Mkazi wa Zanzibar, Pili Hija akiwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar
es Salaam jana na watoto wake walioungana.
- “Kuna pacha ambao wanakuwa kwenye mifuko tofauti na wengine wanakuwa kwenye mfuko mmoja, hawa wanaokuwa kwenye mfuko mmoja ndio mara nyingi wanashindwa kuachiana na hivyo wanazaliwa wakiwa wameungana.”Dk Edna Majaliwa, Msimamizi Wodi ya Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili
Mtoto
huyo ambaye hana kichwa anapumua pia akiguswa anapata hisia na kutingisha mguu
mmoja.
Dar es Salaam.
Mkazi wa Jang’ombe Visiwani Zanzibar, Pili Hija (24), amejifungua watoto
walioungana huku mmoja akiwa hana kichwa.
Watoto hao ambao wapo Wodi namba 36 katika Jengo la Wazazi la Hospitali ya
Taifa Muhimbili mbali na kuzaliwa mmoja akiwa hana kichwa, wameungana sehemu ya
uti wa mgongo, mkono mmoja na wanatumia njia moja ya haja kubwa.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, mama wa watoto hao, alisema:
“Nilijifungulia nyumbani, nilisikia uchungu mara moja na hapo hapo nikajifungua
kwa njia ya kawaida na jirani yangu ndiye aliyenisaidia,”alisema na kuongeza:
“Nilijifungua saa moja asubuhi, nilijua nitazaa pacha kwa kuwa
nilishafanya kipimo katika Hospitali ya Makunduchi, wakaniambia nitajifungua
pacha lakini mmoja si binadamu ni kiwiliwili.
“Nimeolewa, mume wangu ni mwanajeshi, nina watoto wengine wawili mmoja wa
kike na mwingine wa kiume, mume wangu hajui tukio hili kwani yupo kambini Zanzibar na hatuna
mawasiliano yoyote kwa sasa,” alisema.
Daktari wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Zaituni
Bokhary alisema; “Hii ni mara ya kwanza kwa jambo hili kutokea katika miaka ya
hivi karibuni. Mara ya mwisho lilitokea mwaka 1984.
“Tulikuwa tufanye upasuaji leo lakini tumeahirisha na utafanyika Alhamisi
(kesho) asubuhi katika Kitengo cha Mifupa cha Muhimbili (Moi).”
Msimamizi wa Wodi ya Watoto walikolazwa, Dk Edna Majaliwa alisema:
“Hakuna sababu maalumu kitaalamu inayosababisha watoto kuungana, mara
nyingi zinapokutana mbegu za X na Y na kutengeneza mimba kunakuwa na hatua za
ukuaji wiki nne, wiki nane, wiki 12, 16 na kuendelea.