Jan 18, 2014

Mbaroni akidaiwa kutorosha mwanafunzi

MTU mmoja anaejulikana kwa jina la Fadhili Yussuf Khamis (34) mkaazi wa Magomeni na Jambiani Unguja, anashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa kusini Unguja, kwa madai ya kumtorosha mwanafunzi.

Tukio hilo lilitokea Januari 14, 2014 majira ya saa 5:30 za asubuhi katika maeneo ya Jambiani Kikadini mkoa wa Kusini Unguja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa polisi mkoa huo Agostino Ulomi, mtuhumiwa anashughulika na utunzaji wa msikiti wa Jambiani na kwamba uongozi wa msikiti ulimpatia chumba kwa ajili ya kupumzika.

Alisema polisi walipata taarifa za tukio hilo kupitia uongozi wa shehia na walipofika eneo la tukio walimkuta mtuhumiwa akiwa pamoja na mwanafunzi huyo chumbani.


“Mtu huyu anaedaiwa kufanya vitendo hivi anaishi Magomeni ambako ndipo ilipo familia yake lakini shughuli zake nyingi anazifanyia Jambiani kwa sababu amekabidhiwa kazi ya kutunza msikiti na uongozi wa msikiti umempatia chumba,” alisema kamanda huyo.

Alisema mtuhumiwa anashikiliwa kituo cha polisi Paje na anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

Kuhusu kuingiliwa, alisema hawezi kuthibitisha kama kitendo hicho kimefanyika, lakini daktari aliemfanyia uchunguzi anaweza kuthibitisha hilo.

0 comments:

Post a Comment