Mar 5, 2015

Mvua yaua watu 42 Kahama, 91 wajeruhiwa

 
Mkazi wa Kijiji cha Mwakata akizungumza na simu alipokuwa akitoa taarifa kwa jamaa zake baada ya nyumba yake kubomoka kutokana na mvua ya mawe iliyonyesha kijijini hapo wilayani Kahama. 

Mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha juzi usiku imesababisha maafa katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambako zaidi ya watu 42 wameuawa, wakiwamo saba wa familia moja na wengine 91 kujeruhiwa vibaya.
 
Mvua hiyo ya aina yake ilisababisha nyumba 160 kuanguka na nyingine kuezuliwa paa kutokana na upepo mkali na watu wengine 900 wameripotiwa kukosa makazi.
Watu wengi walifariki kutokana na kuangukiwa na kuta za udongo za nyumba za wanakijiji hao na wengine kuuawa kutokana na kuangukiwa na mawe makubwa ya barafu wakati walipokuwa wakijaribu kutafuta hifadhi baada ya mapaa kutobolewa.
Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia gazeti hili kuwa mawe makubwa ya barafu yalikuwa yakidondoka usiku na kuvunja nyumba za wakazi wa kijiji hicho ambazo nyingi ni za udongo.
Waokoaji walilazimika kufumua mabati yaliyoanguka na kufukua vifusi kwa ajili ya kutoa miili ya watu waliofariki na kuokoa walionusurika na baadaye kuwapakia kwenye malori ili kuwapeleka hospitalini.
“Mimi tangu nianze uongozi wa umma sijawahi kukutana na tukio la aina hii,” alisema Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya.
“Nashindwa kulizungumzia (suala hili). 

Hili ni tukio kubwa ambalo limepoteza uhai wa maisha ya watu hivyo nashindwa nianzie wapi lakini kifupi wananchi wa Mwakata wamekumbwa na msiba mzito,” alisema Mpesya, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ezekiel Sanane alisema wakati mvua hiyo inanyesha ilikuwa na upepo mkali na mawe makubwa ambayo yalikuwa yakitoboa nyumba na kutumbukia ndani na kuponda watu, hali ambayo iliwafanya wengine kukimbilia nje ambako pia walipigwa na mawe ya barafu na kufariki.
Sanane alisema wapo wengine walifunikwa kabisa na ukuta wa nyumba na kufariki, lakini wengine wamekufa wakiwa nje ya nyumba zao.
Hata hivyo mkazi wa kijiji hicho, Paulina Nyalulu alisema alinusurika kifo baada ya kukimbilia barabarani. Alisema baada ya kuona nyumba imejaa maji, yeye na familia yake walikimbilia barabarani ambako walishuhudia nyumba zao zikianguka, ingawa hakuna mtu aliyekufa.
“Tunamshukuru Mungu hakuna aliyekufa kwenye familia hii lakini kama unavyoona vitu vyote, vikiwemo vyombo pamoja na vyakula vimezolewa vyote maana maji yalijaa nyumba yote na sisi tulikimbia na ndiyo ilikuwa usalama wetu,” alisema Nyalulu.
Taarifa za awali zilizotolewa na kamanda wa polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Jastus Kamugisha zilieleza kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka kutokana na kazi ya kufukua miili kutoka kwenye vifusi vya nyumba kuendelea hadi jana mchana.

0 comments:

Post a Comment