Jul 1, 2014

ISIS yatangaza miliki ya Khalifa Iraq na Syria

Kundi la wapiganaji wa jihadi wanaoongoza mashambulizi nchini Iraq wametangaza miliki ya Khalifa na kuwataka Waislamu wote duniani kutangaza utiifu kwa kiongozi wao. 

Kundi hilo la Taifa la Kiislamu la Iraq na Syria ISIS, limejibadili jina na kujiita Taifa la Kiislamu IS, na kumtangaza Abubakar al-Baghdad kuwa kiongozi wa Waislamu duniani.

Msemaji wa kundi hilo Abu Muhamad Al- Adnan alitagaza kuundwa kwa miliki ya Khalifa na kuchaguliwa kwa Al-Baghdad kuwa Khalifa katika mkanda wa sauti uliyowekwa kwenye mtandao juzi Jumapili.

"Baraza la Tiafa la Kiislamu limekutana na kujadili suala hili. 

Taifa la Kiislamu limeamua kuunda miliki ya Khalifa na kumteua Khalifa wa dola ya Waislamu. 

Kiongozi wa jihadi Baghdad aliteuliwa kuwa Khalifa wa Waislamu," alisema Al-Adnan.
Msafara wa wapiganaji wa IS mkoan Anbar. Msafara wa wapiganaji wa IS mkoan Anbar.

Kuanzia Iraq hadi Syria
Miliki hiyo ya Khalifa ambayo ni aina ya serikali inayofuata mfumo wa Uislamu ambao ulishuhudiwa mara ya mwisho wakati wa utawala wa sayydna Othman, inaanzia mkoani Aleppo kaskazini mwa Syria hadi mkoa wa Diyala mashariki mwa Iraq, maeneo ambako kundi hilo limepigana dhidi ya tawala zilizoko madarakani.

Taarifa kutoka mjini Washington zinasema kiongozi wa ISIS Abubakari al-Baghdad alizaliwa mjini Samarra mwaka 1971, na alijiunga na uasi uliyoibuka muda mfupi baada ya uvamizi wa Iraq uliyoongozwa na Marekani mwaka 2003. 

Vikosi vya Marekani viliamini mwaka 2005 kuwa vilimuuwa Al-Baghdad katika shambulizi la ndege kwenye mpaka wa Iraq na Syria, lakini hilo linaonekana halikuwa sahihi.

Kundi lake limevutia maelfu ya wapiganaji wa kigeni, ambao wanavutiwa na ushawishi wa Baghdad mwenyewe, juhudi la IS kuunda kile inachoamini kuwa ndiyo dola sahihi ya Kiislamu, na mfumo wa kisasa wa propaganda unaotumiwa na kundi hilo, ambao unachapisha majarida na kutoa mikanda ya video kwa Kiingereza na lugha nyingine kadhaa za Ulaya.
Raia wakipeperusha bendera za IS katika mji wa Raqqa nchini Syria. Raia wakipeperusha bendera za IS katika mji wa Raqqa nchini Syria.

Kilifutwa mwaka 1924
Khalifa ndiyo cheyo walichokuwa wanapewa watawala wa Kiislamu tangu alipofariki mtume Muhammad hadi utawala wa sayydna Othman na kuundwa kwa Jamhuri ya kwanza ya Uturuki mwaka 1924.

Ingawa cheo hicho kilikuwa kimeundwa kwa ajili ya Khalifa moja na taifa moja la ukhalifa, nafasi hiyo ilikuwa inazozaniwa mara kwa mara kati ya Waislamu Wasunni na Washia, na wakati mwingine kwa kufuata mipaka ya kijiografia.

IS inapigania kurejeshwa kwa utawala wa zamani wa ukhalifa wa kisunni katika ulimwengu wa kiarabu. 

Siku ya Jumapili, kundi hilo liliyatolea wito makundi yote kutangaza utiifu kwa khalifa Ibrahmi, ambalo ndiyo jina halisi la Baghdad, hatua ambayo wachambuzi wanaiona kama upinzani wa moja kwa moja dhidi ya Al-Qaeda.

IS iliungana kwa muda mfupi na kundi la Al-Nusra Front, ambalo ni tawi la Al-Qaeda katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, lakini makundi hayo mawili yalivunja uhusiano wote mwezi Februari.
Waziri mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki alipokutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry. Waziri mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki alipokutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry.

Mashambulizi Tikrit
Jeshi la Iraq lilituma vifaru na magari ya kivita mjini Tikrit siku ya Jumapili, kujaribu kuurejesha mji huo wenye utajiri wa mafuta nguvu ya kijeshi kutoka kwa IS. 

Msemaji wa jeshi alisema katika madai ambayo hayakuweza kuthibitishwa, kuwa jeshi lilifanikiwa kurejesha uthibiti wa chuo kikuu cha Tikrit na kuwauwa magaidi 70 mjini humo.

Serikali pia ilinunua ndege tano aina ya Sukhoi kutoka nchini Urusi, ambazo ziliwasilishwa mjini Baghdad siku ya Jumamosi, huku televisheni ya serikali ikisema zitatumiwa katika siku zijazo dhidi ya makundi ya kigaidi ya IS.

Jeshi la Iraq limekuwa likitegemea zaidi helikopta za mashambulizi kutokana na kuwa ndege chache sana zinazoweza kutumia makombora ya kisasa. 

Naibu waziri mkuu anaehusika na masuala ya nishati Hussaini Alshahrishtan, aliilamu Marekani siku ya Jumapili kwa kutofanya vya kutosha kuliimarisha jeshi la Iraq, akisema katika televisheni ya al-Hurra kwamba silaha ziliwasilishwa kwa kuchelewa kuliko ilivyokubaliwa.
Waziri mkuu wa Isreal Benjamin Netanyahu ameiomba jamii ya kimataifa kusaidia mapambano dhidi ya IS Waziri mkuu wa Isreal Benjamin Netanyahu ameiomba jamii ya kimataifa kusaidia mapambano dhidi ya IS

Shinikizo kwa wanasiasa
Wanasiasa mjini Baghdad pia wanashinikizwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa yenye uwezo wa kukabiliana na IS; mchakato huu unatarajiwa kuanza leo siku ya Jumanne.

"Wakikabiliwa na mgogoro wa kitaifa, viongozi wa kisiasa wa Iraq wanapaswa kuweka maslahi ya taifa na watu wake mbele ya kila kitu," alisema mwakilishi maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Nickolay Mladendov katika taarifa siku ya Jumapili, huku kukiwa na ripoti kwamba kundi la waziri mkuu wa zamani Iyad Allawi lenye viti 21 halitahudhuria kikao hicho cha kuundwa serikali.

Huku hayo yakijiri, waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu, ameiomba jamii ya kimataifa kuisaidia Jordan kukabiliana na itikadi kali za Kiislamu, na kuunga mkono uhuru kwa Wakurdi wa Iraq.

Matamshi yake yalifuatia ripoti katika vyombo vya habari vya Israel kwamba maafisa mjini Tel Aviv wanahofu kuwa wapiganaji wa Taifa la Kiislamu huenda wakapanua udhibiti wao katika maeneo ya Jordan baada ya Iraq.

0 comments:

Post a Comment