Maelfu ya watoto wanaofanya kazi katika machimbo ya madini
nchini Tanzania
wanakabiliwa na tishio kubwa la kupata magonjwa na hatimaye kufa.
Shirika la kutetea haki za kibinadam la Human Rights Watch, limefichua
ushahidi zaidi kuhusu unyanyazaji wa watoto nchini Tanzania, baadhi yao wenye
umri wa miaka minane ambao wanafanya kazi kwa zamu, katika migodi ya madini
iliyoko chini ya ardhi, kwa saa ishirini na nne.
Shirika hilo
limesema watoto hao wanakabiliwa na tishio la kuvuta hewa ya sumu inayotokana
na uchimbaji wa madini ya dhahabu na wakati mwingine kuuawa wakati migodi hiyo,
inapoporomoka nyingi zikiwa hazina leseni.
Tanzania ina sheria kali
inayozuia watoto kufanya kazi katika machimbo ya madini lakini shirika hilo limesema, serikali
ya rais Jakaya Kikwete ni sharti iimarishe juhudi zake za kuhakikisha sheria
hizo zimetekelezwa.
Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch limechapisha
ripoti inayoelezea mazingira magumu wanayokumbana nayo watoto wanaojiingiza kwenye
ajira ya uchimbaji madini nchini Tanzania, wengi wao wakiathirika
kiafya.
Ikiwa na kichwa cha habari kisemacho "Ajira ya Watoto katika
Migodi", ripoti hiyo imefichua vitendo vya dhuluma na ukatili wanaokutana
nao watoto wao ambao baadhi yao
wako hatarini kuangukia kwenye matatizo ya kiafya ikiwemo mtindio wa ubungo
kutokana na kemikali zinazokutikana kwenye machimbo hayo.
Ripoti hiyo iliyotangazwa leo jijini Dar es salaam inafuatia utafiti
uliofanyika katika maeneo ya machimbo ambako watoto wengi wameajiriwa.
Maafisa wa Human Rights Watch wamesema kuwa pamoja na kutumika katika kazi
ngumu ya utafutaji madini, lakini baadhi ya watoto hao wanalazimika kutumika
katika biashara za kingono na kukubwa na matukio ya unyanyasaji wa kijinsia.
Ripoti hiyo ambayo pia imeangazia athari zitokanazo na matumizi ya madini ya
zebaki kwenye machimbo hayo, imesema kuwa baadhi ya kampuni binafsi na vikundi
vya watu huwatumia watoto hao kusaka madini jambo ambalo linakwenda kinyume na
sheria za kimataifa.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mtafiti mkuu wa Human Watch, Jenina Morna, alisema
kuwa idadi kubwa ya watoto hao hufanya kazi kwenye mazingira magumu na wakati
mwingine hulazimika kuingia kwenye mapango yaliyoko chini kwa chini kwa ajili
ya kusaka madini.
"Watoto hufanya kazi katika migodi yenye kina kirefu mno, watoto hawa
husafirisha mizigo mizito ya dhahabu, na wakati mwingine hutumia vifaa
hararishi kusaka madini kama vile mawe."
Alisema Morna.
Moja ya sababu kubwa inayowasuma watoto wengi kuingia kwenye migodi ni hali
ya kipato duni iliyopo kwenye familia nyingi, kama
inavyothibitika katika makala fupi iliyoandaliwa na Human Watch ikionyesha kina
mama na watoto wakihangaika na maisha.
Kwa sasa Tanzania ni nchi
ya tatu barani Afrika kwa kuzalisha kwa wingi madini ya dhahabu, ikizidiwa na
nchi za Afrika ya Kusini na Ghana.