Jun 30, 2014

Wizi wa kimataifa · Walitaka kuibia Serikali ya Mapindizi Zanzibar zaidi ya 4bn/- · Walighushi saini za viongozi

_MG_5149ZAIDI ya shilingi bilioni nne zimenusurika kuibwa katika mfuko mkuu wa hazina ya serikali baada ya mtandao wa watuhumiwa wa wizi wa kimataifa kutiwa mbaroni 

walipowasilisha madai ya kughushi ya kulipwa euro milioni 200 na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Watuhumiwa hao ambao ni raia wa Marekani, Oman na Tanzania, waliwasilisha nyaraka hizo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Zanzibar, Khamis Mussa, ili walipwe kiwango hicho ambacho wanadai kuikopesha serikali ya wamu ya sita.

Uchunguzi  umegundua kwamba watuhumiwa hao walifanikiwa kughushi saini za aliekuwa Rais wa Zanzibar wa awamu ya sita, Dk. Amani Abeid Karume, Waziri aliekuwa akisimamia masuala ya fedha, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini na Katibu Mkuu Wizara ya fedha wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya tano, Dk. Salmin Amour Juma, Omar Sheha Mussa.

Hata hivyo, walipotakiwa kueleza kitu gani walichoikopesha serikali walishindwa kuainisha.

Kwa mujibu wa wapasha habari wetu, baada ya kuwasilisha madai hayo, Katibu Mkuu fedha alishtuka kuiona saini ya aliekua Katibu Mkuu wa wizara hiyo katika serikali ya awamu ya tano, Omar Sheha, ambae hakuwahi kuwa Katibu Mkuu fedha katika serikali ya awamu ya sita, huku watuhumiwa wakidai kwamba wameikopesha serikali ya awamu ya sita.

“ Watuhumiwa wa wizi huu walishtukiwa baada ya kutakiwa kuleta mikataba yao waliotiliana saini na Serikali na kutakiwa kueleza waliikopesha nini Serikali ndipo walipoleta mikataba ya kughushi na kukutikana saini za viongozi hao ambazo inaaminika kuwa sio sahihi,” alisema mmoja wa wapasha habari wetu ambae hakutaja jina lake litajwe.

Watuhumiwa hao walitambulika kwa majina ya Said Gamaleldin mwenye paspoti ya Marekani, Yaqoob Sulaiman Al- Mahrouqi raia wa Oman na mwenyeji wao Mtanzania alietambulika kwa jina la Shiraz Haroun Jaffer mkaazi wa Moroko jijini Dar es Salaam.

Alipoulizwa Naibu Mkurugenzi wa makosa ya jinai Zanzibar (DCI), Yussuf Ilembo, juu ya suala hilo alikiri kukamatwa kwa watu hao.


Alisema kwa vile upepelezi bado haujakamilika ni mapema kutoa taarifa za wahusika hao kwa kuepuka kuharibu upelelezi.


“Ni kweli tumewakamata watu watatu wanaosadikiwa kufanya kosa hilo ila kwa sasa bado mapema kutoa taarifa zao kwa kuepuka kuharibu upelelezi, tutapokamilisha upelelezi tutatoa habari zao,” alisema.

Habari kutoka mahakamani zinasema kuwa washtakiwa hao tayari wameshafikishwa mahakama ya mkoa Vuga , chini ya Hakimu George Kazi ambapo walisomewa mashitaka mawili.

Shitaka la kwanza ni la kughushi nyaraka za serikali na la pili ni la kuwasilisha nyaraka za kughushi za serikali kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya fedha kwa lengo la kulipwa euro milioni 200.

Washitakiwa hao wote watatu wamepelekwa rumande hadi Julai 10 ambapo kesi yao itatajwa tena.

Aidha dhamana yao ilikataliwa baada ya upande wa mashtaka uliongozwa na Wanasheria wa Serikali, Walid Mohamed Adam, Mohammed Saleh na Karima Alawi kukataa dhamana kwa madai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Aidha walisema washtakiwa wawili kati ya watatu ni wageni hivyo kupewa dhamana wanaweza kukimbia.

Itakumbukwa katika kikao cha Bajeti cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea hivi sasa Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee, alitoa tahadhari ya kuwa fedha za Serikali hazitolipwa kiholela bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kina.

0 comments:

Post a Comment