JESHI la Magereza limetangaza nafasi mbalimbali za ajira katika jeshi
hilo ambapo watakaochaguliwa watapatiwa mafunzo ya awali ya askari
magereza yatakayoendeshwa na Chuo cha Magereza Kiwira, Tukuyu Mbeya.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamishna wa jeshi hilo, John Minja, ilisema kuwa mwisho wa maombi hayo ni Oktoba 15 mwaka huu.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa watakaofanikiwa kuitwa katika usaili
watajulishwa kupitia tovuti ya Jeshi la Magereza. www. magereza. go. tz,
magazeti na katika mbao za matangazo ofisi za wakuu wa magereza wa
mikoa na bwalo kuu la maofisa wa magereza lililopo Ukonga jijini Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwombaji anatakiwa kuwa raia wa Tanzania
na kwamba awe na sifa mbalimbali ambazo ni pamoja na kutoajiriwa katika
taasisi yoyote ya Serikali.
Sifa nyingine ni kwamba, asiwe ameoa au kuolewa na wala asiwe na
mtoto.
Mwombaji ambaye ni mhitimu wa shahada ya kwanza anatakiwa kuwa na
umri wa kuanzia miaka 18 hadi 28 na wasiokuwa na shahada wawe na umri
18 na 24.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa, mwombaji mvulana awe na urefu
usiopungua sentimeta 170.2 au futi 5 na inchi 7 na msichana awe na urefu
usiopungua sentimeta 167.64 au futi 5 na inchi 4.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa, mwombaji ambaye amehitimu elimu yake
kati ya mwaka 2012 hadi 2014 awe na afya nzuri iliyothibitishwa na
daktari anayetambulika kisheria.
Taarifa hiyo ilizidi kufafanua kuwa, mwombaji awe hajawahi kushtakiwa
au kupatikana na kosa lolote la jinai pia awe na tabia na mwenendo
nzuri.
Ilibainisha kuwa awe na shahada katika fani au taaluma mbalimbali
ambazo ni pamoja na shahada ya sheria, utekelezaji wa sheria, takwimu,
uchumi na mipango, mazingira, usanifu majengo, ukadiriaji majengo,
mipango na usimamizi wa miradi, uhandisi wa umeme, uhandisi wa mitambo
ya kilimo na tiba ya mifugo.
Taaluma nyingine ni pamoja na misitu, uchumi, kilimo, bima, uhasibu
na usimamizi wa vyama vya ushirika, uhandisi mazingira, sayansi na
kompyuta, udaktari wa binadamu, ualimu wa masomo ya sayansi, kama
fizikia, kemia, hisabati na baiolojia.
Ilibainisha kuwa mwombaji awe na taaluma ya ualimu wa masomo ya biashara na Kifaransa. Ukutubi, mahusiano, biashara na masoko.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwombaji mwenye stashahada (Diploma)
anatakiwa kuwa na cheti ambacho chuo chake kinatambulika na Serikali.
Mwombaji huyo anatakiwa kuwa na fani au taaluma mbalimbali ambazo ni
pamoja na ukutubi, biashara na mipango, bima, uhasibu na usimamizi wa
vyama vya ushirika.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa, taaluma nyingine ni pamoja na Mipango
na Usimamizi wa Miradi, Utabibu, Uuguzi, Maabara na Mazoezi ya Viungo,
Uhandishi wa Habari, Ufundi Magari, Ujenzi, Umwagiliaji, Mitambo ya
Kilimo, Umeme, Usanifu Majengo, Ushauri Nasaha, Uhandisi Mitambo, Sanaa, Ualimu wa Masomo ya Biashara, Uchumi na Kifaransa,
Mwombaji mwenye astashahada anatakiwa kuwa na fani mbalimbali ambazo
ni pamoja na cheti cha majaribio ya ufundi katika fani za Uhandisi Maji,
Ujenzi, Ufundi Magari, Umeme wa Magari, Waunganishaji Nondo.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa fani nyingine ni pamoja na Useremala,
Bomba, Rangi, Ushonaji, Utengenezaji Sabuni, Ufumaji, Utengenezaji
Viatu, Maabara,Utamaduni, Uuguzi na Ukunga, Utabibu Msaidizi.
Taarifa hiyo iliwataka waombaji kuzingatia masharti yaliyotajwa ikiwa
watabainika wamefanya udanganyifu wowote ikiwamo wa kutotimiza masharti
yaliyotajwa hapo juu maombi yake yatatupwa.
Ilibainisha kuwa mwombaji ambaye atagundulika alifanya udanganyifu
huo baada ya kupatiwa ajira, jeshi hilo litasitisha ajira yake,
kuachishwa kazi na kufikishwa mahakamani.
Taarifa hiyo iliwataka waombaji kuwasilisha maombi yao moja kwa moja
kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Makao Makuu ya Magereza kwa kutumia
sanduku la posta 9190.
Ilieleza kuwa barua zote ziambatane na nakala zote za elimu, ujuzi,
cheti cha kuzaliwa cha mwombaji pamoja na picha ndogo mbili za hivi
karibuni.
Vyeti halisi vitatakiwa kuonyeshwa wakati wa usaili, hati ya mitihani
haitapokelewa isipokuwa kwa wahitimu ambao vyeti vyao havijatoka katika
vyuo husika pekee.
Sep 22, 2014
JIPATIE AJIRA MAGEREZA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment