Nov 14, 2014

Balozi za Misri,UAE zashambuliwa huko Tripoli


Balozi za Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika mji mkuu wa Libya Tripoli leo zimeshambuliwa kwa mabomu yaliyotegwa kwenye magari lakini hakuna taarifa yoyote kuhusu vifo au majeruhi katika mashambulizi hayo.

Mlipuko wa kwanza wa bomu la gari ulitokea kwenye ubalozi wa Misri nchini Libya ulioko kwenye eneo la Al-Dahra, na kuharibu jengo mbele ya ubalozi huo na nyumba zilizoko karibu na ubalozi huo. 

Mlipuko mwingine ulitokea kwenye ofisi za jengo la ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu na kusababisha uharibifu mdogo.

 Mabalozi wa nchi hizo mbili nchini Libya waliondoka Libya miezi kadhaa iliyopita kutokana na kuongezeka machafuko na mapigano nchini humo.

Kwa miezi kadhaa sasa Libya inashuhudia machafuko na mapigano kati ya makundi yenye silaha na vikosi vya usalama ambayo yamepelekea mamia ya watu kuuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.

0 comments:

Post a Comment