Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amewatumia salamu za kheri na fanaka Waislamu wa nchi hiyo kwa mnasaba wa kuwadia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Katika ujumbe wake, Rais Kenyatta amesema Ramadhani ni mwezi maalumu kwa Waislamu nchini Kenya na kote duniani ambapo huwa wanajikurubisha kwa Mwenyezi Mungu huku wakiwasaidia wasiojiweza katika jamii na kutoa fursa kwa jamaa na marafiki kukutana.
Rais Kenyatta amesema kwa kuzingatia kuwa Mwezi wa Ramadhani ni wakati ambao Waislamu huonyesha huruma kwa wanadamu wenzao, anatoa wito kwa Waislamu wa Kenya kuiombea nchi hiyo ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi hivi sasa.
Aidha amewataka Wakenya kuuungana pasina kuzingatia misingi ya kikabila na kidini.
Rais Kenyatta pia amewapongeza Waislamu ambao wametoa mchango mkubwa katika ustawi wa Kenya hasa katika kueneza amani.
Halikadhalika amewataka Waislamu kusaidia juhudi za kuimarisha maelewano baina ya wafuasi wa dini mbalimbali nchini Kenya.
Wakati huo huo aghalabu ya Waislamu duniani wametangaza tarehe 29 Juni kuwa tarehe mosi ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
0 comments:
Post a Comment