 hadi 13, mwaka huu, Katibu wa Tawi kuzifikisha fomu za wagombea udiwani kwa Katibu Kata, Machi mosi hadi 10, mwaka huu, wanachama kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea ubunge na zitachukuliwa ofisi za kata.

Alisema Machi 15 hadi 30, mwaka huu, mikutano mikuu ya kata kura za maoni kwa udiwani, Machi 11 hadi 20, mwaka huu, Katibu wa kata kuzifikisha fomu za wagombea ubunge kwa Katibu wa wilaya.

Alisema Machi 31 hadi Aprili 4, mwaka huu, kutakuwa na maandalizi ya mikutano mikuu ya wilaya kwa ajili ya kura za maoni.

Mketo alisema Aprili 5 hadi 15, mwaka huu, itakuwa ni mikutano mikuu ya wilaya ya kura za maoni na Aprili 17 hadi 19, mwaka huu, ni Kurugenzi kufanya uchambuzi wa fomu za wagombea ubunge ili kuwasilisha kwa Kamati ya Utendaji ya Taifa.

Alisema Aprili 20 hadi 21, mwaka huu, ni kikao cha Kamati ya utendaji ya taifa kuweka sifa za wagombea ubunge, Aprili 22 hadi 23, mwaka huu, ni maandalizi ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

Aprili 24 hadi 25, mwaka huu ni kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kufanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea wa ubunge na uwakilishi.

Mkurugenzi huyo alivitaja hadharani viwango vya ada kwa kila nafasi kwenye mabano kuwa udiwani (Sh. 10,000), ubunge/uwakilishi (Sh. 50,000) na Urais (Sh. 500,000).

“Utaratibu wa uchaguzi utatolewa muda mfupi ujao kwa kupitia kanuni ya uchaguzi ndani ya chama,” alisema.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alionyesha kumpigia kampeni Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba, kuwa ni mwenye sifa za kutosha kuwania nafasi ya urais na kwamba atasimama kwenye nafasi hiyo.

“Baada ya mchakato tumeona Prof. Lipumba ana sifa zote za kugombea urais kwa kuwa amewahi kufanya hivyo mara kadhaa…hivyo nina imani naye kuwa anastahili kusimama katika nafasi hiyo,” alisema.

Profesa Lipumba aligombea urais mara nne mfululizo kupitia CUF kuanzia mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010.

0 comments:

Post a Comment