Sep 22, 2014

AL SHABBAAB YAUNDWA NA WATANZANIA;BALOZI

 Balozi wa Umoja wa Mataifa, Augustine Maiga, akitoa mada  wakati maadhimisho ya Siku  ya Amani Duniani yaliyojadili Nafasi ya Vijana katika Kudumisha Amani yaliyofanyika mkoani Dodoma jana. Kulia ni mtoa mada mwenzake kutoka Baraza la Dini la Kudumisha Amani, Shekh Mohammed Khamis Said. Picha na Silvan Kiwale

 Balozi wa Umoja wa Mataifa, Augustine Maiga, akitoa mada wakati maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani yaliyojadili Nafasi ya Vijana katika Kudumisha Amani yaliyofanyika mkoani Dodoma jana. Kulia ni mtoa mada mwenzake kutoka Baraza la Dini la Kudumisha Amani, Shekh Mohammed Khamis Said. 

BALOZI wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa, Augustine Mahiga, amesema vijana wa Tanzania ni kati ya wapiganaji wanaounda kundi la kigaidi la Al-Shabaab lililoko nchini Somalia.

Amesema kwamba, yeye binafsi amewahi kuwaona vijana hao nchini humo na kwamba aliwahi kuzungumza nao ili kujua sababu zilizowapeleka katika kundi hilo.

Balozi Mahiga ambaye pia amewahi kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini, alitoa taarifa hiyo jana alipokuwa akizungumza na vijana mjini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani.

“Nyinyi vijana ndiyo mtakaoweza kuleta amani na nyie ndiyo wenye jukumu kubwa la kulinda amani yetu.

“Kwa hiyo nawaombeni mlinde amani yetu kwa sababu kama ikitoweka itakuwa vigumu sana kuirejesha na mifano halisi ya maeneo yaliyopoteza amani mnayajua.

“Siku hizi vijana wamekuwa wakijiunga na vikundi vya kigaidi vikiwamo Al-Shabaab kwani wakati nikiwa nchini Somalia, nilishuhudia vijana wa Kitanzania wakishiriki katika kundi hilo.

“Wapo niliozungumza nao nikawauliza wamejiunga huko kwa sababu gani nao wakaniambia wanatafuta maisha. 

Tena Watanzania wengine niliwashuhudia wakiwa wameuawa, yaani inaumiza sana kuona wenzako wameuawa.

“Siyo kwamba vijana hao wako Al-Shabaab peke yake, wengine wako kule Yemen na tatizo hili si la Tanzania peke yake, ni tatizo la dunia kwani katika makundi ya kigaidi wako pia Wakenya na hata Waganda.

“Hili tatizo la vijana wetu kujiunga huko, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinajua kwamba kuna uandikishaji wa vijana wetu unaendelea ila hapa nilichokifanya ni kuwatonya tu,” alisema Balozi Mahiga.

Katika mazungumzo yake, alizungumzia jinsi hali ilivyo mbaya nchini Somalia na kusema kuwa wakati akifanya kazi za Umoja wa Mataifa nchini humo, alisaidia kuziunganisha pande zilizokuwa zikipingana na pia alisaidia kuundwa kwa Bunge la pamoja na uwepo wa Serikali ya kidemokrasia.

“Vijana msiombe nchi ikakosa amani, wanaopigana vita hawana ubinadamu kabisa, wao hawana muda wa kula, yaani mwenzao mmoja akianguka chini, mwingine anachukua bunduki yake na kusonga mbele.

“Kwa maana hiyo, nawaomba sana muilinde amani yetu, msikubali kutumika kwa namna yoyote kwa sababu amani ikitoweka ni gharama sana kuirudisha,” alisema.

Balozi Mahiga alizitolea mfano nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Liberia na Sieraleone ambazo alisema wananchi wa nchi hizo wanaishi maisha ya shida kwa sababu hakuna amani.

Wakati huo huo, Mwakilishi wa Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mohamed Said, aliwataka vijana wajitokeze kwa wingi wakati wa uchaguzi mkuu ujao ili wawachague viongozi bora na kuwakataa viongozi wasiofaa.

0 comments:

Post a Comment