Oct 21, 2013

PAC Ipuuzwe-CUF

  Wiki iliyopita, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe alisema licha ya kuwa vimepokea ruzuku ya jumla ya Sh67.7 bilioni kwa vyama tisa vya siasa tangu mwaka 2009, vyama vyote vinavyopata ruzuku ya Serikali havijawahi kupeleka ripoti yoyote ya ukaguzi wa fedha kwa CAG.
 
Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kinakusudia kumwandikia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda kikimwomba azielekeze kamati mbalimbali za Bunge jinsi ya kufanya kazi zao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema chama chake kimesikitishwa na taarifa zilizotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
“Chama chetu kinatafakari hatua za kuchukua ikiwemo kumwandikia Spika ili azifundishe kamati zake namna bora ya kufanya kazi zake kama kamati za umma. 

Tumesikitishwa na kauli tulizozisikia kupitia vyombo vya habari kuwa, chama chetu ni miongoni mwa vyama kadhaa ambavyo havijawasilisha hesabu kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha miaka minne sasa. 

Tunaomba Watanzania wazipuuze taarifa hizo kutuhusu kwa sababu hazina ukweli wowote,” alisema Mtatiro.
Wiki iliyopita, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe alisema licha ya kuwa vimepokea ruzuku ya jumla ya Sh67.7 bilioni kwa vyama tisa vya siasa tangu mwaka 2009, vyama vyote vinavyopata ruzuku ya Serikali havijawahi kupeleka ripoti yoyote ya ukaguzi wa fedha kwa CAG.
Kamati hiyo vilevile ilitangaza kusitishwa mara moja utoaji wa ruzuku kwa vyama vyote vya siasa nchini mpaka hapo hesabu zake zitakapokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Mtatiro alisema CUF kimesikitishwa na kufadhaishwa na hatua ya kamati kuvihukumu vyama vyote vya siasa wakati jambo hili ni la chama kimoja kimoja.
“Mbaya zaidi ni pale ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya PAC,  Zitto amekuwa akishinda kwenye mitandao ya kijamii akishupalia kuvichukulia hatua vyama – kikiwemo chama chetu, huku akiwa hana taarifa za kina za namna tulivyotekeleza wajibu wetu,” alisema.
Alisema ni jambo la kufedhehesha kwa kamati ya Bunge kushinda kwenye mitandao ya kijamii ikihukumu na kutoa taarifa za uongo kwa umma bila hata kuwasiliana na vyama vya siasa na kumwomba Spika azipe mwongozo kamati hizo.

0 comments:

Post a Comment