- ALIKUWA NA WENZAKE
- WAPORA MAMILIONI
Kashfa zinazidi kulisakama JESHI la Polisi baada ya Jeshi hilo Mkoa wa Ilala, kuwashikilia watu wanne akiwemo
askari wake mmoja kwa tuhuma za kufanya ujambazi kwa kutumia silaha (bastola)
na kupora dola za Marekani 20,000, sawa na sh. milioni 32 za Tanzania.
Askari huyo amefahamika kwa jina la
Mohamed Mhina ambaye kituo chake cha kazi ni Oysterbay, Mkoa wa Kipolisi
Kinondoni, ambaye akiwa na wenzake wanne, walikwenda kufanya uhalifu nyumbani
kwa mkazi mmoja wa eneo la Klabu ya Wazee,iliyopo Bungoni, Ilala, Dar es Salaam.
Kuna taarifa ya kwamba askari huyo alihamishiwa kituoni hapo akitokea Kituo cha Polisi
Kimara,ambapo katika uhamisho wake alikuwa bado hajaanza kuutekeleza kwa sababu
alikuwa likizo.Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana baada ya askari huyo
na mwenzake, kupata taarifa kuwa kuna mtu ambaye si raia wa Tanzania aliyekuwa
na fedha; hivyo walikwenda kumvamia nyumbani kwake ili wazichukue.
Watuhumiwa hao walifanikiwa kuingia
nyumbani kwa mtu huyo, kumtaka awape fedha alizonazo na kupewa dola za Marekani
20,000 baada ya kumtisha kwa bastola.Wakati wakijiandaa kutoka nje ya nyumba
hiyo, rafiki za mtu aliyevamiwa na kuporwa fedha hizo walifungua geti, kuingia
ndani na kukuta hali tofauti; hivyo baada ya kuuliza kuna nini, aliyeporwa
fedha hizo baada ya kusikia sauti za rafiki zake aliitika kwa sauti “nimevamiwa
na majambazi”.
Wakati huo, askari huyo na wenzake walijificha nje ya nyumba hiyo
na baada ya kusikia sauti hiyo, aliyekuwa na fedha hizo ambaye pia ndiye
aliyekuwa ameshika bastola, aliruka ukuta na kutokomea kusikojulikana akiwaacha
wenzake.Rafiki wa mtu aliyeporwa fedha hizo, walipambana na askari huyo pamoja
na wenzake watatu ambao walichelewa kuruka ukuta na kufanikiwa kuwakamata.
Watuhumiwa hao wamefikishwa katika Kituo cha Polisi Msimbazi
ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alithibitisha
kukamatwa kwa askari huyo na kusema taarifa zaidi juu ya tukio hilo atazitoa leo.Naye Kamanda wa Mkoa wa
Kipolisi Kinondoni, Camilus Wambura, amekiri kuwa askari huyo alihamishiwa
kituoni kwake, lakini amekamatwa kwa ujambazi.
Majina ya watuhumiwa wengine pamoja na nile la mtu aliyeporwa
fedha hizo, hayakuweza kufahamika mara moja.Taarifa za uhakika kutoka kwa
baadhi ya askari, zinasema mama mzazi wa askari huyo anafanya kazi ofisi moja
na kigogo wa jeshi hilo
Makao Makuu ya Polisi.