Aug 6, 2014

Mmoja afariki kwa maradhi ya Ebola nchini Saudia

Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imetangaza kuwa mhanga wa kwanza wa maradhi ya Ebola amefariki dunia nchini humo. 

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imeeleza kuwa, watu wote waliokutana na mhanga huyo baada ya kurejea safari ya kikazi nchini Sierra Leone wanapasa kuwa chini ya uangalizi maalumu wa kiafya.
Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imeongeza kuwa, vipimo vya kimaabara vilivyochukuliwa kwa mgonjwa huyo vilionyesha kwamba, raia huyo wa Saudia alikumbwa na maradhi ya Ebola wakati alipokuwa nchini Sierra Leone kikazi.

Mara baada ya kutangazwa kujitokeza maradhi ya Ebola katika nchi za Sierra Leone, Liberia na Guinea Conakry, serikali ya Saudi Arabia ilichukua hatua za tahadhari za kukabiliana na maradhi hayo hatari yasiyokuwa na tiba wala chanjo, kwa kupiga marufuku utoaji viza kwa mahujaji wa nchi hizo. 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya kesi 1,600 za maradhi hayo zimeripotiwa katika nchi za Sierra Leone, Liberia na Guinea Conacry, ambapo watu zaidi ya 880 wamefariki dunia. 

Shirika la WHO limeeleza dalili za ugonjwa wa Ebola kuwa ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuuma kichwa na vidonda kooni. 

Imeelezwa kuwa, mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa hutokwa damu ndani na nje ya mwili.

Ugonjwa wa homa ya Ebola huambukiza kwa kasi na unaenea kati ya mtu na mtu kwa kugusa damu na majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo. 

Aidha imeelezwa kuwa, mtu huambukizwa ugonjwa huo kwa kugusa maiti au mizoga ya watu au wanyama waliopatwa na maradhi hayo.

0 comments:

Post a Comment