Sep 22, 2014

Waziri Mkuu wa Yemen ajiuzulu

Waziri Mkuu wa Yemen ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huo baada ya kushadidi mgogoro wa kisiasa nchini humo. 

Muhammad AbdulSalaam Msemaji wa Harakati ya Ansarullah amesema kuwa, Muhammad Salim Basindawa  Waziri Mkuu wa Yemen ameshakabidhi barua ya kujiuzulu kwa Rais Abd Rabbu Mansour Hadi wa nchi hiyo.
AbdulSalaam ameongeza kuwa, wanamgambo wa Ansarullah wanadhibiti makao ya makuu ya majeshi, majengo ya redio  ya taifa na ofisi za Waziri Mkuu nchini humo. 

Imeelezwa kuwa, kujiuzulu Muhammad Basindawa Waziri Mkuu wa Yemen ilikuwa  moja ya matakwa ya wapinzani nchini humo, ambao wanafanya maandamano kila siku kwa wiki kadhaa sasa. 

Wapinzani wa serikali wanataka yatekelezwe makubaliano ya mazungumzo ya kitaifa na kufutwa mpango wa kuongezwa bei ya mafuta nchini humo. 

Wakati huohuo, Rais wa Yemen ametia saini makubaliano ya amani na wanaharakati wa al Houthi, mbele ya Jamal bin Omar Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen. 

Fares as Saqqaf Makamu wa Rais wa Yemen amesema kuwa, wanaharakati wa al Houthi wanapaswa kuyaachilia majengo mengi ya serikali wanayoyashikilia. 

Makamu wa Rais ameongeza kuwa, pande hizo mbili zimekubaliana juu ya kusimamishwa machafuko katika mji mkuu wa nchi hiyo, kujiuzulu serikali na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa katika kipindi cha wiki moja hadi mbili zijazo.

0 comments:

Post a Comment