Nov 14, 2014

Saudia kubomoa sehemu alipozaliwa Mtume SAW


Waislamu duniani wameelezea wasi wasi wao kuhusu mpango tata wa utawala wa Saudi Arabia wa kubomoa sehemu alimozaliwa Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad SAW katika mji mtakatifu wa Makka.
Kwa mujibu wa Wakfu wa Utafiti wa Turathi za Kiislamu, Nyumba ya Mawlid, sehemu alimozaliwa Mtume Muhammad SAW inapangwa kubomolewa hadi kufika mwisho wa mwaka huu na sehemu yake kujengwa kasri ya kifalme kwa ajili ya Mfalme wa Saudia Abdullah ibn Abdulaziz anapotembelea Makka.

Kwa mujibu wa Irfan Alawi, mkurugenzi mtendaji wa Wakfu wa Utafiti wa Turathi za Kiislamu, mwenye makao London, sehemu alimozaliwa Mtume inakabiliwa na tishio la kusahauliwa. 

Ameongeza kuwa, "Sasa baada ya kumalizika msimu wa Hija, ujenzi unaendelea kwa masaa 24 kila siku. 

Wamemaliza upanuzi wa sehemu moja ya Masjidul Haram. Kasri la kifalme litakuwa mara tano kubwa zaidi ya kasri lililopo hivi sasa." 

Wiki iliyopita pia wakuu wa Saudi Arabia walibomoa nguzo za kihistoria ambazo zilikuwa kumbukumbu ya mahali Mtume Muhammad SAW alipoanzia safari ya Israa na Miiraj ya kupaa kuelekea mbinguni. 

Hivi karibuni pia kulifichuliwa mpango unaoandaliwa na Saudi Arabia wa kubomoa kaburi la Mtume Muhammad SAW lililoko Masjid al-Nabawi mjini Madina. 

Ikumbukwe kuwa takribani miaka 90 iliyopita, Mawahabi wa Saudi Arabia walibomoa makaburi ya Ahlul Bait wa Mtume SAW ambayo yako Baqii, katika mji mtakatifu wa Madina. 

Saudi Arabia inakosolewa vikali kwa kubomoa mamia ya maeneo ya kihistoria ya Kiislamu kwa kisingizio cha kupanua maeneo ya ibada Makka na Madina.

0 comments:

Post a Comment