Dec 19, 2013

12 mahakamani kwa ukeketaji

Watuhumiwa wa ukeketaji wakiwamahakamani,Same,Tanzania.

Wanawake 12 ambao ni wazazi wa wasichana 21 waliofanyiwa ukeketaji wilayani Same, mkoa wa Kilimanjaro, kaskazini mwa Tanzania, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Same, wakati waliposomewa mashitaka yao kwa mara ya kwanza tangu wakamatwe mwishoni mwa wiki iliyopita.

Watuhumiwa wote wanashitakiwa kwa kosa la Ukatili dhidi ya watoto na kuwasababisha maumivu makali, shitaka ambalo wote wamekana.
Tisa kati ya watuhumiwa hao 12 wameachiliwa kwa dhamana, huku watatu wakibaki mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni shilingi milioni mbili za Tanzania, sawa na dola 1250 za Kimarekani.

Miongoni mwa washitakiwa, mmoja alikabiliwa na mashitaka mawili, moja akiwa mzazi wa mmoja wa wasichana waliokeketwa na pia akiwa ngariba.

Kutokana na mila na desturi ya baadhi ya makabila nchini Tanzania, ukeketaji unafanyika japo ni kinyume cha sheria, huku watu wanaokamatwa kuhusika na ukeketaji wakichukuliwa hatua za kisheria.

Kama watapatikana na hatia, wanawake hao wanakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka mitano jela au kutozwa faini kubwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 30 Desemba 2013, wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.

0 comments:

Post a Comment