Jan 12, 2015

MABALOZI WAITAKA SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WALIOTAJWA KUTAFUNA FEDHA ZA ESCROW.


Balozi wa Vatican nchini, Francisco Montecillo Padilla (kushoto) akizungumza na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Hani Mominah wakati wa sherehe za mwaka mpya ziliyoandaliwa kwa ajili ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao na mashirika ya kimataifa. Picha na Anthony Siame
Licha ya Rais Jakaya Kikwete kutoa ufafanuzi wa sakata la uchotaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu na kutangaza kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya viongozi na watendaji, nchi wahisani wamesema bado suala hilo linawachanganya na wanasubiri tamko la Serikali.


Nchi hizo, ambazo zilizuia takriban Sh1 trilioni za ufadhili na kuchangia nakisi ya bajeti ya Serikali, juzi zilikiri kuanza kuruhusu sehemu ya fedha hizo baada ya baadhi ya maazimio ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kuanza kutekelezwa, ikiwa ni pamoja na kumvua uwaziri Anna Tibaijuka, kumsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na kumuweka kiporo waziri wake, Sospeter Muhongo na kusababisha Jaji Fredrick Werema kujivua wadhifa wake wa Mwanasheria Mkuu.


Tayari Rais Jakaya Kikwete ameshaeleza kuwa fedha hizo hazikuwa za Serikali.


Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili juzi, Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini, Timothy Clarke alisema kwamba Serikali imeonyesha jitihada za mwanzo, lakini wanasubiri kuona hatua kali zaidi zikichukuliwa pamoja na kuja na kauli moja kuhusu fedha hizo.


Alisema alichobaini ni kwamba wananchi wengi wanataka kujua hatima ya sakata hilo ndiyo maana walitumia vyombo vya habari kufanya mijadala mbalimbali kuzungumzia wizi wa fedha za escrow ambazo haijawekwa wazi kuwa ni za umma ama ni za Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.


Balozi Clarke alisema kwa upande mwingine, Serikali imeonyesha tabia ya kusita katika kutoa uamuzi kwenye suala hilo na kwamba walitarajia kusikia tamko kali pamoja na tamko la kuzuia vitendo hivyo visiendelee.


Alieleza kuwa hadi sasa nchi nyingi hazijaipa fedha Tanzania kama zilivyokuwa zinatarajiwa kwa kuwa bado zinasubiri hatua zaidi kutoka serikalini.


Sakata la escrow, lililohusu uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka akaunti hiyo, lilisababisha Taasisi ya Marekani ya MCC inayosaidia nchi zinazoendelea, kutangaza kusitisha kusaini mkataba wa awamu ya mpango huo wa maendeleo kuishinikiza Serikali kushughulikia kashfa hiyo.


Bodi ya Wakurugenzi ya MCC ilitoa taarifa yake Desemba 16 mwaka jana, ikieleza kuwa mkutano wake wa Desemba 10 mwaka huu uliruhusu kuanza maandalizi ya kusaini mkataba wa awamu ya pili ya mpango huo, lakini ulielezea hofu na masikitiko kuhusu hali ya rushwa inavyoendelea Tanzania.


Fedha ambazo Tanzania ilipaswa kupata kupitia mradi huo wa MCC awamu ya pili ni Dola 450 milioni ambazo ni sawa na Sh765 bilioni.


“Japokuwa bodi ilipiga kura kwa dhati kabisa ya kuiruhusu Tanzania iendelee na maandalizi kwa ajili ya mkataba wa pili, inaihimiza Serikali ya Tanzania kuchukua hatua thabiti na mahsusi za kukabiliana na rushwa kama sharti la msingi kwa bodi hiyo kufanya uamuzi wa mwisho wa kuidhinisha mkataba huo.


Sakata la escrow lilihusisha fedha zilizokuwa zimehifadhiwa Benki Kuu wakati kesi baina ya Shirika la Umeme (Tanesco) na IPTL zikipambana mahakamani. Pande hizo mbili zilikubaliana kufungua akaunti hiyo ya escrow ili kutunza fedha ambazo Tanesco ilitakiwa iilipe IPTL ikiwa ni malipo ya ununuzi umeme.


Hata hivyo, akaunti hiyo ilifungwa kwa njia ambayo ilitia shaka na fedha hizo kulipwa kwa Kampuni ya Pan African Power Solution Limited (PAP) ambayo ni mmiliki mpya wa IPTL na kukiwa na mambo mengi yaliyotakiwa kufanyiwa kazi kabla ya malipo hayo, ikiwa ni pamoja na kulipwa kwa kodi ya Serikali na kukokotoa upya gharama ambazo Tanesco ilitakiwa ilipe baada ya mzozo wao kuisha mahakamani.


Pia, fedha hizo zililipwa kwa James Rugemarila aliyekuwa akimiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL na ambaye baada ya malipo alitoa mgawo wa fedha kwa watu kadhaa, wakiwamo viongozi wa dini, watumishi wa umma, mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa zamani, hali iliyotia shaka zaidi kuhusu fedha hizo.


Tayari Tibaijuka amewajibishwa baada ya kupokea Sh1.6 bilioni kutoka kwa Rugemarila, hali kadhalika Andrew Chenge, ambaye pia alipewa Sh1.6 bilioni na William Ngeleja (40.4 milioni) wametakiwa kuondolewa kwenye uenyekiti wa Kamati za Bunge sambamba na Victor Mwambalaswa na Fredrick Werema, akitangaza kujiuzulu wadhifa wake wa Mwanasheria Mkuu kwa maelezo kuwa ushauri wake haukueleweka na kuzua tafrani.


Naye Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose alisema mazungumzo na Serikali bado yanaendelea na kwamba hali itaendelea kuwa nzuri kadri mazungumzo yanavyoendelea.


“Bado tunaendelea na mazungumzo na Serikali huku tukisubiri tamko,” alisema Dianna.


Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa mfuko wa maendeleo wa wahisani, Sinikka Antila juzi ilieleza kuwa mpaka sasa zimekwishatolewa Dola 84 milioni sawa na asilimia 15 ya msaada wote kwenye bajeti ya 2014/2015.


Kwa upande wake, kiongozi wa mabalozi waliopo nchini, Juma Mpango alisema Tanzania imeonyesha jitihada katika kuleta maendeleo na kupambana na rushwa.


Balozi Mpango, ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), alisema Serikali imeonyesha nia ya kupunguza matukio ya kifisadi.


“Tumefuatilia namna ambavyo Tanzania imefanya vita kubwa kuondoa madhara ya ufisadi katika nchi, ilikuwa kubwa sana,” alisema Balozi Mpango.


Nchi na wadau wanaochangia kwenye bajeti na sekta nyingine za maendeleo ni; Canada, Denmark, Finland, Ujerumani, Ireland, Japan, Sweden, Uingereza, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jumuiya ya Ulaya (EU) na Benki ya Dunia

0 comments:

Post a Comment