Oct 2, 2014

OIC yasisitiza kukabiliana na 'Kuogopwa Uislamu'

OIC katika moja ya mikutano yake  
OIC katika moja ya mikutano yake
Mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC wamesisitiza udharura wa kukabiliana na njama za kutaka Uislamu uogopwe.
Wakizungumza kwenye mkutano wa kila mwaka pambizoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje wanachama wa OIC wameitaka jamii ya kimataifa kukomesha vitendo vya kichochezi na uchokozi dhidi ya Waislamu.
 Taarifa inasema kuwa, juhudi zaidi zinapasa kufanyika kwa lengo la kuimarisha vigezo vya kuishi pamoja sambamba licha ya kuwepo utamaduni unaotofautiana. 

Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC wamesisitiza kwamba, umma wa Kiislamu unapasa kuipatia kipaumbele kadhia ya Palestina na Quds Tukufu na kuzitaka nchi zote wanachama kuiunga mkono serikali na wananchi wa Palestina ili waweze kufikia malengo yao likiwemo suala la kuundwa nchi huru na mji mkuu wake ukiwa Quds Tukufu. 

Mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje wanachama wa OIC wamelaani kiburi cha utawala wa Kizayuni wa Israel cha kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds. 

Taarifa ya OIC imeeleza kuwa, ugaidi ni hatari na wala haufungamani na nchi, dini wala utaifa na kusisitiza kwamba nchi za Kiislamu na Waislamu wamekuwa wahanga wakubwa wa ugaidi.

0 comments:

Post a Comment