Dec 16, 2013

AUAWA BAADA YA KUTUHUMIWA KUUA


 
Mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina ameuawa na wananchi wenye hasira baada ya kuzuka mgogoro wa ardhi baina yao.
 

Mabina aliuawa katika Kata ya Kisesa, baada ya wananchi wenye hasira kumtuhumu kumuua kwa kumpiga risasi mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

Jina la mkazi aliyepigwa risasi halikupatikana na kwamba alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali kwa matibabu.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Joyce Masunga alithibitisha kuuawa kwa Mabina, ambaye miezi ya karibuni alikuwa ni mwenyekiti wake.


Masunga alisema taarifa zilizomfikia zinaeleza kuwa Mabina alijikuta anaingia kwenye mgogoro na wananchi hao saa 11:00 asubuhi.

Alisema mgogoro huo ulianza wakati kundi la watu waliotumwa na Mabina walipoanza kuweka alama za mipaka kwenye shamba linalodaiwa kumegwa kwenye eneo la wakazi hao.

Wakazi hao walipopata taarifa hizo, walijitokeza kuzuia kundi hilo lisitekeleze kazi hiyo.

Kundi hilo lilipopata upinzani huo, liliwasiliana na Mabina kumweleza kwamba wamezuiwa kufanya kazi aliyowaagiza.

Inadaiwa kuwa Mabina kusikia hivyo, aliharakisha kwenda eneo hilo ili kujaribu kusuluhisha mgogoro huo ili maelekezo yake yafanyike kama alivyopanga.

Miongoni mwa watu waliokuwa kwenye eneo hilo, alisema wakati wanajibizana na wananchi hao, Mabina alimpiga risasi mmoja wa wakazi hao na kuanguka chini.

Walieleza kuwa tukio hilo liliwapandisha hasira wakazi hao na kusababisha wamshambulie kwa kumrushia mawe, vipande vya miti na silaha mbalimbali kwa kadri kila mmoja alivyoweza.
 
 ENZI ZA UHAI WAKE CLEMENT MABINA.

0 comments:

Post a Comment