Jun 30, 2014

Magdalena Sakaya Apokea Kijiti

KUFUATIA uchaguzi wa Chama cha Wananchi (CUF), kwa ngazi ya kitaifa, uliyomalizika wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, Chama hicho kimemchagua Magdalena Sakaya kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, upande wa Tanzania Bara.

Kabla ya hapo, Cheo cha Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, kwa upande wa Tanzania Bara, kilikuwa kikishikiliwa na Julius Mtatiro.
Aidha, kwa upande wa Zanzibar, Baraza Kuu la CUF, limemchagua waziri wa Biashara wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho. 

Kabla ya mabadiliko haya, cheo hicho kilikuwa kikishikiliwa na Hamad Masoud. 

Akitoa salaam zake maalumu kwa Naibu katibu Mkuu mpya wa CUF, uongozi wa juu wa chama na wanachama wote wa chama hicho, Julius Mtatiro anaeleza kama ifuatavyo:

HONGERA MHE MAGDALENA SAKAYA (MB). ‘I am proud of you’ dada ‪Magdalena Sakaya‬ (MB), NAIBU KATIBU MKUU MPYA, Chama Cha Wananchi CUF – Tanzania Bara.

Wewe pamoja na sekretariati mpya ya chama, nawatakia kila la heri katika majukumu ya kujenga chama chetu. 

Nakuahidi wewe binafsi, viongozi na wanachama wetu wote ushirikiano mkubwa sana wakati wote ambapo mtakuwa mkipambana kukijenga chama.

Jambo moja ambalo ni muhimu, mimi naamini sana katika uwezo wa kina mama. 

Wewe umekuwa mbunge wetu muhimu sana na umeing’arisha CUF ndani na nje ya Bunge.
 
Natumai kuwa utatumia uzoefu wako mkubwa kukilinda na kukijenga chama katika nafasi ya NAIBU KATIBU MKUU BARA ambayo tumekukabidhi leo.

Nitumie fursa hii pia kuwashukuru viongozi wetu wakuu wa chama, Prof. Lipumba, Juma Duni Haji na Maalim Seif Hamad bila kumsahau Makamu Mwenyekiti mstaafu, Mzee Machano Khamis Ali.

Katika nyakati zote tulizofanya kazi pamoja nimejifunza mengi kutoka kwenu, nidhamu ya uongozi, uvumilivu, busara, hekima, mashirikiano na mengine mengi.

Miaka mitatu ambayo nimeongoza ofisi ya Naibu Katibu Mkuu (Bara), nimekuwa mkomavu sana, nimekuwa kiongozi imara na nimechota hekima, busara, uadilifu na nidhamu kutoka kwenu. 

Kupumzika majukumu haya makubwa ni faraja kwangu na kunanipa sasa muda wa kutosha wa kukamilisha shahada yangu ya tatu ya sheria.

Sitasita kuzidi kutumia uzoefu niliopata kuineza CUF na kuhakikisha inaweka mizizi Tanzania Bara.

CUF ni kila kitu kwangu na bado najiona NINA DENI KUBWA katika chama changu, bado leo, kesho na kesho kutwa nitakuwa nafikiria NINI NIKIFANYIE CHAMA CHANGU na siyo CHAMA KINIFANYIE NINI.

Baraza Kuu lililochaguliwa hivi sasa lina uwezo mkubwa sana kuliko lililopita, hili lina wajumbe wengi vijana, wengi wanawake na wazee washauri wachache. Baraza hili litatuvusha vyema chini ya uongozi wenu.

Nitazidi kuwa balozi wa chama changu usiku na mchana. Nimekuwa Mkurugenzi wa kitaifa wa chama nikiwa na miaka 26 na nimekuwa Naibu Katibu Mkuu nikiwa na miaka 28, ni nadra sana vijana kupata fursa kwa umri huo. 

Ni mara chache sana vijana wanaaminiwa kiasi hicho.

Naishukuru sana familia yangu, mke wangu Zakia Hassan na watoto wangu Faustina, Alexander, Elvis na Alma kwa kuwa wavumilivu wakati wote ambapo nilitingwa na majukumu ya kitaifa.

Nawashukuru sana ndugu zangu wote ambao walinipa ushauri muda wote, marafiki na wote wenye mapenzi mema na kila aliyekuwa na mchango muhimu katika utendaji wangu.

Julius Mtatiro,
Naibu Katibu Mkuu Mstaafu,
Chama Cha Wananchi (CUF)
Tanzania Bara.
28/06/2014.

0 comments:

Post a Comment