Oct 1, 2014

Mahakama Misri yawafunga jela wafuasi 68 wa Mursi

Mahakama ya Misri imewahukumu watu 68 kifungo cha hadi miaka 15 jela kwa ajili ya kuandamana na kumuunga mkono rais aliyeondolewa madarakani nchini humo na jeshi Muhammad Mursi.  
Watu hao walikuwa wakituhumiwa kushiriki katika mandamano Oktoba mwaka uliopita ambapo zaidi ya waandamanaji 50 walipigwa risasi na kufa mjini Cairo wakati wa makabiliano na polisi. 

Hukumu hiyo ya pamoja ni ya hivi karibuni zaidi kutolewa dhidi ya wafuasi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin nchini humo.  

Duru za mahakama zimeripoti kuwa, watuhumiwa 63 miongoni mwao wamehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela na watano kifungo cha miaka 10.

Polisi ya Misri imekuwa ikiwakandamiza vikali wafuasi wa rais Muhammad Mursi tangu alipopinduliwa na jeshi Julai mwaka uliopita wa 2013, ambapo maelfu wameuawa katika machafuko na wengine wengi kutiwa mbaroni.

0 comments:

Post a Comment