Nov 18, 2014

Maalim Seif awahimiza wana-CUF kujiandikisha

Maalim Seif
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad (pichani), amewahimiza wanachama na wapenzi wa chama hicho kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura na wajiandae kuwachagua wagombea watakaosimamishwa na Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika uchaguzi wa serikali za mitaa Desemba 14, mwaka huu.

Maalim Seif alitoa wito huo katika mikutano yake ya hadhara akiwa katika ziara ya kutembelea uhai wa chama, kuzindua ofisi mpya za mitaa, vijiji na kata katika majimbo ya Temeke, Ukonga na Kinondoni jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.

Alisema uchaguzi wa serikali za mitaa ambao zoezi la uandikishaji wapiga kura litaanza Novemba 23, mwaka huu ndiyo wakati muafaka kwa vyama vinavyounda Ukawa kukipa salamu CCM kijiandae kukaa pembeni katika uchaguzi mkuu wa mwakani kwa sababu kimeshindwa kutimiza ndoto za Watanzania na kuondoa shida zao.

Maalim Seif alisema Tanzania inahitaji mabadiliko na kwamba wakati wa mabadiliko umefika, hasa baada ya vyama vinne vinavyounda Ukawa kuamua kuunga nguvu zao kwa pamoja katika masuala ya Katiba mpya na uchaguzi kwa dhamira ya kukiondoa madarakani CCM na kuwatumikia wananchi inavyostahili.

Hata hivyo, Maalim Seif alisema dhamira hiyo itaweza kufanikiwa pale wanachama wa CUF na wananchi wote watakapojitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura ili waweze kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

“Uzoefu wetu katika mfumo huu wa vyama vingi unaonyesha wapinzani tukiingia kwenye uchaguzi mmoja mmoja tunagawana kura ambazo ukizijumuisha tunaiangusha CCM,” alisema Katibu Mkuu huyo wa CUF.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwembeyanga, Jimbo la Temeke, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema CCM hivi sasa wamekumbwa na hofu kubwa kutokana na uamuzi wa vyama hivyo vinne kuwa na umoja katika suala la wagombea.

0 comments:

Post a Comment