Feb 25, 2014

Serikali ya Misri yajiuzulu ili kumpisha al Sisi

Waziri Mkuu wa Misri Hazem la Beblawi amesema kuwa serikali yake imejiuzulu, hatua ambayo inaonekana imechukuliwa ili kumuandalia mazingira Jenerali Abdul Fatah al Sisi ili aweze kutangaza kugombea urais.

Beblawi amesema, Baraza la Mawaziri limeamua kujiuzulu na kwamba katika kipindi lilichohudumu limefanya jitihada kubwa ili kuiondoa Misri katika mkwamo wa kisiasa, matatizo ya kiusalama, na mashinikizo ya kiuchumi. 
Hata hivyo Beblawi hakutoa maelezo kwa nini serikali yake imeamua kujiuzulu. Msemaji wa serikali ya Misri Hany Saleh amewaambia waandishi habari kwamba, uamuzi huo umechukuliwa kwa kuwa anahitajika shakhsia mpya kuiongoza Misri.

Hata hivyo ili al Sisi aweze kugombea uchaguzi wa urais atapaswa ajiuzulu wadhifa wake wa Waziri wa Ulinzi. Uchaguzi wa rais wa Misri unatarajiwa kufanyika miezi kadhaa ijayo.  

0 comments:

Post a Comment