Aug 11, 2013

KATIKA KUSHEHEREKEA IDDIL FITRI MASHEIKH NA MAIMAMU WA MISIKITI MINNE WACHUANA VIKALI.


  • MUHAJIRINA YAICHABANGA ANSWAAR MAGOLI MAWILI.
Na mwandishi wetu wa munirablog.
Ilikuwa ni burdani ya aina yake pale timu mbili zilipochuana vikali katika mechi ya kirafika ya kusheherekea sikukuu ya iddil fitr iliyofanyika jana katika uwanja wa barafu uliopo katika shule ya msingi magomeni.

Timu hizo ziliundwa na masheikh,maimamu na maustadhi wa misikiti na madrasa zilizopo magomeni makuti iliyojipa jina la MUHAJIRINA FOOTBAL CLUB dhid ya masheikh,maimamu na maustaadh wa madrasa na misikiti ya magomeni mapipa waliojiita ANSWAAR FOOTBAL CLUB.


Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Butembo hadi mapumziko timu hizo zilikuwa suluu licha ya timu ya ANSWAAR kulisakama mara kwa mara lango la MUHAJIRINA lakini uimara wa beki wa kati Said Bopo na mlinda mlango Idd Azzan (Mbunge) ulikuwa ni kikwazo cha kupata goli.

kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa huku Imamu wa Masjid Uhud Sheikh Ramadhan akionekana kuwa ni mwiba mkali dhidi ya timu ya MUHAJIRIIN.

Dakika ya tisa ya kipindi cha pili imamu msaidizi wa Masjid Tawwab Ustaadh Muhamad Idrisa aliwainuwa mashabiki kwa kufunga goli baada ya kuwaburuza walinzi wa timu ya ANSWAAR ambao walikuwa wana msindikiza.

Kuingia kwa goli hilo kuliifanya timu ya MUHAJIRINA kuongeza kasi ya mashambulizi huku wakiwatumia washambuliaji wake wa  pembeni Ustaadh Abdu shakur Fadhil (imamu mkuu masjid Tawwab) aliyecheza winga ya kushoto na ustaadh Juma Rashid (mwalimu wa madrasat muniira) ambaye alicheza namba saba na kusababisha kupatikana kwa goli la pili kupitia kwa Khalid Said aliyecheza nafasi ya mshambuliaji wa kati.

Hadi mwisho wa mchezo timu ya Muhajiriin ilitoka uwanjani kifua mbele kwa ushindi wa goli mbili kwa bila.

Baada ya mchezo huo uliovuta hisia za wengi,waumini mbalimbali walitoa maoni yao hasa wakisifia uwezo wa masheikh,maimau na maustaadh katika kusakata kabumbu.

"Kwa hakika tumefurahi kwani hii ilikua ni burdani ya aina yake,dhana ya wengi ni kwamba masheikh na maustaadh ni mamwinyi lakini hali umeona mwenyewe namna imamu wa masjid uhudi (Ustaadh Ramadhan) licha ya unene na kitambi alicho nacho alivyoweza kuichachafya ngome ya MUHAJIRINA,wamshukuru goli kipa wao mbunge Idd Azzan ambaye alidaka na kupangua mashuti yake,lakini pia hatukuamini kama Imamu wa masjid Tawwab (Ustaadh Abdul shakur) anauweza mpira lakini kamudu mwanzo mwisho hata Ustaadh Juma Rashid (munira madrasa) anaonekana ni hodari sana kwani aliisumbua beki ya pembeni kiasi cha kuchezewa rafu mara kwa mara,kwa kweli tumefurahi.alisema shabiki mmoja bila kutaja jina lake.

katika hatua nyengine kumekuwa na michezo mbalimbali inaendelea katika uwanja huo huku mchezo wa bembea ukionekana kuwavutia watoto wengi.



 HII NDIYO TIMU YA ANSWAAR CHINI YA NAHODHA USTAADH AHMAD MCHENI (WA TATU KUTOKA KUSHOTO WALIOSIMAMA) IMAMU WA MASJID HAQIIR.

 NA HIKI NI KIKOSI CHA MUHAJIRIIN CHINI YA KOCHA WAO IDD MOSHI (MNYAMWEZI) MWENYE FULANA YENYE MISTARI MEUSI,AMBACHO KILIIBAMIZA TIMU YA ANSWAAR MAGOLI MAWILI KWA BILA

 WATOTO WAKIBEMBEA