Oct 31, 2013

Waandamana Kupinga Kubakwa

Wanaharakati 300 wanaowakilisha mashirika ya kutetea haki za wanawake kote nchini hii leo wameandaa kufanya maandamano ya kulaani kitendo cha washukiwa waliombaka msichana mmoja mwenye umri wa miaka kumi na sita na kupewa adhabu ya kukata nyasi.

Wakereketwa hao wameelezea kukasirishwa na adhabu hiyo na kuhoji kwa nini polisi hawakufanya uchunguzi ili kumtendea haki msicha huyo.
Lengo la maandamano yao hii leo ni kuwasilisha ombi lililotiwa saini na zaidi ya watu milioni moja kwa mkuu wa polisi kutaka washukiwa kukamatwa na kushitakiwa ili msichana huyo anayejulikana kama Liz kupata haki.

Pia wanataka polisi waliowaadhibu washukiwa na kisha kuwaachilia kukamatwa na kufunguliwa mashitaka.

Maandamano yanatarajiwa kuanzia katika bustani la Uhuru Park katikati mwa mji wa Nairobi hadi katika makao makuu ya polisi kumkabidhi mkuu wa polisi ombi lao lililoanzishwa na mwanaharakati Nebila Abdulmelik kwenye mtandao.

Ombi hilo ambalo limetiwa saini na wanawake milioni 1.2 litatiwa ndani ya kijisanduku cha mbao na kukabidhiwa polisi.

Pia wataanika nguo za ndani kwenye kamba zikiwa na ujumbe wa kutaka mageuzi .

Tayari wanawake milioni 1.2 wameunga mkono kampeini hiyo iliyoanzishwa na mwanaharakati Nebila katika mtandao wa kijamii wa Avaaz ulio na wanachama milioni ishirini na saba kote duniani na inaarifiwa idadi ya wanawake wanaopinga kitendo cha wakabakaji na kile cha polisi kuwaadhibu kwa kukata nyasi, inaendelea kuongezeka.

Kampeini hii imekuja baada ya msichana Liz kubakwa na genge la wanaume sita ambao baadaye walimtupa ndani ya shimo la choo.

Liz alipata majeraha mabaya sana na hata kuvunjika uti wa mongo na sasa amelazimishwa kutumia kiti cha magurudumu na hadi sasa amefanyiwa upasuaji katika sehemu zake za siri.

Polisi waliwakamata watatu kati ya wanaume waliodaiwa kumbaka msichana huyo, lakini baadaye wakawaachilia baada ya kuwaadhibu kwa kukata nyasi nje ya kituo cha polisi.

0 comments:

Post a Comment