RAIS
Jakaya Kikwete amekubali kuongeza muda wa Bunge Maalumu la Katiba
katika mazungumzo aliyofanya na mwenyekiti wake, Samuel Sitta.
Hayo yalisemwa na
Mwenyekiti huyo wakati akijibu swali la waandishi wa habari katika
mkutano wake jana, Dar es Salaam, baada ya kumaliza mkutano wake na
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu.
Ziara hiyo ambayo
amesema ni utaratibu aliouanza kukutana na viongozi wa dini, pia
ilimkutanisha na Mufti wa Baraza la WaislamU Tanzania (BAKWATA), Shekhe
Issa Bin Shaaban Simba. Sitta alikutana na Rais Kikwete juzi.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa Sitta, Rais Kikwete hajataja ni lini Bunge hilo
litaanza tena kwa nyongeza ya siku 20 kwa mujibu wa sheria, baada ya
siku 70 zinazomalizika mwezi huu, kuisha ili kufanya jumla ya siku 90.
Lakini amesema uongozi wa Bunge umekusudia lianze tena Agosti mwaka huu.
Alisema lengo la kukutana na viongozi hao wa kidini ni
kuwaeleza kinachoendelea Dodoma, kwa kile alichodai viongozi hao wana
ushawishi na wafuasi wengi nyuma yao, hivyo si busara kusikia mitaani.
Katika
mkutano huo Sitta alikanusha habari ya gazeti moja lililodai anakwenda
kuwaangukia viongozi hao na kusema hana dhambi za kufanya hivyo.
“Leo
(jana) nimepanga kukutana na viongozi wa dini zetu na si hawa tu
nitakaokutana nao, nitaendelea na utaratibu huu kwa viongozi wengi hata
wenye wafuasi wachache, hawa wana ushawishi japo hawahusiki sana na
siasa lakini ni viongozi wa jamii, wanapaswa kupata taarifa sahihi ya
nini kinachoendelea Dodoma,” alisema Sitta.
Alisema katika
mazungumzo yake na Kardinali Pengo jana asubuhi, amemweleza kwa kifupi
mchakato unavyoendelea Dodoma na yeye (Pengo) alimhakikishia kuwa Kanisa
Katoliki linaliombea Bunge Maalumu la Katiba na wajumbe wote ili lengo
lifikiwe na Watanzania wapate Katiba mpya na yenye ubora.
Baada
ya kutoa maelezo hayo mafupi ya mkutano wake na Pengo, Sitta akijibu
maswali ya waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa Bunge hilo, ikiwemo
kama muda wa takribani wiki tatu uliobaki unatosha kumaliza kazi iliyo
mbele yao, alisema muda huo hautoshi.
“Ni dhahiri mpaka Aprili
28 tutakuwa hatujamaliza Bunge, itabidi tupishe Bunge la Bajeti la
Muungano, Wawakilishi watarejea Zanzibar na sisi wengine tutabaki
Dodoma, bajeti itafanyika si chini ya miezi miwili, yaani Mei na Juni,”
alisema na kuongeza: “Jana nilionana na Rais Jakaya Kikwete nikamweleza
hali halisi ilivyo, kimsingi alikubali ataongeza muda ingawa hatukufikia
kutaja ni lini.
Ila sisi tunakusudia tuanze tena
Agosti, nimemweleza kwa undani maana hata baadhi ya nchi nyingi
zimechukua muda kuandika Katiba, akaona ukweli huu akatuongezea”.
Sitta
alisema Bunge litatangaza rasmi utaratibu huo utakapokamilika ila
alisisitiza kuwa, kwa hali inavyoendelea hawawezi kuendelea kubaki
Dodoma kwa ajili ya Katiba kwa kuwa kisheria siku zitakwisha na pia
mwingiliano wa sikukuu za Pasaka na Muungano Aprili 26, zitapunguza
siku.
Muundo wa Muungano:
Awali, akizungumzia kuhusu
muundo wa muungano hasa baada ya kuibuka kwa madai ya kutaka Hati ya
Muungano wakati wa mjadala wa sura ya kwanza ya sita ya Rasimu ya Katiba
uliofanyika katika kamati, Sitta aliwataka wabunge kutopoteza muda
kujadili serikali ngapi ziwepo.
Aidha, Sitta amesema ipo hatari
ya kupoteza muda mwingi kuzungumzia muundo wa serikali uweje, jambo
analoona kwa baadhi ya watu, wanataka serikali nyingi kwa uchu wa
madaraka wakijua wakikosa uongozi upande mmoja, watapata upande
mwingine.
Alisema ingawa suala la serikali ni muhimu kwa kuwa
ndio linalotoa dira, ila haja kubwa ipo katika kuipitia rasimu Ibara kwa
Ibara kama alivyoagiza Rais Kikwete.
