Jan 18, 2014

Rouhani: Maadui wanazusha hitilafu katika Umma

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, madola ya kibeberu yangali yanafanya njama za kuzusha hitilafu na mifarakano katika ulimwengu wa Kiislamu.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa 27 wa Umoja Kiislamu na kusisitiza kwamba, kuna makundi yanayotumia mgongo wa Uislamu kwa ajili ya kufikia malengo yao katika eneo la Mashariki ya Kati. 

 Rais Rouhani amebainisha kwamba, njama nyingine za maadui ni kukuza hitilafu za kimadhehebu na hivyo kuandaa uwanja wa kufikia malengo yao ya kutokuweko umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu. 

Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa mshika bendera ya kukabiliana na njama za maadui za kuugopesha Uislamu na kuupaka matope.

Rais Rouhani amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake hiyo kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikiandamwa na maadui kutokana na kushikamana kwake na mafundisho ya Kiislamu. 

Amesema, maadui wamekuwa wakiiandama Iran kwa kisingizio kwamba, inataka kutengeneza silaha za nyuklia, katika hali ambayo taifa hili limetangaza bayana tena mara chungu nzima kwamba, halina mpango wa kumiliki silaha hizo na kwa mujibu wa fatuwa ya Ayatullahi Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ni haramu kumiliki silaha hizo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amewahimiza Waislamu kufuata sira ya Mtume Muhammad (saw) ambaye alisisitiza umoja na mshikamano na kuyaunganisha makabila yaliyokuwa yakihasimiana kwa miaka mingi. 

Amesema Mtume (saw) alifuta hitilafu na kuwaunganisha pamoja watu wa mataifa na rangi tofauti kama Bilal al Habashi, Salman al Farsi na Suhaib al Rumi. Vilevile amekemea baadhi ya makundi yanayojiita ya Kiislamu ambayo yanachafua sura ya dini hiyo kutokana na ufahamu wao finyu wa mafundisho ya Uislamu.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa wazungumzaji wengi wa siku ya kwanza ya mkutano huu wamesisitiza juu ya udharura ya kuungana Waislamu na kuwa macho mbele ya njama za makundi yanayowakufurisha Waislamu na kumwaga damu zao katika nchi mbalimbali kama Syria, Libya, Iraq, Lebanon na Afghanistan.

Mkutano wa 27 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran unahudhuriwa na wasomi, wanafikra na maulamaa wa madhehebu mbalimbali za Kiisalmu kutoka nchi 50 duniani. Mkutano huo wa siku tatu unafanyika mwaka huu chini ya kaulimbiu ya :Qur'ani Tukufu na Nafasi yake katika Umoja wa Waislamu.

0 comments:

Post a Comment