Jun 28, 2014

Balozi Seif Azitaka Kamati za Misikiti Kuendelea kuwa Imara



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akisisitiza jambo wakati wa hafla ya ufunguzi wa msikiti wa Ijumaa wa Kiboje Mamboleo baada ya kumalizika kwa sala ya ijumaa.
 Balozi Seif akizungumza na waumini wa Dini ya Kiislamu wa Kijiji cha Kiboje Mamboleo mara baada kuufungua msikiti wao wa Ijumaa uliofanyiwa matengenezo makubwa.

Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza Hassanali akielezea mikakati ya kamati ya ujenzi wa misikiti, Madrasa na maskuli nchini ilivyopania kuendeleza malengo yake.
Na Othman Khamis Ame
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amezikumbusha Kamati za Misikiti hapa  nchini kuendelea kuwa imara kwa kutowaruhusu watu wanaopenda kujipenyeza ndani ya kamati hizo kwa nia ya kuanza kutoa madarasa ya uchochezi na kuwagawa waumini kimadhehebu.

Alisema uimara huo ndio njia sahihi itakayoilinda misikiti hiyo na wimbi la vurugu na migogoro ambayo hatiae husababisha mmong’onyoko mkubwa wa  ukosefu wa maadili  katika jamii za kiislamu.

Akiufungua msikiti mpya wa Ijumaa uliofanyiwa matengenezo makubwa katika Kijiji cha Kiboje Mambo leo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema msikiti ni taasisi yenye mchango mkubwa wa kuutangaza ukweli dhidi ya unafiki pamoja na mambo ya kheri kwa jamii ya Kiislamu.

Balozi Seif alisema katika kuihuisha nyumba ya Mwenyezi Muungu  Msikiti ni vyema kwa waumini hao mbali ya kutekeleza vipindi vya sala lakini pia ni vyema wakaendeleza madarasa hasa kipindi hichi kinachokaribia cha  mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kujifunza masuala ya dini yao.

Alisema waumini wa dini ya  Kiislamu wanaotekeleza ibada zao na kusimamisha sala katika vipindi vitano kwa siku hupata baraka na neema ya kuwa wageni wa mola wao aliyewaumba.

“ Nani miongoni mwetu hataki kuwa mgeni wa mola wake mara tano ? Kama jawabu ni ndio basi tuhakikishe tunaswali mara tano kama tulivyoamrishwa na mola wetu. Na zile Baraza la manzese zisiwepo tena hapa mtaani penu“. Alisisitiza Balozi Seif.   

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi wananchi wa maeneo hayo hasa vijana kuachana na maasi ya unywaji pombe kiholela ambayo huchangia vitendo vya wizi wa mazao na mifugo katika maeneo mbali mbali nchini.

0 comments:

Post a Comment