Alitolea mfano suala la uadilifu na kushauri wajumbe wakipitia vizuri, watashauri mfumo gani uwekwe kuwabana zaidi viongozi.
“Kiongozi
anapaswa ajue anaingia katika utumishi wa umma si kuchota fedha na
kufanya ufisadi bali suala kubwa ni maendeleo ya nchi, ustawi wa
wafanyakazi, wakulima na vijana, kuhakikisha sheria zinakuwepo kuzuia
mikataba mibovu, kwa mfano Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania)
inavyopandisha umeme, wananchi wanaumia.”
“Tukiingia katika sura
nyingine za rasimu, Katiba lazima ibane tutunge sheria zilizo wazi,
angalia suala la Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, tunajaza fomu
kisha zinakuwa siri, sasa zina haja gani, ni za nini, si bora tuache,
maana naweza kujaza nina kijumba kibovu kimoja, kumbe nina majumba,”
alitoa mfano Sitta.
Alisema, “Ili kuzuia viongozi kujitajirisha,
ni lazima sheria ziwe kali la sivyo wizi utaendelea, sheria inapaswa
kuwakwamisha wanaopenda madaraka…., maombi yangu kuhusu mchakato, pamoja
na purukushani, kutaka kuonekana, vijana machachari, lakini wengi
wanataka Katiba mpya ipatikane.”
Sitta akifafanua kuhusu ama
serikali tatu ama mbili, alinukuu alichowahi kusema mwanasiasa mkongwe
nchini, Kingunge Ngombale- Mwiru kuhusu suala hilo kwamba ni kama
wanaotaka serikali tatu wanataka madaraka, kwamba akikosa uongozi katika
upande mmoja, apate kwingine.
Hati ya Muungano;
Sitta
aliwaambia waandishi wa habari kumekuwepo na madai ya hati ya Muungano
katika kamati na kwamba, ni ajabu kuona ndoa iliyodumu kwa miaka mingi,
wahusika sasa wamekuwa vikongwe, anatokea mtu anadai cheti cha ndoa.
“Ni
kama haamini kwamba hiyo ndoa ilifungwa ama! Ni ajabu kweli, vielelezo
ni pamoja na Sheria ya Bunge ya Aprili 5 mwaka 1964, Msekwa akiwa Katibu
wakati huo alikwenda katika kamati kueleza yaliyotokea wakati ule,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amekwenda kueleza.”
“Ndoa watu wamefunga miaka, wamekuwa vikongwe, wajukuu leo wanadai cheti
cha ndoa, ni upuuzi, mtu anayehitaji utafiti aendelee, hakuna
anayemzuia ila haituzuii sisi kuendelea,” alieleza Sitta.
Ripoti za Kamati;
Kwa
mujibu wa Sitta, Alhamisi na Ijumaa wiki hii, taarifa za kamati
zitatolewa bungeni na maoni ya wengi na ya wachache yataelezwa ili
kuruhusu mjadala kuanza ndani ya ukumbi na kwamba katika sura ya kwanza
hadi ya sita, kila mjumbe atachangia.
“Baada ya hapo kazi
itakuwa nyepesi, siwezi kutabiri kitakachotokea lakini hoja yenye maana
itashinda, ukiacha wachache wenye utamaduni wa fujo, wengi wanataka
ifike mahali tupate Katiba mpya, tusichezee mabilioni ya Watanzania
bure.
Uzoefu wa Kenya;
Sitta alitumia nafasi hiyo
kutolea uzoefu wa nchi jirani ya Kenya mwaka 2007 walipoingia katika
machafuko ya kisiasa baada ya kushindwa kufanya mabadiliko katika Katiba
yao na kufanya uchaguzi.
Alisema kazi inayofanyika Dodoma ni
kubwa hivyo inapaswa kufanyika kwa umakini mkubwa vile vile. Akiwa na
Mufti Mkuu Akizungumza mara baada ya kukutana na Mufti wa Tanzania,
Shekhe Issa Bin Shaaban Simba, Sitta alisema ujumbe wake ulipokewa
vizuri katika Ofisi za Bakwata, Dar es Salaam na kwamba Mufti alishukuru
hatua hiyo ya Waislamu kushirikishwa.
“Ukweli Mufti amefurahia
huu ujio wangu hapa na kuueleza kuwa anafuatilia kwa makini kile
kinachoendelea kwa sasa kule Dodoma na zaidi ameuombea mchakato huu
uweze kuisha kwa amani na utulivu hadi katiba mpya itakapopatikana”
“Zaidi ametutaka wajumbe wote kuvumiliana na kufanya kazi yetu
tukitanguliza maslahi ya Taifa na kuachana na misuguano ili hatimaye
katiba iweze kupatikana,” alisema Sitta.HABARILEO
Apr 9, 2014
SAMUEL SITTA USO KWA USO NA MUFTI SIMBA NA KADINAL PENGO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment