Sep 21, 2014

HAKUNA UWEZEKANO WA SERIKALI TATU;BALOZI SEFUE


 

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema hakuna uwezekano wa kubadili muundo wa muungano kutoka Serikali mbili kwenda Serikali tatu katika mchakato wa Katiba.
Kauli ya Balozi Sefue imekuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa Kituo cha Demokrasia (TCD) na kutoa uamuzi wa kuahirisha mchakato wa Katiba hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Suala la muundo wa muungano lilichukua mjadala mkali ndani ya Bunge Maalumu la Katiba huku wajumbe wanaounda kundi la Ukawa wakiunga mkono mapendekezo ya Rasimu ya Katiba ya muundo wa Serikali tatu na wajumbe wa CCM wakisisitiza muundo wa Serikali mbili.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti la mwananchi, Balozi Sefue alisema mchakato wa Katiba unahitaji maridhiano, lakini suala la muundo wa muungano halina maridhiano katika jamii hivyo litachelewesha upatikanaji wa Katiba:
“Katika historia ya nchi yoyote, wakati unafika wananchi wakawa na maridhiano fulani, wakaamua kuyaingiza ndani ya Katiba. 

Tatizo linajitokeza pale watu au makundi fulani yanapong’ang’ania kuingiza ndani ya Katiba mambo ambayo ni dhahiri hayana maridhiano ndani ya jamii. 

Mfano ni suala la muundo wa Muungano,” alisema na kuongeza:
“Uzoefu wa Bunge Maalumu hadi sasa ni kuwa hakuna uwezekano wa kupata maridhiano ya kubadili muundo wa Muungano kutoka Serikali mbili kwenda tatu. 

Hutapata maridhiano hayo ndani ya Bunge Maalumu na hutapata maridhiano ukienda kwa wananchi,” alisema.
Alisema anaamini wajumbe wa Bunge Maalumu walifanya uamuzi wa busara kuliweka kando jambo hilo linalotugawa, na kuendelea kujadili Rasimu ya Katiba kwa msingi wa mfumo uliopo wa Serikali mbili,” alisema.
Balozi Sefue aliongeza kuwa tangu suala hilo liwekwe kando kumekuwa na kasi na matumaini ya kupata Katiba Mpya.
Alisema jambo hilo ni kubwa na uzoefu unaonyesha lina uwezo mkubwa wa kutugawa na kuchelewesha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Balozi Sefue alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliamini yatapatikana maridhiano kuhusu kubadili muundo wa Muungano, ilivyo sasa, ni wazi kuwa maridhiano kuhusu mabadiliko hayo hayapo na hayatapatikana.
“Hakuna idadi ya makongamano na maandamano yatakayobadili hali hiyo sasa,” alisema.
Licha ya kusema kuwa kuna matumaini ya kupata Katiba Mpya, Balozi Sefue alisema ikishindikana Katiba iliyopo itafanyiwa marekebisho ili ituvushe hadi mchakato utakaporejeshwa tena.

0 comments:

Post a Comment