Nov 14, 2014

Uamsho kutaka mamlaka kamili ya Zanzibar si ugaidi ni haki yakila Mzanzibar.

pope-resigns-reax


Habari kubwa wiki hii imekuwa ni ile ya Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu kwa ufupi na kwa umaarufu zaidi UAMSHO. 

Viongozi wa Serikali ya Zanzibar na wale wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wamekuwa wakiitaja hadharani.

Makamo wa Rais Dk. Muhammed Gharib Bilali ameitaja kuwa ni hatari na kufika hata kuiweka kundi moja na Al Qaida, Al Shabab; Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd ametoa agizo kuwa bendera zake zipachuliwe na Rais wa Zanzibar Dk Ali Muhammed Shein amesema kuwa yeye hapaswi kulaumiwa kwa kuchukuliwa viongozi wa UAMSHO kushtakiwa Dar es Salaam kwa hoja kuwa hata viongozi wa Kiafrika hupelekwa The Hague kushtakiwa.

Kwa wasiojua basi UAMSHO ni jumuia halali iliyosajiliwa Zanzibar na mpaka leo hivi kadri ninavyojua usajili wake bado upo na kwa hivyo wallahi inanishangaza mno kauli na vitendo dhidi yake vinavyofanywa na Serikali, ilhali ikibakisha uhalali wake
.
UAMSHO ilipata kusikika zaidi baada ya kujitokeza kupinga muundo wa Muungano wa Tanzania, kiongozi wake Farid Hadi kuichana Rasimu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mbele ya Samuel Sitta na Samia Suluhu na pia vurugu ya wiki moja iliyotokea mwezi Oktoba, 2012.


Jumuia hiyo imehusishwa na matukio kadhaa yanayotajwa kuwa ni ya ugaidi kama vile kuchomwa sehemu za kuabudia za Wakristo, miripuko ya mabomu, mashambulizi ya tindi kali dhidi ya wageni na viongozi wa Kiislamu na na kushambuliwa viogozi wa Kikristo kwa tindi kali na risasi kama yule padre aliyeuliwa.

Hadi sasa kwa upande wa Zanzibar hakuna hata kesi moja ya UAMSHO ilowatia hatiani washitakiwa wake na kwa kiasi kikubwa kwa kweli kesi hizo zipo zipo tu Mahakamani, yaani zimedorora. Kwa kuwa bado zimo mchakatoni tunajizuia kutoa maoni yoyote ili tusikhalif sheria.



Lakini kwa miezi minne iliyopita viongozi kadhaa wa UAMSHO wamekuwa wakichukuliwa kushtakiwa kwa makosa ya ugaidi na inaelekea kwa vitendo vilivyotokea Zanzibar na vile vya Tanzania Bara kwa kuunganishwa na washtakiwa wengine na wanasheria kadhaa wa Zanzibar pamoja na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Othman Masoud wamesema ni kinyume cha sheria.
Pia kumekuwa na madai makubwa ya utesaji yanaendelea katika sehemu wanazoshikiliwa washtakiwa hao lakini si Serikali ya Tanzania, Serikali ya Zanzibar, si taasisi za haki za binaadamu na wala si ofisi za kibalozi zilizotoa katazo au kemeo la vitendo hivyo vya utesaji, ambavyo vinakiuka haki za wafungwa au watu wanaozuiliwa rasmi.
Makala hii haikusudii kuhoji nafasi ya Serikali kulinda raia wake na kuhakikisha kuwa usalama upo kwa raia, wageni na mali zao, lakini hatujizuwii wala tusizuiliwe kuhoji juu ya namna hatua hizo zinavyochukuliwa, migongano katika kauli za viongozi na pia maamuzi yanayofanywa ambayo hayana tija.
Kauli ya Dr Bilal kwa kweli inatisha na inatufanya wengine tuamini kuwa yeye kama kiongozi wa kitaifa ana taarifa za kutosha za kuweza kufananisha UAMSHO na makudi makubwa na sugu ya kigaidi. Na ndipo ninapojiuliza iwapo hali imefikia hivyo ni kwa nini usajili wa UAMSHO usifutwe tukaelewa kuwa haipo tena kisheria? Na kama hali haipo hivyo jee huku si kuiweka Tanzania pabaya kwenye macho ya dunia?
Viongozi wa Zanzibar hivi karibuni walitoa amri ya kupachua bendera za UAMSHO huko Mkoa wa Kaskazini, Unguja ambako ndiko zilikotanda na kukubalika sana. Siku chache baada ya kauli ya Balozi Seif Ali Idd ndipo Mkuu wa Mkoa Juma Kassim Tindwa akaendesha operesheni ya kuzipachua bendera za UAMSHO, tabaan kwa kutumia vyombo vya ulinzi.
Ingawa hilo si ajabu kwa Zanzibar, baada bendera za CUF zilikuwa zikipachuliwa kwa staili hiyo hiyo, lakini mtu aweza kujiuliza uhalali wa hatua ya SMZ dhidi ya taasisi ambayo bado ina usajili halali wa kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kueneza fikra zake na kutumia nembo na alama zake na UAMSHO ikiwa pia huko nyuma kupatiwa hata kibali cha kuwa Muangalizi wa Uchaguzi.

Kuna busara yoyote kuzipachua bendera hizo kwa nguvu? SMZ inadhani kuzipachua bendera hizo kutazuia kuungwa mkono UAMSHO? Jee kupachua bendera hizo kutazuia kazi ya kuhamasisha watu kuujuburi muundo wa Muungano ambao wanaona haona faida na Zanzibar? Na jee kutawafanya wananchi waichukukie na kuitosa jumuia hiyo?
Na kauli ya Dk Shein huko Pemba kuwa yeye asilaumiwe kwa kunyakuliwa viongozi wa UAMSHO na kushtakiwa Bara itasaidiaje katika suala hili? Itawasaidia kuwatoa watu kwenye mahaba ya UAMSHO na kuwakurubisha kwa Serikali? Itawaondosha imani yao kwa viongozi wao wa kidini? Itamfutia lawama Dk Shein hasa kwa jinsi watu wanavyosikia viongozi wao wakiteshwa na kukashifiwa?
Jee kauli na vitendo vya kuitenga UAMSHO havitakuwa na athari ya kuisukuma kwenda mafichoni na kufanya kazi chini kwa chini? Bila ya kutoa maoni kuhusu mashtaka yalio mahakamani, ni imani ya watu wengi kuwa viongozi wa UAMSHO wako mashitakani zaidi kwa sababu ya misimamo yao ya kuukataa Muungano, na wanaoamini hivyo huna vya kuwabadilisha.

Fikra zangu suala hili linataka umakini zaidi maana binaadamu husukumwa kuenda katika mawazo hasi kadri anavyotendewa visivyo, kukosa haki, kukosa nafasi na kukosa sauti. Bado tuna wakati wa kutafakari kwa sababu ukweli ni kuwa UAMSHO iko katika nyoyo za Wazanzibari wengi.

0 comments:

Post a Comment